Shajara ya Mwanamzizima: Diwani (Chief) Mwinchuguuni

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,915
30,259
SHAJARA YA MWANAMZIZIMA:
Mjue Diwani (Chifu) Mwinchuguuni aliyewatimua Wakamba Bagamoyo

Na Alhaji Abdallah Tambaza

MNAMO karne ya 1600 ama 1700 hivi, kabla nchi hii haijawa Tanganyika tuijuayo; maeneo mbalimbali yalikumbwa na mashambulizi kutokana na uvamizi wa kabila la Wakamba kutoka Kenya.

Bagamoyo, mji wa mwambao uliokuwa ukikaliwa na makabila ya Wadoe, Wakwere, Washirazi na Wazigua; ulikuwa mafikio ya watu kutoka mataifa mbalimbali ya nje kama vile India, Uajemi na Uarabuni ulikumbwa na tishio la kuvamiwa kivita na Wakamba hao.

Diwani Mwinyimadi Mwinchuguuni, mwenyewe akijiita ‘Wa Mwambao’, ndiye aliyekuwa kiongozi wa kijadi wa eneo hilo lilokuwa na bandari kongwe; maarufu kwa biashara za utumwa na pembe za ndovu.

Katika kipindi hicho, kwenye maeneo ya Ukutu, kule Dutumi, Morogoro, kulikuwa na chifu aliyesifika sana kwa upiganaji vita wa kimazingaombwe.

Majeshi yake yaliwategemea mbwa wa kunusanusa maadui walipo. Jina lake akiitwa Pazi Kibamanduke.

Kutokana na tishio la uvamizi wa Wakamba, Diwani Mwinchuguuni, alilazimika kufunga safari hadi Dutumi, kule Ukutu; kumwomba Kibamanduke aje kusaidia kupambana na Wakamba.

Alipofika Dutumi hakumkuta; alikuwa safarini vijiji vya jirani. Mwinchuguuni alimwagizia dadake aliyeitwa Nyapazi; kwamba Pazi atakaporudi aje Pwani kuonana naye kuhusiana na uvamizi unaotegemewa kutokea.

Pazi Kibamanduke, aliwasili Bagamoyo na kutiliana mkataba na Diwani Mwinchuguuni wa kushiriki kwenye vita hiyo na Wakamba; na malipo yatafanyika baada ya kuutokomeza uvamizi ule.

Sasa, wakati Pazi akiwa Bagamoyo, mke wa Diwani Mwinchuguuni aliyekuwa mjamzito, alijifungua mtoto wa kiume na kwa heshima ya Pazi, Chifu Mwinchuguuni akampa mwanawe jina la Pazi.

Huyo akawa Pazi Mwinyimadi Mwinchuguuni; akiwa Pazi wa mwanzo kuzaliwa mwenye asili ya mwambao; ambako sasa, karne nyingi baadaye, kumetapakaa majina ya Pazi wasio na idadi!

Aidha, Pazi huyu aliyepewa jina la Pazi wa Ukutu; ndiye baba wa hayati Mzee Mussa Pazi Mwinyimadi wa Mwinchuguuni wa pale Mtaa wa Mafia namba 33, Kariakoo, Dar es Salaam.

Mtoto mkubwa wa hayati Mzee Mussa Pazi wa Kariakoo, Dar es Salaam, akiitwa Mwinyimadi, jina lilotokana na babu yake— Diwani Mwinyimadi Mwinchuguuni— aliyekuwa ‘chifu’ wa Bagamoyo.

Aidha, kijijini Bagamoyo, kabla Wakamba hawajaingia; ilitia nanga, jahazi ya kibiashara kutoka sehemu za Barawa kule Persia, ikiwa mali ya mfanyabiashara Mohammed Shari Hatimi.

Diwani Mwinchuguuni alizungumza naye awape bidhaa alizokujanazo ili mauzo yake yawape fedha za kupigania vita na Wakamba.

