Serikali sasa iwalipe walimu madai yao

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,318
33,125
maoni%20ya%20katuni%20june%207.jpg


Towa Maoni ya Katuni

Mvutano baina ya serikali na walimu nchini unaelekea kuibuka upya kutokana na serikali kutoa ahadi za uda mrefu zisizotekelezeka za kuwalipa walimu malimbikizo ya madai yao.


Walimu wamekuwa wakidai stahiki zao kwa muda mrefu kiasi kwamba hali hiyo imekuwa ikiibua mvutano baina yao na serikali. Hata hivyo, kwa muda mrefu walimu walijaribu kuepusha shari kutokana na viongozi wao kuahirisha migomo ambayo walikuwa wanatangaza kuiitisha kama njia ya kuishinikiza serikali kuwalipa.


Hali hiyo iliifanya serikali takribani miaka miwili iliyopita kufanya uhakiki wa madai ya walimu na kuahidi kwamba ingewalipa walimu malipo yao yote mwishoni mwa mwaka jana, lakini ahadi hiyo imeshindikana kutekelezwa.


Baada ya kushindikana, walimu walitishia kugoma Januari mwaka huu, lakini baadaye walilazimika kuusitisha mgomo huo ili kuepuka usumbufu pamoja na athari ambazo zingeweza kutokea wakati wa kufungua shule.


Kutokana na hali hiyo, juzi Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kilitangaza mgogoro mwingine na serikali na kutoa siku 30 ilipe madai yao, vinginevyo watagoma nchi nzima.


Mgogoro huo ulitangazwa na Rais wa CWT, Gratian Mukoba alipokuwa akifungua mkutano wa dharura wa Baraza Kuu la CWT lililofanyika mjini Dodoma..


Mukoba alisema serikali inatakiwa kutimiza mambo mbalimbali ya walimu mojawapo likiwa ni pamoja na mishahara ya walimu kuongezwa kwa asilimia 100 ya mshahara wa sasa.


Alisema pia serikali inatakiwa kuongeza posho kwa walimu ya kufundisha masomo ya sayansi iwe ya asilimia 55 ya mshahara wa kila mwezi.


Pia walimu wanataka posho ya kufundisha masomo ya sanaa ipandishwe kwa asilimia 50 ya mshahara wa kila mwezi na kwamba walimu wanaofundisha kwenye maeneo yanayotambulisha kuwa ni ya mazingira magumu walipwe posho ya mazingira magumu kwa asilimia 30 ya mshahara wao wa kila mwezi.


Chama hicho kinataka malipo hayo kwa walimu yaanze kutolewa Julai mwaka huu.


Kutokana na walimu kuonyesha uvumilivu kwa muda mrefu wa kudai malipo yao ikiwa ni pamoja na kusitisha migomo ambayo wamekuwa wakiiandaa, serikali kwa upande wake ilipaswa kuhakikisha kwamba inatekeleza ahadi yake ya kuwalipa.


Kwa kuwa serikali ilishafanya uhakiki wa kuwalipa walimu hao basi ingehakikisha kwamba yale madai yote halali inayalipa haraka kama ilivyowahidi walimu.


Kibaya zaidi ni kwamba hata malipo ya awali baadhi ya walimu katika mikoa kadhaa nchini wamelalamika kulipwa kiasi kidogo huku wakipewa maelezo yasiyoridhisha kutoka katika halmashauri husika.


Madai ya walimu ya kupandishiwa mishahara na viwango vya posho ni ya msingi kutokana na kupanda kwa hali ya maisha pamoja na mazingira magumu ambayo walimu wanafanyia kazi.


Sekta ya elimu hivi sasa inakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na mambo mbalimbali yanayotokea yakiwemo kushuka kwa kiwango cha elimu katika shule za msingi na sekondari kutokana na wanafunzi katika shule za serikali kufeli mitihani.


Shule zetu nyingi hazina walimu kutokana na mazingira mabaya ya kufundishia, mishahara midogo; ukosefu wa nyumba za walimu, madarasa, madawati, vitabu nakadhalika.


Hali hii inachangia walimu kukimbilia kufundisha katika shule binafsi ambazo zinawalipa walimu vizuri pamoja na mazingira ya kufundishia kuwa ya kuridhisha. Kutokana na hali hii, serikali ilipaswa kuhakikisha kwamba inawajengea walimu mazingira mazuri ili wavutiwe kufundisha katika shule za serikali.


Tutakuwa tunajidanganya kusemaserikali inachukua hatua za kuboresha elimu nchini kama walimu ambao ndio wadau muhimu katika elimu wataendelea kunyimwa haki zao.


Ushauri kwa serikali ni kwamba sasa ichukue hatua za haraka za kulipa madai ya walimu ili kuondoa mvutano usio na tija ambao baadaye unaweza kuzua mgomo na kuwaathiri wasiohusika.


Kwa kuwa suala hili limezuka upya wakati huu ambao serikali inaamdaa bajeti ya mwaka 2012/13, ni bora bajeti hiyo ikajumuisha fedha za madai ya walimu ili suala hilo limalizike kabisa.


Ni vizuri wizara zainazohusika zikaketi pamoja na kupanga mikakati ya kumaliza tatizo hilo ili kuwarejeshea walimu ari ya kufundisha watoto wetu.







CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom