Bishop Hiluka
JF-Expert Member
- Aug 12, 2011
- 7,140
- 14,678
- Thread starter
- #201
136
Kisha kikapita kitambo kifupi cha ukimya mle ndani huku kila mmoja akionekana kuzama kwenye tafakuri yake. Macho ya Olivia yalikuwa yananitazama kiwiziwizi na mdomo wake ulikuwa unanisubiri huku akili yake ikiwa mbali, mkono wake mmoja ulikuwa shingoni. Sikujua tafsiri halisi ya hali hiyo na hivyo kujikuta nikiwa njia panda.
“Samahani Jason, sikuwa nimekujulisha mapema kuhusu hiki kilichonifanya nije nyumbani kwako saa hizi, lakini naamini utanisamehe na kukubali ombi langu,” hatimaye Olivia alivunja ukimya, kisha akaongeza, “Naomba kama una nafasi unisindikize sehemu. Sikuwa nimepanga kwenda na wewe lakini nimegundua kuwa wewe kwa sasa umekuwa mtu muhimu sana kwangu.”
“Unataka nikusindikize wapi?” nilimuuliza Olivia huku moyoni mwangu nikihisi kuwa na furaha ya aina yake.
“Kuna sehemu nataka twende… nina kikao cha kibiashara na wawakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) leo saa 8:00 mchana, kwa ajili ya ile project yangu. Nakwenda kufanya presentation,” Olivia alisema huku akitabasamu.
“Dah, sasa mbona umenishtukiza? Ungeniambia mapema ili nijiandae,” nilisema huku nikishusha pumzi.
“Mapema ipi na wakati tumekutana jana tu na kikao hiki kilishapangwa wiki mbili zilizopita? Wazo la kukushirkisha nimelipata usiku nikiwa kitandani, nisamehe kwa hilo,” Olivia alisema huku akionekana kukata tamaa.
“Kwa hiyo unataka nijiandae sasa hivi twende?” nilimuuliza kwa shauku huku nikiinua mkono wangu wa kushoto kutazama saa yangu.
“Ndiyo, kama hautojali,” Olivia alisema huku akiendelea kutabasamu.
“Usihofu, nina nafasi ya kutosha, nipe dakika chache tu nijimwagie maji chapchap,” nilimwambia huku nikiinuka na kuelekea chumbani.
Ilinichukua dakika kumi na tano tu kujiandaa na kuvaa suti niliyoamini ingeendana kwa kiasi kikubwa na suti ya Olivia. Ilikuwa suti nzuri ya rangi ya samawati brandi ya Dunhill, shati zuri la rangi ya maruni la kitambaa brandi ya Barba, tai shingoni ya rangi ya bluu na viatu ghali vya ngozi halisi kutoka nchini Switzerland vya rangi ya maruni. Kisha nikajipulizia manukato ya gharama kubwa aina ya Clive na kukamilisha utanashati wangu ulionipa mwonekano wa kijanja.
Nilirudi pale sebuleni nikitembea kwa madaha, nikamkuta Olivia akiwa amesimama akiitazama kwa umakini picha kubwa ya Rehema. Alipogundua kuwa nimerudi aligeuza shingo yake kuniangalia kisha akaachia mshangao. Ukweli nilikuwa nimependeza sana, maana ukiambatana na mrembo kama huyo kwenda sehemu inakubidi uwe umetoka ‘chicha’ ili mwendane.
“Wow! You look so handsome,” Olivia aliniambia huku akiachia tabasamu kisha akageuza shingo yake kuitazama ile picha ya Rehema pale ukutani.
“Huyu ukutani ndiye Rehema?” Olivia aliniuliza huku akielekeza kidole chake cha shahada kwenye picha ya Rehema. Niliitazama ile picha kana kwamba nilikuwa naiona kwa mara ya kwanza kisha nikabetua kichwa changu kukubali.
“Wala hukusema uongo, ni kweli tunafanana sana!” Olivia alisema huku akianza kupiga hatua taratibu akianza kutoka nje.
