Selelii aja juu: "Mawaziri wanatudharau.."

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,534
40,160
Habari Leo

Baadhi ya wabunge wa Mkoa wa Tabora wametishia kutounga mkono bajeti za baadhi ya wizara kutokana na kitendo cha serikali kushindwa kutekeleza ahadi zake hasa katika ujenzi wa barabara ya kutoka Itigi, Tabora kwenda Kigoma.

Wa kwanza aliyesema wazi hataunga mkono bajeti za wizara ya Maendeleo ya Miundombinu, Nishati na Madini na Maji na Umwagiliaji ni Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii (CCM). Katika mchango wake, Selelii alisema Serikali katika Bajeti ya 2006/7, iliahidi kutengeneza barabara; lakini safari hii barabara hiyo haimo hata kwenye vitabu vya Bajeti ya Serikali.

Alisema, "safari hii hatoki mtu humu ndani hadi nielezwe kwa nini barabara hii haikutengewa fedha wakati serikali ilituahidi." "Mwaka 2006, Spika uliniomba nikae kimya kwa kuwa wewe ni kaka yangu, lakini safari hii sitakubali kukaa kimya maana nimesoma vitabu vya bajeti na kitabu cha matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu sijaona barabara hizi," alisema Selelii.

Alisema kitendo hicho cha serikali kushindwa kuipangia bajeti barabara hiyo ni dharau kwa wananchi wa mikoa ya Magharibi na Kanda ya Ziwa. "Humu ndani mawaziri wanatukebehi sisi wabunge…mawaziri wanatudharau sisi na wananchi wa mikoa hii," alisema.

Alihoji, "hivi hadi tuseme Kinyamwezi na Kisukuma humu bungeni ndipo tutaeleweka? Spika akamjibu "Hapana hizo siyo lugha rasmi." Akaendelea kusema, "inauma sana Spika maana hata kuitaja tu barabara hiyo sikuona, inaonyesha serikali haina habari nayo."

Selelii alisema barabara hiyo ikiwamo ile ya Ipole kwenda Nzega zilishafanyiwa upembuzi yakinifu tangu miaka ya nyuma; lakini serikali imeshindwa kuanza ujenzi. Mbunge huyo alihoji "Hivi sisi tumeikosea nini Serikali hii?

Akamwangalia Spika na kumweleza, "Spika wakubwa wenzako humu ndani wana uwezo wa kwenda katika majimbo yao kwa barabara, lakini wewe huwezi ni lazima ukitoka hapa urudi Dar es Salaam ndipo upande ndege kwenda jimboni kwako. Kwa nini sisi tuwe watu wa kudanganywa tu?

Alisema barabara hizo ni muhimu kwa utalii wa mikoa ya Magharibi na Kanda ya Ziwa pamoja na shughuli nyingine za uzalishaji mali, hivyo aliomba mwongozo wa Spika kuona Ofisi ya Waziri Mkuu itafanya nini ili hiyo barabara iingizwe kwenye hotuba yake na Spika akamjibu asubiri kwanza majibu ya Serikali.

Akizungumzia usafiri wa treni, Mbunge huyo alisema tangu reli ya kati ilipokodishwa kwa wageni, abiria wa mikoa ya Magharibi wanapangwa kama kuni kutokana na shida ya usafiri iliyopo. Alisema watu wa mikoa ya Magharibi na Kanda ya Ziwa ni Watanzania wanahitaji usafiri wa uhakika ili kukuza shughuli zao za uchumi.

Hoja hiyo ya Selelii iliungwa mkono pia na Mbunge wa Viti Maalumu, Aziza Sleyum Ally (CCM), ambaye alitaka Waziri Mkuu ampe sababu tano za serikali kutoipangia fedha barabara ya Itigi kwenda Tabora hadi Kigoma.

"Hizi sababu tano mimi na wananchi wetu zitatupa fursa ya kufahamu sababu ya serikali kuisahau barabara hii," alisema Aziza ambaye pia aligusia suala la usafiri wa reli ya kati na kuhoji iweje baada ya kupewa Wahindi tatizo la usafiri wa treni limekuwa kubwa tofauti na hapo awali.

Alisema wasafiri wa treni wanapewa tiketi ambayo haina namba ya kiti hivyo anayewahi ndiye anayekaa. "Yaani hawa wanatufanya kama hapa ni India, hapa sisi ni Watanzania hatukuzoea shida za namna hii." Naye Mbunge wa Singida Kusini, Mohamed Missanga (CCM), alihoji sababu ya serikali kutotunga sera itakayotoa fursa ya miundombinu ya barabara kutengenezwa kwa ubia na sekta binafsi.

Alisema licha ya suala hilo kuafikiwa na serikali, lakini utekelezaji wake unachukua muda mrefu. Missanga alisema licha ya serikali kuwa na kaulimbiu ya kasi mpya, lakini kwa upande wa maamuzi hiyo kasi mpya haionekani kwani kuna mambo mengi likiwamo suala la ujenzi wa daraja la Kigamboni kushindwa kutekelezwa licha ya nia ya ujenzi kuwapo.

