Wadau,
Hili andiko la bwana joseph limeenda skuli sana hebu tulipitie bila jazba.
MBUNGE wa Maswa Mashariki na mwanachama asiye wa siku nyingi wa Chadema, John Shibuda, amejikuta katika mtafaruku na ‘wenye chama chao', kwa linaloitwa kosa la kutangaza kuwania urais wa Tanzania kwa tiketi ya chama hicho mwaka 2015.
Kinachowauma Chadema kupitia Baraza lake la Vijana (Bavicha) chini ya Mwenyekiti John Heche, ni kwanza kujitangaza kwa Shibuda mapema, pili kujinasibu kwamba atamwomba
Rais Jakaya Kikwete awe Meneja wake wa kampeni, lakini tatu mahali alikotangazia.
Bavicha wanalalamika Shibuda kutangaza azma yake hiyo katika semina ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Dodoma, lakini wanaloliona baya zaidi ni aliposema kwamba hakuna chama cha upinzani chenye uwezo wa kuongoza Dola kama CCM.
Hapo ndipo wanapotamka wazi, kuwa kama anaona hakuna chama cha upinzani chenye uwezo wa kuongoza Dola huku kila chama kikiwania kushika Dola, basi na aende katika chama anachoona kina uwezo huo, ambacho kwa mujibu wa Shibuda ni CCM.
Chadema wana haki ya kujibu pigo hilo la Shibuda, hasa pale ilipoona kama inabezwa kuwa si
miongoni mwa vyama vyenye uwezo wa kushika Dola, huku kikijinasibu kuwa ndicho kinachoelewa matatizo ya wananchi na kimbilio lao, lakini pia mpaka kikaonya dhidi ya
wanaotaka kukizuia kushika Dola mwaka 2015.
Pande hizi mbili za mgogoro huu zina haki ya kimsingi, kwamba Shibuda ana haki zote za kutangaza azma yake kama Mtanzania huru lakini mwanachama wa chama kinachojinasibu kujenga demokrasia na maendeleo kwa mujibu wa jina lake.
Lakini Chadema nayo ina haki ya msingi ya kujitetea, ili isidharauliwe wala kutibuliwa mipango yake ya kutwaa madaraka na kumsimamisha mgombea inayemtaka, ingawa hata
alichokifanya Shibuda kinaweza kuirahisishia kupata mgombea wake.
Ila kilichofanywa na Bavicha kumshambulia Shibuda, kinaonesha wazi kuwa demokrasia ndani ya Chadema ni ya hatihati, na huenda kuna wateule wachache ndani ya chama hicho wanaojua nani atagombea muda ukifika – ni kinyume cha Demokrasia.
Tumeshuhudia Mbunge wa Kigoma Kaskazini, ambaye ni mwanachama wa siku nyingi, Kabwe
Zitto, akisakamwa ndani ya Chadema pale alipotangaza kwamba urais anautaka na muda mwafaka ukifika atagombea.
Tulipata kushuhudia alivyosakamwa Zitto alipotaka kugombea uenyekiti wa Chadema dhidi
ya Mwenyekiti wa sasa Freeman Mbowe; lakini ilikuwa vivyo hivyo kwa marehemu Chacha Wangwe, alipoonesha nia ya kugombea pia nafasi hiyo huko nyuma.
Chadema inataka kutwambia nini sisi ambao tulidhani kweli inajenga demokrasia sawa na jina lake? Inataka kutueleza kuwa ni ya wateule wachache na ndiyo wenye haki ya kugombea uongozi wa juu wa Taifa hili? Kwa nini iwe nongwa kwa wengine kujitangaza?
Mimi nadhani Shibuda hajakosea kiasi hicho kama ambavyo Bavicha inataka kuufahamisha umma, yeye alionesha nia na kuitangaza, ambalo si kosa katika Katiba ya chama chochote
achilia mbali ya nchi.
Kutangazia mbele ya wajumbe wa NEC ya CCM nalo si tatizo, kwa sababu Shibuda hakwenda pale kama mwanachama wa CCM, bali mjumbe wa Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Afrika (APRM) ambao ndio ulikuwa umeandaa semina ile kwa wajumbe wa NEC.
Shibuda kumwomba Rais Kikwete awe Meneja wake wa Uchaguzi nayo ni hiari yake kwa sababu kwanza ni mtani wake, lakini pia wakati huo Kikwete atakuwa amemaliza muda wake wa uongozi na kubaki kuwa Rais mstaafu, ambaye yawezekana kabisa hatakuwa na kikwazo.
Badala ya Chadema kumlalamikia Shibuda kwa uamuzi wake huo alioutangaza uwe mzaha, utani au uliodhamiriwa kwa dhati ya moyo wake, ungemtumia kujitangaza na kujenga uhusiano chanya na vyama vingine vya siasa vinavyoamini katika ujenzi wa demokrasia nchini.
Lakini pia kinapaswa kuwapa uhuru wanachama wao kutangaza azma zao mapema na hivyo kupata fursa ya kuona ni nani pumba na nani mchele, badala ya kubana fikra za wanachama katika kutoa hisia zao.
Chadema mlimpokea Shibuda kwa nderemo, vifijo na vigelegele alipohama CCM mkamsaidia mpaka akapata ubunge, iweje anapotaka urais mnaanza kumletea mikingamo na mizengwe na kuamini kuwa si afaaye?
SOSI:
HabariLeo | Lipi kosa la Shibuda katika medani hii?
Msaidieni badala ya kumkatisha tamaa.