sheria mpya ya mifuko ya pension | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

sheria mpya ya mifuko ya pension

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Return Of Undertaker, Jul 24, 2012.

 1. Return Of Undertaker

  Return Of Undertaker JF-Expert Member

  #1
  Jul 24, 2012
  Joined: Jun 12, 2012
  Messages: 2,368
  Likes Received: 8,437
  Trophy Points: 280
  (Kusomwa Mara ya Pili)
  MWENYEKITI: Ahsante Katibu, sasa naomba nimwite mtoa hoja wa Muswada huu, aweze kutupa maelezo; Mheshimiwa Waziri karibu.
  WAZIRI WA KAZI NA AJIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja kwamba, Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Hifadhi za Jamii (The Social Security Laws (Amendments) Act, 2012), pamoja na marekebisho yake sasa usomwe kwa mara ya pili.
  Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachukua nafasi hii kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa Kamati yako ya Bunge kwa Maendeleo ya Jamii chini ya Uenyekiti wako Mheshimiwa Jenister Mhagama, Mbunge wa Peramiho na Makamu Mwenyekiti, Mheshimiwa Juma Suleiman Nkamia, Mbunge wa Kondoa Kusini na Wajumbe wa Kamati, kwa ushirikiano wao mkubwa sana katika maandalizi ya Muswada huu. Aidha,
  55

  shukrani za pekee ziende kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali hususan Mwandishi Mkuu wa Sheria na Wasaidizi wake, kwa kazi kubwa ya kuandika Muswada huu.
  Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada huu unakusudia kufanya marekebisho katika Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, kwa madhumuni ya kuiwezesha Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii, kufanya kazi yake kikamilifu na kusimamia na kudhibiti Sekta ya Hifadhi ya Jamii. Muswada umeandaliwa kwa kuwashirikisha Wadau wote wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii, wakiwemo Wafanyakazi, Waajiri na Serikali, ikiwemo Mifuko yenyewe kupitia Vikao vya Wadau na pia Baraza la Ushauri wa Masuala ya Kazi Jamii na Uchumi, yaani RESCO. Kimsingi, wadau wote waliunga mkono mapendekezo yaliyomo katika Muswada huu.
  Muswada ulishasomwa Bungeni kwa Mara ya Kwanza, yaani First Reading, mnapo tarehe 1 Februari, 2012 na sasa unawasilishwa Bungeni kwa mara ya pili na ya tatu ili uweze kujadiliwa na kupitishwa na Bunge lako Tukufu.
  Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yaliyomo ndani ya Muswada huu, yatawezesha kupanuliwa kwa wigo wa wanachama kwenye Mfuko kwa kuruhusu wafanyakazi wanaoingia kwenye ajira kwa mara ya kwanza ama kujiajiri wenyewe ili waweze kujiunga na Mfuko wowote wa Hifadhi ya Jamii ambao umeanzishwa kwa sheria ya Bunge. Mapendekezo ya Muswada pia yanakusudia kuoanisha Sheria za Mifuko na Sheria za Mamlaka. Maeneo yanayoainishwa katika Muswada huu ni pamoja na kufanya tathmini ya mali na madeni ya Mifuko, yaani actuarial valuation na uwasilishaji wa taarifa ya tathmini hiyo kwenye mamlaka, uwasilishaji wa taarifa za fedha za kila mwaka za Mfuko kwa mamlaka na Mifuko kuwekeza kwa kufuata miongozo ya uwekezaji, yaani investment guidelines iliyowekwa na Benki Kuu kwa kushirikiana na mamlaka.

  Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada huu umegawanyika katika sehemu nane; sehemu ya kwanza inaweka masharti ya utangulizi ambayo inajumuisha Jina la Muswada na maudhui ya kutungwa kwa Sheria hii. Sehemu ya pili inapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa (LAPF), Sura ya 407. Muswada unapendekeza kufanya marekebisho katika kifungu namba tatu cha sheria hii kwa kufuta, kuongeza na kurekebisha baada ya tafsiri ya maneno na misamiati iliyotumika katika Sheria hiyo.
  Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada pia unapendekeza kufanyia marekebisho kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Mfuko huo wa LAPF kwa kufuta jina la sasa la Mfuko na kupendekeza jina jipya ambalo linaondoa dhana ya awali iliyoanzisha Mfuko huo uliolenga wanachama kutoka sekta moja ili kuongeza wigo wa wanachama kutoka Hifadhi ya Jamii hasa baada ya kutungwa kwa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii, Sura ya 135 hususan kifungu namba 30. Aidha, kifungu cha 22 kinapendekeza kufanya marekebisho ili kutoa haki kwa mfanyakazi ambaye anaachishwa kazi aweze kulipwa mafao ya pensheni au mafao ya mkupuo, yaani gratuity. Pamoja na pendekezo la kurekebisha kifungu cha 22, inapendekezwa kuongezwa kifungu kipya cha 24(a) ili kutambua mamlaka ya udhibiti wa Hifadhi ya Jamii hususan wajibu wa Mfuko kuwasilisha taarifa ya tathmini ya mali na madeni kwa mamlaka.
  Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada pia unapendekeza kuongeza kifungu kipya cha 27(a) ili kumwezesha mwajiliwa ambaye baada ya kufikia umri wa kustaafu kwa lazima na bado anaendelea kutoa michango yake katika Mfuko kuwa na stahili ya kulipwa bonus. Muswada pia unapendekeza kupitia kifungu cha 49, uwekezaji wa Mfuko uzingatie mwongozo wa uwekezaji utakaotolewa na Benki Kuu kwa kushirikiana na mamlaka. Aidha, Muswada huu unapendekeza kufuta kifungu cha 65 na kuanzisha kifungu kipya ili kutoa uwezo kwa Mkurugenzi Mkuu, Mkaguzi Mkuu au Mfanyakazi


  eyote wa Mfuko ambaye amethibitishwa na Bodi kufungua mashtaka ya jinai dhidi ya mtu ambaye atavunja masharti ya kifungu cha 71 baada ya kupata kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka, yaani DPP. Sehemu hii pia inapendekeza kufanyiwa marekebisho Jedwali la Kwanza kuhusu Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ili kuzingatia utatu kutimiza vigezo vya Shirika la Kazi Duniani ambalo Tanzania ni Mwanachama.
  Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya tatu inapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Taifa ya Mfuko wa Bima ya Afya, Sura ya 395 (The National Health Insurance Fund Act, Cap. 395). Inapendekeza marekebisho katika Sheria hii kwa lengo la kuainisha Sheria hii na Sheria ya Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii, Sura ya 135. Marekebisho yanayopendekezwa katika sehemu hii ni pamoja na kuweka tafsiri mbalimbali ya maneno ambayo yatatumika katika Sheria. Pia marekebisho haya yanakusudia kuweka masharti ambayo yataiwezesha Bodi kuangalia upya viwango vya michango kwa kuzingatia kanuni, miongozo na maelekezo yanayotolewa na mamlaka. Aidha, marekebisho yanayokusudia kuweka masharti ili kuipa Bodi uwezo wa kutoa maelekezo kwa Mfuko kufanya tathmini ya mali na madeni ya Mfuko kila baada ya miaka mitatu au wakati wowote itakapopendekezwa na mamlaka. Sehemu hii pia inapendekeza kuweka masharti ambayo yataipa mamlaka uwezo wa kuelekeza Bodi kuwasilisha taarifa yake ya tathmini ya mali na madeni kwa mamlaka.
  Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya nne ya Muswada inapendekeza marekebisho katika Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii, Sura ya 50 (The National Social Security Fund Act, Cap. 50).
  Ili kuboresha utendaji wa kazi, sehemu inapendekeza marekebisho katika Sheria kwa lengo ya kuoanisha Sheria yenyewe na Sheria ya Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii, Sura ya 135. Marekebisho

