SoC03 Serikali iruhusu matumizi ya simu na kompyuta kwa wanafunzi wa ngazi zote katika ulimwengu huu wa digitali

Stories of Change - 2023 Competition

Nengay

Member
Aug 26, 2022
39
65
Kasi ya ukuaji wa sayansi na teknolojia imepelekea shughuli mbalimbali za kijamii, uzalishaji na mawasiliano kufanyika kidigitali zaidi kupitia mitandao ya kijamii. Dhana ya mitandao ya kijamii na haki za kidigitai inahusisha moja kwa moja matumizi ya vifaa vya kielektroniki kama vile simu, saa ya mkononi ya kisasa, kishikwambi na kompyuta.

Andiko hili fupi linalenga kuangazia mchango wa ukuaji wa teknolojia na matumizi ya vifaa vya kielektroniki katika jamii zetu na kuunga mkono harakati za kutengeneza wataalamu wenye tija na mchango katika taifa.

Haki za kidigitali na matumizi ya mitandao ya kijamii kwa watoto yametazamwa katika upande hasi zaidi katika nchi za kiafrika jambo linalopelekea watoto kukosa haki ya kutumia vifaa vya kielektroniki kupata taarifa mbalimbali muhimu pamoja na kujifunza kitaalamu zaidi.

Ukilinganisha na mataifa yaliyoendelea duniani, Watoto/wanafunzi wa kitanzania wanaosoma kuanzia shule za msingi mpaka kidato cha sita hawaruhusiwi kutumia simu au kompyuta wakiwa shuleni na hata nyumbani.

Ambapo Walimu, wazazi/walezi na wadau wa elimu wanaamini matumizi ya vifaa hivi vinaharibu maadili na kusababisha changamoto kwenye malezi kutokana na maudhui yanapatikana katika mitandao, hivyo baadhi ya shule na vyuo zina sera ya kuweka vizuizi kwenye matumizi ya simu za mkononi kwenye masomo, kuzima simu wakati wa masomo, au kuhifadhi simu kwenye chumba cha maegesho.

Wazazi na walimu wanatakiwa kuelewa kasi ya ukuaji wa teknolojia ni kubwa na hatuwezi kushindana nayo zaidi ya kutengeneza mazingira ya kuendana nayo. Vizuizi na sheria zilizowekwa sio suluhisho kwani havijaweza kumdhibiti mtoto kutotumia simu wengi wanatumia kwa siri na kupata maudhui machafu zaidi kutokana na kua na uhuru bila usimamizi.

Mpango wa taifa wa miaka mitano 2022/2026 "Katika kipengele cha kukuza ujuzi tathmini ya soko la ajira iliyofanywa na na tume ya mipango ya mwaka 2014 kuhusu maendeleo ya ujuzi utakaowezesha Tanzania kuwa na uchumi imara na shindani ifikapo mwaka 2025, inabainisha umuhimu wa kutatua changamoto kati ya ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na ujuzi unaotolewa na taasisi za elimu na mafunzo ambapo tathmini hiyo ilibainisha kuwa viwango vya ujuzi vya watafuta ajira viko chini ya kiwango kinachohitajika na waajiri" ambapo katika kipengele kidogo cha kwanza kinadai uendelezaji wa elimu kuanzia ngazi ya awali ili kuandaa vijana kwa ajili ya elimu ya juu na utengenezaji wa watu wanaoweza kujiajiri. Tathmini ya mpango huu haijaainisha wala kudokeza matumizi ya vifaa vya kidigitali katika utekelezaji wake jambo ambalo litakwamisha Uzalishaji wa watu wenye ushindani.


Njia za usimamizi.
Katika vifaa vya kielektroniki kuna sehemu inayotoa nafasi (option) kwa mzazi/ mlezi kusimamia kifaa cha mtoto wakati wote, Kwenye simu sehemu hiyo (option) inaitwa "parental controls" inayopatikana (goggle).Kuna njia nyingi za kidigitali ambazo zinaweza kutumika kusimamia matumizi sahihi ya vifaa vya kielektroniki kwa watoto, kama vile;

• Matumizi ya Google Family Link na Ourpact hizi programu zinazosaidia kudhibiti matumizi ya vifaa vya kielektroniki. Ambayo inatoa nafasi ya kuweka vikomo vya muda wa kutumia kifaa, kufuatilia matumizi ya vifaa vya watoto, kuzuia maudhui yasiyofaa na kufunga kifaa cha mtoto kila inapohitajika.