Kama ilivyokuwa kwa Chifu Pazi, Mohammed Shari aliridhia na aliahidiwa ujira baada ya mapigano kumalizika na tishio la Wakamba kutoweka.

Sasa, ili kumfanya atulie, Washirazi wa Bagamoyo walimwozesha mke aliyetokana na wao akiitwa Mwakazija; na akapewa eneo aanzishe biashara ya kutengeneza chumvi, aliyokuwa na ujuzi nayo. Chumvi ile akiwauzia wenyeji mpaka vijiji vya jirani.

Sasa, ndoa yake na binti wa Kibagamoyo ilimpatia mtoto aliyejulikana kama Shari Mohammed, aliyetokana na baba Mbarawa na mama Mshirazi wa Bagamoyo.

Mpaka hapo haikuwapo si tu Tanganyika, bali hata Mzizima na Dar es Salaam kulikuwa mapori tu.

Kizazi kilichofuata ndicho kilichojulikana kama wachumvi, washomvi na baadaye ikatoholewa kuwa Wamashomvi; walitokana na asili ya utengenezaji chumvi, bidhaa iliyokuwa adimu kabisa siku hizo hapa kwetu.

Vita ikapiganwa na Wakamba wavamizi wakatimuliwa kwa ustadi na mbinu za upiganaji za Chifu Pazi Kibamanduke kutoka Dutumi, kule Ukutu.

Pazi, alidai malipo yanayofanana na urefu wa mti wa Mvinje; akitaka mali ipangwe kwenda juu urefu wa mti huo.

Hakukuwa na malipo ya kipesa kama ifanyikavyo sasa.

Sasa, pamoja na kuitumia ile mali waliyopewa na Mohammed Shari kulipia vita pia; bado mti wa mvinje ukawa ni mrefu kufikika kipimo chake.

Hapakuharibika kitu; mazungumzo yakafanyika, kwamba kuanzia wakati huo, watu wa Bagamoyo, kila mwaka watakapolima na kuvuna, watenge sehemu ya mazao ijulikane kama ‘Kanda la Pazi’ (mzigo mkubwa) liwe linapelekwa Ukutu.

Kupeleka ‘Kanda la Pazi’, ilibakia kuwa sehemu ya mila na utamaduni wa Kibagamoyo kwa miaka nenda miaka rudi!
Wakati huohuo, Mohammed Shari naye akalalamika aongezewe eneo kwa sababu mali aliyoitoa vitani ilikuwa nyingi ikifananishwa na ardhi aliyopewa.

Wenyeji wakampa eneo lote la kusini ya Bagamoyo ikiwamo Winde, Mbweni, Ununio, Kunduchi, Msasani, Upanga, hadi Magogoni—Mzizima.

Mohammed Shari, sasa akijulikana kwa jina la Shomvilhaji akiwa na mwanawe Shari Mohammed, sasa akiitwa Shomvilaali; walikwenda kuweka makazi mapya eneo la Magogoni iliyokuja kuwa Mzizima baadaye.

Shari Mohammed Shomvilaali, alikuja kuwa na watoto 9 wa kiume, kwa mama tofauti; isipokuwa Tambaza na Uweje ni mama mmoja. Watoto wake wengine ni Kitembe, Kuuchimba, Uzasana, Zarara, Gungurugwa, Sagamba na Ndugumbi.

Shomvilaali na wanawe hao ndio babu na baba wa Wamashomvi wote wa Mzizima; ambao leo wametapakaa si Dar es Salaam peke yake, bali hadi sehemu za Mafia, Msumbiji, Mombasa na kwengineko. Chimbuko na asili ikibakia kule Bagamoyo hadi Magogoni Mzizima, iliyopo Ikulu.

Shomvilaali, pamoja na kujishughulisha na utengenezaji chumvi na uvuvi baharini, alibuni pia maeneo ya kulima mpunga, viazi, mihogo na matunda.

Baada ya kufariki Diwani Shomvilaali ‘Baba wa Wamashomvi’, watoto wake akina Kitembe na nduguze, kila mmoja akadai eneo lake la utawala ama udiwani.

