SIMULIZI: Dunia duara

JOTO LA MOTO

JF-Expert Member
Apr 11, 2018
758
555
SIMULIZI: DUNIA DUARA.

KUTOKA KWA JOTO LA MOTO.

SEHEMU YA KWANZA.

KIJENGE JUU ARUSHA-MSURURU WA VYUMBA VYA KUPANGA-NJE-ASUBUHI.
Rose, Mwanadada mrembo wa miaka 20, yupo nje ya nyumba anapiga mswaki, anakuja Mlela, kijana wa miaka 21, huku akiwa mkononi ameshikilia fulana kuu kuu, “mimi ngoja niwahi maji kabla hakujawa na foleni” anasema Mlela huku akiwa anaivaa ile fulana aliyoibeba, “jitahidi basi maana pale sina maji kabisa” anasema Rose, Mlela anabaki amesimama akimuangalia Rose, “nini tena?” anauliza Rose baada ya kuona Mlela bado ameduwaa, “tairi moja haina upepo na mfukoni sina hata sumni” anasema Mlela, Rose anashusha pumzi, “hivi pesa zako huwa unapeleka wapi?” anauliza Rose, “ni pesa gani ile ninayoipata Rose?” anasema Mlela, “chukua elfu tano pale ndani kwenye ile pochi kubwa nyeupe” anasema Rose na kumfanya Mlela kuondoka na kuelekea ndani ya chumba, Rose anaendelea kuswaki.


MTAANI-CHUMBA CHA MAMALISHE-NDANI.
Rose amesimama kwenye kona akimimina chai kwenye kikombe kutoka kwenye thermos, kisha anachukua kikombe kile na sahani yenye chapati mbili na kupeleka kwa mmoja wa Wateja kadhaa waliopo pale ndani. Nje anafika Mlela, akiwa ameloa jasho sehemu ya kifuani na makwapani huku mkononi ana kitambaa akijifuta jasho usoni, anasimama mlangoni akimuangalia Rose anayeweka kikombe na sahani ya chapati mezani kwa Mteja na kisha anapokea pesa, Rose anainua kichwa na kumuona Mlela akiwa amesimama pale nje, anamfuata “vipi..mbona umechelewa hivyo tena jamani?” anasema Rose huku akifika pale alipo Mlela, “tairi la mkokoteni limesumbua tena”, “maji nimeleta jaba tano” anasema Mlela, “afadhali..nikuwekee chakula?” anauliza Rose, “nadhani nikimbie kwanza kwa Mama mwenye nyumba” anasema Mlela na kumfanya Rose kushtuka na kuingiza mkono kwenye mkoba wake aliouvaa kiunoni na kutoa pesa kadhaa, “hebu kweli mpelekee hela yake yule Mama..maana tangu amesikia tumeanza kujenga ni visa juu ya visa” anasema Rose huku akihesabu pesa zile, “uchukue na elfu ishirini pale ndani juu ya meza” anasema Rose huku akimpatia Mlela zile pesa, Mlela anapokea na kuziweka mfukoni, “ukirudi pitia basi mkaa kwa Abuu” anasema Rose, “naenda kwanza shuleni wamenipigia wanahitaji maji” anasema Mlela, “sawa basi ukimaliza hiyo kazi ya shule upite kwa Abuu” anasema Rose, “poa” anajibu Mlela huku akiondoka, “na naomba leo ukipata hela huko ulipe deni la Mukulu..sipendi anavyokuja kusumbua pale nyumbani” anasema Rose na kumfanya Mlela kusita kwa muda, “kama ticha atalipa vizuri nitamlipa Mukulu” anasema Mlela na kuondoka,“dada ongeza maharage” inasikika sauti kali ya Mteja kutoka ndani inayomshtua Rose na kumfanya kuingia ndani kwa haraka.


MIAKA NANE BAADAE.

NYUMBANI KWA ROSE NA MLELA-NJE.
Gari zuri aina ya Toyota Harrier nyeupe imesimama nje ya geti, mbele ya nyumba moja nzuri ya kuvutia, Mlela yupo ndani ya gari ametulia huku akionekana kufurahia muziki laini wa bongo fleva unaotoka redioni, geti linafunguka anatoka Rose akiwa amevalia kitenge maridadi na kupendeza, mkononi amebeba pochi nzuri, anafunga geti lile na kuingia kwenye gari, “nilikuacha umeshavaa lakini bado umetumia zaidi ya dakika ishirini” anasema Mlela huku akiwasha gari na kuweka gia na kuondoa, “nilikuwa kwenye maombi” anasema Rose, kinapita kimya kifupi, “naona wewe siku hizi maombi kwako si muhimu tena?” anasema Rose, “maombi ni popote Rose..mimi nimeomba nikiwa huku kwenye gari” anasema Mlela, Rose anamkata Mlela jicho, “tangu lini?” anauliza Rose, Mlela anabaki kimya, “miaka yote mpaka tumefika hapa tulipo ulikuwa ukiheshimu sana maombi Mlela” anasema Rose, “sijasema siheshimu maombi..usiniwekee maneno mdomoni Rose” anasema Mlela kwa sauti ya chini lakini inayoashiria kughafilika, wanakuwa kimya kwa muda, “alafu nikisema siku hizi umebadilika sana unakuwa mkali” anasema Rose kwa sauti ya chini kama Mtu anayenung’unika, kisha anashusha pumzi nyepesi na kutulia, huku Mlela akimkata jicho bila kujibu neno.


