feya bugalama
Member
- Oct 6, 2016
- 91
- 20
Siasa ni sehemu ya maisha ya kila siku ya binadamu na kwa mantiki hiyo kutojihusisha kwa wananchi katika shughuli za kisiasa ni sawa na kutojihusisha na mustakabali mzima wa maisha yao.
Zifuatazo ni faida kwa wananchi kushiriki katika shughuli halali za kisiasa.
Husaidia wananchi kuwa na uelewa wa pamoja wa maswala muhimu ya kitaifa. Ushiriki wa wanachi katika shughuli halali za kisiasa kama mikutano ya hadhara ya serikali, chama tawala na upinzani. Hili ndilo jukwaa pekee ambalo hubainisha mbivu na mbinchi zinazoendelea nchini.Pia kupitia majukwaa haya ndipo ufafanuzi wa kina hutolewa kuhusiana na maswala mbalimbali ambayo kwa namna moja au nyingine wananchi wanakuwa hawayajui kiundani. Siasa bubu muda mwingi hueneza upotoshaji na hivyo wananchi kukosa uelewa sahihi juu ya mambo mazuri au mabaya yanayoendelea kwenye taifa lao. Hivyo ni muhinu kwa taifa kuwa na siasa za uwazi ili zisikike na kutolewa ufafanuzi mzuri na serikali.
Huwapa wananchi nafasi ya kufanya maamzi sahihi wakati wa kupiga kura. Ushiriki wa wananchi katika shughuli za kisiasa huwasaidia wananchi kuwajua vyema viongozi wao. Hali hii husaidia wananchi kuwapima viongozi wao na kufanya maamzi sahihi katika sanduku la kura.Hii husaidia pia wananchi na taifa kuondokana na viongozi mizigo na wasio kuwa na misimamo thabiti (bendera fuata upepo). Bila ushiriki wa wananchi katika shughuli za kisiasa ni ndoto kupata viongozi waadilifu na wenye nia ya dhati kuwatumikia wananchi. Siasa bubu huzaa viongozi bubu, wasio na maono na nia thabiti ya kuwatumikia wananchi.
Huwasaidia wananchi kuwa na vipaumbele au vigezo vyao wenyewe katika kuwachagua viongozi wao. Kupitia mawazo mbalilmbali yanayotolewa kupitia majukwaa ya kisiasa huwasaidia wananchi kujua mahitaji na matarajio kwa viongozi wanaowachagua. Hii husaidia wananchi kutorubuniwa kwa vitu visivyonatija katika mustakabali wa maisha yao. Pia ndiyo mwarobaini wa ilani za vyama zisizotekelezeka na kutozingatia uhalisia wa maisha, matarajio na mahitaji ya wananchi.
Licha ya kuwa siasa ni chimbuko na njia ya kuwapata viongozi kwa amani, lakini ni lazima kuwe na utaratibu mahususi wa uendeshaji wa shughuli hizi. Hii itasaidia kuepukana na matatizo mbalimbali yanayotokana na siasa chafu na zenye upendeleo.Pia pamoja na utaratibu huo vyombo vinavyosimamia ni vyema vikatenda haki kwa makundi yote yanayojihusisha na shughuli halali za kisiasa pasipo kupendelea au kuonea kundi lolote.Usawa katika uwanja wa kisiasa husaidia kupatikana viongozi wanaokubalika na makundi yote na hivyo viongozi kuwa na kazi ndogo katika katika kuwaunganisha wananchi. Pia inakuwa rahisi kwa wananchi kujitolea na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo kwenye maeneo yao.Daima jamii iliyofarakanika kwa misingi ya kisiasa, kidini, kikabila, kikanda n.k haiwezi kuendelea kwani makundi yasisyo na mamlaka (madaraka) huhisi kuonewa na hivyo kulipa kisasi kwa kuhujumu juhudi na mikakati ya maendeleo ya kundi lililo madarakani.