SoC03 Ajira za Walimu isiwe kikwazo kwa Wahitimu, Serikali iwajibike

Stories of Change - 2023 Competition
Dec 10, 2020
15
14
Kwanza, Asante sana Jamii Forums kwa jukwaa la Stories of Change naweza kusema ni sauti ya mafanikio ya jamii nzima.

Pili, ningependa kuwaalika ndugu jamaa na marafiki, na umma wa watanzania kutumia jukwaa hili zaidi kubadilisha jamii kwa kuandika kwa wingi maandiko ya msingi kuliko hata mitandao mingine ya kijamii yenye hisia nyingi tofauti.

Tatu, ningependa kuwaomba watanzania kupenda kusoma stori nzima na kuacha kusoma sehemu tu ya maandiko kwani hii inasababisha kuibua tofauti na kusudio ama kupata ujumbe tofauti kutokana na kutokumaliza kusoma andiko.

Nikiridi katika mada, ningependa kuanza moja kwa moja katika hali ilivyo ya ajira za walimu.

Ukweli ni kwamba kumekuwa na ongezeko kubwa la walimu wanaohitimu vyuoni hii ni kitokana na shule nyingi za sekondari za kata zilizojengwa kila kata nchini kote kutoa wahitimu kila kata.

Ongezeko la wahitimu wa shule za elimu ya kidato cha nne ni kubwa na hii ni kutokana na jitihada ya serikali kuwafikia watoto wengi.

Ongezeko hili linaenda sambamba na ongezeko la wahitimu wa vyuo vya ualimu ikiwemo vyuo vya kati na vyuo vikuu.

Kuwepo kwa mambo hayo kumechangia kuwepo kwa wahitimu wengi ambao serikali imeshindwa kuwaingiza katika mfumo rasmi wa ajira.

Ikumbukwe kuwa kati ya mwaka 2015 hadi 2019 ajira za walimu zilikuwa zimekoma na pale zilipotolewa zilikuwa zinasuasua sana.

Hali haikuwa hivyo katika kipindi cha miaka 10 nyuma kwani ukiacha mwaka 2013 hadi 2015 kwa wahitimu wa kidato cha nne wa mwaka 2010 ndio kidogo walianza kuchelewa kuingia katika mfumo wa ajira rasmi.

Wahitimu waliohitimu Astashahada ya Ualimu wengi wao wa mwaka 2010 ndio walihitimisha diriaha la ajira za moja kwa moja.

Kutokana na kubadilika kwa mfumo wa ajira ambapo walimu walikuwa wakihitimu vyuoni na kupangiwa moja kwa moja vituo vya kazi mara tu wanapohitimu masomo yao kubadilika na kuwepo kwa mfumo wa maombi ya ajira pamoja na kutokuwepo kwa ajira za walimu kwa kipindi fulani kumechangia wahitimu kuongeka zaidi na kutengeneza tatizo la ajira kubwa hapa nchini.

Kuwepo kwa tatizo hili kumesababisha kuongezeka kwa idadi kubwa ya walimu wasio na ajira hapa nchini na idadi wa wanaoajiriwa kuwa ndogo huku wanaohitimu kila mwaka kuongezeka tatizo linazidi kukua siku hadi siku.

Hii imesababisha serikali kushindwa kumudu kuwaajiri wahitimu wengi na hivyo kwa kutaka kulikimbia tatizo serikali imeanza mchakato mwingine wa kuwa na mfumo mpya wa namna ya kupata watakoajiriwa ili iweze kuwaacha wahitimu wengine kwa kigezo cha kutofuzu mtihani hii ni kulikimbia tatizo walilotitengeneza miaka mingi nyuma.

Hapa ni wazi viongozi ama kwa kufahamu ama kwa kutokufahamu wanataka kulikimbia tatizo na kuwatupia mzigo mkubwa wahitimu waliowaandaa kwa mfumo wao wa elimu rasmi kuwa hawana sifa.

Hii inaibua maswali mengi kama vile Je, ikiwa vijana hawa watakosa ajira na waliwekeza kwa miongo kadhaa katika elimu nani anaweza kufidia muda wao?

