BWANAHARUSI ALIYEJERUHIWA
Sehemu ya 106
Majibu ya daktari wa kitengo cha Moyo, Hopsitali ya Muhimbili alithibitisha na kuungana na yale majibu ya Hospitali ya Regency, mwanangu alikuwa na tatizo la moyo, kulikuwa na valve zilizokuwa zimezorota, hivyo alitakiwa kufanyiwa upasuaji ili kupandikiza mishipa mingine.
Wakati napewa majibu hayo, tayari nilikuwa nimekwisha pitisha uamuzi mgumu. Sikuwa tayari kabisa kuuza nyumba yangu ya Kinondoni. Nyumba ya ndoto zangu.
Kitu pekee nilichokuwa nimewaza ni kuweka rehani nyumba hiyo ya mamilioni ya fedha.
Kuliko kuuza heri niweke rehani. Nilikuwa nikijiambia kimoyomoyo. Na Hadi wakati huo nilikuwa nimekiwsha pata mahali pakwenda kupewa milioni 16 ambayo ningeongezea na ile milioni nane niliyokuwa nayo benki.
Nilichofanya baada ya kupewa majibu ya mwanangu, nilikwenda kwenye tasisi ya mikopo iitwayo Wezesha mzawa, ipo Sinza. Nikajaza fomu na kuandika barua ya kuomba mkopo, siku tatu badaye nikabidhi hati ya nyumba, kisha nikapewa kiasi kile cha fedha.
Upesi sana nilianza kufanya mchakato wa wa safari ya India, na kwa kuwa nilikuwa na pesa mkononi, hakuna kilichonikwamisha.
Baada ya kukamilisha masuala yote ya viza na passport, nikalipia kabisa matibabu ya mwanangu kupitia benki za kimataifa. Siku chache zilizofuata nilikuwa ndani ya ndege ya shirika la Fly Emerates Airlines.
Masaa saba ama nane tukiwa angani, mhudumu wa ndege alitutaka abiria wote tufunge mikanda kwani ndege ile kubwa, ilikuwa inakaribia kutua kwenye uwanja wa New Delhi nchini India...
Nilimwangalia mwanangu aliyekuwa amelala katika kitanda chake maalum akiwa anapigania uhai wake. Nikafanga mkanda huku nikisali kimoyomoyo Mungu atujali heri kwenye taifa hilo geni.
Ndege iliserereka katika aridhi ya India, dakika za kuhesabu badayem, abiria wote tulianza kuteremka.
Kwa kuwa taarifa zangu zilikuwa zimekwisha pokelewa na hospitali ya Fortis escorts heart institute, nilikuta gari la wagonjwa likinisubiri nje ya uwanja wa ndege.
Baada ya kushuka tu. Mtoto alingizwa garini, harakaharaka safari ya kuwenda hospitali ya moyo ya Fortis escorts heart institute ilianza.
Kwa kuwa nilikwisha fanya malipo ya matibabu kupitia benki za kimataifa zitumiwazo na hospitali hiyo, mtoto wangu Mwanda hakucheleweshwa. Tulipowasili hospitali aliingizwa moja kwa moja chumba cha upasuji.
“Atapona dokta?” nilimuuliza daktari mmoja wa kihindi mwenye uso wa upole na mkalimu aitwaye Rajn Kanabar.
“Kila kitu kinawezekana.”
“Itachukua muda gani?”
“Upasuaji wake unaweza kuchukua masaa matatu au manne au zaidi ya hapo. Inavyo anaonesha mwanao alikawia mno kupata tiba, ”alinijibu.
Nilibakia nje katika benchi, nilikaa pale kusubiri majibu ya oparesheni. Nikiwa katika benchi nikapitiwa na usingizi, sikumbuki muda gani ulipita, ninachokumbuka nilistushwa na dokta Rajn Kanabar akinitaka nimfuate ofisini kwake.
Uso wa dokta Rajn Kanabar haukuonesha hali yoyote ya faraja.
“Mwanangu ni mzima!” nilihoji, sikuwa tayari kabisa kusikia habari za kifo.
“Bado anaishi...”alisema, akaendelea.
“Atapona, ila hawezi kuishi muda mrefu.” aliniambia.
Nikabakia nimeganda kama sanamu la askari. Sikuilewa kabisa kauli ya doktari yule.
“Sijakuelewa hapo?”
“Katika huu ulimwengu, kila mtu atakufa siku yake ikifaka, mwanao bado anaishi ila siyo vizuri kukueleza kwamba ataweza kuishi kwa muda mrefu.”
“Nini mantiki ya kauli yako?” niliunguruma. Niliona daktari yule ananiongelea mafumbo tu.