Kwenye mgao uliofuata; Diwani ya Kitembe ikawa ni kuanzia Magogoni, Malindi mpaka Kurasini; Diwani ya Tambaza na nduguye Uweje ikawa ni Upanga yote kuanzia ilipo Shule ya Jangwani hadi darajani Salander, ikiwamo na eneo lote la Diamond Jubilee na Msikiti wa Maamur kuelekea Kisutu na viwanja vya Gymkhana.

Eneo la Kisutu, ambako ndiko alikozaliwa mwandishi huyu, liliwahi kuwa diwani ya Sheikh Mwinyikheri Akida Kitembe, ambaye alikuwa mwasisi na Imam wa Msikiti wa Mwinyikheri ambao uwepo wake ni takriban miaka 150.

Kutokana na majukumu yake ya kidini, Sheikh Mwinyikheri, alimkabidhi udiwani, mjukuu wake hayati Abdallah Saleh Tambaza wa Shomvilaali, ambaye ni baba mkubwa wa mwandishi huyu.

Upande wa Kigamboni kwenye Chuo cha Mwalimu Nyerere lilikuwa eneo la Diwani Mwinyimbegu Kitembe na maeneo ya Mjimwema hadi Mbwamaji lilienda kwa Diwani Zarara bin Shomvilaali.

Sasa, maeneo mengine kama Msasani yalikwenda kwa Diwani Kuuchimba. Magomeni Kota, kule Makanya Makaburini ni eneo alilopewa Diwani Ndugumbi Kitembe.

Kule mitaa ya Mwinyimkuu jirani na yale makaburi, alimpa hayati Mwinyimkuu Mshindo, ambaye anakuwa binamu na Ndugumbi.

Diwani Kitembe pia, alitoa eneo la kuanzia juu pale Shule ya Jangwani kuelekea jangwa la Magomeni mpaka juu kule mtaa wa Kionga, kwa binti yake Mwasemeni bint Kitembe.

Eneo hilo lilirithiwa na watoto wake hayati Mussa Pazi na dadake Mwapembe bint Pazi.

Sasa, kaburi alimozikwa Pazi Mwinyimadi Mwinchuguuni, mtoto wa Diwani Mwinchuguuni Wamwambao kutoka Bagamoyo; lipo pale mahala ambapo sasa umejengwa Msikiti wa Kionga, Magomeni.
Hali kadhalika, Kaburi la Mwapembe Binti Pazi Mwinyimadi, nalo liko mahala hapo hapo, ambako sasa ni makazi ya mjukuu wake Mzee Ibrahim Abeid Uweje Shomvilaali.

Hayati Mzee Mussa Pazi Mwinyimadi, baba wa watoto kadhaa mashuhuri wa Mzizima na Dar es Salaam, aliyekuwa mjukuu wa Diwani Mwinyimadi Mwinchuguuni wa Mwambao, alifariki mwaka 1972 akiwa na umri wa miaka 100 na ushei, alizikwa pembezoni mwa barabara ya Somanga, makaburini Ndugumbi.

Miongoni mwa watoto wake yumo Alhaji Mwinyikhamis Mussa Pazi, mudir wa Madrassa ya Nuur l’Huda na Mwenyekiti wa Wadhamini wa Masjid Mwinyikheri.

Mwengine ni hayati Mwapapo bint Mussa, ambaye ni mama mzazi wa Sheikh maarufu, Mahdi Muharram Swaleh Kitembe, Kadhi Kata ya Kariakoo, Dar es Salaam.

Kwa ufupi, hiyo ndiyo ‘silisila’ ama uzao wa Wamashomvi wa Mzizima; je, Wazaramo nao walitokea wapi?

Baada ya ile vita ya kuwafukuza Wakamba kumalizika, wale wapiganaji (mercenaries) kutoka Ukutu kwa Pazi Kibamanduke, walipata ajira mjini Bagamoyo na Mzizima kwenye shughuli za chumvi za Mohammed Shari Shomvilhaji.

