Shairi

Mokes Junior

Member
Joined
Aug 20, 2022
Posts
7
Reaction score
0
CHINI YA MPARACHICHI.

1 Kivuli chake kitamu, mfaidi hafaidi
parachichi zake tamu, wengine wanafaidi
matunda yake ni sumu, tiba yao makuadi
Chini ya mparachichi, nadondokewa na mawe.

2 Matunda yakikomaa, mzee huwa mkali
unaweza kulemaa, ukimwambia ukweli
maisha ya ujamaa, yalishakwenda na meli
Chini ya mparachichi, nadondokewa na mawe.

3 Sifa zake naskia, matunda wakisifia
wanadai yavutia, matamu kuyabugia
mdomoni kuyatia, sijawahi ambulia
Chini ya mparachichi, nadondokewa na mawe.

4 Majaniye kudondoka, taka taka kuongeza
fagio wenye mashaka, kusafisha naumiza
maneno nayo sadaka, ukweli unajiweza
Chini ya mparachichi, nadondokewa na mawe.

5 Anajali marafiki, wanae kutudhihaki
hataki tukate keki, rafiki hababaiki
watoto twalia dhiki, lawama hazikwepeki
Chini ya mparachichi, nadondokewa na mawe.

6 Mkweli hawezi dumu, daima kumdhulumu
ukweli hatari sumu, darasa bila kalamu
kushindia vuta ndumu, daima kosa nidhamu
Chini ya mparachichi, nadondokewa na mawe.

7 Urithi wetu shakani, hatuoni ahueni
uhuru wetu shambani, unasubiri hisani
hakuna kwenda sokoni, mfadhili mlangoni
Chini ya mparachichi, nadondokewa na mawe.

8 Barafu siyo kinywaji, hata ukila hushibi
tunataabika maji, nyumbani shamba la bibi
tunashindwa pata uji, kelele zenu kinubi
Chini ya mparachichi, nadondokewa na mawe.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…