Sawa mtamkabidhi na Bashir ICC, lakini i wapi Mahakama ya Afrika?

Rubawa

JF-Expert Member
Dec 25, 2015
2,055
3,238
NA MOHAMMED ABDULRAHMAN

Wiki iliopita Sudan ilitangaza kuwa hatimaye sasa itamkabidhi kiongozi wake wa zamani Omar Hassan al-Bashir kwa Mahakama ya jinai ya Kimataifa na maovu dhidi ya binadamu ICC.

Uamuzi huo wa Sudan umekaribisha kwa shangwe na wengi wa Wasudan ambao kiu chao kwa muda mrefu kilikuwa kuona haki inatendeka. Itakumbukwa wito wa kutaka Bashir awajibishwe kuhusiana na maovu yaliofanywa katika kipindi cha miaka 30 ya utawala wake wa kiimla ni miongoni mwa madai ya msingi ya waandamanaji.

2019 wakati alipokuwa bado madarakani Umoja wa Afrika (AU) uliingia kwenye mzozo na mahakama ya ICC pale viongozi wakuu wa Umoja huo walipoamua kutoshirikiana na mahakama hiyo kuhusu kesi ya Bashir.

Viongozi walipitisha azimio mjini Addis Ababa, lililozitaka nchi za kiafrika zisitowe ushirikiano wa aina yoyote. Kupitishwa azimio hilo kukawa na maana Bashir hatokabidhiwa kwa ICC. Zaidi ya hayo ikaamuliwa Kiongozi yeyote wa kiafrika aliyeko madarakani ana kinga na hatowajibika kwa mahakama hiyo. ICC ilitoa waranti wa kukamatwa Bashiri 2009, akikabiliwa na mashtaka ya kuhusika na mauaji ya raia katika jimbo la magharibi la Darfur kufuatia harakati za makundi ya waasi kupambana na serikali .

Bashir alipinduliwa Aprili mwaka jana na wanajeshi wenzake baada ya vuguvugu kubwa la upinzani wa umma lilioanza Desemba 2018 kupinga hatua kali za kiuchumi katika wakati ambao tayari hali ya maisha ilikuwa imevuka kiwango cha uvumilifu.

Mwanzoni wanajeshi walijaribu kudhibiti madaraka kuzuwia mabadiliko lakini walipoona maji yamezidi unga kutokana na umma kuendelea kujizatiti wakasalimu amri na Kiongozi wa kijeshi Luteni Jenerali Abdelfatta Abdelrahman al-Burhani akakubali kuanza mazungumzo ya kuundwa serikali ya Umoja wa kitaifa na kugawana madaraka na raia. Ilikuwa ni baada ya mtangulizi wake Jeneral Awad Ibn Auf kujiuzulu siku moja tu baada ya kumuangusha Bashir kufuatia kukataliwa na Wasudan waliomuona kuwa ni Bashir mwengine kikwazo kwa mabadiliko wanayoyapigania.

Kushirikiana na ICC ni jambo moja, lakini jee atakabidhiwa au kesi yake itasikilizwa na Sudan kwenyewe lakini kwa ushirikiano na ICC?

Kuna wadadisi ambao tayari wana shaka wakiashiria matatizo yaliopo na maswali yanayojitokeza kuhusu kile kinachoonekana ni kuandamwa kwa wahalifu kutoka bara la Afrika pekee.

Uhalifu wa kivita na maovu dhidi ya binadamu haukutendeka sio barani humo tu lakini Amerika Kusini eneo lenye historia ndefu ya tawala za kidikteta ukiukaji wa haki za binadamu na mauaji na hata Asia ambako mfano mmoja ni Sri Lanka katika mzozo na wapiganaji wa Kitamili.

Vita hivyo vilidumu miaka 26 hadi vilipomalizika pale serikali 2009 na serikali kutangaza ushindi. Lakini Sri Lanka imeyakataa madai yote kwamba ilihusika na mauaji na uhalifu wa kivita. Zote mbili Sudan na Sri Lanka si wanachama wa ICC.

Kumeulizwa maswali mengi kwanini Rais wa zamani wa Marekani George W. BUSH na aliyekuwa Waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair wasiwajibishwe kwa kusababisha kwa janga la Iraq kwa kudanganya ulimwengu kwa sababu zisizo na ukweli kuhalalisha uamuzi wao?

Jengine panapohusika na utendaji wa ICC ni kwanini Sudan imekubali kumkabidhi Bashir wakati mwanzoni Luteni Jenerali al-Burhan alisema Sudan haitafanya hivyo na kama kuna kesi ya kujibu itasikilizwa ndani ya Sudan?

Inaelekea ni ule usemi wa mwenye nguvu mpishe na masikini hana chaguo.

Huenda hatua hiyo inatokana na jitihada za Sudan kutaka kustawisha tena uhusiano wake na Jumuiya ya kimataifa na hasa nchi za Magharibi yakiongozwa na Marekani. Chini ya uongozi wa Bashir ikishutumiwa kuwa mongoni mwa mataifa yaliokuwa yakifadhili au kuunga mkono ugaidi, madai ambayo Bashir aliyakanusha. Juu kabisa katika orodha hiyo ni Iran.

Ingawa Sudan kimsingi iliondolewa vikwazo vya kiuchumi na Marekani 2017 kuipa fursa ya kuzungumza na Shirika la Fedha Duniani IMF kuhusu mzigo wake wa madeni na msaada mpya imekuwa ikikabiliwa na tatizo jengine. Tatizo hilo ni kuwemo katika orodha ya Marekani ya mataifa yanaunga mkono ugaidi.
Ombi la Sudan lilikabifhiwa kwa naibu Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Sullivan alipoizuru Mei mwaka jana.