Wakati serikali inasitisha kuajiri kwa muda haikufahamu kuwa inatengeneza tatizo? Na pia ilijipangaje kuja kuhakikisha mara itakapoanza kuajiri kutokana na kusita kwa muda inakuja kubeba jukumu kubwa?

Maswali haya yanenda moja kwa moja katika wizara husika ikiwemo Wizara ya Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia.

Hii ni kwa sababu za wazi kuwa wizara hizi hazikuwa na ushirikiano wa kimikakati kwa kuwa zinategemeana?

Wakati wizara ya Elimu inaratibu miongozo ya kimafunzo ikishirikiana na taasisi mbalimbali zikiwemo vyuo vya kati na vyuo vikuu, Tume ya vyuo Vikuu Tanzania (TCU) hazikuwa na mipango ya kufatilia idadi ya uhitaji na ubora wa walimu wanaohitimu?

Tukichukulia idadi ya uhitaji ni wazi kukiwa na ushirikiano thabiti na ufatiliaji ni dosari ndogo sana zinaweza kujitokeza na si kama zinazozungumzwa leo.

Mfano, idadi ya shule zilizopo za msingi na sekondari inajulikana, idadi na uwiano wa mwalimu kwa mwanafunzi unaotakiwa unajulikana, mahitaji ya kila shule ya walimu yanajulikana, ongezeko la idadi ya watu kutokana na takwimu za sensa zilizopo zinajulikana.

Hii ingesaidia kuweza kuweka mpaka wa wanatakiwa kujiunga na mafunzo ya ualimu ili kuja kukidhi mahitaji. Lakini ni wazi iko tofauti.

Vijana sasa wanalaumiwa na wanaonekana hawawezi kuwa walimu, hawana sifa si jambo zuri.

Suala hapa lilitakiwa viongozi kukiri kuwa kwa vigezo vya kujiunga na mafunzo ya ualimu vilivyokuwepo vilisaidia na hivyo kwa sasa wanataka kubadilisha vigezo.

Suala la mabadiliko siyo baya hata kidogo lakini huwa ni kutokana na wakati na mahitaji ya wakati huo.

Kuanza kulaumu vijana leo si jambo zuri, wapo kweli wanaokiuka maadili hata serikalini ambao ni tofauti na walimu na hata walimu wenyewe suala hapa ni kuwa na udhibiti tu wa wale wanaokiuka maadili na si kuwachukulia wale waliohitimu kama wote hawana maadili ambao hawana ajira kuwa hawana maadili.

Pia binadamu hupatwa na mabadiliko mbalimbali hata kama walimu watafanya mtihani wa kufuzu kuajiriwa na wakafuzu na wakaajiriwa wapo pia wanaoweza kuja kukiuka maadili hata kama wamepitia hatua hizo za ajira.

Msingi mkuu ni kuwa na ushibiti kuweka namna nzuri ya kufuata yule anayetenda kinyume na maadili ya kazi si tu katika ualimu hata kazi nyingine za kiserikali kuchukuliwa hatua kwa uwazi na ikiwa tu wamejiridhisha.

Ushauri wangu kwa serikali na jamii kwa ujumla.

Viongozi watambue kuna sehemu ambazo zinakubali mabadiliko ya papo kwa papo na haziwezi kuleta athari kubwa hasi katika mabadiliko yoyote yatakayofanyika kwa makini.

Zipo pia sehemu ambazo hazikubali mabadiliko ya papo kwa papo na zinaathari hasi katika kipindi cha muda mrefu.

Kwa kuzingatia hayo, mifumo kama mfumo wa elimu unahitaji mabadiliko kwa kuzingatia muda mrefu.

Mfano, matokeo ya kupata walimu walio bora si tukio la mabadiliko ya muda mfupi tu na ndani ya muda mfupi unapata walimu bora si hivyo.

Mabadiliko hayo yanahitaji kufanywa leo huku yakipewa muda mrefu zaidi wa kuja kuingia katika utekelezaji wake.

Tuchukulie mabadiliko ya namna ya kupata walimu bora kutoka katika mfumo wa elimu ulivyo leo.

Walimu hawawezi kuwa bora tu kama umejiridhisha kabisa kuwa hawakufuzu mafunzo ya vyuoni vizuri na ukaona njia pekee ni kufanya mtihani wa usaili. Kama lengo ni kupata walimu bora basi hili si jibu sahihi.

