Gazeti: Uhuru
Magari ya serikali yapigwa marufuku kulazwa mitaani
* Ni baada ya moja kutumika katika ujambazi
NJUMAI NGOTA NA TUMAINI KAWOGO, RCT
JESHI la Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limepiga marufuku magari ya wizara na taasisi za serikali kuegeshwa na kulazwa mitaani, badala yake kutafuta maeneo rasmi ya kuyaegesha.
Hatua hiyo inatokana na kukamatwa kwa gari la serikali linalomilikiwa na Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, likishiriki kwenye tukio la ujambazi lililotokea juzi katika kituo cha mafuta cha GAPCO mjini Dar es Salaam.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Suleiman Kova, ametoa wiki mbili kwa wizara na taasisi za serikali kutafuta maeneo rasmi ya kuegesha magari hayo na kuwa baada ya muda huo, magari yatakayokiuka amri hiyo yatakamatwa na madereva wake kuchukuliwa hatua.
Alitaja gari lililokamatwa katika tukio hilo kuwa ni lenye namba za usajili STK 4431 aina ya Toyota Land Cruiser GX mali ya wizara hiyo, chini ya kitengo cha maeneo ya uzalishaji kwa ajili ya uuza nje (EPZ). Hata hivyo, taarifa za awali za polisi zilisema gari hilo ni la Tume ya Mipango.
Kova alisema hadi Julai 10, mwaka huu, gari litakalokutwa limeegeshwa au kulazwa holela, dereva wake atachukuliwa hatua na kulikamata.
"Tukikuta magari ya serikali yameegeshwa ovyo au sehemu zisizo rasmi tutayashika, ikiwemo kumkamata dereva wake na kumchukulia hatua," alisema Kova.
Alisema magari mengi yamekuwa hayafuati utaratibu wa uegeshaji, hivyo kuchochea madereva kufanya uhalifu au kuibwa.
Kova aliwataka watafute sehemu ya kuegesha magari yao na kuweka ulinzi wa kutosha, kwani yamekuwa yakiibwa sana. Alitoa mfano hivi karibuni kuwa, gari la serikali liliibwa likiwa na kompyuta.
Alisema baada ya wiki mbili, wataanza kuyakamata magari hayo kwani kazi yao ni kulinda usalama wa raia na mali zao.
Kuhusu sakata la wizi katika kituo cha mafuta, aliwataja watuhumiwa waliokamatwa saa 6.15 usiku wakiwa na gari hilo wakifanya uhalifu katika kituo kilichopo mtaa wa India, mali ya Ghulam Chakaar (55).
Kova alisema watuhumiwa hao walivunja kasiki kwa kutumia mitungi miwili ya gesi na vifaa vingine, vikiwemo bisibisi, koleo na panga.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa dereva wa gari hilo ambaye awali alikuwa askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) namba MT. 68050 wa 701 KJ-Kigamboni aliyeacha kazi mwaka 1998, Geoffrey Barweta (38), mfanyabiashara wa vyuma chakavu Edwin Bitesigilwe (21) na fundi wa kuchomea vyuma Mbwana Shemumea (22).
Kova alisema watuhumiwa walikula njama na watuhimiwa wengine ambao wanaendelea kutafutwa na kwamba upelelezi wa tukio hilo unaendelea na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika