Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 20,916
- 30,259
SHEIKH SULEIMAN TAKADIR NA BENARD MEMBE ''WAKOROFI'' NDANI YA TANU 1958 NA CCM 2020
Ilikuwa baada ya L'Asr siku nilipokwenda nyumbani kwa Sheikh Haidar Mwinyimvua katika wanachama wa mwanzo wa TANU na mjumbe katika Halmashauri Kuu ya TANU na mmoja wa wajumbe wa Baraza la Wazee wa TANU.
Nilikuwa katika utafiti wa kuandika historia ya TANU.
Mjukuu wake ndiye alikuwa kanichukua kunipeleka kwa babu yake anieleza kisa cha Sheikh Suleiman Takadir vipi alivunja moja ya mwiko mkubwa wa TANU na adhabu yake ikawa ''kutoswa.''
Miaka ile ukifukuzwa TANU inaitwa umetoswa, yaani umetupwa baharini uliwe na papa na samaki wengine au maji yakupeleke mbali kabisa ukiwa maiti.
Niliposikia Benard Membe kafukuzwa CCM ilinijia picha ya Sheikh Suleiman Takadir jinsi alivyofukuzwa TANU mwaka wa 1958 akatengwa na jamii nzima ya Dar es Salaam, Barza maarufu iliyokuwa nyumbani kwake Mtaa wa Msimbazi ikahama na yeye akapewa jina, ''Takadiri Mtaka Dini.''
Wakati wa enzi yake ananisimulia Sheikh Haidar Mwinyimvua tumekaa ukumbini kwake nyumbani kwake nyumba ya vyumba sita ya National Housing, Magomeni Mapipa, ''Sheikh Suleiman Takadir tukimuiita Makarios kwa kuwa alikuwa sheikh mwanasiasa mpigania uhuru kama Askofu Makarios wa Cyprus.''
Sheikh Suleiman Takadir kisa chake kinatisha kiasi watu walikuwa wanaogopa kukihadithia hadi leo kwani si historia ambayo mtu atapenda kuieleza.
Kisa cha Sheikh Suleiman Takadir hakika kinatisha na katika utafiti wangu baadhi ya wana TANU nikiwauliza habari za Sheikh Takadir wakikwepa kueleza historia ya sheikh ingawa ni kisa maarufu.
Huwezi kuandika historia ya TANU na kupigania uhuru wa Tanganyika usimtaje Sheikh Suleiman Takadiri.
Wakati wake Sheikh Suleiman Takadir siku hizo si wengi walikuwa wanamfahamu Nyerere, yeye alikuwa anatangulia kupanda jukwaani katika mikutano ya mwanzo pale Mnazi Mmoja kusoma dua na kumtambulisha Nyerere kwa wananchi.
Nyerere atapanda jukwaani huku akisindikizwa na nyimbo maarufu, ''Muheshimwa nakupenda sana wallahi sina mwingiewe In Shaa Allah Mungu yuko Tanganyika tutajitawala.''
Huyo Bi. Hawa bint Maftah na Bi, Titi Mohamed na akina mama wengine wanaimba.
Wanasema wasemaji nyimbo hii ilikuwa ikimliza Nyerere kila alipoimbiwa.
Turudi kwa Makarios.
Ikutoshe tu kuwa baada ya kufukuzwa TANU Sheikh Takadiri hakuwa na maisha tena akafa akiwa mtu aliyedhalilika kupita kiasi.
Sitegemei kama Membe atapigwa pande na jamaa zake wala sidhani kama atadhalilika na atakufa kwa simanzi kwa kufukuzwa chama kama alivyokufa Sheikh Suleiman Takadiri.
Lakini Membe ikiwa kama atabahatika kuisoma historia ya TANU na historia ya Sheikh Suleiman Takadiri atajifunza mengi.
PICHA: Kulia ni Bi. Titi Mohamed, Clement Mtamila, Sheikh Suleiman Takadiri, Julius Nyerere. Nyuma kulia John Rupia, Rajab Diwani na Mama Maria Nyerere.