Sherehe za miaka 10 ya EAC zafana Arusha, lakini?.

Dr. Chapa Kiuno

JF-Expert Member
Sep 11, 2009
443
18
lC.gif
rC.jpg

bul2.gif
Mkapa na Moi 'wasahauliwa' kualikwa

bul2.gif
Ndiyo walioasisi EAC mpya



JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) ilifanya maadhimisho ya kutimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, wiki iliyopita, Novemba 20 katika sherehe kubwa zilizofanyika katika mji wa Arusha huku mmoja wa waasisi wa jumuiya hiyo, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa akikosa hudhuria kwa kile kinachodaiwa "kusahauliwa" kualikwa.
Katika kilele cha maadhimisho ya shrehe hizo, viongozi wa nchi tano wanachama walitia saini Itifaki ya Soko la Pamoja ikiwa hatua muhimu sana kwa nchi hizo kuelekea katika muungano wa kisiasa.
Viongozi waliotia saini Mkataba wa Itifaki ya Soko la Pamoja ni Rasi Jakaya Kikwete (Tanzania), Yoweri Museveni (Uganda), Paul Kagame (Rwanda), Mwai Kibaki (Kenya) na Pierre Nkurunzinza (Burundi).
Mchakato wa kuanzishwa kwa jumuiya mpya ya EAC baada ya kuvunjika kwa ile ya awali mwaka 1977 ulianza mapema wakati wa utawala wa awamu ya pili chini Rais Ali Hassan Mwinyi kwa upande wa Tanzania na mazungumzo yaliendelea hadi awamu ya tatu wakati wa utawala wa Rais Benjamin Mkapa.
Baada ya mazungumzo yaliyochukua zaidi ya miaka saba hivi, hatimaye mkataba wa jumuiya hiyo ulisainiwa Novemba 30 mwaka 1999 mjini Arusha na viongozi wa nchi tatu waanzilishi wa jumuiya ya EAC.
Viongozi waasisi wa kwanza kutia saini mkataba wa kuanzishwa kwa jumuiya ya ushirikiano wa Afrika Mashariki walikuwa ni Rais Benjamin Mkapa (Tanzania) , Daniel Arap Moi (Kenya) ambao tayari wamestaafu na Rais Yoweri Museveni (Uganda) ambaye bado yuko madarakani hadi sasa.
Katika kipindi cha miaka 10 jumuiya hiyo imekuwa kwa kasi ambapo nchi wanachama zimeongezeka kutoka tatu za awali hadi kufikia tano baada ya Rwanda na Burundi kuruhusiwa kujiunga mwaka jana.
Sherehe za Jumuiya kutimiza umri wa miaka 10 zilivuta hisia za watu wengi kutoka nchi hizo tano wanachama na wageni wengi kutoka jumuiya ya kimataifa, lakini katika hali ambayo haikutarajiwa na wengi viongozi waasisi waliotia saini mkataba huo mwaka 1999 marais wastaafu Benjamin Mkapa na Daniel arap Moi wa Kenya “walisahauliwa”.
Katika hali isiyotarajiwa, Sekretarieti ya Jumuiya hiyo inadaiwa kushindwa kuwaalika viongozi na waasisi muhimu ambao ndiyo walioweka misingi ya jumuiya iliyopo leo hii.
Habari za kutoka ndani ya Jumuiya hiyo zilieleza kuwa maafisa wa kamati ya maandalizi hawakutuma mwaliko kwa viongozi hao ingawa jukumu hilo lilikuwa linaangukia chini ya jumuiya hiyo hadi wiki moja tu kabla ya sherehe zenyewe.
Hakuna sababu rasmi zilizotolewa za kwa nini viongozi hao wawili hawakuhudhuria sherehe hizo. Katibu Mkuu wa EAC, Balozi Juma Mwapachu alipoulizwa swali hilo na waandishi wa habari wakati akieleza ratiba ya sherehe hizo, alidai kuwa suala la mialiko yao lilikuwa mikononi mwa nchi husika.
Balozi Mwapachu alitoa kauli hiyo jioni ya Novemba 16 ikiwa ni siku nne kabla ya sherehe zenyewe kufanyika.
“Suala la marais wastaafu (Mkapa na Moi) kuhudhuria sherehe za EAC kutimiza miaka 10 liko mikononi mwa nchi zao……tulitarajia wizara husika zitakuwa zimepeleka mialiko kwa viongozi hao”, alisema Mwapachu.
Hata hivyo, mmoja wa maafisa wa Wizara ya Afrika Mashariki aliyeomba jina lake lihifadhiwe alipinga kauli hiyo ya Mwapachu na kueleza kuwa Sekretarieti yake ndiyo yenye majukumu ya kuwaalika viongozi hao.
“Nia yangu kukupa ufafanuzi si kuleta malumbano lakini Sekretarieti ya EAC ndiyo yenye majukumu ya kutoa mialiko kwa wageni wote bila kujali vyeo vyao…..kwani sherehe hizo za kutimiza miaka 10 za kwao”, alisema ofisa huyo.
Ofisa huyo alieleza zaidi kuwa habari alizonazo ni kwamba mwaliko wa Mkapa ulipelekwa ukiwa umechelewa. Baada ya Sekretarieti kugundua “kumsahau” walituma mwaliko kupitia msaidizi wake lakini msaidizi huyo aliwaeleza kuwa Rais huyo mstaafu tayari alikuwa ameshapanga ratiba nyngine ya shughuli zake.