Waziri mkuu Abdullah Hamdok akasisitiza pia juu ya haja ya nchi yake kufutwa katika orodha hiyo ili kusaidia kufanikiwa mchakato unaoendelea wa kipindi cha mpito alipofanya ziara mjini Brussels kuzungumza na Umoja wa Ulaya mwezi Novemba kutafuta uungaji mkono.

Upande mwengine ni Njia moja wapo ya kuhakikisha serikali ya mseto kati ya wanajeshi na raia ilioundwa kuongoza kipindi cha mpito haitumbukii kwenye msukosuko. Kipindi hicho ni cha miaka mitatu ambapo itaandaliwa katiba mpya na uchaguzi utakaopelekea Sudan kurejea katika utawala kamili wa kiraia.

Pamoja na hayo kungali na wasiwasi miongoni mwa makamanda wa kijeshi. Hofu walio nayo juu ya kumkabidhi al-Bashir katika mahakama ya ICC ni kwamba hatimaye wanaweza wakajumuishwa na wengine miongoni mwa makamanda na wanajeshi wa kawaida walioshiriki vita vya Darfur, 2003 hadi 2008. Kati ya wanaonyooshewa kidole na wanaharakati wa haki za binadamu ni kiongozi wa kikosi maalum (RSF) Jenerali Mohamed Hamdani Dagalo maarufu kwa jina la Hemeti

Na ndiyo maana haikushangaza awali pale Luteni Jenerali al-Burhan aliposema Sudan haitomkabidhi Bashir bali mashtaka yanayomkabili yatasikilizwa nchini Sudan ingawa alinukuliwa hivi karibuni wakati akizungumzia kuwa sasa iko tayari kushirikiana na ICC akisema” hakuna mtu aliye juu ya sheria.”

Tayari al-Bashir anatumikia kifungo cha miaka 2 kwa ufisadi. Akiwa amehamishia gereza jengine, kabla ya kesi yake, mara tu alipoangushwa alipelekwa gereza la Kober ambako kwa miaka mingi ndiko alikowafunga wapinzani wake.

Bado haijajulikana lini utaanza mchakato wa kumkabidhi Bashir The Hague makao makuu ya mahakama hiyo ya Kimataifa.
Utata uliopo ni kuwa Luis Moreno-Ocampo Muargentina aliyekuwa mwendesha mashtaka mkuu wa ICC na mtu aliyetoa waranti wa kukamatwa Bashir 2008 na kutaja mashtaka 10 yanayomkabili ametajwa na baadhi ya wananaomkosoa alikuwa mtu aliyeshindwa kuwajibika ipasavyo..

Uaminifu wake ulianza uliekewa mashaka aliposhindwa kuhakikisha haki inapatiokana kwa wahanga katika kesi wanasiasa wawili Uhuru Kenyatta na William Ruto kuhusu kuhusika kwao na machafuko na mauaji yaliotokea wakati wa uchaguzi mkuu Desemba 2007. Karibu watu 1,000 waliuwawa.

Kesi hiyo hatimaye ilifutwa kwa kile kilichotajwa kuwa ni kukosekana ushahidi kuweza kuishawishi mahakama kwamba wanasiasa hao walikuwa na mashtaka ya kujibu.Wakati wa machafuko hayo, Uhuru na Ruto walikuwa katika kambi tafauti za kisiasa kabla baadaye kuungana kisiasa 2012 na kushinda uchaguzi kwa Uhuru kuwa rais naRuto naibu wake. Walichaguliwa tena 2017.

Ikiwa Bashir hatimaye atapandishwa kizimbani atakuwa wa Kiongozi wa tatu wa zamani baada ya Charles Taylor wa Liberia na Laurent Gbagbo, lakini pamoja na kwamba haki lazima itendeke, itazidisha malalamiko ya kwamba wanaoendelea kuandamwa na mahakama hiyo ni waafrika peke yao. Taylor alihukumiwa kifungo cha miaka 50 anachokitumikia nchini Uingereza, kwa kupatika na hatia ya kuhusika katika vitendo vya uhalifu wa kivita na maovu dhidi ya binadamu katika nchi jirani ya Sierra Leone alikowasaidia waasi na kunufaika kwa kuchota almasi.

Gbagbo kwa sasa bado anaishi Ubeligiji tokea alipoachiwa huru na mahakama ya kimataifa mjini Tha Hague, ilipomkuta asiye na hatia, kuhusiana mashtaka ya uhalifu wa kivita na maovu dhidi ya binadamu kufuatia vurugu baada ya uchaguzi nchini mwake Cote d´Ivoire 2010.

Bila shaka kupandishwa kizimbani kwa waafrika tu The Hague ni matokeo ya udhaifu wa Afrika kuhakikisha mahakama yake yenyewe inafanya kazi kama ilivyokusudiwa kusimamia sheria na haki barani humo. Mahakama ya Afrika iliundwa 2004 ikiwa na makao yake mjini Arusha Tanzania na wadadisi wanasema utashi wa kisiasa umechangia mno kuzorotesha utendaji wake.

Wakati huohuo, pamoja na kuwepo kwa hisia tafauti na maoni yanayokinzana kuhusu Rais wa zamani wa Sudan kukabidhiwa mahakama ya ICC, lakini yaliomkuta Omar Hassan al-Bashir ni ujumbe kwa watawala wengine wa kimla ni kwamba ukandamizaji wa demokrasia na haki za binadamu hauwezi kudumu milele, siku moja sheria huchukua mkondo wake.

Chanzo Raia Mwema/ Baruapepe : mamohamed55@hotmail.com
Twitter: mamkufunzi




Sent using Jamii Forums mobile app
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom