Serikali iache hadaa Mikopo ya wanafunzi Elimu ya Juu

Abdul Nondo

JF-Expert Member
Oct 28, 2016
515
2,875
Ngome ya Vijana tunatambua jitihada za serikali kupitia Bodi ya Mikopo katika utoaji wa mikopo elimu ya juu kwa wanafunzi mbalimbali.

Lakini jitihada hizi zimekuwa na kasoro mbalimbali katika utoaji wa mikopo kwa wanafunzi kila mwaka wa masomo. Kasoro hizo zimekuwa zikijitokeza katika sura tofauti, jambo linaloondoa dhamira mahususi ya utoaji mikopo kwa wanafunzi wenye uhitaji na wasio na uwezo wa kujisomesha ili kufikia malengo yao ya kitaaluma katika ngazi ya elimu ya juu.

Kasoro na changamoto hizi zimekuwa zikijirudia kila mwaka zikiwa na lengo la kupunguza idadi ya wanafunzi wanufaika wa mikopo Elimu ya juu na zikiwa na lengo la serikali kujiondoa taratibu katika utoaji wa mikopo elimu ya juu. Ndio maana kila mwaka lazima kutokee kituko kipya au jambo jipya lifanywalo na Bodi ya mikopo dhidi ya wanafunzi.

Kuanzia 2016 kurudi nyuma utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wanufaika ulikuwa ukizingatia uainisho ufuatao katika miongozo yake yote ya kila mwaka.

-Fedha ya kujikimu yaani chakula na malazi ni Tsh. 510,000 kwa kila mnufaika kwa siku 60 yaani miezi 2.

-Fedha ya vitabu na steshenari Tsh 200,000 kwa kila mnufaika kwa mwaka mmoja.

-Fedha ya mafunzo kwa vitendo /Field Practice Tsh.10,000 kwa siku, jumla ya siku 56 ya mafunzo kwa vitendo ni Tsh 560,000 na

-Fedha ya nauli kwa mnufaika huwa inafika 600,000 kwa kila mnufaika.

-Fedha ya Ada, hii ndio ilikuwa inatofautiana kati ya mwanafunzi na mwanafunzi kutokana na uwezo wao. Hivyo Bodi ya mikopo walikuwa wanatumia asilimia katika ugawaji wa Ada tu kulingana na uwezo na uhitaji wa wanafunzi. Njia hii inaitwa Means Testing.

Hata hivyo, kuanzia 2016, 2017, 2018 na 2020 dhamira ya serikali kuendelea kukopesha wanafunzi mikopo elimu ya juu iliendelea kufifia kwani Serikali kupitia Bodi ya Mikopo walianza kutoa mikopo katika category hizo juu kwa asilimia tofauti tofauti kwa kila mwanafunzi hadi kwenye chakula na malazi. Wanafunzi wengine waliwahi kupewa Tsh. 20,000 chakula na malazi kwa siku 60.

Jambo ambalo ni kinyume na dhamira ya kukopesha wanafunzi wenye uhitaji. Baada ya kelele nyingi ndipo Waziri Ndalichako alitenguo utaratibu huo wa kugawa fedha ya chakula na malazi kwa asilimia hivyo ikawa ni Tsh. 510,000 kwa kila mwanafunzi mnufaika kwa siku 60. Lakini kategori zingine zote hapo juu zikawa zinatolewa kwa asilimia yaani Means Testing jambo ambalo sio sahihi.

UGAWAJI WA MIKOPO KWA MWAKA HUU 2021/2022.

Ugawaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu katika mwaka huu 2021/2022, umekuwa na kasoro nyingi na ujanja mwingi. Mbali na kwamba bajeti ya mkopo iliongezwa mwaka huu kufikia Tsh. Billioni 570 tofauti na mwaka jana 2020 ambapo ilitolewa Tsh.464 bado dhamira ya kumsaidia mtoto wa kimaskini na mwenye uhitaji kupata mkopo ili aweze kukamilisha mzunguko wa elimu yake ngazi ya juu inaweza isifikiwe.