  yanayopendekezwa katika sehemu hii ni pamoja na kufuta baadhi ya tafsiri ya maneno na kuweka tafsiri mpya. Vilevile tafsiri ya maneno mapya imeongezwa. Marekebisho mengine yanayopendekezwa yana lengo ya kuipa mamlaka uwezo wa kuamua kiwango cha pensheni atakayopewa mwanachama kwa mwezi kwa kuzingatia tathmini ya mali na madeni ya Mfuko, yaani actuarial valuation. Aidha, Muswada unapendekeza kukifanyia marekebisho kifungu cha 62 cha Sheria kwa kuweka masharti ambayo yataitaka Bodi ya Wadhamini kutekeleza Sera ya Utekelezaji kwa kufuata miongozo ya uwekezaji itakayotolewa na Benki Kuu kwa kushirikiana na mamlaka.
  Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya tano ya Muswada inahusu marekebisho katika Sheria ya Mfuko wa Mashirika ya Umma, Sura ya 372, yaani The Parastatal Organization Pension Scheme Act, Cap. 372. Marekebisho haya yanahusu Jina la Sheria pamoja na dhamira ya kuepusha dhana ya kuwa Mfuko huu ni kwa ajili ya kuhudumia Sekta ya Mashirika ya Umma na Taasisi za Serikali tu, wakati Sheria yenyewe sasa inahusu pia waajiriwa wa makampuni binafsi na watu kutoka katika sekta isiyo rasmi.
  Mheshimiwa Mwenyekiti, Jina la Sheria limerekebishwa na badala yake litakuwa PPF Pensions Fund 2012, kwani kuendelea kutumia neno Parastatal kunakinzana na dhana ya kuruhusu Mfuko huu kufungua wigo kwa wanachama wa sekta rasmi na isiyo rasmi. Vilevile inapendekezwa kufanya marekebisho katika Sheria hii ili kutambua wanachama ambao ni waajiriwa walioko katika majaribio na pia kutambua uanachama wa mwajiriwa ambaye amebadili ajira au amejiuzulu.
  Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu hii pia inaweka majukumu ya mwajiri, ikiwa ni pamoja na kusajili wafanyakazi wapya kwenye Mfuko huu wa PPF kwa wale ambao si wanachama wa Mfuko wowote na kuwasilisha michango

  kamili ya wafanyakazi, pale ambapo wafanyakazi hao wamesimamishwa kazi kwa nusu mshahara. Aidha, marekebisho hayo yameweka wazi umri wa kustaafu kwa hiari kwa mwanachama kuwa ni kuanzia miaka 55, isipokuwa uanachama wake utakoma pale ambapo mwanachama huyo atatimiza umri wa miaka 60. Inapendekezwa pia kwamba, mwanachama ambaye hajatimiza muda wa kuchangia, yaani qualified period, anapostaafu apewe michango yake na ya mwajiri pamoja na riba. (Makofi)
  Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya sita inapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Mafao ya Hitimisho la Utumishi wa Umma, Sura ya 371, yaani The Public Service Retirement Benefit Act, Cap. 371, kwa kufanya marekebisho katika kifungu cha tatu kwa kupanua wigo wa Sheria ili waajiriwa wa sekta rasmi na isiyo rasmi waweze kuwa wanachama. Sehemu hii pia inapendekeza marekebisho kwa kufuta baadhi ya tafsiri za maneno na kuyatafsiri upya ili kwenda sambamba na vifungu vya Sheria ya Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii, Sura ya 135.
  Sehemu hii inapendekeza kufanya marekebisho katika kifungu cha 33 ili kuweka masharti ambayo yataitaka Bodi kusimamia na kuongoza Mfuko kwa kufuata masharti ya Sheria ya Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii, miongozo na maelekezo yatakayokuwa yanatolewa na mamlaka hiyo. Aidha, yapo mapendekezo ya kurekebisho kifungu cha 52 kuruhusu kuwa na Bodi inayozingatia uwakilishi wa utatu.
  Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya saba inahusu marekebisho katika Sheria ya Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii, Sura ya 135, yaani The Social Security Regulatory Authority Act, Cap. 135. Marekebisho haya yanapendekeza kurekebisha kifungu cha sita ili kuipa mamlaka uwezo kutoa maelekezo mbalimbali ya usimamizi kwa ajili ya Sekta nzima ya Hifadhi ya Jamii. Sehemu hii pia inapendekeza