SUPER MARKET-NJE.
Gari la Mlela linafika na kusimama nje ya jengo moja zuri lenye bango juu yake linalosomeka “M and R SUPERMARKET”, wanateremka Mlela na Rose na kupokelewa na vijana wawili, Donii na Riki waliokuwa wameketi pale nje ya jengo lile, Mlela anampatia Riki ufunguo, Riki na Donii wanaanza kufungua kofuli za milango ya pale Supermarket.


SUPER MARKET-NDANI-BAADAE.
Wateja kadhaa wakipita huku na kule ndani pale wakichagua bidhaa, Mlela yupo kaunta, mbele yake yupo Mimi Mars, binti mrembo, 26, wanaonekana wakiongea huku kila mmoja akiwa na tabasamu pevu usoni, Rose yupo amesimama mita kadhaa kwenye kona akiwaangalia Mimi Mars na Mlela, huku Riki(kijana wa kazi) akiweka bidhaa mbalimbali kwenye mifuko, kisha Riki anachukua mifuko ile na kutoka akifuatana na Mimi Mars, Rose anakuja kwa Mlela pale kaunta, “mbona sijaona huyo dada akilipia hivyo vitu?” anauliza Rose, “amesema amesahau pesa ataleta kesho” anasema Mlela, “hii ni mara ya pili nashuhudia huyu dada anaondoka na vitu bila kulipa Mlela” anasema Rose, "tatizo lako ni kumuhudumia Mteja huku nimetabasamu au nini Rose?“ anasema Mlea, "tatizo ni kuwa unachofanya ni kutoa zawadi badala ya kufanya biashara Mlela", "Rose please” anasema Mlela kwa sauti ya chini akimkatiza Rose, “hebu naomba nihudumie Wateja” anasema Mlela kisha anamgeukia Bwana mmoja wa makamo anayefika pale kaunta akiwa amebeba chupa kubwa ya maji, Mlela anapokea pesa kutoka kwa Bwana yule, Rose anabaki pale pembeni akimuangalia Mlela huku akishusha pumzi inayoashiria hasira imemkaba kifuani kwake, “karibu tena” Mlela anamwambia Mteja yule huku akimpatia chenji na risiti na yule bwana anaondoka, “naomba baadae tuwe na mazungumzo Mlela” anasema Rose kwa sauti inayoashiria amechukizwa na kisha anandoka pale.


NYUMBANI KWA ROSE NA MLELA-NJE-JIONI
Gari la Mlela linafika getini na kusimama, ndani yupo Mlela na Rose “kuna mahali nafika mara moja nitarudi sasa hivi” anasema Mlela mara baada ya kuvuta hand break, “naomba tuingie ndani tukazungumze kwanza Mlela ndio uende unapoenda”, anasema Rose, “nimesema narudi sasa hivi Rose” anasema Mlela kwa sauti ya kusisitiza, Rose anafungua mlango na kuteremka, Mlela anaondoa hand break, anaweka gia kurudisha gari nyuma na kisha kuondoka, Rose anaenda getini na kubofya kitufe cha kengele, muda kidogo geti linafunguliwa na Nandi, binti mrembo, 20. Rose anaingia na kufunga geti.


NYUMBANI KWA ROSE NA MLELA-NDANI-USIKU.
Mlango unafunguka, anaingia Mlela, anabofya switch pale ukutani kuwasha taa, anashtuka kumuona Rose ameketi kochini ametulia kimya, “upo gizani?” anauliza Mlela, “ndio nipo gizani ndio maana nataka leo nijue ni nini kinaendelea kwa sasa Mlela maana mwenzangu sikuelewi” anasema Rose kwa sauti tulivu, “alafu saa hizi ni saa tano..na ulisema ungerudi mapema?” anauliza Rose, “nilipata kikao cha dharura” anasema Mlela huku akiketi kochini, mezani kuna hotpoti mbili, sahani na vijiko, Rose anachukua sahani na kijiko na kufungua hot poti, “mimi sitakula” anasema Mlela, Rose anabaki anamuangalia Mlela na kisha anashusha pumzi na kuifunga ile hotipoti, Mlela anachukua remote control ya TV iliyopo pale mezani na kuwasha TV, “kama huli basi naomba twende chumbani tukazungumze” anasema Rose, “naaangalia mechi kwanza” anasema Mlela huku akibofya remote mara kadhaa kabla ya kukutana na mechi ya mpira, anaiweka remote mezani, Rose anaangalia kwenye TV, “jamani hiyo mechi si ni marudio?” anasema Rose, “ndio..nataka nirudie kuangalia”, anasema Mlela, Rose anabakia akimuangalia Mlela kwa jicho kali, kisha anainuka na kuondoka, zinapita sekunde kadhaa, Mlela anainuka na kwenda meza iliyo pembeni na kuchukua chupa ya whisky na glasi, anamimina whisky kwenye glasi nusu na kurudi kuketi pale kochini, zinapita sekunde kadhaa huku akipiga funda kadhaa. Anapita Nandi na kumfanya Mlela kushtuka na kugeuka, kisha Mlela anainuka na kwenda alipoelekea Nandi.


NYUMBANI KWA ROSE NA MLELA-JIKONI-USIKU.
Nandi anafika pale jikoni kwenye sinki na kuanza kuosha vyombo, anakuja Mlela na kusimama mlangoni akiwa na ile glasi ya whisky mkononi, “mpaka saa hizi bado hujalala?” anauliza Mlela na kumfanya Nandi kushtuka na kugeuka kumuangalia Mlela, huku Mlela akiendelea kupiga funda ya whisky, “nilikuwa naangalia tamthilia” anasema Nandi, kisha Nandi anageuka na kuja mlangoni akitaka kutoka, Mlela anaziba mlango kumzuia, Nandi anamuona Rose akiwa amesimama nyuma ya Mlela, Nandi anajaribu kumpa Mlela ishara ageuke nyuma, Mlela anageuka nyuma na kumuona Rose, kisha anasogea kumpisha Nandi kutoka, Mlela na Rose wanabaki wanaangaliana kwa muda, kisha Rose anaondoka, Mlela anarudi na kuketi kochini na kuendelea kuangalia TV.


NYUMBANI KWA MLELA-CHUMBANI KWA NANDI-USIKU.
Nandi ameketi kitandani, Rose anaingia na kuketi pembeni ya Nandi pale kwenye kitanda, akiwa amejiinamia na macho yake yakiwa yamejaa machozi, “Nandi mdogo wangu” anasema Rose na kumfanya Nandi kushtuka na kubaki makini kumsikiliza Rose, “kuna nini kinaendelea kati yako na Mlela?” anauliza Rose, “hakuna chochote Dada” anasema Nandi, wanabaki kimya kwa muda, “mimi sio Mtoto Nandi..na kama kuna chochote nitajua tu Nandi...kwa hiyo usipoteze muda kunificha” anasema Rose kwa sauti tulivu lakini ya kusisitiza, “kweli Dada Rose hakuna chochote kinaendelea” anasema Nandi, Rose anashusha pumzi ndefu kisha anapanda kitandani pale na kujilaza, huku Nandi akibaki ameketi pale kitandani.


NYUMBANI KWA ROSE NA MLELA-SEBULENI-ASUBUHI.
Rose na Nandi wameketi kwenye meza ya chakula, Rose akiwa na simu mkononi akiibofya mara kadhaa huku Nandi akimuangalia kwa makini, “kwa nini hakuna kumbukumbu ya simu ulizowahi kupiga au kupigiwa?” Rose anauliza, “huwa sipendi tu kuzihifadhi”, anasema Nandi huku akiangalia chini na kumuacha Rose akibaki anamkodolea macho, wanabaki kimya kwa muda wa sekunde kadhaa, mara wanashtushwa na mlio wa ile simu kuita, Rose anaiangalia simu na kuonyesha mshtuko mkubwa usoni kwake, “Mungu hamfichi mnafiki Nandi” anasema Rose huku akimuonyesha namba inayoonekana kwenye simu, Nandi anabaki anaangalia huku akibaki kimya ameduwaa, “naomba upokee” anasema Rose huku akimpatia Nandi simu, Nandi anapokea na kutaka kuiweka sikioni, Rose anamshika mkono na kumzuia, anaichukua simu na kubofya kitufe na kuifanya simu kuwa kwenye mfumo wa loud speaker kisha anaiweka mezani, “hallow” inasikika sauti ya Mlela, “hallow” anajibu Nandi huku akionekana kuwa na uoga, “uko sawa?” sauti ya Mlela inauliza, “nipo sawa tu” anajibu Nandi, “huyo Kipepe ameshaondoka?” anauliza Mlela, Nandi anamuangalia Rose, Rose anampa ishara aseme ndio, “ameshaondoka” anasema Nandi, “ok nakuja unipe stori za nini kiliendelea jana” inasema sauti ya Mlela na kisha simu inakatika, Rose anabaki anamuangalia Nandi ambaye ameinamisha kichwa huku kaweka mkono shavuni, “kwa nini mnaniita Kipepe?” anauliza Rose, Nandi anabaki kimya kwa muda, “anasema zamani ulikuwa unapenda kufunga nywele zako kwa nyuma kama yule kipepe wa gazetini” anasema Nandi na kumfanya Rose kubaki ameduwaa kwa sekunde kadhaa machozi yakimlenga, anashusha pumzi “Nandi kweli mdogo wangu?” anasema Rose kwa sauti ya chini inayotetema kwa majonzi na jazba, “ulikuja na heshima zote..huna hili wala lile” anaendelea Rose, “Watu nje hata hawajui kama wewe ni dada wa kazi humu ndani kwa jinsi ninavyoishi na wewe kwa upendo?” anaendelea Rose huku akilengwa na machozi, “kweli haya ndio malipo yako?” anaendelea Rose huku Nandi bado amejiinamia, wanabaki kimya kwa muda, mara Nandi anainuka kwa haraka, Rose anashtuka na kumuangalia, Nandi anaondoka huku akionyesha dalili za kutaka kutapika.


NYUMBANI KWA ROSE NA MLELA-CHOONI.
Nandi anaingia chooni kwa kasi na kuinama kwenye sinki la choo na kuanza kutapika, Rose naye anafika na kusimama nyuma ya Nandi, “ni nini?” anauliza Rose huku akijaribu kumsaidia kwa kumshika mabegani, Nandi anaendelea kutapika kwa mara kadhaa kisha anatulia kwa sekunde kadhaa, “bado unajisikia vibaya?” anauliza Rose kisha anamuinua na kutoka naye nje.


NYUMBANI KWA ROSE NA MLELA-SEBULENI.
Nandi ameketi kochini, Rose anakuja na glasi ya maji na kumpatia, “bado unajisikia kichefuchefu?” anauliza Rose huku akimpatia Nandi ile glasi, “sasa nasikia afadhali” anajibu Nandi kwa sauti ya kichovu huku anapokea glasi na kupiga funda mara kadhaa, Nandi anashusha pumzi nzito huku akiiweka glasi mezani, wanabaki kimya kwa muda, “haya ngoja mimi niende umsubiri huyo mgeni wako” anasema Rose na kisha anaelekea mlangoni na kutoka.


SAKINA-MGAHAWANI-NJE.
Rose na Mai, dada wa makamo, 34, wameketi wote wakiwa na vikombe vya chai mbele yao, kimya kinatawala kwa muda, “au ananifanyia hivi kwa kuwa sijajaliwa kuzaa” anasema Rose kwa sauti ya kinyonge, “hakuna lolote Rose” anang’aka Mai akimkatiza Rose, “wangapi hawajapata Watoto na bado wanaheshimiana bana” anaongeza Mai, “anachofanya huyu Pimbi ni dharau za kipimbi tu” anasema Mai kwa sauti iliyojaa shari, wanabaki kimya kwa muda, “umedharau mwiba sasa mguu umeota tende Rose..nilikwambia umtoe yule binti pale kwako hukusikia” anasema Mai”, Rose anabaki kimya, “na yule Malaya atatoka pale ndani” anasema Mai na kumfanya Rose kuinua kichwa kumuangalia Mai, “kwa kosa lipi Mai?” anasema Rose na kumfanya Mai kugeuka na kumkata jicho kali, “mwenye kosa ni Mlela sio Nandi” anaongeza Rose, “hapo tu ndio huwa unanichefua Rose” anasema Mai, “jitu mpaka limebeba mimba ndani kwako bado huoni kosa lake?..tunaanza na yule Malaya kisha tunahamia kwa huyo Pimbi wako” anaendelea Mai, “Mai naomba mimi sitaki vurugu zisizo na maana” anasema Rose na kumfanya Mai abaki anamkata Rose jicho kali, “Pale mlipofika ni juhudi zako Rose” anasema Mai, “mchango wa yule Pimbi ni mdogo sana..wakuachie nyumba yako wakatafute kwa kuishi na huyo Malaya wake”anang'aka Mai kwa sauti kali huku anainuka “tena twende sasa hivi kwa huyo Malaya” anasema Mai na kumfanya Rose bado ameduwaa, “nyumba sio yangu naenda kumtoa” anasema Mai huku akichukua mkoba wake na funguo za gari pale mezani, “twende” Mai anamuamrisha Rose, “tukafanye nini haswa Dada Mai” anauliza Rose, “we twende” Mai anaamrisha huku akimshika Rose mkono na kumuinua na kumkokota kuelekea lilipo gari la Mai, Mai anafungua mlango wa gari na kuingia, Rose naye pole pole anaelekea upande mwingine wa gari na kuingia, Gari linaondoka.
RNDYML.jpeg
 
SEHEMU YA PILI & TATU & YA MWISHO.

NYUMBANI KWA ROSE NA MLELA-SEBULENI.
Rose na Nandi wamesimama pembeni, Mai akishindilia rundo la nguo kwenye mfuko mkubwa almaarufu kama ‘shangazi kaja’, anamaliza na kufunga zipu ya mfuko, “twende” Mai anamuamrisha Nandi huku akimkabidhi fuko lile na kisha kumsukuma kwa mikono miwili kuelekea mlangoni, “tunaenda mpaka stendi nahikikisha umepanda basi la huko kwenu Mbulu ndio narudi” anasema Mai huku wote wakitoka
na kufunga mlango.

WIKI MOJA BAADAE.