Hii inatokana na Serikali kupitia Bodi ya Mikopo kutumia njia za ujanja ujanja ili kukwepa wajibu na majukumu ya kumsadia mwanafunzi maskini na asiye na uwezo kukamilisha mzunguko wake wa elimu ya juu kama isemavyo sera ya elimu ya 2014 kifungu cha 3.6 na 3.3.2

Serikali kuendelea kugharamikia elimu na kuondoa vikwazo vitakavyozuia wanafunzi kumaliza mzunguko wao wa elimu. Inachofanya Serikali kupitia Bodi ya mikopo ni kuweka vikwazo na kupunguza kugharamikia elimu.

Mwaka baada ya mwaka idadi ya wanafunzi inaongezeka ikienda sambamba na ongezeko la wanafunzi wenye uhitaji wa mikopo elimu ya juu. Bajeti ya mikopo ya 2021/2022 Billioni 570 Serikali kupitia Bodi ya mikopo ilitenga fedha hizo kwa tathimini ya jumla ya wanafunzi 160,000 kati ya hawa wanafunzi wa mwaka wa kwanza ni 62,000 na wanaoendelea au waliopo chuoni ni wanafunzi 98,000.

Sisi tunajikita kwa wanafunzi hawa wapya wa mwaka wa kwanza 62,000 ambao serikali imenuia kuwapa mkopo. Lengo la serikali na Bodi ya mikopo ni kuonesha umma kwamba serikali mwaka huu imetoa mkopo kwa wanafunzi wengi wa mwaka wa kwanza ikiwa sio kweli.

Ujanja uliotumika mwaka huu na bodi ya mikopo na serikali ni kuongeza idadi ya wanafunzi wanaonufaika na kupunguza kiwango cha fedha kwa mnufaika huyo, jambo ambalo ni sawa na bure kwani halijapunguza mzigo kwa familia nyingi za kimaskini .

Mfano,Ngome ya vijana tumekuwa tukipokea taarifa kutoka kwa wanafunzi wanufaika wahanga waliokumbwa na changamoto hii na hawajui hatma yao baada ya kutoka Batch ya kwanza na ya pili.

Ada ,asilimia 75 % ya wanufaika wamepewa ada Tsh.400,000 tuu kwa mwaka.Hii imeoneshwa dhahiri kwenye PDF BATCH 1 iliyotolewa na Bodi ya mikopo. Ada za wanafunzi zimetofautiana kulingana na vyuo.Wapo ambao ada za vyuo vyao ni Tsh.1500,000, wengine 2000,000, 3000,000 hadi 4000,000 hasa vyuo vya afya ila ada wamepewa na bodi ya mikopo ni Tsh.400,000 hadi 200,000 mwingine tumepata taarifa zake fedha zote alizopewa na bodi ya mikopo ni 2,750.

Na sio kwamba hawana sifa ,wengi wana sifa walisoma shule za kata,wengine ni mayatima ,wametokea familia za kimaskini na wengine wanasomea Sayansi ila wengi wamenyimwa.Mfano,wanafunzi wengi waliochaguliwa course ya MD na BSN vyuo vyote MUHAS, KCMC, CUHAS, UDOM, UDSM, KAIHURUKI, wamepewa fedha kategori ya chakula na malazi yaani fedha ya kujikimu Meals and accomodation uku Ada wakiwa hawajapata kitu yaan 0 na wengine wakiwa wamepewa Tsh.400,000.

Wanafunzi na wazazi wengi hawatakuwa na uwezo wa kuongezea kiasi kilichobaki hivyo watapoteza matumaini ya kusoma chuo kikuu sababu haiwezekani mzazi anayeshindwa mlipia ada ya sekondari mtoto wake hadi Serikali kusomesha bure kwamba leo hii mzazi huyu awe na uwezo wa kuongezea 1000,000 au 1500,000 au Tsh. 800,000 kwenye ada ya mtoto wake kwenda chuo.

Fedha ya vitabu na viandikwa ,asilimia 90% ya wanufaika wa mkopo wamenyimwa kabisa hawajapewa. Kwa utaratibu wanapaswa pewa Tsh.200,000 kwa mwaka kwa ajili ya matumizi ya kupiga kopi na vitabu au kununulia notisi steshenari.Hivyo wanafunzi wengi wataathirika katika kupata viandikwa na vitabu hata huduma ya stasheneri hivyo itawaathiri katika taaluma zao.

