Serikali haina nia thabiti ya kumkomboa Mkulima. Kauli ya kudhibiti Lumbesa ni danganya toto

Tipstipstor

JF-Expert Member
Nov 29, 2021
1,531
3,331
Ahlan wa sahlan

Kuelekea kuadhimisha sikukuu ya wakulima maarufu kama Nane nane, serikali kupitia makamu wa Rais ,Mheshimiwa Dk. Philip Mpango, imetoa taarifa kudhibiti lumbesa.Ila kauli hii imekuwa ikitoka miaka nenda miaka rudi huku wakulima wakiendelea kuumia tu. Wakala wa vipimo na mizani Tanzania (WMA) wamekuwa ni kitengo tu cha kuchukua faini (milungula) na si kutekeleza maagizo ya serikali ,kitendo kinachopelekea wakulima kuzidi kukosa matumaini na kilimo.

Kama mjuavyo kuwa bei ya mbolea na mafuta ya petrol na dizeli yamepanda sana kitendo kinachopelekea kuongeza gharama za uzalishaji wa mazao kuwa kubwa zaidi halafu bado mazao yanauzwa kwenye lumbesa hii inapelekea wakulima kuzidi kuumia tu.

Wachuuzi wa mazao wamekuwa wakiendelea kununua na kupakia mazao yao kwenye lumbesa kama kawaida huku wakinufaika na mlango mdogo wa faini uliowekwa na wakala wa vipimo na mizani (WMA) ambapo hulipa faini ndogo tu ya shilingi laki moja mpk laki tatu na kuendelea kuingiza mizigo ya lumbesa kwenye masoko yetu.

Serikali izunguke kwenye masoko ya mwanza, Dar, Mbeya, Shinyanga n.k jinsi wajionee malumbesa yanavyoingia masokoni.Kumpiga faini ya shilingi laki moja mfanyabiashara aliyefunga mzigo kwenye lumbesa katika Tandam (Fuso) au mende (scania) yenye kubeba gunia zaidi ya 140 ni sawa tu na kumsukuma mlevi. Kwani faini hiyo ukiigawa kwa kila gunia ni sawa na shilingi 800-1000 tu kwa gunia. Jambo ambalo halimuathiri mfanyabiashara hata kidogo.

Ombi langu ni kwa serikali, imbane kamishna wa wakala wa vipimo na mizani kuongeza ukali wa udhibiti wa malumbesa katika mizani zote nchini. Ikiwa mfanyabiashara atashikwa na mzigo wa lumbesa (gunia linalozidi uzito wa kg 100) basi apigwe faini ndefu na aamriwe ashushe mzigo chini na aufungue aufunge upya katika ujazo wa kg 100. Mazao yanayoongoza kufungwa ktk vifungashio vinavyozidi uzito wa kg 100 ni Viazi, Vitunguu,Matango,Maembe,ukwaju,Dagaa nyama (maji chumvi),Hoho,njegere,biringanya,Tangawizi n.k

Wakala wa vipimo na mizani (WMA) inatakiwa iweke maafisa wake katika mageti yote ya masoko hususani masoko makubwa kama ilala,sterio,Mabibo,Machinga complex kwa jijini Dar es salaam, kilombero jijini Arusha,mwanza n.k

Pia wakulima wanatakiwa wawe na mizani ili kuhakikisha kuwa pindi mnunuzi anapokuja kununua mazao kwake basi wapimiane kwa kilo na zisizidi kilo 100.

Kama serikali ina nia thabiti ya kuzuia lumbesa basi iache janjajanja ya kutoza faini (ndogo) halafu kumruhusu mfanyabiashara aondoke pasi na kuufungua mzigo na kuufunga upya katika ujazo wa kilo 100. Kufanya hivyo kutawafanya wafanyabiashara wasinunue na kufunga mizigo kupita kg 100.

Maafisa wa Wakala wa vipimo na mizani (WMA) waache kula rushwa kutoka kwà wafanyabiashara ili kuruhusu malori yaliyobeba lumbesa kupita katika mizani. Pia wanatakiwa kuweka maafisa katika mageti yote makubwa ya kuingia masokoni ili kuwakamata wafanyabiashara waliohonga maafisa ktka mizani zote nà kupenya mpaka masokoni. Kamateni mizigo ya malumbesa na muamuru wafanyabiashara waifungue mizigo na kuifunga upya ktk ujazo wa kilo 100.
 
Leo hii wanunuzi wa mazao wakinunua tu mazao katika lumbesa hukata faini ya shilingi laki moja hukohuko katika mageti ya mazao vijijini ambapo faini hiyo huwa ni shilingi laki moja tu na hapo hupewa risiti ambayo anatembea nayo kupita katika mageti yote ya mizani.Akionesha tu kuwa kapigwa faini ya lumbesa shilingi laki moja basi anaruhusiwa kutembea na matokeo yake ni kuwa lumbesa haiishi masokoni.

Pia mizigo ya malumbesa inaua afya za wapagazi ( wabebaji wa mizigo) masokoni.Kijana kwenye kilo 65 anabebeshwa gunia la ukwaju, vitunguu,tangawizi au dagaa nyama lenye uzito wa kilo 180-200. Hii sio sawa hata kidogo.Matokeo yake ni kuua afya na migongo ya hawa wachukuzi.
 
Mageti yote ya udhibiti wa mazao katika halmashauri ni kuhakikisha kuwa mizigo ya lumbesa haikatishi kutoka katika halmashauri husika.
 
Back
Top Bottom