HOTELI YA ARUSHA CITY-NDANI.
Rose ameketi kwenye moja ya meza iliyopo kwenye kona, akiwa na glasi ya juisi mezani, anamuona Nandi akiingia mlangoni, Rose ananyoosha mkono kumpa ishara, Nandi anamuona Rose, na polepole anakuja pale alipo Rose, Rose anainuka na kumkumbatia Nandi ambaye anaonekana ni mwenye hofu, “pole na safari” anasema Rose, kisha Rose anarudi kuketi, “karibu uketi” Rose anamwambia Nandi ambaye bado amesimama, “Dada ungeniambia tu ulichoniitia mimi niondoke” anasema Nandi, “naomba uwe na amani Nandi..naomba uketi” anasema Rose na kumfanya Nandi aketi huku akionekana aliyejaa wasiwasi, “nipo mwenyewe kwa hiyo ondoa wasiwasi” anasema Rose huku Muhudumu anafika pale, “utakula nini?” Rose anamuuliza Nandi, “nimeshakula” anajibu Nandi kwa sauti ya kinyonge, “mletee juisi” Rose anamwambia Muhudumu, Muhudumu anaondoka, Rose anashusha pumzi, “Nandi mdogo wangu..naijua hali yenu na bibi yako pale kijijini...na hiyo mimba kule utateseka bure tu” anasema Rose, “nimekuita urudi tu pale nyumbani uendelee na maisha yako” anasema Rose, Muhudumu anafika na kuweka glasi ya juisi mezani na kuondoka, “umenielewa mdogo wangu?” anauliza Rose, muda huu wote Nandi amejiinamia, Rose anashusha pumzi, “kunywa hiyo juisi urudi zako pale nyumbani..hiyo mimba inahitaji matunzo mpaka kujifungua Nandi” anasema Rose, wanabaki kimya kwa muda, “kesho ukachukue mizigo yako kijijini uje uendelee na maisha” anaendelea Rose, wanabaki kimya kwa muda huku Nandi bado amejiinamia, “umenielewa Nandi?” anauliza Rose, zinapita sekunde kadhaa kisha pole pole Nandi anaonyesha ishara ya kuitikia kwa kichwa kukubaliana na Rose.

BAADAE-NYUMBANI KWA MAI-NDANI.
Mai yupo kwenye kochi akitumia Lap top, mlango unafunguka anaingia Rose, Mai anainua kichwa kumuangalia Rose “enhe..nipe mrejesho shoga” anasema Mai huku akionyesha shahuku ya kumsikiliza Rose, “naanza kazi jumatatu” anasema Rose huku akiketi kochini na tabasamu kubwa usoni, “Rose..tumetoka mbali rafiki yangu” anasema Mai kwa sauti tulivu iliyojaa hisia, “lengo langu kukuombea kazi pale kwa Mpishi Joshi nataka muda si mrefu uje ununue hisa...nitasimamia hilo mimi mwenyewe...nataka uwe mmiliki mwenza kwenye ule Mgahawa Rose” anaendelea Mai na kumfanya Rose bado amebaki akimsikiliza kwa makini, “ule Mgahawa ni maarufu hapa mjini na umri unamtupa Mzee Joshi..na hana wa kumuachia kwani Watoto wake wote wanaishi nje ya nchi..naujua uwezo wako wa kazi Rose..kwa hiyo natarajia makubwa ndani ya muda mfupi sana” anaendelea Mai, Rose anashusha pumzi na kubaki kimya kwa muda, “siku zote umekuwa Mtu mwenye kuona mbali sana Dada Mai” anasema Rose kwa sauti ya upole, “kama nilivyowahi kukuonya kuhusu huyo bwege wako” anasema Mai, “naomba tusiende huko dada Mai” anasema Rose na kumfanya Mai kurudi na kuendelea kutumia Lap top yake pale mezani na wote wanabaki kimya.

NYUMBANI KWA ROSE NA MLELA-NJE.
Nandi pole pole anafika mlangoni na kugonga mlango, anagonga mara kadhaa, bado kunabaki kimya, anafungua mlango na kuingia.

NYUMBANI KWA ROSE NA MLELA-NDANI.
Nandi polepole anaingia na kurudishia mlango, anabakia amesimama pale karibu na mlango huku akionekana mwenye hofu, inasikika sauti ya mlango wa chumbani ukifunguka, kisha anatokea Mlela akiwa amevaa kaptula na kifua chake kikiwa wazi, wanabaki wakiangaliana na Nandi kwa muda, “vipi?” anauliza Mlela, Nandi anabaki kimya akimuangalia Mlela, “umepotea njia?” anauliza tena Mlela, “nimerudi” anasema Nandi kwa sauti inayotetema kwa hofu, “umerudi kwani ulikuwa wapi? anauliza Mlela, “si nilikwambia nilifukuzwa na Dada Rose na rafiki yake” anasema Nandi, “wewe ulitakiwa kunisikiliza mimi..lakini ukanipuuza ukamsikiliza yule mshamba..sasa naomba urudi ulipotoka” anasema Mlela, mara anatokea Mimi Mars, Nandi anashtuka “kuna nini beibii” anauliza Mimi, “naona kuna Mtu kapotea njia” anasema Mlela, “unamfahamu?” anauliza Mimi, Mlela anabaki kimya kwa muda kisha anashusha pumzi, “namfananisha na aliyekuwa Dada wetu wa kazi” anasema Mlela, “kwa nini usiniachie mimi nimsikilize..labda nitamuelewa?” anasema Mimi, “uwanja ni wako beibii” anasema Mlela, wanabusiana lips kisha Mlela anaondoka, “enhe..nakusikiliza bibie” anasema Mimi kwa sauti iliyo na nusu kebehi nusu ukali, Nandi anabaki kimya, zinapita sekunde kadhaa, “kama huna la kusema mlango huo hapo..hapa hatuhitaji house girl” anasema Mimi, Nandi anabaki amezubaa, “usinifanye nikuharibu uso binti” anasema Mimi kwa sauti kali huku akionyesha kucha zake ndefu za mkononi, Nandi anageuka, anafungua mlango na kutoka.

NYUMBANI KWA MAI-SEBULENI.
Rose na Mai bado wameketi, Mai akitumia Lap top huku Rose akifuatilia anachofanya Mai, simu ya Rose inaita na kukatika, Rose anaichukua simu na kuiangalia, kwa haraka anaibofya na kuiweka sikioni, “vipi?” Rose anasema kwenye simu na kubaki kimya kwa sekunde kadhaa akisikiliza kwa makini, kisha anashusha pumzi nzito, “hebu dakika moja nitakupigia” anasema Rose na kuitoa simu sikioni, anamuangalia Mai ambaye naye amemkazia macho akisubiri kumsikiliza, “best kuna tatizo” anasema Rose, “tatizo gani?” anauliza Mai, “utanisamehe sikukwambia mapema..lakini” anasema Rose na kusita, “hebu ongea Rose usinipe hofu zisizo na sababu” anasema Mai, “nilimpigia Nandi arudi Arusha..ili arudi pale nyumbani” anasema Rose na kumfanya Mai kutoa macho kama Mtu anayemeza chakula cha moto, “sasa ndio ananipigia simu anasema Mlela tena kamfukuza” anasema Rose huku Mai bado amebaki ameduwaa, “nataka nimuelekeza aje hapa” anaendelea Rose, Mai bado amebaki amekodoa macho akimuangalia Rose, “Rose nadhani aliyekuloga wewe atakuwa ameshakufa siku nyingi” anasema Mai, “ndio maana yule bwege amekudhulumu kila kitu” anasema Mai, “hajanidhulumu akili yangu Mai” anasema Rose, “ndio maana mimi sitaki kusikia hii kitu kinaitwa wokovu” anasema Mai, wanabaki kimya kwa muda, “nimuelekeze aje?” anauliza Rose, “fanya unavyotaka Rose mimi sikuingilii tena..nimenawa mikono Rose” anasema Mai, Rose anabofya simu na kuiweka sikioni.

MWAKA MMOJA BAADAE.

A & M SUPERMARKET-NDANI-USIKU.
Mlela yupo kaunta akionekana yupo makini na calculator/kikokotozi na vitabu kadhaa na kalamu mkononi, akiandika na kubofya kikokotozi, Mimi ameketi kwenye kiti pembeni akiwa na kopo la kinywaji baridi akipiga funda kadhaa, Mlela anainua kichwa na kushusha pumzi na kisha anajikuna kichwani kama Mtu aliyekwazwa na jambo, “vipi?” anauliza Mimi, “bado kuna kitu hakipo sawa” anasema Mlela,“kuna kitu naweza kusaidia?” anasema Mimi, “nadhani hizi hitilafu ni msaada tosha ulionipa tangu uwepo hapa” anasema Mlela na kumfanya Mimi kubakia anamkodolea macho, “hebu ngoja kwanza..kwa hiyo unataka kutupa lawama zako kwangu sio?” anauliza Mimi, wanabaki kimya kwa muda,“ok fine” anasema Mimi huku anainuka pale kwenye kiti, “naona mimi ndio unataka kunifanya Mbuzi wa kafara” anasema Mimi huku akielekea mlangoni na kujaribu kufungua mlango, mlango umefungwa, “unaenda wapi?” anauliza Mlela kwa ukali, “najua ninapoenda wewe fungua mlango nitoke” anasema Mimi huku akitikisa kitasa cha mlango ule kwa nguvu, “unaenda wapi usiku huu?” anauliza Mlela huku akimfuata Mimi na kumshika mkono, “niache bana” anasema Mimi kwa ukali huku akiendelea kutikisa kile kitasa, Mlela anamshika kwa mikono miwili na kumvuta pembeni, kisha yeye anasimama pale mlangoni, “nimechoka kutupiwa lawama kwa kila linaloharibika hapa dukani” anasema Mimi kwa sauti ya ukali, “sijakulaumu nimekuuliza” anasema Mlela, “kama unaona nakuharibia basi niache niende zangu” anasema Mimi kwa ukali, “huendi popote usiku huu” anasema Mlela, wanabaki wanaangaliana kama Paka na Panya, “unaharibu kazi mwenyewe alafu unanisingizia mimi” anasema Mimi, “nani aliyeshauri tununue ile benzi..tumepoteza pesa bure na sasa ipo juu ya mawe ..nani alishauri kila mwisho wa mwezi tuwe tunaenda Dubai..”, anasema Mlela kabla ya kukatishwa na sauti kali ya Mimi, “ninapokushauri kwani na wewe huna akili zako?” anasema Mimi, Mlela anashusha pumzi, “nataka tukae chini wawili..tuangalie wapi tunakosea turekebishe..hicho ndio tunatakiwa kufanya kwa sasa Mimi” anasema Mlela, “sina huo muda” anasema Mimi kwa sauti kali, huku wote wakibaki bado wamesimama pale mlangoni wakiangaliana.

KWA MPISHI JOSHI-NDANI.
Mafundi mbalimbali wakijishughulisha huku na kule, Nandi ameketi kwenye kiti pembeni akitumia simu yake, mlangoni aniangia Mai, akiwa mwenye haraka huku mkononi ana ufunguo wa gari, “Dada Maimartha” anasema Nandi kwa sauti ya bashasha huku akiinuka kutoka pale kitini, “vipi?” anasema Mai, “safi”, “Rose yuko wapi?” anauliza Mai, ametoka na fundi..kuna vifaa wameenda kuchukua..pole na safari?” anasema Nandi, “nimeshapoa” anasema Mai huku akiangalia huku na kule ndani pale na kuonekana kuvutiwa sana na hali anayoiona ndani pale, “ama kweli mmedhamiria..hongereni sana”, anasema Mai huku akizunguka huku na kule mgahawani pale, “na nimesikia Mpishi Joshi ameshawakabidhi biashara rasmi” anasema Mai, “tangu wiki iliyopita na ameshasafiri kwenda Paris kwa Wanawe..ndio maana tunafanya ukarabati tuanze fresh” anasema Nandi, “hakika Mungu ni mwema” anasema Mai huku bado akionekana kufurahia muonekano wa pale ndani, zinapita sekunde chache huku akishika hiki na kile “umeshasikia mpya ya baba Mtoto wako” Mai anauliza, “amefanyeje?” anauliza Nandi huku akionyesha kushtuka,“taarifa zilizopo ni kwamba muda wowote ile Supermarket inatiwa minyororo na TRA” anasema Mai na kumshtua zaidi Nandi,“hiyo tisa..kumi ile nyumba nayo ipo chini ya benki” anasema Mai na kumfanya Nandi azidi kubaki ameduwaa, “mimi naenda..mwambie Rose nitarudi” anasema Mai na kuondoka akimuacha Nandi akiwa kwenye tafakuri.

NYUMBANI KWA ROSE NA MLELA-SEBULENI.
Mlela amejilaza kochini akionekana ni Mtu aliyezama kwenye mawazo mazito, zinapita sekunde kadhaa, mlio wa simu juu ya meza unamshtua, anainuka na kuichukua na kuiweka sikioni, “njoo huku river camp club umuone manzi wako bro” inasikika sauti ya kiume kwenye simu, “nani anaongea..hallow..hallow”, anauliza Mlela huku simu ikikatika, Mlela anaitoa simu sikioni na kuibofya mara kadhaa kisha anaiweka tena sikioni, "namba unayopiga haipatikani kwa sasa" inasikika sauti kwenye simu, anaitoa simu sikioni na kwa haraka anainuka na kutoka.

RIVER CAMP CLUB UNGALIMITEDI-NJE.
Bodaboda inaingia getini na kufika nje ya lango kuu, anateremka Mlela huku akiangalia kibao kilichopo juu pale kilichoandikwa ‘river camp club’, anampa dreva noti ya elfu mbili na kuelekea mlangoni.

RIVER CAMP CLUB UNGALIMITEDI-NDANI.
Mlela anaingia, anaenda hatua chache na kusimama akiangalia huku na kule, sauti ya muziki inasikika huku kukiwa na Watu kadhaa, baadhi wanakunywa, baadhi wanakula, na baadhi wanacheza muziki,
kwenye kona kuna Watu wengine kadhaa wamezunguka meza wakicheza pull, Mlela anamuona Mimi akiwa ni mmoja wa wale wacheza pull, anashtuka na kwa haraka anaanza kuelekea mezani pale, “oyaa” Mlela anashtushwa na sauti nzito na mkono mgumu uliomshika begani, anageuka na kukutana na Tizo, kijana mweusi mrefu, mwenye ndevu nyingi zilizokosa matunzo, “mbona umekaa kisnichi snichi sana..tukusaidie nini?”, Tizo anauliza, “namemfuata Mke wangu” anasema Mlela huku akionyesha kidole kwa Mimi, Tizo anamuangalia Mlela, “Kyekuu” Tizo anaita kwa sauti ya juu na kumfanya Mimi kuinua kichwa na kuangalia walipo Mlela na Tizo, “unamjua huyu jombaa” Tizo anamuuliza Mimi, Mimi anabaki kimya kwa muda, “zamani sana..kwa sasa sina ishu nae tena” anasema Mimi na kisha anarudi kuzingatia mchezo wake pale kwenye pull, “bebii unasemaje hivyo?” Mlela anasema kwa sauti ya juu iliyoambatana na mshtuko mkubwa huku akijaribu kumfuata kabla ya kuzuiliwa na Tizo,“sepa zako Jombaa..au hujaelewa kiswahili” anasema Tizo kisha anamsukuma Mlela kwa nguvu na kumfanya aanguke chini, Mlela anainuka na kumpiga Tizo ngumi nzito ya shavu inayompeleka Tizo chini, wanakuja Miso na Beka na kumshikilia Mlela asiendelee kumpiga Tizo, “hivi unanijua mimi ni nani mbwiga wewe”, anasema Tizo huku anajishika shavuni na kutema damu inayomtoka mdomoni, “bro naomba tuachie huu msala” inasikika sauti kali ya Vumba ikitokea kaunta, jamaa wa miraba minne mwenye macho mekundu aliyefunga kitambaa kichwani na kijiti cha kuchokonolea meno mdomoni, Vumba anakuja na kufika kwa Tizo na kugongeana mikono, “pole bro” anasema Tizo, Miso na Beka wanamkokota Mlela na kutoka naye mlango uliopo upande wa nyuma wa club.