Fedha ya Mafunzo kwa vitendo ,asilimia 90% ya wanufaika wamenyimwa fedha ya mafunzo kwa vitendo.Ambayo kwa utaratibu wanapaswa kupewa Tsh.560,000 kwa siku 56 wawapo kwenye mafunzo kwa vitendo.

Jambo hili litaondoa ufanisi kwa wanafunzi kufanya mafunzo kwa vitendo kwani wanafunzi hawatafanya kwa umahiri watakapo kwenda huko hivyo tutazidi jenga jamii ya nadharia zaidi kuliko matendo .

Fedha ya Tafiti ,90% ya wanufaika wanaofanya tafiti katika masomo yao wamenyimwa fedha ya tafiti.

Ilichofanya bodi ya mikopo ni kuwapa wanafunzi fedha ya kujikimu yaani chakula na malazi wote sawa ,takribani Tsh.2000,000 kwa mwaka kila mwanafunzi na ikafanya janja kubebesha mzigo kwenye Ada ,mafunzo kwa vitendo,viandikwa na steshenari na tafiti mzigo huu wote amerejeshewa mzazi maskini wa mwanafunzi bila kujali uwezo wa mzazi au mwanafunzi huyo.

Alafu serikali na Bodi ya mikopo wanajisifu kwamba wametoa mikopo kwa wanafunzi wengi ,hakika wameongeza idadi ya wanafunzi waliokopeshwa sio walionufaika au watakaonufaika na huu mkopo sababu wengi hawataweza kulipa kiasi cha fedha wanachopaswa lipa vyuoni hivyo hawatonufaika na hatimaye hawatakwenda vyuoni au wengi wataishia kati. Wanafunzi wengi watafanya fedha ya kujikimu kuwa fedha ya kuongezea kulipa ada hivyo idadi ya wanafunzi wanaosha vyombo kefeteria za chuo ili wapate chakula itaongezeka,idadi ya wanafunzi wa kike kupata vishawishi ili wapate fedha ya kula itaongezeka ,mateso ya wanafunzi kushindia mikate na maji wakiwa chuo yataongezeka,mateso ya wanafunzi kutoelewa kikamilifu darasani sababu ya njaa yataongezeka,idadi ya wanafunzi kutoroka chuo ili kwenda kutafuta vibarua ili wapate fedha ya kujikimu itaongezeka ,hii ni aibu kwa wanafunzi ngazi ya chuo kikuu kusoma katika changamoto hizi .

Hii inachangia haswa elimu katika vyuo vyetu kuzidi kuporomoka na kupata wahitimu wasio na uwezo kupambana katika soko la ajira.
MAPENDEKEZO YETU

#Serikali iongezee fedha bodi ya mikopo ,mbali na kwamba Rais alikwisha ongeza Bilion 70 kufikia hiyo Billioni 570 .Ukweli ni kwamba wanafunzi wenye uhitaji ni wengi sana na kama serikali haitoweza ongezea bodi ya mikopo fedha kuna dalili zote wanafunzi wengi mwaka huu wakaahirisha masomo na wengine kuacha kabisa.

#Bodi ya mikopo iache kuhadaa umma kwa kujisifu imetoa mikopo kwa wanafunzi wengi wakati imewaongezea mzigo wanafunzi kwa kuwanyima ada,viandikwa na mafunzo kwa vitendo ikiwapa fedha ya kujikimu na kuwahesabu kwamba ni miongoni mwa wanufaika ikiwa haijawasaidia wanafunzi kunufaika na mkopo huo kikamilifu na haitawasaidi.

Hivyo bodi ya mikopo na serikali waone namna ya kusaidia wanafunzi hawa ili na wao waweze kunufaika na huu mkopo zaidi.Aidha jambo hili lirekebishwa wakati huu kwa kuwaongezea fedha wanafunzi hawa au serikali kupitia bodi ya mikopo irekebishe jambo hili kupitia dirisha la rufaa ,jambo la msingi ni vyema fedha iongezwe ili kuokoa idadi ya wanafunzi ambao tunaweza kuwapoteza kwa kushindwa kubeba hizi gharama.


Imetolewa na

Abdul Omary Nondo,
Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ACT wazalendo Taifa.

23/Oktoba/2021.
 
Back
Top Bottom