Zack Abdul
JF-Expert Member
- Mar 9, 2026
- 497
- 487
Kwa Nini Waziri Mkuu Lazima Awe Karibu na Wananchi? Mtazamo wa Kikatiba
Anaandika Thomas Joel Kibwana, Mchambuzi wa Siasa
Katika siku za hivi karibuni, baadhi ya wabunge na wanasiasa wa upinzani wamejitokeza kuhoji mantiki ya ziara za Waziri Mkuu zinazolenga kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi.
Inawezekana baadhi yao ni wageni katika siasa za kitaifa au hawajapata fursa ya kuisoma kwa kina Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu majukumu ya Waziri Mkuu. Inawezekana pia wanafanya hivyo kama sehemu ya wajibu wao wa kisiasa wa kuhoji Serikali. Hata hivyo, kabla ya kutoa hukumu kuhusu umuhimu wa ziara hizo, ni muhimu kwanza kuangalia Katiba inasemaje.
Ibara ya 52 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza wazi majukumu ya Waziri Mkuu kama ifuatavyo:
52(1) Waziri Mkuu atakuwa na madaraka juu ya udhibiti, usimamizi na utekelezaji wa siku hadi siku wa kazi na shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
52(2) Waziri Mkuu atakuwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni.
52(3) Katika utekelezaji wa madaraka yake, Waziri Mkuu atatekeleza au kusababisha utekelezaji wa jambo lolote au mambo yoyote ambayo Rais ataagiza kwamba yatekelezwe.
Ukiisoma kwa makini Ibara ya 52(1) na 52(3), utaona wazi kuwa ziara za Waziri Mkuu si jambo la hiari wala la anasa za kisiasa. Ni sehemu ya utekelezaji wa wajibu wake wa kikatiba.
Kwa lugha rahisi, kama Serikali ingekuwa kampuni, Rais angefananishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, wakati Waziri Mkuu angekuwa Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) anayesimamia utekelezaji wa maamuzi, sera na maelekezo ya uongozi wa juu katika shughuli za kila siku za taasisi hiyo.
Sasa jiulize: Kama Waziri Mkuu ndiye mwenye jukumu la kusimamia utekelezaji wa shughuli za kila siku za Serikali na kuhakikisha maagizo ya Rais yanatekelezwa, atafanyaje kazi hiyo kwa ufanisi bila kwenda kuona hali halisi iliyopo maeneo mbalimbali nchini?
Atajuaje changamoto zilizopo katika shule, hospitali, miradi ya maendeleo, huduma za maji, miundombinu au uwekezaji bila kukutana na wananchi wanaopokea huduma hizo kila siku?
Utawala bora haujengwi kwa kusoma ripoti pekee. Unajengwa kwa viongozi kwenda eneo la tukio, kuona hali halisi, kusikiliza wananchi moja kwa moja na kuchukua hatua stahiki. Hicho ndicho ambacho ziara za Waziri Mkuu hufanikisha.
Kwa mantiki hiyo, wanaodhani kuwa Waziri Mkuu hapaswi kusikiliza au kushughulikia kero za wananchi kwa sababu ya hadhi ya nafasi yake, kwa hakika wanapendekeza kuwepo kwa kizuizi kati ya Serikali na wananchi. Wanataka Waziri Mkuu ategemee taarifa za karatasi pekee badala ya kupata mrejesho wa moja kwa moja kutoka kwa watu ambao Serikali inawahudumia.
Kimsingi, ziara hizi zinatoa faida mbili kubwa. Kwanza, zinawapa wananchi fursa ya kueleza changamoto zao moja kwa moja kwa msimamizi mkuu wa shughuli za Serikali. Pili, zinampa Waziri Mkuu taarifa za moja kwa moja zinazomwezesha kufanya maamuzi sahihi, kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya Serikali na kuwawajibisha watendaji pale panapohitajika.
Ndiyo maana katika nchi yoyote inayozingatia misingi ya uwajibikaji, viongozi wa ngazi za juu hawajifungii ofisini wakisubiri ripoti pekee; wanakwenda kwa wananchi ili kujionea hali halisi na kupata taswira kamili ya utekelezaji wa sera na mipango ya Serikali.
Kwa hiyo, kwa yeyote anayeelewa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hasa Ibara ya 52, ni vigumu kuhoji mantiki ya ziara za Waziri Mkuu. Badala yake, hoja inayopaswa kujadiliwa si kwa nini Waziri Mkuu anatembelea wananchi, bali ni jinsi gani ziara hizo zinaweza kuimarishwa zaidi ili kuongeza ufanisi wa Serikali, uwajibikaji wa watendaji na ubora wa huduma kwa wananchi.