  kumtoa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka kwenye Bodi na kumfanya awe Katibu wa Bodi hiyo. Sehemu hii vilevile inapendekeza kuipa uwezo mamlaka kusimamia mambo ya kitaalam kwenye maeneo ya huduma za afya kwa kushauriana na Waziri anayehusika na masuala ya afya.
  Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya nane inahusu marekebisho katika Sheria ya Bima, Sura ya 394. Marekebisho katika Sheria hiyo yanapendekeza kufanya marekebisho kwenye kifungu cha 13 cha Sheria kwa lengo la kuweka bayana idadi ya Wajumbe wa Bodi ambayo haitazidi saba na kwamba idadi ya Wajumbe kutoka Tanzania Zanzibar haitapungua wawili.
  Mheshimiwa Mwenyekiti, marekebisho hayo pia yanabainisha sifa za mtu anayefaa kuwa Mjumbe wa Bodi kuwa ni mtu mwenye elimu na uzoefu katika masuala ya Bima, Uchumi, Sheria, Fedha, Utawala na Uhasibu.
  Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na marekebisho haya ya Sheria za Hifadhi ya Jamii, wadau walileta maoni mbalimbali yaliyopelekea Jedwali la Marekebisho ya Muswada, yaani Schedule of Amendments ambayo yatasomwa pamoja Muswada huu.
  Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo hayo ni kama ifuatavyo:-
  Kwanza, kupanua wigo wa Hifadhi ya Jamii kwa waajiriwa katika sekta binafsi na wanaojiajiri katika sekta rasmi na isiyo rasmi kwa Mfuko wa LAPF.
  Pili, kumtaka mwajiri kuwasilisha michango ya waajiriwa wake ambao ni raia wa kigeni kwenye Mfuko husika.


  Tatu, kuongeza uwakilishi wa Wajumbe wa Bodi kati ya saba na tisa ili kuweka uwiano kati sawa wa vyama vya waajiri na vyama vya waajiriwa.
  Nne, kuwianisha tafsiri ya neno mwajiriwa katika Mifuko yote ili iwe na tafsiri moja ambayo ipo katika Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini, Namba Sita ya Mwaka 2004 na Sheria ya Taasisi za Kazi, Namba Saba ya Mwaka 2004.
  Tano, kuruhusu mwajiriwa aliyeacha kazi na kutokuwa mwanachama kwa kipindi fulani kurudia uanachama wake baada ya kuajiriwa tena kwa Mfuko wa PPF.
  Sita, kutoa adhabu kwa mwajiri anapochelewa kulipa mafao ya mwanachama.
  Saba, kuhamasisha baadhi ya majukumu ya Mamlaka, kuhamisha baadhi ya majukumu ambayo ni ya kisera kwenda kwenye Wizara ya Kazi na Ajira.
  Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumalizia kwa kuwashukuru wadau wote ikiwa ni pamoja na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi, Chama cha Waajiri na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, kwa maoni na ushauri wao uliochangia katika kuboresha Muswada huu. Aidha, napenda kuwashukuru wataalam wetu wa Sheria na Watendaji wa Wizara na Taasisi nyingine zilizohusika katika hatua mbalimbali za maandalizi ya Muswada huu.
  Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia kukushuru tena wewe binafsi na Kamati yako, kwa kazi nzuri na ushirikiano mkubwa mliotupatia sisi Wizara katika kukamilisha Muswada huu.
  Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja. (Makofi)
   
Loading...