BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,790
- 288,088
Serikali nzima kitanzini |
Tuesday, 19 July 2011 21:11 |
Neville Meena, Dodoma Mwananchi WAKATI umma wa Watanzania ukisubiri hatua zitakazochukuliwa na Rais Jakaya Kikwete dhidi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC) inakusudia kuchukua hatua za kufuatilia fedha zote zilizotolewa na mashirika ya umma kwa kigezo cha kusaidia kupitisha bajeti. Habari ambazo Mwananchi lilizipata jana na kuthibitishwa na Mwenyekiti wa POAC, Zitto Kabwe zinasema kwamba hatua hiyo inalenga kubaini kiasi cha fedha ambacho Wizara za Serikali zimekuwa zikidai kutoka katika idara na taasisi zilizoko chini yake kwa kigezo kwamba fedha hizo zinatakiwa kusadia kupitisha bajeti. Akithibitisha taarifa hizo, Zitto alisema; "Tunapaswa kufanya uchunguzi ili kubaini kiasi cha fedha za umma ambazo zimetumika katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, maana kuna uwezekano kwamba huu ndio mchezo ambao umekuwa ukifanywa na wizara zetu hizi". Tuhuma zinazomkabili Jairo Jairo anakabiliwa na tuhuma za kuwaandikia barua wakuu wa idara zote zilizoko chini ya wizara yake, ili watoe fedha kwa ajili ya kusaidia kupitishwa kwa bajeti ya wizara hiyo, fedha ambazo zinatafsiriwa kwamba zilikuwa ni kwa lengo la kutoa rushwa. Mbunge wa Kilindi (CCM), Beatrice Shellukindo ndiye aliyemlipua Jairo Bungeni juzi kwamba amekusanya kiasi cha Sh1 bilioni kutoka taasisi 21 zilizopo chini ya Wizara yake na kwamba fedha hizo hazina maelezo. Shellukindo aliendelea kusema kuwa barua hiyo inaonyesha kuwa kila idara na taasisi hizo ziliagizwa kuingiza kiasi cha Sh50 milioni kila moja kwenye akaunti namba 5051000068 inayomilikiwa na Geological Survey of Tanzania (GST) (Taasisi ya Utafiti wa Jiojia) iliyopo kwenye benki ya NMB, tawi la Dodoma. Taarifa ambazo Mwananchi ilizipata bungeni juzi zilidai kwamba mara baada ya Shellukindo kurusha kombora hilo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliagiza kutafutwa kwa taarifa za akaunti husika, na kwamba katika muda mfupi ilithibika kwamba fedha hizo ziliingizwa kisha kutolewa. Hata hivyo haikiwekwa bayana kiasi halisi cha fedha zilizoingizwa na idara hizo na siku ambayo zilichukuliwa. Akizungumza wakati wa kuondoa hotuba ya makadirio ya Wizara ya Nishati na Madini bungeni juzi jioni baada ya bajeti hiyo kukataliwa na wabunge, Pinda alisema alikuwa akifanya utaratibu wa kuwasiliana na Rais Kikwete aliyekuwa safarini Afrika Kusini ili kupata ridhaa ya kuchukua hatua dhidi ya Jairo. "Kikwazo pekee nilichokipata ni kwa sababu Rais hajatua South Africa (Afrika Kusini) na mwenye mamlaka ya kuteua Makatibu Wakuu ni Rais mwenyewe. Nikatamani sana nije hapa mimi niwaambieni nimeishachukua hatua, nimeamua hivi. Lakini, nikaambiwa utakuwa unaingia katika maeneo ambayo si ya kwako,"alisema Pinda na kuongeza: "......kwa hiyo, kwa hili, naomba niwaombe Waheshimiwa Wabunge, kwa dhati kabisa, kwamba kwa sababu sina mamlaka juu ya mtu huyu ya kumtimua kazi leo au kumwambia ondoka, mwenye mamlaka ni Rais mwenyewe, kwa hili mnipe baraka zenu, akifika South Africa, jioni ya leo mimi nitawasilisha maelezo haya kwake". Kwa mujibu wa