Simulizi:Death Of Innocent

*Sehemu ya 04.*


“Baba mwache mama! Kwanini unampiga hivyo si keshakufungulia mlango?”
“Wee unanishika unataka kunichangia na mama yako siyo?”

“Sitaki kukupiga baba lakini naomba usimpige mama kiasi hicho hana kosa!”
Wakati Prosper akiongea maneno hayo tayari Kasanda na Nyamizi walishafika na kumnyanyua mama yao aliyekuwa amelala chini akiwa amepoteza fahamu huku damu nyingi zikimtoka mdomoni, midomo yake ya juu na chini ilikuwa imevimba kwa ngumi aliyopigwa na mume wake, wakambeba na kumpeleka chumbani kwao ambako walimmwagia maji akarejewa na fahamu.
“Mama twende polisi!” Kasanda alimshauri mama yake.

“Hapana watoto wangu tukienda polisi baba yenu atafungwa! isitoshe sisi Wanyamwezi hatutakiwi kabisa kushtaki polisi tunapopigwa na waume zetu”

Watu wote katika kijiji cha Tutuo barabara ya kwenda Sikonge walikoishi Prosper na wazazi wake walitambua ukorofi wa mzee Kabaka na hakuna mtu aliyediriki kumkemea, kila mtu alimuogopa.

Kama ungefanikiwa kukutana na mama Kalunde, sio siri machozi yangekutoka, alikuwa ni mama wa makamo, mrefu mwenye umbile la kitutsi,rangi ya ngozi yake ilikuwa nyeusi lakini iliyojaa makovu mengi, kwa kumwangalia ungegundua kabisa kuwa mama huyo aliwahi kuwa tishio wakati wa ujana wake!

Alikuwa ni mama mwenye mateso, alipigwa karibu kila siku na mume wake,hakuwa na sikio moja tayari lilishakatwa na mumewe! Jicho lake la kulia lilikuwa chongo baada ya kupasuliwa na mume wake wakati wa kupigwa miaka miwili kabla ya siku hiyo! Alikuwa ni mama aliyepata mateso makubwa mno katika maisha yake ya ndoa.

Wakati hayo yote yakitokea Prosper alikuwa na umri wa miaka 17 akimalizia kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Sikonge, pamoja na matatizo aliyokuwa nayo alifanikiwa kuchaguliwa kuendelea na kidato cha tano katika shule ya sekondari ya St.Magreth ilikuwa ni shule ya bweni, na ilikuwa ni lazima aende kuishi bwenini akiwaacha dada zake Kasanda na Nyamizi pamoja na wazazi wake.

“Prosper tutaweza kweli kumhimili baba akimpiga mama?”
“Mungu atawasaidia dada zangu sina budi kwenda shule ili niwasaidie baadaye!” Prosper aliwaeleza dada zake wakati wa kuagana, akaondoka kwenda zake Moshi shuleni.

Alipofika shuleni kwa mara ya kwanza alikuwa amechelewa na kilichomchelewesha zaidi ilikuwa ni ada, mama yake Kalunde alilazimika kufanya vibarua katika mashamba ya watu ili aweze kupata pesa za kumwezesha Prosper kwenda shule! Baba yake hakujali kabisa.

“Prosper mwanangu usifanye michezo shuleni, si unaona maisha yetu yalivyo na unaona nilivyohangaika? Baba yako hana msaada wowote, yeye ni pombe kila siku na kunipiga mimi tu, familia nzima tunakutegemea wewe uje kuwa mkombozi wetu kajitahidi mwanangu!”
“Sitakuangusha mama nakuahidi! “
“Sawa mwanangu!”

Darasa lao lilikuwa na wafunzi hamsini na mbili kati yao wasichana wakiwa kumi na saba! Ni Prosper peke yake aliyeonekana kuwa na uwezo mdogo kifedha na watu wengi walimdharau, alikuwa na nguo zilizochanika na madaftari yake yalikuwa ni ya kurasa shirini na nne ambayo hayakutumiwa na wanafunzi wengi shuleni hapo! Yalidaiwa kuwa ya watoto wa shule za msingi.

Pamoja na umasikini wake Prosper alijitahidi sana na masomo kama alivyomuahidi mama yake na hiyo ni kwa sababu aliifahamu familia yake, alitaka asome ili apate uwezo wa kuwakomboa ndugu zake, barua zilizokuja kutoka nyumbani kwao zilimweleza juu ya kipigo alichopata mama yake na Prosper alilia.

Wanafunzi wengi walimtenga sababu ya umasikini wake isipokuwa msichana mmoja tu aliyeitwa Belinda!Msichana huyo alimsaidia Prosper kwa vitu vingi shuleni ikiwemo Sabuni, mafuta na hata sukari na wakatokea kuwa marafiki wakubwa.

Katika mtihani wa mwisho wa muhula aliwashangaza wengi pale alipoibuka na kushika namba ya kwanza kati ya wafunzi wote! Ni matokeo hayo ndiyo yalianza kumpa heshima na marafiki wengi shuleni.
******

Shule zilipofungwa kwa sababu Prosper hakuwa na nauli ya kumrudisha hadi nyumbani kwao Tabora, ilibidi abaki shuleni peke yake akijisomea! Alimkumbuka sana mama yake na alitaka kwenda nyumbani lakini kwa sababu hakuwa na nauli alilazimika kubaki peke yake shule nzima.

Shule zilipofunguliwa wanafunzi wote walirejea shuleni na yeye na Belinda msichana aliyeonekana kutoka familia tajiri jijini Dar es Salaam, walisoma na kufanya kila kitu pamoja Belinda alikuwa miongoni mwa wasichana wagumu kuelewa masomo yao, lakini Prosper alitumia muda wake mwingi kumfundisha hatimaye akawa miongoni mwa wasichana waliofanya vizuri katika mitihani yao.

Mwisho wa muhula wa pili Prosper alishika tena namba ya kwanza darasani kwake na Belinda aliibuka katika kumi bora! Kila mtu mpaka walimu wake walishangaa,hilo liliukomaza zaidi uhusiano wao.

“Prosper utakwenda Tabora likizo hii?”
“Mimi? Mimi? Hapana sitakwenda!”
“Kwanini?”

“Sina nauli ya kunipeleka nyumbani nendeni tu mtanikuta!”
“Hapana Prosper this time ni lazima uende!”

“Nitakwenda na nini sina nauli Belinda?”
“Nitakupa nauli ya kukupeleka na kukurudisha!” Alisema Belinda.

Prosper hakuamini aligeuka na kumwangalia Belinda usoni, wote wawili walijikuta wakitabasamu na baadaye kukumbatiana na kuanza kupigana mabusu usoni, Belinda alijaribu kuupenyeza ulimi wake kuuingiza mdomoni kwa Prosper lakini Prosper aliuma meno yake kuonyesha hakupenda kitu hicho kitokee!

“Belinda unataka kufanya nini?”
“Nakupenda Prosper tafadhali tunyonyane ndimi!”

“Nitatapika Belinda sijawahi kufanya kitu kama hicho hata siku moja!”
Belinda alishindwa kuendelea lakini alijua ni kwanini Prosper alisema hivyo, alimwachia na wakaendelea na safari yao kuelekea mabwenini kujipumzisha wakisubiri siku inayofuata.

Asubuhi kitu cha kwanza alichofanya Belinda ni kumkabidhi Prosper kiasi cha shilingi 50,000 kwa ajili ya nauli ya kumpeleka Tabora na kumrudisha shuleni.
“Belinda mbona pesa hizi ni nyingi sana!”
“Zitakazobaki utawanunulia wazazi na ndugu zako zawadi!”

“Ahsante Belinda, sikutegemea!”
“Ahsante wewe kwani bila wewe mimi nisingefanikiwa kimasomo? Isitoshe nakupenda Prosper huwezi kupata taabu wakati mimi nina kitu!”

“Belinda mzazi wako ni nani hasa hapa nchini?” Ilibidi Prosper aulize, sababu alishangazwa na msichana mdogo kama Belinda kuwa na kiasi kile chapesa.

Belinda alimweleza kila kitu kilichokuwepo katika maisha yake, alieleza pia juu ya utajiri wa baba yake na jinsi baba yake alivyompenda sababu alikuwa mtoto pekee wa kike! Hakuacha kumweleza juu ya mama yake wa kambo.

“Nina kila kitu nyumbani isipokuwa upendo wa mama, mama yangu wa kambo ananitesa sana, hanipendi amewafanya hata kaka zangu wa kambo pia wanichukie!”

“Unafikiri ni kwanini?”
“Kwa sababu wanajua baba ananipenda na kuna uwezekano wa kupata sehemu kubwa sana ya mali yake akifa, hiyo nafikiri ndiyo sababu kubwa!”
“Pole!”

“Ahsante, lakini nataka uelewe nakupenda na tukirudi kutoka likizo safari hii nataka kila mtu aelewe jambo hapa shuleni ili wavulana waache kunisumbua!”

“Huogopi kuchekwa Belinda!”
“Kwanini?”
“Sababu mimi ni masikini!”
“Nakupenda kwa jinsi ulivyo Prosper!”
Ni kweli Prosper alikuwa na sura ya kumvutia kila mwanamke kilichomsumbua kilikuwa ni umasikini.

Je, nini kitaendelea?
 
Belinda alikua mtoto wa kishua, na mtunzi anasema mshua wake alikua anampenda kinoma. Natamani sana kujua nini kilitokea mpaka ifkie hatua akose hata hela ya chakula xmass, achilia mbali kumnunulia mwanae nguo za sikukuu. Maybe mzee wake alimtenga baada ya Belinda kumpenda jamaa wa hali ya chini

the Legend☆
 
 

Here we Go! [emoji39][emoji39][emoji39][emoji39][emoji91]


Sent from my iPhone using JamiiForums
 

Here we Go! [emoji39][emoji39][emoji39][emoji39][emoji91]


Sent from my iPhone using JamiiForums
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…