[MSUGUANO wa vijana wa Chadema (Bavicha) na Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki , John Shibuda, umezidi kuongeza joto la kisiasa ndani ya chama hicho baada ya mbunge huyo kumrushia kombora Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa, akisema ndiye anayewatumia vijana hao kumhujumu.
Tayari Shibuda ameigawa Bavicha baada ya Mwenyekiti wake, John Heche kupingana hadharani na makamu wake, Juliana Shonza kuhusu msimamo wa baraza hilo dhidi ya hatua ya mbunge huyo kutangaza dhamira ya kuwania urais mwaka 2015 ndani ya Nec ya CCM na kumwomba Mwenyekiti wa chama hicho tawala, Rais Jakaya Kikwete awe kampeni meneja wake.
Wakati kauli zake hizo ndani ya Nec ya CCM zikitarajiwa kumweka katika hatari ya kufukuzwa ndani ya Chadema kipindi hiki ambacho amekuwa katika uangalizi maalum, Shibuda jana aliliambia Mwananchi kwamba, yuko tayari kwa lolote na wakati wowote tena kwa asilimia 100.
Shibuda alifafanua kwamba anatuhumiwa kukihujumu chama huku akiwa hajawahi kukiuka maagizo yoyote ya Kamati Kuu ndani ya Chadema , lakini amebaini kuna baadhi ya watu wanatumiwa na viongozi wa juu wa chama hicho akiwamo Dk Slaa kwa lengo la kumfanyia fitina na hujuma.
Alisema kitendo cha Dk Slaa kukalia kimya shutuma zinazoelekezwa kwake na vijana hao wa Chadema kinampa fursa ya kuamini kwamba vigogo wa chama hicho wako nyuma yao na kumtaka sasa Dk Slaa aeleza hadharani uovu wake huo ili Watanzania wafahamu ukweli kuhusu sakata hilo.
"Mimi sina kosa lolote ila ninachofikiria ni kwamba Bavicha wanatumiwa na viongozi wa juu wa Chama ili kutaka kuniharibia lakini cha msingi ni vyema Katibu Mkuu wetu (Dk Slaa), akaweka hadharani maovu yangu ili Watanzania wajue makosa yangu ni yapi," alisema Shibuda na kuongeza:
"Ni wakati wa Chadema kupitia viongozi wake wakuu kueleza ubora wake wa kuwaongoza wananchi uko wapi kwani kama mtu anatangaza nia na kuonekana ameenda kinyume, sidhani kama kuna uongozi thabiti."
Kitisho cha kufukuzwa
Akizungumzia kitisho cha kuweza kufukuzwa Chadema, Shibuda alisema kwa sasa yupo tayari kwa asilimia 100 kupokea jambo lolote litakalotokea dhidi yake ndani ya chama hicho na kwamba kinachotakiwa ni kuonyeshwa makosa yake.
"Kwa asilimia 100, kutoka moyoni nasema nipo tayari kwa lolote litakalotokea kwangu ndani ya Chadema, kwani mimi natambua wazi sina kosa nililolifanya na kama nina makosa basi yaanikwe hadharani ili wananchi nao watambue," alisema.
Akizungumzia kupewa barua ya karipio kali, Shibuda alisema kwamba, hata siku moja hajawahi kupewa barua yoyote ya karipio kali na hafahamu chochote juu ya suala hilo.
"Sikiliza ndugu mwandishi, mimi sijawahi kupewa barua yoyote ya karipio kali na sifahamu chochote juu ya suala hilo labda hao walionipa barua hiyo wangeeleza lini walinipa," alisema.
Kauli ya Dk Slaa
Akizungumzia tuhuma hizo za Shibuda, Dk Slaa alisema asingependa kuingizwa katika mjadala huo kwani hajawahi kumzungumzia Mbunge huyo kuhusu jambo lolote wakati wowote tangu mjadala wake na Bavicha ulipoanza.
Alisema haoni suala la Shibuda kama ni jambo la kuzungumzia kwa sasa kwani halina msingi na kuna mambo mengi ya kujadili ili kuliwezesha taifa kupambana na umasikini.
"Mimi nisingependa kuhusishwa na suala la Shibuda kwani sijawahi kuzungumza chochote kumhusu yeye na kwamba, nina mambo mengi ya kuangalia na sio Shibuda," alisema Dk Slaa na kuongeza:
"Sipendi kuzungumzia kauli za watu hata kidogo kwani tunakazi kubwa ya kupambana na kuwakomboa wananchi kutoka katika umasikini."]
Safi sana......FOCUS ya katibu iko vzuri kweli zipo ishu nyingi za ku deal nazo sio kupoteza muda na huu ujinga.....Bavicha wenyeviti wa matawi au wana jamii twaweza kuchangia na kurumbana tuache jembe letu lifanye kazi za msingi!