Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ametangaza kuwa Serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan itatumia kiasi cha Shilingi Bilioni 669 kwa ajili ya ujenzi wa barabara na madaraja katika mikoa ya Lindi na Mtwara kwa lengo la kuboresha usafiri na kuifungua mikoa hiyo kiuchumi.
Akizungumza mkoani Mtwara, Ulega alisema barabara na madaraja hayo yatajengwa kupitia barabara za Mtwara –Mingoyo (Mnazi mmoja)-Masasi (km 201) itakayogharimu kiasi cha shilingi bilioni 401 huku barabara nyingine ya Mtwara Tandahimba-Newala-Masasi itagharimu kiasi cha shilingi bilioni 268 hadi kukamilika kwake.
Waziri Ulega amewaambia wananchi wa Mtwara kwamba kiasi hicho kikubwa cha fedha katika ujenzi wa miundombinu hiyo unaonyesha dhamira ya dhati aliyonayo Rais Samia kwa wananchi wa Mikoa ya Kusini na lengo kubwa ni kuhakikisha inafunguka kiuchumi na kuwapa wananchi fursa za kiuchumi.
“Wananchi wa mikoa ya Kusini, ninawaletea salamu hizi za Rais wenu Samia Suluhu Hassan. Hizi barabara zikikamilika kutakuwa na taa za barabarani takribani 4800 kutoka Mtwara hadi Masasi. Kusini kutang’ara kwa mwanga nyakati za usiku na kutapendeza. Kwenye barabara nzuri, uchumi unafunguka na kwenye mwanga kwa saa 24, biashara zinafanyika muda wote,”alisema Ulega.
Ulega yuko katika ziara ya kikazi mkoani Mtwara ambapo pamoja na mambo mengine anafuatilia maagizo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kuangalia maendeleo ya ukarabati wa barabara na miundombinu mingine ya ujenzi iliyoharibiwa wakati wa mvua za masika na kimbunga cha Hidaya kuanzia mwishoni mwa mwaka jana hadi mwaka huu.
Akitoa mchanganuo, Ulega alisema katika kiasi hicho cha fedha, zaidi ya shilingi bilioni 230 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Mnivata - Newala - Masasi (km 160) kwa kiwango cha lami pamoja na Daraja la Mwiti (m 84) ili kuzifungua Wilaya za Masasi, Newala, Tandahimba na Mtwara kiuchumi kupitia usafirishaji wa abiria na mazao.
Ulega amewataka Makandarasi wanaojenga barabara ya Mnivata-Masasi kuhakikisha wanatoa kipaumbele cha ajira kwa wananchi wazawa wa maeneo barabara inakopita kwa kushirikisha ofisi za Serikali za Mtaa na Kata za Wilaya.