Si jibu sahihi kwa sababu kupata walimu ni mchakato na mchakato huo ni wa muda mrefu sana.

Kuanzia mwanafunzi anapoanza masomo yake darasa la kwanza hadi kufikia mafunzo ya ualimu chuoni. Ufuatiliaji wake ni wa msingi mno.

Suala la ufaulu pia kama litazingatiwa linaweza kuwa na maana au halina maana

Linaweza kuwa na maana kwa sababu kama mwanafunzi amefaulu vizuri kutoka mwanzo anatarajiwa kuwa mwalimu mzuri lakini si lazima kwa sababu wapo wengine wameshindwa kufaulu vizuri kutokana na changamoto mbalimbali na si kwamba hawana uwezo.

Mfano, kuna wale walipata daraja la nne katika kidato cha nne kwa sababu tu siku ya mtihani hawakuwa vizuri.

Lakini pia wapo ambao hawakufanya vizuri kutokana na serikali yenyewe kushindwa kuwatimizia mahitaji yao na wangefanya vizuri zaidi.

Mfano, kuna shule hazikuwa na walimu wa kutosha hasa zingine zilikosa hata walimu wa Sayansi hasa shule za sekondari mfano mzuri ni shule niliyosomea mimi kati ya mwaka 2010-2013. Ilikuwa na walimu wawili tu mkuu wa shule na msaidizi wake ambao niliwakuta kidato cha kwanza na mmoja alikuwa mwalimu wa masomo ya sayansi.

Hata hivyo mwalimu huyo hakaka nikiwa mwaka wa kwanza tu akaondoka. Hakukuwa tena na mwalimu wa masomo ya sayansi wa kuajiriwa hadi nahitimu kidato cha nne.

Hakukuwa na maabara na walimu wa kujitolea walikuwa wanakuja na kuondoka. Mfumo uliolazimisha nisome masomo ya sanaa na nikafaulu. Sikutaka lakini n

Ilinilazimu kwa kuwa hata uwezo wa kusoma twisheni haukuwepo. Wengi wanafahamu familia nyingi zilivyo haina uwezo kiuchumi.

Nimesoma hadi chuo kikuuu masomo ya sanaa na kupata shahada ya Elimu na Sanaa na leo hii kuna mlundikano wa wahitimu.

Jukumu la serikali lilikwepwa mapema sana la kutokuajiri walimu wa masomo ya sayansi na hata hivyo kulikuwa na uhitaji mkubwa tu wa walimu katika shule niliyohitimu ambayo sitaitaja hapa.

Wengi wamehitimu wa wahitimu kwa miaka ya hivi karibuni wa ualimu ni masomo ya sanaa.

Kumekuwa na ongezeko kubwa la walimu wa masomo hayo hasa wa shahada na ajira ni chache.

Kitu cha kushangaza kabisa pamoja na kutokuwepo kwa walimu wa masomo ya sayansi shuleni bado serikali ilithubutu kuruhusu wahitimu wengi wa ualimu kuwa wa masomo ya sanaa. Hapa najiuliza leo hii ni kweli kuwa hawakupaswa kuwa walimu kama inavyosikika leo?

Kama hawakupaswa, kwa nini serikali iliruhusu udahili wa idadi kubwa ya wanafunzi wa ualimu wasikidhi vigezo?

Je ni kweli kuwa walimu hawa walikidhi wakiwa katika shule za sekondari vigezo vya kujiunga na ualimu lakini hawakukidhi vyuoni?

Jibu linakuja hapana, serikali iwajibike.

Serikali inatakiwa kuwajibika kuwa inahakikisha kuwa wahitimu walipo sasa wa ualimu inawaajiri wale wote watakaokosa shule za binafsi huku ikiweka mpango thabiti wa kupata walimu kwa mfumo mpya na endelevu utakaoanza kuleta matunda hata miaka ya 2070.

Wakati ikifanya hayo, inatakiwa kuandaa mazingira mazuri ya kutoa mafunzo kwa walimu inaowaajiri wakiwa kazini.