Wengine walihamia kwenye miji ya Mkamba (walikofukuziwa Wakamba); na wengine walisehelea kwenye mji mingine ya uzaramuni ya sasa, kama vile Pugu, Masaki, Mkuranga, Maneromango mpaka Kisiju.

Sasa hao wahamiaji ndio walioitwa Wazaramu; kwani asili yao ni Ukutu, kule Morogoro. Kushindwa kurudi kwao baada ya vita, ndugu zao kule Ukutu wakawaita ‘wamezarama kuko’, ikiwa na maana kwa Kiluguru ama Kizaramu, kwamba wamehamia, wamesehelea, au wamebakia huko.

Kina Pazi hawa ‘waliozarama’ bila kurudi walikotoka ndio waliokuja kuzaa kina Pazi wapya, ambao sasa wameijaza miji ya Pwani na Mwambao wote.

Chifu Pazi Kilama Lukali wa Uzaramo kule Kisarawe na Masaki ya leo; ametokana na kizazi cha wahamiaji hao ‘waliozarama’ kutoka Ukutu.

Basi tukutane juma lijalo tukizidi kuwadadavua machifu na madiwani wa Kimashomvi wa Mzizima.
Alamsiki!

atambaza@yahoo.com, 0715808864
 
Asante sana mzee Mo Said, hakika nimepata elimu kubwa. Wewe ni hazina ya elimu na maarifa ya kale. Usichoke kutupa elimu
 
Mohammed Said,

..jina la timu ya basketball ya Pazi, asili yake ni haya aliyoandika Bwana Tambaza?

Tunaona pia athari ya ''Dini' katika kupoteza Historia hasa katika majina. Ni ngumu sana ku'trace' ikiwa mtu ana jina la Abdallah Hussein Mohamed au John Joseph Williams.
Ni rahisi sana kujua asili ya Mwapembe, Shomviaali, Mwinyiheri, Pazi , Tambaza n.k.

Jina la mwandishi ni Tambaza ,linanifanya niwe karibu sana na anachokieleza kuliko kama ingalikuwa Abdallah AbdulMaliki. Kila mstari wa mwandishi niilikuwa na hamu ya kujua unaofuata umebeba nini. Ni mwandishi mzuri

Leo nimejifunza kitu , kumbe hapa Dar es Salaama sisi sote ni ''Wazaramo''
Na kwamba, Wazaramo tunaowajua ni wakaazi wa Pwani si wenyeji wa Pwani na kunasibisha Uzaramo na Upwani si sahihi.
 
Tunaona pia athari ya ''Dini' katika kupoteza Historia hasa katika majina. Ni ngumu sana ku'trace' ikiwa mtu ana jina la Abdallah Hussein Mohamed au John Joseph Williams.
Ni rahisi sana kujua asili ya Mwapembe, Shomviaali, Mwinyiheri, Pazi , Tambaza n.k.

Jina la mwandishi ni Tambaza ,linanifanya niwe karibu sana na anachokieleza kuliko kama ingalikuwa Abdallah AbdulMaliki. Kila mstari wa mwandishi niilikuwa na hamu ya kujua unaofuata umebeba nini. Ni mwandishi mzuri

Leo nimejifunza kitu , kumbe hapa Dar es Salaama sisi sote ni ''Wazaramo''
Na kwamba, Wazaramo tunaowajua ni wakaazi wa Pwani si wenyeji wa Pwani na kunasibisha Uzaramo na Upwani si sahihi.
Uko sahihi sana ila Hapo utagombana na Mohamed Said anatukuza majina ya kiarabu kuliko ya asili,
 
Wakati nasoma sheria za ardhi nikakutana na warithi wa she Mbaruku na wengine wakiitwa wamashimvi,nikajiuliza wamashimvi ni akina nani? Kumbe Sasa nimefahamu ni akina nani .Asante Mzee Tambaza Asante JF.

Sent from my TECNO B1f using JamiiForums mobile app
 
Back
Top Bottom