Sehemu ya 109
Mfaume alikuwa ni mzazi mwenzangu, niliona inafaa nimweleze kila kitu kilichojili hadi mtoto wetu mauti ikamfika.
Mrembo yule alilia na kulia, hata hivyo kilio chake hakikubadili ukweli wa jambo lile. Mwananetu alikuwa ametutoka.
*****
Niliyanza maisha mapya, bila mtoto, mchumba, wala mke. Ni wiki mbili na siku kadhaa zilikuwa zimepita tangu niondoke jijini Dar na kuja kuyaanza maisha mapya kijijini Nguruka.
Kama nilivyokwisha simulia mwanzo kabisa, kitaaluma nilikuwa nina shahada ya ualimu ya chuo kikuu cha Dar es salam, hivyo pale kijijini, nilikuwa nimefungua kituo maalumu cha kufundisha masomo ya ziada kwa wanafunzi wa sekondari(tution center)
Kwa kuwa kipindi hicho kulikuwa na upungufu mkubwa wa walimu hasa wa masomo ya Sayansi, kazi ile ilinipa kiasi fulani cha fedha ambacho kiliyaendesha maisha yangu na ya mama yangu bila tatizo lolote.
Kila wakati nafsi yangu ilikuwa ikinisuta na kujicheka mwenyewe, kitendo cha kuporomoka kutoka kwenye mafanikio makubwa hadi kuangukia kwenye ualimu, ilikuwa tusi baya maishani, ualimu ni kazi iliyodharaulika hata na mtoto mdogo.
Niliapa kutorudi tena Dar es salam, niliweka nadhiri ya kumalizia maisha yangu katika kijijini kile.
Mwaka ulikatika, kazi ya kufundisha, haikuleta matokeo yoyote, ndipo fikra za kujiingiza kwenye kilimo cha tumbaku zikaanza kutembea kichwani kwangu. Mwaka huohuo nikaanza kutengeneza mazingira ya kujiingiza kwenye kilimo kabla ya mvua za masika kuaanza.
Nilimshirikisha mama juu ya mawazo hayo, hakuwa na pingamizi, aliniunga mkono. Nakumbuka siku hiyohiyo, nilinyonga baiskeli hadi kijiji kimoja kinaitwa Nyangabo, wenyeji wa Nguruka watakuwa wanapafahamu sehemu hii.
Huko alikuwa akiishi babu yangu upande wa ubabani kwangu, anaitwa mzee Nswima Mpangalala, lengo la kwenda huko ilikuwa ni kumwomba sehemu ya shamba lake ambalo ningelitumia kwa kilimo cha tumbaku kwa mwaka huo kabla ya mvua za masika kuanza.
Bahati nzuri babu yangu yule nilikuwa nimeshibana naye sana, kipindi kile nikiwa Dar es salam, kila mwezi nilikuwa nikimwagizia suti za bei mbaya na viwalo vya hapa na pale. Hivyo kwa siku hiyo nilipo mwomba sehemu ya ardhi kwa kilimo hakuwa na pingamizi kabisa.
Nilirudi nyumbani nikiwa na furaha, lakini nilipofika na kuingia ndani, nikamkuta mama amelala huku akilalamika maumivu makali ya kiuno. Alikuwa akijinyonga nyonga huku akigumia maumivu makali.
Nilichofanya ni kumnunulia dawa za maumivu na kumpa.
Lakini wapi, mama alizidi kulalamika kiuno. Niliamua kumkimbiza hospitali ya Nguruka. Alipokelewa na kuingizwa chumba cha uchunguzi. Nilibakia nje katika benchi roho ikinidunda.Baada ya kama dakika 20 kupita mama alitolewa akiwa kwenye kitanda cha magurudumu, alipelekwa wodini.
“Ana tataizo gani dokta” nilihoji.
“Amepatwa na maumivu ya mfupa katika kiuno, ni hali inayotokea mara nyingi kwa wazee, misuli na mifupa ya upande wa chini wa mgongo huchoka kutokana na umri.”
“Mungu wangu! Kwa hiyo atapona?”
“Ndio atapona, ila atachukua muda mrefu hadi kusimama na kutembea kama ilivyokawaida.”
Ilikuwa ni habari iliyonivunja moyo wangu, hakika niliamini lile lilikuwa ni bomu jingine ambalo lingeweza kuupasua moyo wangu maishani kama siku moja lingelipuka.
Kitendo cha kuambiwa itamchukua muda mama yangu hadi kusimama ilinichanganya sana.
Wiki moja badaye, tuliruhusiwa kurudi nyumbani. Tulirudi mama akiwa kwenye kiti cha magurudumu matatu, hakuweza kusimama kabisa, dokta alinipatia maelekezo ya kumpeleka kwenye kliniki ya mazoezi iliyopo hospitalia pale kila mwisho wa wiki.
ilinibidi nimpigie simu dada yangu wa Geita ili aje anisaidie kumuguuza mama, hasa kwa kumpa huduma za msingi kama kumwongesha, hata kumpeleka chooni.
Hata hivyo majibu aliyonipa baada ya kumweleza jambo hilo yalinichoma mno, alisema:
“Mume wangu amekataa nisije huko, hivyo nasikitika kumwambia siwezi kuja kumuuguza mama.” Sikuamini kusikia maneno hayo kutoka kwa ndugu yangu huyo.
“Hutaki kumuuguza mama yako?”
“Sio sitaki, bali mume wangu ndio hataki!”
“Kwa nini?”
“Haniamini?”
“Kivipi?”
“Anahisi nikiwa mbali naye nitakuwa na mwanaume mwingine.”
“Whaat!!”nilimaka kwa hasira.
Nilimsihi sana nikimtaka aje nyumbani, lakini ndugu yangu aligoma, niliwasiliana na mumewe ambaye kwangu ni shemeji yangu, ili amruhusu mke wake aje kunisaidia kumuguza mama, lakini jamaa yule naye alinikatalia bila aibu. Dada yangu naye alimtii!
Usikose sehemu ya mwisho mwisho ya mkasa huu wa aina yake.