Miss Zomboko
JF-Expert Member
- May 18, 2014
- 4,564
- 9,428
Pia katika mwaka huo, Baraza litaendesha mtihani wa kidato cha Nne kwa watahiniwa 495,207 mwishoni mwa mwaka huu 2020.
Akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wiziri wa Wizara hiyo, Profesa Joyce Ndalichako Ijumaa, Aprili 23, mwaka huu alisema, Baraza hilo litaendesha upimaji wa wanafunzi darasa la nne, la saba na kidato cha pili, nne na kidato cha sita mwaka wa fedha 2020/21.
Profesa Ndalichako alisema Baraza hilo litafanya upimaji kwa wanafunzi wa darasa la nne wapatao 1,825,387 na litaendesha mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kwa watahiniwa 1,009,938 kote nchini.
Pia Baraza hilo litaendesha upimaji wa kitaifa wa kidato cha pili kwa watahiniwa 612,745. Pia litaendesha mtihani wa maarifa kwa watahiniwa 15,044 sambamba na kuendesha mitihani ya ualimu katika ngazi ya astashahada na stashahada kwa watahiniwa 8,135.
Pia litaendesha upimaji wa kitaifa wa umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa sampuli ya watahiniwa 33,350 wa darasa la pili Januari, 2021.
Vilevile, Waziri Ndalichako alisema Wizara hiyo imetoa ufadhili wa wahadhiri 620 kwa ajili ya kusoma masomo ndani na nje ya nchi.
Kati yao, wahadhiri 196 wanasoma shahada ya uzamili na wahadhiri 424 wanasoma shahada ya uzamivu kwa lengo la kuongeza idadi yao katika kutoa elimu katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu.
Pia wizara hiyo katika mkakati wa Mapinduzi ya nne ya viwanda nchini, imeanzisha mfumo wa kufundisha kozi mbalimbali katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, Chuo Cha Sayansi cha Nelson Mandela Arusha na Chuo cha Ufundi Mbeya.
Vyuo vyote hivyo vimeanzisha kozi za kuhusu mapinduzi ya viwanda ili kusukumba mbele katika kufikia azma ya kuwa nchi ya viwanda na kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.
Wakati huo huo, Profesa Ndalichako amesema, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania katika mwaka wa fedha 2020/21,itakagua Vyuo Vikuu 25 kwa lengo la kuhakiki ubora wake.
Alisema pia itafanya tathmini ya programu 200 za masomo mbalimbali katika Vyuo Vikuu nchini na kuzisajili zile zitakazokidhi vigezo na itafanya tathmini na kutambua tuzo 5,000 zilizotolewa katika vyuo vikuu nje ya nchi.
Profesa Ndalichako amesema, itaratibu udahili na kuhakiki maombi ya wanafunzi takribani 100,000 wa mwaka wa kwanza watakaoomba kudahiliwa katika vyuo vya elimu ya juu katika programu mbalimbali.
“Itaandaa miongozo ya ulinganifu kwenye programu za masomo ya Uhandisi na Sayansi ya Tiba ya Binadamu,” alisema.
Pia alisema, itafanya utafiti ili kuweza kuishauri Serikali kuhusu masuala mbalimbali yenye lengo la kufanya maboresho kwenye mfumo wa utoaji elimu ya juu nchini.
Chanzo: HabariLeo