Pinda, tuhuma dhidi ya Jairo si jambo ambalo halina maelezo kwani liko dokezo lililioloandikwa na kusomwa bungeni ambalo linathibitisha kwamba Katibu huyo wa zamani wa Rais Kikwete ana hatia. Ngeleja amruka Jairo Habari zaidi zilizopatikana jana mjini Dodoma zilidai kwamba Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja alikanusha vikali kufahamu chochote kuhusu utekelezaji wa mpango huo wa wizara yake kukusanya fedha hizo kwa ajili ya kuwezesha upitishaji wa bajeti. Habari za uhakika kutoka ndani ya kikao cha Kamati ya Wabunge wa CCM kilichofanyika juzi mchana zinadai kwamba kauli ya Ngeleja kwamba hafahamu chochote, zilifuatia hoja iliyotolewa na Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka akitaka Waziri huyo kujiuzulu. "Alisema haiwezekani Waziri asifahamu kuhusu mpango huu wa ukusanyaji wa fedha, wala haiingiii akilini kwamba hajui chochote, mimi nadhani wakati tukitaka Katibu Mkuu afukuzwe ifikapo leo saa 11 jioni, basi hata waziri naye aachie ngazi,"chanzo chetu kilimnukuu Ole Sendeka. Gazeti hili lilipomtafuta mbunge huyo wa Simanjiro kuhusu taarifa hizo, hakukanusha wala kukubali zaidi ya kusema kuwa: "hayo yalikuwa ni mambo ya ndani ya chama na waziri mkuu alishatoa msimamo wa Serikali, mimi sina lolote la kuongeza". Kwa upande wake Ngeleja aliliambia Mwananchi kuwa hawezi kuzungumza chochote kuhusu suala la Katibu Mkuu wake kwani tayari lilikuwa limechukuliwa na viongozi waandamizi wa Serikali kwa ajili ya kulifanyia kazi. Habari kutoka ndani ya kikao cha kamati ya wabunge wa CCM zinasema kuwa wabunge hao walikuwa wametoa muda kwa Serikali kwamba hadi saa 11 jioni juzi Jairo awe amefukuzwa kazi. Kwa mujibu wa habari hizo, wabunge hao pia waliitaka Serikali kuielekeza Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru) kuaza uchunguzi wa jinsi fedha hizo zilivyotolewa na matumizi yake, ili ikibainika vinginevyo wahusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria. Kashfa rushwa Nishati Wiki mbili zilizopita, gazeti hili liliporipoti kuhusu jaribio la maofisa wa wizara hiyo kutaka kuwahonga baadhi ya wabunge katika Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kwa kile kilichodaiwa kutaka bajeti ya wizara hiyo kupita kwa urahisi. Jumatatu, Julai 4, 2011 Mwananchi lilinukuu vyanzo vyake mjini Dodoma na Dar es Salaam vikibainisha kuwa taarifa za uovu zilifikishwa mezani kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye alinukuliwa akisema kuwa angezishughulikia baada ya kuwa amewasiliana na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja. Kwa mujibu wa habari hizo suala hilo pia lilifikishwa kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda na kwamba Kamati ya Uongozi ya Bunge anayoiongoza pia iliarifiwa kuhusu suala hilo. Waziri Mkuu, Pinda alipozungumza na Mwananchi alikiri kupata taarifa za tuhuma hizo japokuwa halikuwa limefikishwa rasmi kwake. Habari zilizolifikia Mwananchi zilidai kwamba, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Makamba ndiye aliyewashtaki wajumbe wa kamati yake kwa Spika huku akiwachongea watumishi wa Wizara ya Nishati na Madini kwa Pinda kutokana na kujihusisha na vitendo vya rushwa. http://reddit.com/ |