Lakini pia iende sambamba na takwimu mpya za kuhakikisha inatumia kanzidata ili kujua inakuwa na idadi ya wahitimu wa ualimu walio bora itakayoenda sambamba na mahitaji kuhakikisha haizalishi kiwango ambacho kinazidi maradufu uhitaji wa soko la ajira za shule, vyuo vya serikali na binafsi.

Kwa kufanya hivyo, serikali haiwezi kuwabebesha mzigo wahitimu pekee kwani mpaka sasa walishahitimu na hivyo haiwezi kuyabadilisha hayo kwa sasa badala yake mabadiliko yanaweza kutokea taratibu hadi mfumo bora utakapokamilika kuingia moja kwa moja kwa taratibu.

Suala la kuzingatia kwa viongozi wa serikali na serikalo yenyewe, wanapaswa kuweka mazingira na kuweka mipango ya rasilimali za kuliondoa tatizo la ukosefu wa ajira za wahitimu wa ualimu waliopo.

Serikali ikidhamilia kufanya jambo la msingi kwa raia wake haiwezi kushindwa.

Inatakiwa kutambua hawa ni raia wake, itambue na ithamini elimu waliyoipata katika nchi yao kwa kipindi chao, wapate kazi waitumikie nchi yao na taifa lao kwa amani na furaha na iwawekee mazingira mazuri ya kazi.

Lakini pia, wanaoajiriwa watambaue kuwa hawakuingia katika sekta ya elimu kwa kubahatisha, hawakuingia ili kujipatia kipato bali watambue dhamira ni kusaidia taifa la kesho na wafanye kazi kwa bidii na kwa weledi mkubwa ili hata wanapopata mishahara yao wajivunie kulifanyia kazi taifa na kustahili kulipwa.

Wito wangu kwa viongozi ni kuwasaidia vijana hawa, watambue kuwa, kiongozi ni jicho la pekee. Kiongozi anaona na kufanyia kazi tatizo la raia wake kwa kuzingatia namna anavyohitaji msaada.

Kiongozi ni mzalendo, asiyependa maslahi yake binafsi, kiongozi anatazamwa na kila raia kama mkombozi.

Kiongozi anaposhindwa kuona vizuri anaharibu pasipo kutarajia na kiongozi anapoacha tatizo liende huku akiwa analiona anaharibu pakubwa mno kuliko raia wa kawaida kwa maana maamuzi yake yanaathiri taifa.

Mwisho, Misingi mipya ya Elimu inatakiwa kuwekwa katika taifa letu, kwa kuwa sekta hii ni nyeti sana ni vyema misingi hii mipya iwekwe kikatiba.

Katiba iweke mielekeo thabiti kuhusu namna ya kupata walimu bora, viwango vya ufaulu, mifumo ya ajira, mishahara na posho za walimu, wajibu wa viongozi, waajiri na isitikiswe mara kwa mara kulingana na kiongozi yupi anataka yapi kwa wakati wake badala yake ilinde matakwa hayo kwa vizazi kadhaa na ioneshe uwajibishwaji kwa viongozi na waajiri watakaoenda kinyume.

Kuwepo kwa jambo hilo, kutaleta miongozo inayoenda sambamba na matakwa ya kikatiba na mitaala bora itakayoboresha elimu ya mtanzania kwa asili yake na mazingira yake halisi sambamba na mabadiliko mbalimbali ya kiasayansi na kiteknolojia na mahitaji ya wakati huo.

Kwa kufanya hivyo, elimu itapata thamani yake halisi, wahitimu bora wenye uwezo kuajirwa na kujiari, katika sekta mbalimbali lakini kuwepo na sekta ambazo serikali italazimika kuhakikisha wahitimu wa fani hizo zinakuwa na uhakika wa wa kuajiriwa moja kwa moja serikalini na idadi ya watakaodahiliwa kujiunga na mafunzo ya fani hizo iende sambamba na idadi ya mahitaji ya watakaoajiriwa hata ikiwepo ziada iwe inayowezekana kuchukuliwa yote kwa wakati mmoja huku ikitarajia wahitimu wapo.

Zingatio kubwa kwa wote ni kuwa suala hili lisichukuliwe kisiasa bali liwe suala la kitaifa, kila raia na kiongozi atambue na kusimamia katika nafasi yake kwa kufuata taratibu zote na kwa ukweli na uwazi.

 
Back
Top Bottom