Rutashubanyuma
JF-Expert Member
- Sep 24, 2010
- 219,470
- 911,174
Serikali inaumwa, inajimwaga Loliondo
Josephat Isango
Josephat Isango
Ingekuwa ujinga unatibika katika dawa za Loliondo, basi serikali ilipaswa kuwapanga watendaji wake wote watibiwe akili ili waweze kufikiri sawasawa.
Suala la ujinga ni hali ya kutokujua, na linasababiswa na uzembe wa kufikiri. Viongozi wengi wa serikali, tena viongozi wakubwa nao ni wazembe wa kufikiri. Wanakubali majibu yanayotolewa na msemaji wa kwanza bila kujiuliza kwanini mtu huyu kasema hivi na si vile.
Suala la tiba ya Loliondo limekuwa gumzo sana katika nchi yetu kwa siku za karibuni. Katika makala haya sitajihusisha kusema kuwa tiba hiyo ni halali au si halali, inatibu au haitibu, isipokuwa ninajikita zaidi katika kauli ya serikali iliyotolewa kuwa dawa hiyo haina madhara.
Serikali haikuona aibu, na wataalamu waliotumwa hawakufikirishwa vichwa vyao, wakalipeleka suala hili kisiasa, akili zao zikasitisha mkataba wa kufikiri, wakafikiri kinyume na hawakugundua mpaka sasa kuwa wamewahadaa watanzania. Kweli Tanzania bado tuna safari ndefu sana.
Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania, KKKT, alisema hadharani wala hakusema kwa siri kuwa dawa yake imepata uponyaji wa kimungu.
Ni neno la Mungu ndilo linatibu. Tena akaeleza kuwa dawa yenyewe ameoteshwa katika ndoto na Mungu, hivyo akakiri kuwa dawa yake ni tofauti na dawa nyingine kwani dawa nyingine mgunduzi ni mwanadamu na zimefanyiwa utafiti.
Lakini hii ya Loliondo ni ya neno la Mungu lililomjia katika ndoto. Serikali yetu isiyofikiri sawa sawa, na watendaji wake wasio makini, wanaopendelea kufanya siasa katika kila kitu, wakakurupuka, wakaunda timu kwa ajili ya kufanya utafiti.
Serikali yetu mara kadhaa imekiri hadharani kuwa yenyewe haina dini, vipi kwa suala la Loliondo ambalo linaonekana kuwa chimbuko lake ni dini wamekuwa tayari kutoa ushirikiano kwa kila hali?
Tunukuu kauli ya serikali na wataalamu wake. Serikali imesema imeridhishwa na dawa inayotolewa na Mchungaji Ambilikile Mwasapile wa Kijiji cha Samunge, Loliondo ikisema haina madhara yoyote kwa matumizi ya binadamu.
Akitoa tamko la timu ya wanasayansi waliofanya uchunguzi wa awali wa tiba hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Charys Ugullum, alisema timu hiyo ilianza utafiti wake wa awali Machi 7, mwaka huu.
Alisema timu hiyo ilijumuisha wataalamu kutoka Wizara ya Afya, TFDA, Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Mkemia Mkuu wa Serikali na Taasisi ya Utafiti wa Dawa za Asili ya Chuo Kikuu cha Afya ya Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).
Serikali yetu imenukuliwa ikisema imeridhishwa na dawa inayotolewa na Mchungaji Mwasapile wa Kijiji cha Samunge, Loliondo tena haina madhara yoyote kwa matumizi ya binadamu.
Katika suala hili kwanza serikali imechelewa kutoa tamko, kama dawa hiyo ingekuwa na madhara kwa wanadamu wangapi wangeathirka, na kwanini serikali ilisubiri muda mrefu wote mpaka karibu viongozi wote wa serikali wamekunywa ndipo inatoa tamko. Ni uzembe au kutokuwa makini?
Tamko la timu ya wanasayansi waliofanya uchunguzi wa awali wa tiba hiyo, lilisemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Charys Ugullum, kuwa ilianza utafiti wake wa awali Machi 7, mwaka huu.
Hivi wasomi hawa wote hawakufikiri hata mara moja kuwa ni ujinga kupima kitu kilichosemwa ni neno la Mungu kwa kutumia vifaa vya maabara?
Tangu lini na wapi ndoto zinapimwa kwa kutumia vifaa vya maabara, Mkemia Mkuu anajua nini kuhusu Elimu ya ndoto?
Dawa inayosemekana inatoka kwa Mungu, inayolingana dozi kwa kila ugonjwa, inayohusisha imani kabisa bila nguvu za kisayansi, kweli serikali ilipaswa kutenga pesa kutafiti kama neno la Mungu linatibu?
Serikali yenyewe ingemwona wapi Mungu na kuuliza nguvu ya uponyaji ya huo mti uliokuwepo katika mazingira hayo kila siku?
Serikali bila aibu inasema, tena kinachofuata sasa tutachunguza kama kweli dawa hiyo inatibu magonjwa hayo matano aliyoyasema Babu. Hivyo wananchi wawe na subira ili watupe nafasi tufanye utafiti wa kina zaidi. Je, ikitokea kuwa dawa hiyo haitibu watachukua hatua gani?
Serikali ikaamua kujiingiza kisiasa, tena kichwa kichwa kuzungumzia suala la hatimiliki, Mkurugenzi wa Uendelezaji na Uratibu Utafiti kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia, Dk. Rose Kingamkono akasema wanafuatilia ili waweze kujua kama kuna hatimiliki ya tiba hiyo.
Wananchi wasitoe mbegu au mti huo ovyoovyo maana wajanja wanaweza wakauchukua kwenda kutengeneza dawa kisha kuja kutuuzia tena kwa gharama kubwa. Jamani viongozi wa serikali yetu wanafikiri sawa sawa? Mti upo porini, inasemekana umetiwa nguvu ya uponyaji na Mungu kwa kupitia mchungaji Mwasapile, wala si mtu mwingine, ndiyo maana hata wataaalamu hao wa tiba hadi sasa hawajachukua mizizi kupeleka Muhimbili, Bugando au KCMC kutibu wagonjwa, iweje mtu afikirie neno la Mungu kuwekewa hatimiliki, na kuzuia nguvu ya utendaji au uponyaji wa Kimungu usiende kwingine?
Je, mtu mwingine akiota Kenya leo, Uganda kesho na Uturuki wiki ijayo na kupewa uwezo kama wa Mwasapile, serikali yetu itazuia huduma za ndoto za Kimungu katika mataifa mengine kwa kuwa mtanzania ndio alikuwa wa kwanza kuota ndoto na kupewa maelekezo na Mungu?
Msajili wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, Dk. Paulo Mhame alisema hivi sasa wako katika hatua za mwisho za kumpatia cheti cha usajili Mchungaji Mwasapile. Wanampatia kama mganga wa jadi kwa utaratibu upi?
Dawa ni ya neno la Mungu, mchungaji anakiri kuwa yeye hatibu ila anatibu Mungu kwa kupitia dawa aliyomuotesha mchungaji huyu. Je, cheti hicho na hatimiliki kitaandikwa jina la Mungu au neno gani? Na kama wanampatia leseni, ni kwa sababu Babu wa Loliondo ameomba au serikali inayofanya siasa hata kwa neno la Mungu imeamua kujipendekeza?
Kuna mengi sana tunapaswa kuhoji kwanza kabla ya kuyatolea matamko. Katika suala hili serikali yetu imechemka. Kwanza kuunda timu, pili, kutumia pesa, tatu kutoa tamko, nne kutoa michango, tano kuanza kupima kwa kutumia maabara vitu vya kiimani.
Walipaswa kujiuliza neno la Mungu halifanyiwi kazi na timu, ndiyo maana Mungu hakutoa ndoto hiyo kwa timu ya serikali, walipaswa kutotumia pesa kuanza kufanya utafiti kwa mambo yasiyoonekana, ila ni ya kusadikiwa tu, akili iliyoumbwa inawezaje kufanya utafiti kuelewa kilichowekwa akilini na Muumbaji?
Zaidi ya hayo ni udhaifu sana kupima kinachosadikiwa kuwa ni neno la Mungu kwa kutumia vifaa vya maabara, na ukatoka hadharani ukasema kitu hiki hakina madhara, tukiendelea hivyo basi kila maabara inaweza kupima na kujua dini ya mtu bila kumuuliza.
Serikali yetu imesema uongo, haijafikiri sawa sawa, inakurupuka, haijifikirishi kutoa matamko, inafanya kazi kwa staili ya ujima, na kutoa majibu kana kwamba Watanzania wote tuna sare ya mawazo kama ya wataalamu hao.
Namnkuu paroko mmoja aliyetupa mawazo ya kujifikirisha kidogo kuwa "Sina chuki wala tatizo lolote na tiba ya Loliondo, lakini kama unataka kwenda lazima ujiulize maswali manne yafuatayo:
Kwanza, tiba inayotokana na miujiza ya Mungu lazima iwe endelevu, isiwepo kwa kipindi kifupi tu.
Pili, watu wajiulize kama miujiza kutoka kwa Mungu huwa na masharti?
Tatu, wajiulize kama tiba hiyo inafanya kazi ndani ya Loliondo, kwanini isifanye kazi Dar es Salaam na kwingineko?
Nne, wajiulize kuhusu tiba hiyo ya magonjwa sugu ukiwemo ukimwi, je, Mungu aliwaumba wanadamu na kisha kuamua kuwaangamiza? Au wanadamu wanaangamia kutokana na vitendo vyao vya ujanja ujanja?
0786426414