RIVER CAMP CLUB UNGALIMITEDI-UWANI.
Miso na Beka wanatoka wakimkokota Mlela na kumsukuma chini, mlangoni anatoka Vumba akiwa ameshika kipande cha nondo,“katika siku umekosea ni leo jombaa..yule bro ndio anatuweka hapa mjini” anasema Beka huku anavua shati, “leo umeingia cha kike arifu” anasema Miso akiwa ameshika chupa ya bia iliyovunjika nusu mkononi, wote kwa pamoja wanaanza kumshambulia Mlela kwa kipigo cha Mbwa mwizi.

MIEZI MITATU BAADAE.

HOSPITALI YA KCMC-KILIMANJARO.
Mai anafika getini akiwa na simu sikioni, “mko kwa wapi?” Mai anauliza kwenye simu, kisha anakaza mwendo kuelekea upande wake wa kulia, “Rose nimekuja tu nihakikishe kwa kinywa chako haya niliyoyasikia..ningeweza kukupigia simu lakini nimelazimika ku drive kutoka Arusha” anasema Mai mara tu baada ya kufika walipoketi Nandi na Rose, “kuhusu nini tena Maimartha Dada yangu” anasema Rose kwa mshangao, “nimesikia kwamba ni wewe umegharamia matibabu ya huyu jamaa..na tena umemuagizia wheel chair?” anasema Mai, “kwani tatizo liko wapi Dada Mai?” anasema Rose, “pamoja na ule ufedhuli wote aliokufanyia?”, anauliza Mai kwa sauti ya mshangao, "yale yameshapita Mai"anasema Rose, wanabaki kimya kwa muda “na hilo la kwamba eti unataka kumpokea tena nyumbani kwako?” anauliza Mai, “sasa ataenda wapi kwa hali ile Dada Mai?” anauliza Rose, “nyumba yako ile ile uliyomaliza kujenga tu juzi..na yeye ndiye amesababisha nyumba yenu ya kwanza ikauzwa na benki..yeye ndio amesababisha umeenda kuanza maisha upya” anaendelea Mai, “kwa sasa Mlela anahitaji msaada Dada Mai kuliko wakati mwingine wowote” anasema Rose na kusababisha Mai kutulia kimya akimshangaa Rose, “Rose Rose Rose Rose” anasema Mai, “Dada Mai..Mlela kwa sasa amepooza kuanzia kiunoni kwenda chini..hajiwezi kwa lolote..ni wa kubeba..ni wa kulisha” anasema Rose, “ngoja nikuulize..kwani mpaka hao Majambazi wakampiga kipigo kile kama mwizi unajua kawakosea nini?” anasema Mai, “sio lazima kujua walimpiga kwa nini Dada Mai..ninachojua sasa hivi ni mlemavu na anahitaji msaada...Mai tukimtelekeza Mlela ataishia kuwa omba omba tu mtaani”, anasema Rose, “ok..kwa heri nadhani nimeshapata jibu” anasema Mai na kuondoka, Rose na Nandi wanabaki pale kimya, zinapita sekunde kadhaa “Nandi..yaliyotokea yameshatokea..siwezi kulipiza kisasi mimi..na ndio maana huwa tunaomba kwa Mungu tusamehewe makosa yetu kama tunavyowasamehe waliotukosea” anasema Rose, “chochote utakachoamua tupo pamoja Dada Rose” anasema Nandi na kisha wanakumbatiana.

NYUMBA YA ROSE-NDANI.
Rose na Nandi wapo kochini, Mlela yupo pembeni akiwa kwenye kiti cha matairi huku kukiwa na kijitabu kidogo na kalamu mbele yake, wapo wanaangalia TV iliyopo mbele yao, Rose akiwa amempakata Mtoto anayelia,"hebu mnyonyeshe" anasema Rose huku akimuinua Mtoto na kumpa Nandi, "baba Tifa uletewe ule mtori sasa hivi?" Rose anamuuliza Mlela, Mlela anatikisa kichwa kuashiria "hapana", kisha Mlela anachukua kalamu na kuandika kwenye kile kijitabu chake, na kumpatia kijitabu kile Rose, "kwenye maombi tunaenda baadae jioni" anasema Rose baada ya kusoma kilichoandikwa kwenye kijitabu kile, Mlela anatikisa kichwa kuashiria kukubaliana na Rose, "na kuanzia jumatatu tutakuwa tunaenda wote pale Mgahawani..tunashinda wote jioni tunarudi wote nyumbani...sawa" anasema Rose, Mlela anatikisa kichwa kuashiria kukubali.

MWISHO.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom