Sehemu ya 107
ILIPOISHIA...
Sikuwa na jinsi, fedha iliyokuwa imesalia ni ilitosha kwa nauli yangu tu. Nilichofanya ni kukubaliana na kile nilichokipinga mwanzo. Kumzika mwanangu katika ardhi ya India.
Nilikwenda katika Musikiti, nikaomba msaada wa mazishi ya mtoto, nashukuru Mungu Waislamu wa taifa lile walinipa ushirikiano mkubwa sana, mwanangu alizikwa kwa heshima zote.
Huo ndio ukawa mwisho wa mtoto wangu mpenzi Mwanda Faraji Mpangalala, niliyezaa na Nasra Mfaume, mwanamwali mzuri wa sura niliyechaguliwa na wazazi wangu.
Siku chache badaye, nilirejea Dar es salam. Nilipofika Nyumbani, mama akanipokea kwa kilio.
SONGA NAYO...
MSIBA ukaanza upya, ndugu, marafiki, pamoja na majirani, wakakusanyika nyumbani kwangu.
Tukaweka matanga kwa siku tatu mfululizo, katika nyakati hizo za matanga nilikuwa nikipokea salamu za rambirambi kutoka kwa watu mbalimbali niliofahamiana nao.
Miongoni mwa salamu za rambirambi mojawapo ilitoka kwa Debora, mchumba aliyenitesa na kuuvunja moyo wangu.
Alimtuma mjumbe aliyejitambulisha kama msaidizi wake, aliambatanisha bahasha yenye shilingi laki tatu.
“Yeye yuko wapi?” nilimuuliza yule mjumbe aliyejitambulisha kama msaidizi wake.
“Kwani hujui kama alipanda cheo?” naye akaniuliza.
“Sijui”
“Kwa sasa ni Katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma”
“Wacha wee! Debora huyu huyu!.”
“Huyu huyu.”
“Nyota ya jaa imemwangazia.”
“Naam!”
Zilikuwa ni taarifa ambazo sikujua kama natakiwa nifurahie ama ninune, lakini nilipatwa na wivu kuona mwanamke aliyenitosa akizidi kufanikiwa maishani.
Baada ya siku tatu kukamilika, tukayaanua Matanga. Kabla ya ndugu kuondoka tulikaa kikao kidogo cha wanaukoo ili kujadili mawili matatu kuhusu maisha.
Nilitumia fursa hiyo kuwaeleza juu ya deni la pesa.
Nilikuwa nadaiwa katika benki, ni baada ya kukopa pesa za kumtibia marehemu mwanangu na nyumba niliiweka rehani.
Nikaweka maombi mezani. Nisaidiwe kulipa deni hilo ili kuinusuru nyumba yangu kupigwa mnada.
Watu wote walikuwa kimya, kama ujuavyo mambo ya pesa, kila mtu mdomo uliingia maji.
Nilisali nyuso za dada ndugu zangu wale, walionekana ni watu wanaoguswa na matatizo yangu, lakini uwezo wa kunisaidia tu ndio hawana.
“Sasa tunafanyaje jamani?” mama aliyekuwa mwenyekiti wa kikao alihoji. Akaendelea.
“Lazima lifanyike jambo kuinusuru nyumba ya ndugu yenu.” Alisema.
“Au mnakubali nyumba hii iuzwe kwa deni la milioni 15 tu?” watu wote wakatikisa kichwa kukataa.
“Nyumba hii nimeijenga kwa zaidi ya milioni 80, kuuzwa kwa deni la milioni 15 ni fedheha”nilishadadia.
“Mimi nadhani tupewe muda tu, tutachangia chochote kitakacho patikana.” dada yangu mmoja aitwaye Rehema, ambaye aliolewa na jamaa mmoja msukuma wa huko Geita, alisema.
Kauli hiyo ikaafikiwa kwa vichwa.
“Kwani tarehe ya mwisho ya kuwasilisha pesa hiyo ni lini?” Mtu mwingine akauliza. Watu wote wakageuka kuniangalia.
Nikaliendea begi ili nitoea dokomenti niangalie terehe ya mwisho ninayotakiwa kulipa deni lile.
“Mungu wangu!!” nilimaka baada ya kutupa macho kwenye ile karatasi ya makubaliano, ambayo ilikuwa na maelezo ya lini natakiwa kuwa nimekwisha lipa deni lao.
“Vipi?”
“Umeona nini?”
“Ni lini?”
Nilitupiwa maswali.
“Kesho saa sita mchana ndiyo siku ya mwisho. vinginevyo nyumba yangu itapigwa mnada,” niliwaambia macho nimeyatoa.
Tukutane kesho