SoC03 Serikali ifanye haya kuhusu ajira za walimu hapa nchini

Stories of Change - 2023 Competition
Dec 10, 2020
15
14
Shukrani
Asante sana Jamii Forums kwa jukwaa la Stories of Change naweza kusema ni sauti ya mafanikio ya jamii nzima.

Pia, ningependa kuwaalika ndugu jamaa na marafiki, na umma wa watanzania kutumia jukwaa hili zaidi kubadilisha jamii kwa kuandika kwa wingi maandiko ya msingi kuliko hata mitandao mingine ya kijamii yenye hisia nyingi tofauti.

Kadhalika, ningependa kuwaomba watanzania kupenda kusoma stori nzima na kuacha kusoma sehemu tu ya maandiko kwani hii inasababisha kuibua hisia tofauti na kusudio ama kupata ujumbe tofauti kutokana na kutokumaliza kusoma andiko.

Hali ya ajira za walimu ilivyo kwa sasa
Ukweli ni kwamba kuna ongezeko kubwa la walimu wanaohitimu vyuoni hii ni kitokana na shule nyingi za sekondari za kata zilizojengwa kila kata nchini kote kutoa wahitimu kila kata.Ongezeko la wahitimu wa elimu ya kidato cha nne ni kubwa na hii ni kutokana na jitihada ya serikali kuwafikia watoto wengi.

Ongezeko hili linaenda sambamba na ongezeko la wahitimu wa vyuo vya ualimu ikiwemo vyuo vya kati na vyuo vikuu.

Kuwepo kwa mambo hayo kumechangia kuwepo kwa wahitimu wengi ambao serikali imeshindwa kuwaingiza katika mfumo rasmi wa ajira na wengi wakiwa hawana ajira hata kujiajiri kutokana na fani hii kutegemea zaidi kuajiriwa.

Ikumbukwe kuwa kati ya mwaka 2015 hadi 2019 ajira za walimu serikalini zilitetereka na pale zilipotolewa zilikuwa zinasuasua sana.

Hali haikuwa hivyo katika kipindi cha miaka 10 nyuma kwani ukiacha mwaka 2013 hadi 2014 kwa wahitimu wa kada ya ualimu waliajiriwa moja kwa moja.

Ikumbukwe kuwa baadae mfumo ukabadilika na kuwepo kwa mfumo wa maombi ya ajira. Kubadilika kwa mfumo pamoja na kutokuwepo kwa ajira za walimu kwa kipindi fulani huku vyuo vikiendelea kutoa wahitimu wapya kumechangia wahitimu kuongeka zaidi na kutengeneza tatizo kubwa la ajira hapa nchini. Kuwepo kwa tatizo hili kumesababisha kuongezeka kwa idadi kubwa ya walimu wasio na ajira ikichangiwa na idadi ya wanaoajiriwa kuwa ndogo huku wanaohitimu kila mwaka ikiongezeka na kuchangia tatizo kukua mwaka hadi mwaka.

Hivi karibuni serikali kupitia waziri wa elimu ilitoa tamko la kutaka kuanzisha mchakato mpya wa kutumia ili kuweza kuwapata watakaoajiriwa ikiwa ni pamoja na kufanyiwa mtihani wa usaili lakini kumekuwepo na madai kuwa kuna walimu hawafai kuwa walimu na si kila aliyehitimu anapaswa kuajiriwa atapitia utaratibu huo.

Ni wazi kuwa haya ni matokeo ya serikali kushindwa kumudu kuwaajiri wahitimu wengi na hivyo inaonekana kuacha tatizo kuu, serikali imeanza mchakato mwingine wa kuwa na utaratibu mpya wa namna ya kupata watakoajiriwa ama kwa nia njema lakini ni wazi inaacha kukiri kuwa kuna tatizo la ajira na kwa nini isitoe namna inavyolifanyia kazi.

Hapa ni wazi viongozi ama kwa kufahamu ama kwa kutokufahamu wanataka kukimbia tatizo hili kubwa wanalopaswa kulibeba na kuwapa mzigo wahitimu waliowaandaa kwa mfumo wao wa elimu rasmi kuwa hawana sifa.

Hii inaibua maswali mengi kama vile, Je ni kweli kuwa wahitimu hawakidhi? Kwa nini leo? Kwa nini baada ongezeko la wahitimu? Kwa nini walioko tayari kazini wasizingatiwe ikiwa wapo walioajiriwa hivi karibuni? Kama walioko kazini hawazingatiwi na serikali imebaini tatizo hawawezi je kuharibu?

Na kama wataharibu tatizo litaishaje sasa? Au kuna mbinu? Kama kuna mbinu, je mbinu hiyo haiwezi kutumika kwa wasio na ajira pindi wakiajiriwa? Maswali haya yanenda moja kwa moja katika wizara husika ikiwemo Wizara ya Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia.

Hii ni kwa kuwa, wakati wizara ya Elimu inaratibu miongozo ya kimafunzo ikishirikiana na taasisi mbalimbali zikiwemo vyuo vya kati na vyuo vikuu, Tume ya vyuo Vikuu Tanzania (TCU) hazikuwa na mipango ya kufatilia ubora wa walimu waliko vyuoni kabla ya kuhitimu?

Kwamba, serikali imebaini tatizo la wahitimu kuwa baadhi hawakidhi ni wazi kuwa imejiridhisha tatizo ni kubwa kwa maana lingekuwa ni kiwango kidogo lisingechukuliwa namna hii. Na swali la kujiuliza, serikali imefanya nini katika vyuo husika vinavyotoa mafunzo ya ualimu ili kuhakisha wanazalisha walimu bora? Kwa nini tatizo liwe kwa wahitimu tu na si kwa wanaotoa mafiunzo kama ni kweli? Kama wahitimu si bora vyuo wanavyotoka ikiwa ni pamoja na wahazili na wakufunzi wao wanawezaje kuwa bora?

Ni wazi kuwa tatizo la ajira ndilo linaficha hayo yote la sivyo hatua zingechukuliwa kwanza katika vyuo na baadae kwa wahitimu.

Serikali haikujipanga vizuri ama ilijisahau na sasa imeelemewa na mzigo kwani kukiwa na takwimu nzuri za idadi ya uhitaji na ushirikiano thabiti ikiwemo ufatiliaji na uthibiti ubora dosari ndogo sana zingeweza kujitokeza na si kama zinazozungumzwa leo vinginevyo tunaweza kusema serikali ina jukumu la kutoa ajira bila kuweka vikwazo vingi.

Mfano, idadi ya shule zilizopo za msingi na sekondari inajulikana, idadi na uwiano wa mwalimu kwa mwanafunzi unaotakiwa unajulikana, mahitaji ya kila shule ya walimu yanajulikana kwa nini kuwa na idadi kubwa ya wahitimu tena wasio na uwezo? Je tatizo wamelitengeneza wahitimu au mfumo umetengeneza tatizo? Na kama mfumo umetengeneza tatizo nani alaumiwe?

Mabadiliko ya taratibu yanakubalika lakini yanaathari kubwa sana kwa vijana waliokwisha hitimu yanaweza kuwa mazuri lakini si lazima yaunganishwe na wahitimu wasio na ajira.

Mapendekezo kwa serikali.
  1. Serikali imalize tatizo la ajira za walimu, wahitimu waliopo sasa waingizwe kwenye ajira wakati inaandaa sera na dira mpya itakayoanza kutumika kuanzia miaka 10 au zaidi ijayo ili kuweza kupata maandalizi mazuri.
  2. Serikali ikiwezekana ihakikishe kwa sasa inaanza kupunguza idadi ya wanaotakiwa kupata mafunzo ili iweze kuja kurahisisha uingiaji wa walimu wapya watakaoingia kwa wingi kuja kubadili mfumo
  3. Mabadiliko hayo yaende sambamba na mpango wa maboresho ya kada ya ualimu ikiwa ni pamoja na kuboresha mafunzo kwa kuweka mkazo na kufuatilia suala la maadili kuchukua alama za juu za ufaulu kwa wanadahiliwa vyuoni.
  4. Kuboresha ufuatiliaji wa maadili ya walimu walioko kazini na kuwachukulia hatua wanapokiuka.
  5. Kutowachukilia walimu ambao hawajaariwa kuwa hawana maadili kisa wale wachache walioajiriwa wameonesha tabia za kutokuwa na maadili.
  6. Ili kuboresha elimu na kukabili tatizo la ajira, walimu wa Shahada katika masomo ya sanaa wengi waajiriwe shule za msingi.
  7. Ili kupandisha hadhi ya elimu na ualimu nchini ni lazima thamani ya wahitimu na walimu iheshimiwe na kuepuka kauli zinazoshusha hadhi ya wengi kwa makosa ya wachache.
  8. Ni vyema mhitimu mwenye kosa anyoshewe mkono mwenyewe na kutomhusisha na wengine kwa kuwa tu ni wa kada moja.
 
Umeandika upupu mwingi ila kitu ambacho hujui,mchawi hapo ni masrahi (mishahara iboreshe) ,huwezi kuwajazia mambo mengi kisha mishahara mibovu.
Kila mtu ana nafasi yake katika maoni na kila linalotolewa hata unaloona ni upupu linajenga kitu kipya, muhimu kwako kueleza mwelekeo wako kama uonavyo. Bahati mbaya wengi hukatiza mara waseme ni ujinga, ni upupu lakini kama una hoja ya msingi na unapinga kuna namna ya kupinga na unaweza kuwasilisha mawazo yako pia ya kutokukubaliana na kile kilichosemwa. Ukiwa na maoni zaidi, niandikie si chuki wala si kosa.
 
Back
Top Bottom