Siku 100 za tofauti ya Urais na Ufalme

Kanungila Karim

JF-Expert Member
Apr 29, 2016
20,744
25,446
JULAI 24, 1933, Rais wa 32 wa Marekani, Franklin Delano Roosevelt ‘FDR', alihutubia umma wa taifa lake na kueleza kipimo cha siku 100 tangu alipoingia madarakani. Siku 100 za FDR zilitimia Juni 11, 1933. Aliapishwa kuwa Rais, Machi 4, 1933.

FDR aliingia ofisini akiikuta nchi ikiteswa na mdororo mkubwa wa kiuchumi (Great Depression). Hali hiyo ilisababishwa na anguko la uchumi wa viwanda kwenye nchi za Magharibi.

Katika kuikabili Great Depression, FDR alianzisha kampeni aliyoiita New Deal (Dili Mpya) ambayo utekelezaji wake aliugawa katika mpango alioupa jina la R tatu (3 Rs).

R hizo zilikuwa na maana ya Relief (Nafuu) kwa wasio na ajira pamoja na maskini. Recovery (Uhuishaji) wa uchumi mpaka kufikia kiwango cha kawaida. Reform (Mageuzi) ya mfumo wa kifedha na kudhibiti kutojirudia kwa msukosuko wa uchumi wa viwanda.

Kufikia malengo hayo, FDR ndani ya siku 100, aliliita Bunge la Marekani (Congress), chemba zote mbili, Baraza la Wawakilishi na Seneti.

Kisha, miswada 15 ikapitishwa na sheria mpya 76 zikatungwa ili kuwezesha matokeo yaliyokusudiwa.

Ni kuanzia hapo, siku 100 za mwanzo ofisini, zimekuwa kipimo cha awali cha uelekeo wa nchi baada ya Serikali mpya kuingia madarakani. Leo, Juni 27, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan, ametimiza siku 100 tangu alipokula kiapo cha uaminifu wa kikatiba, kuiongoza dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mageuzi makubwa yametokea tangu Machi 19, mwaka huu, Rais Samia alipoingia madarakani. Kama utaniuliza tofauti ya Rais Samia katika siku 100 za kwanza dhidi ya mtangulizi wake, Dk John Magufuli, jibu langu ni hili: “Tunaona tofauti ya Urais na Ufalme.”
Rais Samia hajataka na haoneshi kusudi la kuwa Malkia. Anasimama kama Rais. Kwa tafsiri, Rais ni neno la Kiarabu lenye maana ya “Kiongozi”. Mfalme kwa mwanaume au Malkia kwa upande wa mwanamke, tafsiri yake ni “Mtawala". Samia ni Rais. Ni kiongozi.

Dk Magufuli alikuwa mtawala. Alitaka nguvu zake zidhihirike kwenye kila mhimili. Alifunika Bunge, akataka awe juu ya Mahakama.

Tabia ya kutaka kuwa nyota wa kila kitu kwenye nchi ni ya watawala. Viongozi hubeba wajibu wa kuongoza.

Watawala hutaka kuwa juu ya wafanyabiashara, wasanii, wanamichezo na hata viongozi wa dini. Ndio maana UK, mtu awe nyota vipi kwenye eneo lake, kama hajatunukiwa tuzo ya Malkia/Mfalme (Most Excellent Order of the British Empire), ili aitwe Sir (mwanaume) au Dame (mwanamke), hujiona bado hajafanya lolote.

Tanzania imetoka kwenye mazingira ambayo ili mfanyabiashara ajione salama basi apate baraka za Rais. Wasanii, wabunge, viongozi wa dini, wanamichezo. Hata majaji jamani! Ndani ya siku 100 za Rais Samia, taratibu anajitenga na zama za kutawala na kuwa juu ya kila mtu na kila kitu. Yeye anaongoza.

Kutoka kukataa kodi za dhuluma hadi ubambikiaji wa kesi. Rais Samia alilitaka Bunge lifanye kazi yake ya kuikosoa Serikali. Kwa maana hiyo hataki Serikali ijazwe sifa za kijinga. Kabla ya hapo, alimwambia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, asifumbefumbe, aseme wazi mahali palipo na madudu.

Rais Samia anata udhaifu wa Serikali uanikwe, ama kwa usimamizi wa kibunge au ukaguzi wa CAG. Viongozi huridhia makosa yao kusemwa. Watawala hutaka waonekane malaika. Wasisemwe. Kama ni kusema basi wao ndio waseme.

Uongozi wa haki na utu umejidhihirisha katika siku 100 za Rais Samia. Hataki watu waonewe na wanaotuhumiwa kuonea watu wanachukuliwa hatua. Lengai Ole Sabaya yupo mahabusu kama unahitaji uthibitisho wa hilo. Wakati huohuo, watu wengi waliokuwa na kesi zisizo na kichwa wala miguu wameshaachiwa. Wapo huru.

Taratibu lakini kwa uhakika, Rais Samia amebadili mengi ndani ya siku 100. Hapelekeshwi na presha za mitandao ila anafuatilia na kuzingatia yote yanayosemwa. Hafanyi uamuzi kwa pupa lakini anajua anachokifanya.

Kwa hakika, siku 100 za Rais Samia zimekuwa njema. Waliokimbia nchi wanarejea. Yusuf Manji amesharejea Tanzania, kama unataka uthibitisho. Kazi inaendelea.

Lipo jambo muhimu la kikatiba Rais Samia amelifanya. Ni kuirejesha Serikali kwenye mfumo wake wa Nusu Urais (Semi Presidential System). Yeye ni mkuu wa nchi, mtendaji mkuu (nahodha) ni waziri mkuu. Tumetoka nyati ambazo Rais alipoka madaraka ya waziri mkuu. Kila kitu akawa anafanya yeye. Waziri mkuu akafunikwa.

Hivi sasa, waziri mkuu ana nafasi kubwa ya kuonekana kuliko ilivyokuwa mwanzo. Uongozi wa Rais Samia unatoa uhuru wa kimamlaka (free reign) ili kila mmoja awajibike kwenye eneo lake. Hivyo, kama waziri mkuu atajibana, atakuwa ni yeye tu. Ndani ya siku 100 za Rais Samia, ameonesha anataka uongozi wa kidemokrasia.

Eneo ambalo ni dhahiri Rais Samia hakutenda haki ni kutovunja Baraza la Mawaziri alipoingia madarakani. Alipaswa kumteua upya waziri mkuu na kumwapisha kama Katiba inavyotaka. Badala yake aliendelea tu. Rais Samia ni binadamu. Anaweza kutenda makosa.
Samia ni Rais. Ni Kiongozi. Ni Mama. Mungu Ibariki Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

©Luqman Maloto
 
Back
Top Bottom