• Google Family Link, screen time na Amazon Free time; Programu hizi husaidia kuweka vikwazo vya umri pamoja na kuunda wasifu wa mtoto kwa ajili ya kuchuja maudhui yaliyomo kwenye mitandao ya kijamii ambayo sio rafiki kwa mtoto.Hii itasaidia kuwalinda watoto kuepukana na maudhui yasiyofaa kama vile picha na video za ngono na lugha chafu.

Pia Programu kama Bark na Net Nanny zinaweza kusaidia kusimamia mawasiliano ya watoto kwenye mitandao ya kijamii na barua pepe, na kuhakikisha masuala ya kiusalama.Hii inasaidia kuzuia mawasiliano na watu wasiowafaa.Kumbuka kwamba njia moja haiwezi kufaa kwa kila familia. Unapaswa kutumia njia ambayo inafaa kwa familia yako na kuzingatia mahitaji na umri wa watoto wako.

Faida au kwanini haki za kidigitali ni muhimu kwa watoto.

• Matumizi ya vifaa vya kielektroniki

kwa watoto yana faida ikiwa yatatumika kwa usahihi na chini ya usimamizi wa mzuri, ambapo yatasaidia kuongeza ufahamu na uelewa, Watoto wanaweza kujifunza mambo mengi kutoka kwenye mitandao ikiwa ni pamoja na elimu, lugha, muziki, na mambo mengine ya kuvutia.

• Yatasaidia Kupata ufahamu na uelewa kuhusu mambo mbalimbali ya kielimu na kijamii: Uhamasishaji wa maswala ya maendeleo, utunzaji wa mazingira, maadili mema, tamaduni na asili za jamii husika , maswala ya lishe bora na afya huelezewa zaidi katika mitandao kwa sasa ukilinganisha na vyombo vingine vya habari kutokana na urahisi wa kufikia watu wengi kwa kasi zaidi.

• Pia yatasaidia kutoa ujuzi na uwezeshaji wa kidigitali, inaongeza ubunifu na kukuza stadi: Vifaa vya kielektroniki kama vile kompyuta na simu za mkononi zinaweza kusaidia kuongeza ubunifu wa watoto, Kwa mfano, watoto wanaweza kujifunza kubuni programu, michezo ya video, lakini pia inachangia Kukuza stadi za kijamii na kiakili, kama vile stadi za lugha, ujuzi wa kusikiliza, ujuzi wa kuhesabu, na ujuzi wa kuandika.

• Vilevile yatasaidia kuhakikisha usalama, ustawi, faragha na ulinzi wa taarifa binafsi; Taarifa binafsi na faragha za watoto ni muhimu na lazima zilindwe. Haki za kidijitali huhakikisha kwamba watoto wana udhibiti wa data zao za kibinafsi na wanalindwa dhidi ya mazoea ya kukusanya data. Hii ni pamoja na kupata idhini ya matumizi ya data, kuzuia uhifadhi wa data, na kutoa mbinu za kukagua na kufuta maelezo ya kibinafsi. Ni wajibu wa serikali, wazazi na wadau wa elimu kudumisha na kuendeleza haki hizi, kuunda sera na desturi zinazolinda na kuwawezesha watoto katika ulimwengu wa kidijitali.

Mchango katika siasa

Suala la utawala bora na uwajibikaji unaochochewa na uelewa mpana wa raia juu ya kila hatua na utendaji wa viongozi wao katika nafasi mbalimbali. Watoto wana haki ya kujua nini kinaendelea katika jamii yetu viongozi ni kina nani na wana wajibu upi, mataifa mengi yenye uwezo wa kuwajibisha viongozi wao wamekuwa na desturi nzuri ya kutengeneza jamii ya watu wenye kujua dira na mwelekeo mzuri wa maisha tangu wakiwa watoto wadogo.

Siasa inagusa maisha ya kila mtu mtoto, kijana na mzee katika nyanja zote kiuchumi, kijamii na kiutamaduni, siasa ndio inayotoa muelekeo na usimamizi wa mifumo yote kama vile elimu, afya na huduma zingine za kijamii, hii ndio maana halisi ya kutengeneza wataalamu wenye mchango kwenye nyanja zote.
 
Back
Top Bottom