“Mishipa fulani katika moyo wa mwanao ilikuwa imekufa, kama ungekawia kidogo sana ungetuletea maiti, hata hivyo, tumepandikiza valve zingine ambazo ni artificial, hizo Valve zinaweza kumsaidia ingawa nazo zinaweza kuharibika muda wowote.
Ndio maana nimekwambia, mwanao ataishi lakini sio kwa muda mrefu.”
“Mungu wangu!!” nilimaka.
“Atatakiwa andelee kukaa hapa, hadi tutakapojiridhisha na afya yake?”dokta alihitimisha.
“Naweza kumwona?”
“Bila shaka.”
Nikapelekwa katika chumba alicholazwa mwanangu, moyo wangu ulijaa simanzi nilipomwona kiumbe yule yupo katika usingizi wa nusu kaputi.
Nakumbuka nilimuuguza mtoto wangu huko nchini India kwa wiki mbili au tatu, ilipoanza wiki ya nne hali yake ikabadirika, akakimbizwa ICU.
Masaa sita badaye alitolewa akiwa katika kitanda cha magurudumu, mwili wake ulikuwa umefunikwa shuka jeupe miguuni hadi kichwani. Mtoto mzuri alikuwa amefariki dunia.
Lilikuwa ni pigo moja takatifu, huwa nashindwa kuelezea kiwango cha maumivu niliyopitia nyakati hizo. Dunia ilinielemea. Kuna wakati nilihisi labda kuna kosa nilimkosea Mungu. ndio maana alikuwa akinipa maumivu maishani.
“Utasafirisha maiti ama utazikia hapahapa?”
hili swali niliulizwa na daktari wa mochwari, lilikuwa ni swali la msingi, lakini ndilo lilinizindua akili yangu na kubaini sikuwa na fedha ya kutosha ya kusafirisha maiti ya mwanangu.
Kumzika mwanangu nchini India inatoa tafsiri kwamba, sintaweza kuliona kaburi lake daima dumu.
Nilihisi akili ikizunguka. Sikuwa tayari kwa hilo kabisa.
Haiwezekani, lazima maiti ya mtoto isafirishwe, lakini nitaisafirisha vipi na fedha sina.
Nilijiuliza.
“Bro nimekuuliza utazikia hapa ama utasafirisha mwili?” jamaa wa mochwari alirudia tena kuniuliza.
“Sijajua” nikamjibu kwa kifupi huku nikikamkata jicho kali utadhani yeye ndiye alisababisha nikose pesa maishani.
“Nimekuuliza hivyo nikiwa na maana”
“Maana ipi?”
“Ili nijue naweza kuhifadhi vipi mwili kulingana na muda utakaotumika kuwa duniani kabla ya mazishi yake.”
Sikuhangaika kumjibu yule bwana, nilichofanya ni kuchukua usafiri na kwenda ubalozi wa Tanzania. Lengo la kwenda ubalozini ni kuomba msaada wa kusafirisha mwili wa mwanangu hadi Dar es salam.
Niliwasili ubalozi wa Tanzania na kueleza shida yangu.
“Amefariki lini?” Katibu muhtasi wa balozi aliniuliza. Alikuwa mwanamke mzuri, mweupe, mrefu, macho makubwa, na umbo namba nane.
“leo asubuhi.”
“Inagharimu kiasi gani?”
“Kama milioni tano za Kitanzania.”
“Sasa nisikilize kwa makini...”alisema, akaendelea
“Nasikitika kukwambia huwa hatuna utaratibu wa kusafirisha maiti. Kila wakati Watanzania wanafariki hapa India, unadhani tutasafirisha miili mingapi? Hatuna utaraibu huo ndugu.” Niliambiwa.
Sikuwa na jinsi, fedha iliyokuwa imesalia ni ilitosha kwa nauli yangu tu. Nilichofanya ni kukubaliana na kile nilichokipinga mwanzo.
Kumzika mwanangu katika ardhi ya India.
Nilikwenda katika Musikiti, nikaomba msaada wa mazishi ya mtoto, nashukuru Mungu Waislamu wa taifa lile walinipa ushirikiano mkubwa sana, mwanangu alizikwa kwa heshima zote.
Huo ndio ukawa mwisho wa mtoto wangu mpenzi Mwanda Faraji Mpangalala, niliyezaa na Nasra Mfaume, mwanamwali mzuri wa sura niliyechaguliwa na wazazi wangu.
Siku chache badaye, nilirejea Dar es salam. Nilipofika Nyumbani, mama akanipokea kwa kilio.
Itaendelea.....