Niliweka vizuri vitu vyangu pale sebuleni kisha nikamfuata Olivia kule nje na kumkuta akiwa tayari amepanda ndani ya gari lake na kuliwasha kisha akakanyaga pedeli ya mafuta na kuusikilizia mvumo wa taratibu wa gari. Nilipanda ndani ya gari na kufunga mkanda.
Baada ya gari kuunguruma kwa dakika chache Olivia akatumbukiza gia ya kurudi nyuma na kukanyaga pedeli ya mafuta huku akinyonga usukani, na hapo gari likaanza kurudi kinyumenyume likipita katikati ya ile barabara nzuri iliyotengenezwa kwa vitofali vidogo vilivyovutia kisha akaligeuza.
Gari lilipokaa sawa nami nikabonyeza kitufe cha OPEN kwenye remote ya kufungulia geti na hapo geti likaanza kufunguka taratibu, gari likasogea hadi kwenye geti na tulipotoka lile geti likajifunga lenyewe taratibu.
Olivia aliliondoa gari na kuingia barabarani kisha alikata kushoto na kuingia katika barabara nyingine na hapo akaongeza mwendo hadi tulipofika katika eneo la Nyihogo akakata na kuingia upande wa kushoto akiifuata barabara kuu ya lami inayoelekea katika nchi za Rwanda, Uganda na Burundi.
Kwa muda huo barabara hiyo ilikuwa na magari mengi hasa malori ya mizigo yaliyoelekea nchi jirani na hivyo Olivia alilazimika kuikwepa foleni ile ndefu ya magari katika barabara ile na kuingia barabara iliyoelekea Uhindini.
Hapo aliongeza mwendo japo barabara ile ilikuwa inapitwa na magari mengi lakini hayakusababisha msongamano, na baada ya kitambo fulani cha safari tulijikuta tumefika kwenye makutano ya barabara nyingine za mtaani na Olivia alikata tena na kuingia upande wa kushoto kama aliyekuwa akiifuata barabara ya kuelekea Zongomera kisha tukaingia tena upande wa kulia kuifuata barabara iliyokwenda kutokea katika stendi ya mabasi ya Kahama.
Baada ya mwendo fulani tulianza kupita katika eneo la stendi ya mabasi ya Kahama upande wetu wa kulia, na upande wa kushoto tuliyapita majengo ya benki ya NMB, jengo la Kampuni ya Simu na benki ya CRDB na hapo tukaingia kushoto kuifuata barabara iliyoelekea ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Kahama. Baada ya mwendo mfupi tukaanza kuyapita majengo ya Hospitali ya Wilaya, kisha Parish ya Kanisa Katoliki, na baadaye Ofisi za Manispaa na hatimaye tuliyafikia majengo ya Chuo cha Maendeleo ya Wananchi cha Mwanva na kisha tukaenda kuungana na barabara kuu ya kuelekea nchi za Rwanda, Uganda na Burundi.
Muda wote nilikuwa nimetulia kimya nikimtazama Olivia kwa chati huku nikiwa sijui tunaelekea wapi. Mwanzoni nilidhani kuwa huenda tulikuwa tunaenda Hotel Latitude lakini sasa nilitambua kuwa si huko. Niliona kabisa Olivia akiendesha kuelekea sehemu nyingine kabisa. Nje ya mji wa Kahama, nikashangaa!
Aliendelea kuendesha na kuingia upande wa kulia sehemu ambayo hakukuwa na makazi mengi ya watu, kulikuwa na nyumba chache zikiwa mbalimbali sana, na baada ya dakika chache tukawa tumefika kwenye jengo moja jipya la ghorofa tano. Hadi hapo tulikuwa tumetumia takriban dakika 35 kutoka nyumbani kwangu eneo la Mwime.
Nje ya lile jengo kulikuwa na milingoti kadhaa yenye bendera za nchi mbalimbali kama Tanzania, Kenya, Uingereza, India, Afrika Kusini na China zilizokuwa zinapepea taratibu.
* * *
Endelea...