“Mheshimiwa Rais Mstaafu tayari ameshapanga ratiba yake na anakwenda Masasi kwa hiyo si rahisi avunje ratiba hiyo kwa kuwa mwaliko wenu umechelewa na vinginevyo itavuruga ratiba ya mzee”, alisema mtoa habari wetu huku akimkariri msaidizi huyo wa Mkapa.
Ingawa suala hilo halikuwekwa hadharani lakini habari zaidi zilieleza kuwa jambo hilo lilileta msuguano wa wa chini kwa chini kati ya maafisa wa Sekretarieti ya EAC na wale wa Serikali ya Tanzania; huku maafisa wa EAC wakitupiwa lawama kwa kukosa umakini katika kuandaa sherehe hizo.
Lakini pamoja na dosari hiyo ya kukosekana kwa waassisi muhimu katika tukio hilo la kihistoria, maadhimisho yalianza kwa wakuu wa nchi hizo kukutana kwa mkutano wa faragha katika chumba maalumu cha VIP katika katika kituo cha mikutano cha AICC na mkutano huo ulianza majira ya saa za asubuhi.
Kikao hicho cha ndani cha wakuu wa nchi kiliendelea hadi majira ya saa nane za mchana na kuchelewa huko kunatokana na kuzuka kwa majadiliano makali ndani ya kikao hicho kabla ya kufikia uamuzi wa kutia saini itifaki hiyo ya soko la pamoja na baadaye waliingia ukumbi wa Simba katika kituo hicho huku muda wote wageni waalikwa wakisubiri kwa hamu kutangazwa kwa maamuzi waliyofikia viongozi hao.
Baada ya kuingia ukumbini na Rais Kikwete kukabidhiwa nafasi yake kama Mwenyekiti mpya, alitoa hotuba yake ambapo alieleza kuwa kusainiwa kwa itifaki hiyo ni moja ya hatua muhimu sana katika kuelekea katika makubaliano ya msingi ya mambo mengine kama ushuru wa forodha, kuwa na sarafu moja, na hatimaye muungano wa kisiasa.
“Tunatia saini itifaki hii tukikubaliana kimsingi kuwa hii ni moja ya hatua muhimu sana katika kufikia malengo tuliyojiwekea ya kuwa na soko la pamoja kwa wananchi wetu wanaofikia milioni 120, na tutakamilisha mambo mengine muhimu katika kipindi cha miaka mitano ijayo”, alisema.
Kwa upande wake, Rais Yoweri Museveni wa Uganda katika hotuba yake iliyogusa watu wengi alisema kutiwa saini kwa jumuiya hiyo ni moja ya hatua muhimu ya kuwaunganisha tena watu wa Afrika Mashariki ambao ni ndugu moja kabla ya kutenganishwa na wakoloni kwa mipaka waliyoweka kwa ajili ya maslahi yao.
Museveni alisema kabla ya wakoloni hao wananchi wa nchi zote tano waliishi bila mipaka katika maeneo yao huku wakifanya shughuli za uzalishaji, biashara na mambo mengine ya kijamii huku watu hao wakiheshimiana kwa kiwango cha juu.
Alisema cha msingi ni kwa nchi hizi sasa kutumia kwa pamoja raslimali walizonazo kwa faida ya wananchi wa nchi zote.
Alisisitiza kwamba Uganda, ambayo imegundua mafuta, itatumia raslimali hiyo pamoja na majirani zake ili kudumisha ushirikiano ulioanzishwa.
“Jambo la kujivunia ni kwamba mafuta haya yamegunduliwa na Waganda wenyewe tofauti na proganda za mataifa ya Magharibi kuwa wao ndiyo wamegundua mafuta ya Uganda. Mikataba ya uchimbaji wake itazingatia maslahi ya Taifa letu pamoja na maslahi ya watu wa Afrika Mashariki”, alisema Museveni.
Pamoja na kusainiwa kwa itifaki hiyo, hata hivyo utekelezaji wake utaanza Julai mosi mwaka 2010.
Miongoni mwa mambo ya msingi katika itifaki hiyo ni kuhusu biashara, uhamishaji wa mitaji kutoka nchi moja kwenda nyingine, uhuru wa watu kufanya kazi katika nchi yoyote, bidhaa zinazozalishwa katika nchi wanachama kutotozwa ushuru na uhuru wa watu kutembea bila kuhitaji viza au hati za kusafiria na masuala ya huduma za kijamii.
Kwa mujibu wa Waziri anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Deodorius Kamala, Tanzania kwa upande wake bado imekataa suala la ardhi na matumizi ya vitambulisho vya uraia badala ya hati za kusafiria kuingizwa katika itifaki hiyo na kuongeza kuwa katika masuala hayo yataamuliwa na sheria mama za nchi husika.
hs3.gif
 
Back
Top Bottom