Serikali yaitibua UN kuhusu uchimbaji wa uranium | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Serikali yaitibua UN kuhusu uchimbaji wa uranium

Discussion in 'Major Projects in Tanzania' started by Zak Malang, Jun 19, 2010.

 1. Zak Malang

  Zak Malang JF-Expert Member

  #1
  Jun 19, 2010
  Joined: Dec 30, 2008
  Messages: 5,410
  Likes Received: 18
  Trophy Points: 0


  Serikali yaitibua UN

  Na Ezekiel Kamwaga


  SERIKALI iko hatarini kuingia kwenye mgogoro na Umoja wa Mataifa (UN) kutokana na kuruhusu uchimbaji madini ya uranium kwenye pori tengefu la Selous.

  Taarifa za kuaminika zinasema tayari serikali imetoa kibali kwa kampuni ya Mantra Resources ya Australia kutafuta madini ya uranium katika eneo hilo.

  Madini ya uranium ni muhimu kwa uzalishaji wa nishati ya umeme na utengenezaji silaha za nyuklia na tayari yamethibitika kuwepo katika mbuga za Selous.

  Taarifa zilizopo zinaonyesha serikali ilitoa kibali cha kutafuta madini hayo mwaka 2006, hatua inayotarajiwa kuzua mgogoro kwa ngazi ya kimataifa.

  UNESCO imepiga marufuku kufanyika kwa shughuli yoyote inayoweza kuathiri mazingira au viumbe hai vilivyopo katika maeneo ambayo yametangazwa kuwa ya kihistoria.

  Eneo la Selous ambalo pia lina mbuga ya wanyama liko katika mikoa ya Pwani, Mtwara na Ruvuma ambako wanapatikana tembo wa kijivu, mamba, aina adimu za nyoka na uoto wa asili wa aina ya kipekee.

  Kutokana na utajiri huo wa wanyama na viumbe anuai na ambavyo ni adimu, shirika la UN la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), lilitangaza eneo hilo kuwa urithi maalum wa dunia (World Heritage Sites).

  Tangazo hilo la UNESCO lilifanywa mwaka 1982 kwa lengo la kuhifadhi utajiri huo kwa vizazi vijavyo.

  Kwa mujibu wa taarifa za Mantra Resources kutoka kwenye tovuti (website) yake, eneo la Selous ni sehemu ya mradi wake mkubwa uliopewa jina la “Mkuju River Project.”

  Mradi wa Mkuju unakadiriwa kuwa na tani milioni 82.3 za uranium na imeelezwa kuwa uchimbaji wake unaweza kuchukua zaidi ya miaka kumi.

  Eneo zima la mradi wa Mkuju, lililoko kusini mwa Tanzania, lina ukubwa wa kilometa za mraba 3,325.

  MwanaHALISI lina nyaraka mbalimbali, zikiwamo barua zinazoonyesha kuwa Mantra Resources ilikabidhiwa kibali cha kutafuta madini hayo katika eneo tengefu.

  Hata hivyo, baadhi ya waliokuwa viongozi serikalini wakati kampuni hiyo ya kigeni ikipewa mradi, wamekana kufahamu chochote kuhusu ruhusa hiyo ya serikali.

  Kwa mujibu wa barua ya tarehe 12 Mei 2006, serikali iliiruhusu kampuni ya Mantra kuanza mara moja shughuli za utafutaji madini ndani ya pori hilo.

  Barua ya serikali kwenda Mantra yenye Kumb. Na. GD/F.40/4/96 inaitaka kampuni hiyo kutumia njia za kisasa kufanya kazi hiyo.

  Barua ilisainiwa na aliyekuwa katibu mkuu wa wizara ya Maliasili na Utalii, Saleh Pamba.
  Bali Athony Diallo, aliyekuwa waziri wakati Pamba anasaini barua hiyo, amekana kufahamu chochote juu ya barua hiyo ya Pamba.

  “Sifahamu chochote katika hilo. Kwanza, sikuwahi kuiona barua hii, sikushiriki katika maamuzi ya kuruhusu uchimbaji na wala sikumbuki kama niliwahi kupeleka suala hili katika baraza la mawaziri kwa ajili ya kupata baraka za serikali,” anasema Diallo katika mahojiano na gazeti hili.

  Majibu ya Diallo yalitokana na gazeti hili kumuoyesha barua inayodaiwa kuandikwa na Pamba.
  Kwa upande wake, Pamba alisema hakumbuki ni nini hasa aliandika kwenye barua ya kuiruhusu kampuni hiyo kufanya shughuli za uchimbaji wa uranium.

  “Unasema barua hiyo niliandika mwaka 2006; sasa unajua mimi nilikuwa katibu mkuu wa wizara na niliandika barua nyingi sana; siwezi kukumbuka kila nilichoandika.,” anaeleza Pamba.

  Hata hivyo, amesema ni Wizara ya Nishati na Madini yenye kazi ya kutoa kibali iwapo kampuni ya madini inataka kufanya shughuli za utafutaji madini hapa nchini.

  “Sasa, kama wizara ya nishati na madini, ambayo nayo ni serikali pia, ilikuwa tayari imewaruhusu hao watu (Mantra) kufanya shughuli za utafutaji madini, mimi ni nani hata nikatae?” ameuliza kwa njia sahihi ya kukiri.

  “Inawezekana waziri hakuona barua hiyo, lakini si kila barua ambayo inapita ofisini kwangu ni lzima pia ipite kwa waziri. Waziri si mtendaji wa kila siku wa shughuli za wizara.

  “Kama suala lina sura au athari za kisiasa kwa wizara, hapo ni lazima waziri angekuwa amehusishwa, lakini si kila kitu waziri atakijua kuhusu wizara,” ameeleza Pamba.

  Madini ya urani hufahamika kwa utoaji wa miale ya Alpha, Beta na Gamma, ambayo imeelezwa kuwa hatari kwa viumbe hai.

  Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya habari ikiwamo wavuti (internet), hakuna hatari yoyote kwa mazingira ya eneo husika wakati wa shughuli za utafutaji wa madini ya uranium kama ilivyofanyika sasa katika eneo hilo.

  Hata hivyo, wizara ya nishati na madini imekiri katika taarifa yake kwa vyombo vya habari mwaka jana kwamba uchimbaji na uchakatuaji wa madini huwa na hatari kwa mazingira.

  Mfano unaotolewa zaidi kuhusu hatari ya uchimbaji wa urani unahusu tukio lililotokea nchini Marekani mwaka 1950 ambapo mamia ya wananchi wa kabila la Navajo katika maeneo ya Utah, Colorado, New Mexico na Arizona walipata magonjwa ya kansa kwa sababu ya mionzi iliyotokana na uchimbaji urani.

  Walipata magonjwa mbalimbali kutokana na uchimbaji wa urani uliofanyika katika eneo hilo.

  Akizungumza na gazeti hili wiki hii, Mkurugenzi wa Habari Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC), Anna Maembe, amesema hana taarifa iwapo ukaguzi wa kitaalamu wa kimazingira (Environmental Impact Assesment) kuhusu mradi huo umekwishafanyika.

  Amesema kawaida, NEMC haifanyi uchunguzi wa athari za kimazingira wa mradi wowote, isipokuwa hutoa kazi hiyo kwa washauri wa kitaaalamu waliosajiliwa kwa kazi hiyo na wao (baraza) hutoa mapendekezo kwa serikalini baada ya kuona ripoti ya wataalamu.

  Katika mazungumzo yake kwa simu na gazeti hili, Ofisa Habari wa UNESCO hapa nchini, Aliamini Yusuph, alisema kabla serikali ya nchi yoyote haijafanya uamuzi wa kufanya lolote kuhusiana na eneo kama Selous, ni lazima itoe taarifa kwa shirika lake.

  “UNESCO inatambua kwamba Selous iko ndani ya Tanzania na kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa, serikali za nchi zenye maeneo haya zina mamlaka yote juu yake,” amesema.

  Hata hivyo, ofisa huyo ameomba kupatiwa muda zaidi kufanya utafiti kuhusu suala hili la Tanzania, ikiwamo kuwasiliana moja kwa moja na wanaohusika na mambo ya hifadhi za maeneo maalumu ndani ya UNESCO.

  Kwa mujibu wa taarifa za kimtandao, mwaka jana pekee kiasi cha tani 50,572 za uranium zilivunwa duniani kote huku asilimia 27 ya kiasi hicho ikitoka nchini Kazakhstan pekee.

  Kazakhstan, Canada na Australia ndiyo wazalishaji wakuu wa uranium duniani.

  Mbali na Selous, Tanzania imeripotiwa kugundua madini ya uranium katika mikoa ya kati.

  Chanzo: Mwanahalisi.
   
 2. Felixonfellix

  Felixonfellix JF-Expert Member

  #2
  Jun 19, 2010
  Joined: Feb 16, 2010
  Messages: 1,680
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 135
  in touble again
   
Loading...