Wabunge leo wataendelea kuchangia katika hotuba ya Waziri Mkuu juu ya matumizi ya ofisi yake pamoja na Wizara ya Tamisemi. Kesho serikali itatoa majibu ya hoja zote. Wabunge 105 wameomba kuchangia kwa mdomo, lakini yawezekana ni nusu yao tu watapata fursa hiyo.
 
sasa bunge la tanzania kidogo kidogo linaanza kuelekea kunakotakiwa. Kila mbunge lazima aikabe koo serikali katika kutetea jimbo lake. Na hali hii ikiendelea, kwenye kikao kijacho cha bunge, serikali itajipanga vizuri sana kabla ya kulisogelea bunge, na labda maendeleo kwa wananchi yatapatikana
 
Ukiangalia ki undani sana mikoa ya magharibi,kanda ya ziwa na mikoa ya Nyanda za juu kusini serikali imeisahau kabisa tena haswaaa angalia miundo mbinu,maji,elimu n.k huwezi kulinganisha na mikoa ya kaskazini ukiafuatilia barabara za huko rami tupu na zile za vumbi kila mwaka zinakarabatiwa kila mwaka.
Kunani huko kaskazini?hapo sera ya majimbo inaweza ikaweza kufanya kazi hapo.
 
Nafarijika nikisikia kauli za kutetea maslahi ya umma na si kwenda bungeni na kusahau kilichokupeleka na baadala yake unafanya kazi ya kusafisha watuhumiwa kweli hii inasikitisha na kudhalilisha wananchi wa jimbo lake na taifa kwa ujumla,sijui waliowachagua waliambiwa kuwa katika majukumu yao ni pamoja na kusafisha watuhumiwa?
 
si dhani hasa kama viongozi wetu wanakaa na kupanga kuendeleza mikoa fulani.
mikoa mingi inayoendelea basi huwa ni kwa juhudi za watu binafsi na si kwa juhudi za serikali.

wageni wakitoka nje ya tanzania wakija nchini wanashangaa kuona huduma za sekta binafsi ni nzuri na zina ufanisi mkubwa, wakati huduma kutoka taasisi za serikali ni ovyo kabisa
 
Baadhi ya wabunge wa Mkoa wa Tabora wametishia kutounga mkono bajeti za baadhi ya wizara kutokana na kitendo cha serikali kushindwa kutekeleza ahadi zake hasa katika ujenzi wa barabara ya kutoka Itigi, Tabora kwenda Kigoma.

Hivi bajeti ya nchi si ilipitishwa kwa kura zote za wana CCM, au? Au bajeti za Mawizara sio sehemu ya ile bajeti ya nchi?

Pili, kwanini Mbunge asilete muswada wake wa fedha (appropriations bill) anasubiri serikali?

Kingine, hawa wabunge wanapotaka maelezo baada ya bajeti kuwasilishwa bungeni vipi wasiporidhika na maelezo wakati bajeti inabidi ipite kuwahi mwaka wa fedha unaoanza siku chache zijazo, mwezi July?

Haya majadiliano sio ilibidi yafanyike mwezi wa tano (kama sio wa nne) ili wabunge wapate muda wa kutoa senti mbili zao na kufanya back-and-forth na serikali?
 
Mimi nashangaa kitu kimoja. Vikao vya bunge vinaendelea hadi aug kujadili bajeti za wizara mbalimbali wakati wakati mwaka wa fedha unaanza julai inawezekanaje?Je wizara zinaanza kutumia bajeti ambayo haijapitishwa na bunge?Au je zinasubiri ? Na kama zinasubiri watendaji wanakuwa wanafanya nini mawizarani?Au ndo kielelezo kushindwa wajibu.Napendekeza vikao vya bunge vipangwe kuanza mapema na kuisha by 20th june.
 
nafikiri kabla bajeti kutangazwa bungeni, ilitakiwa miezi kadhaa nyuma draft ya bajeti itayarishwe na ipatiwe kwa wabunge wote.
kisha kila mbunge alitakiwa kupendekeza miradi yake pamoja na makisio ya fedha zitakazo hitajika kupitia wizara husika ( aipigie debe miradi yake kwa nguvu za hoja)
kisha kila wizara hutakiwa kuunda bajeti yake kulingana na vipaumbele vyake.
kisha bajeti kamili huundwa na serikali kuu.

sidhani kama mtiririko huo ulifatwa. au labda baadhi ya wabunge hawajui suala hilo. au mtiririko huo tanzania haupo.

mwenye maelezo zaidi tunaomba kufahamishwa
 
Ni kweli matatizo yaliyo katika maeneo ya magharibi na kanda ya ziwa yana chosha hata kusikia kwani mara zote wabunge kutoka maeneo hayo lakini hakuna dalili yeyote ya kupatia ufumbuzi wa kudumu.
Binafsi siamini kama kweli Seleli na wenzake wako serious katika kuhakikisha majibu ya maswali yao yanapatikana, kwani hakuna jipya wanalokuja nalo zaidi ya kurudia waliyo kwisha sema kipindi kilichopita na mwisho kupitisha Bajeti, walishindwa nini kuzuia bajeti.
Seleli na wenzake wanatakiwa kukaa chini na watu wao na kuja na Plan B ambayo itakuwa jibu kwa malalamiko yasiyokwisha na kusema wengine wanapendelewa. Mawazo mapya yanahitajika jamani! Kila mbunge anapigana kupata coverage katika media ili kwao wamsikie ameongea. Tunataka solutions.
 
"''"""Spika

uliniomba nikae kimya kwa kuwa wewe ni kaka yangu, lakini safari hii sitakubali kukaa kimya maana nimesoma vitabu vya bajeti na kitabu cha matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu sijaona barabara hizi," alisema Selelii.""""


haya mambo kumbe yamo bunge la tanzania,,,kesho si utasema alisema mpwa wangu nisiseme..jamani hawa watu wanania njema ila inaonyesha ndani ya bunge kuna mambo mengi yamejifisha tofauti tunavyofikiria
mungu ibariki tanzania,,seleli komaa baba ila usisikilize watu uko kwa saababu ya wananchi na si spika wako sitta
 
Back
Top Bottom