Sasa tumekaribia kufika | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Sasa tumekaribia kufika

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by dally, Oct 6, 2010.

 1. d

  dally Member

  #1
  Oct 6, 2010
  Joined: Nov 4, 2009
  Messages: 19
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Na Ruhazi Ruhazi  SIJALI bado umbali gani katika safari yetu, lakini nimepata matumani, nimefarijika na kufurahi baada ya kuona kundi kubwa la watu walipo kwenye safari yetu sasa wamebaini kuwa tumekaribia kufika mwisho.

  Wote wamechoka lakini wanajipa moyo na kujikaza kisabuni, hawajali uchovu tulionao nao sote wanaimba na kushangilia tunajikongoja na kuendelea na safari yetu.

  Kila mmoja wetu anafahamu kuwa safari yetu ni ndefu, yenye mashaka na kwa ujumla ni ya hatari, lakini watu wanahimizana kukaza mwendo, nami napata nguvu za kuuendeleza wimbo wa hamasa kwao.

  Wimbo wetu unakolea kidogo kidogo pamoja na uchovu tulionao, uliotokana na adha tulizokumbana nazo katika safari, lakini nafurahi kuona wenye nia na dhamira ya kufika mwisho wa safari yetu wanaongezeka kila tupigapo hatua.

  Hii inanipa matumani, naagaza kuangalia kule tulikotoka sioni, napaona tulipo, lakini sio mimi wala yeyote miongoni mwetu anayepajua huko tuendako, ila tunapata matumaini ya kukaribia kufika.

  Matumaini yetu yanachochewa na misemo kadhaa ya wahenga, kama vile "Ukiona kiza kinazidi basi ujue kunakucha", na kwa kiza hiki kinachozidi kujitokeza katika kila nukta ya maisha yetu napata imani kuwa karibu Watanzania tutafika huko tuendako japo hatujui umbali uliobaki.

  Safari yetu ni ya kwenda kwenye maendeleo, safari ambayo kwa miaka nenda miaka rudi tumekuwa tukiongozwa na baba na mwana, yaani Chama cha TANU na mwanawe wa kwanza CCM.

  Nadhani ni sahihi nikisema wote hawa uongozi wao haukuwa wa kiuungwana bali kwa nyakati tofauti walizotuongoza wamekuwa wakituburuza, wakitulazimisha kwenda watakavyo na sio kama tutakavyo sisi.

  Lakini sina shaka tena sasa kuwa watanzania wamezinduka kwenye lile lepe la usingizi walilolala na sasa wananena kwa lugha ya nmana moja kwamba hakuna kudanganywa wala kulazimishwa kufanya tusichokitaka.

  Waliosoma makala yangu ya wiki iliyopita watajua vema nilichokisema na kinachotokea sasa, kwa ambao hawakusoma niliandika tujitokeze na kuwasikiliza wagombea kisha tuwaulize ahadi, wale ambao tuliwapa dhamana ya kutuongoza kisha wakatuacha mbugani kabla ya kufika safari yetu.

  Wanajifanya kuturudia tena sasa wamekausha nyuso zao kama vile hakuna kibaya walichotutendea, hawana soni sio watu hawa ni wanyama waovu, hawafai kuendelea kuwepo katika jamii yetu.

  Kilichojitokeza mwishoni mwa wiki iliyopita na kilichotokea juzi katika mikutano ya kampeni ya mgombea urais kupitia CHADEMA, DK. Willibrod Slaa, huko Kyela, mkoani Mbeya kinadhihirisha pasipo shaka kuwa tunakaribia kufika.

  Wananchi walimpokea kwa mabango, wakamwambia karibu rais wetu mteule, wakanyanyua mabango yasemayo hatudanganyiki tena tunafanya uamuzi ambao hatutaujutia wa kukupa urais.

  Lakini hawakuwa waongo, wanafiki wala vizabizabina, bali walimweleza wazi kwamba pamoja na dhamira yao ya kumpigia kura za urais, ila kwa upande wa ubunge hawatampigia kura mbunge kutoka CHADEMA, bali watamchagua tena mbunge wao wa sasa Dk. Harrison Mwakyembe kutoka CCM.

  Walifafanua hapo hapo kwamba Mwakyembe anazijua na kuzijali shida zao, ni mtetezi wao anataka kuwapelekea maendeleo japo anakwamishwa na watu wengine ndani ya CCM na hilo wao wanalijua hivyo hawawezi kumuhukumu kwa sababu ya kuangushwa na watu wengine.

  Maneno matamu sana haya kutoka kwa wana Kyela, na ndiyo yanayonifanya niamini kuwa karibu tunafika katika safari yetu, mabango yao yasemayo "Kikwete bye bye Dk. Slaa karibu Ikulu, Kofia, Kanga, T Shirt na Pombe si mahitaji yetu kwa sasa" yamebeba ujumbe mzito kwa mwenye akili, yanaonyesha ni jinsi gani walivyozinduka na walivyo tayari kwa mapinduzi.

  Wananchi hawa wanaonyesha ni jinsi gani sasa wako tayari kupigania haki yao, ni vipi wataweza kujinusuru kwa kura zao na pia wanasimama kuwakumbusha wengine kwamba muda wa kutizamana usoni na kuchaguana kwa sababu tu ya kutoka CCM umepita.

  Wamewapa Watanzania wote tafsiri moja tu kuwa inawezekana tukaikomboa Tanzania ya kesho, iwapo sisi sasa tutaacha unafiki, tukawa wakweli, tukaacha kuhukumu kwa kuwafurahisha watu fulani, tukawasikiliza wagombea na kuwaambia ukweli.

  Wale ambao wamefanya vema licha ya kufanya kazi katika mazingira magumu ya kubanwa na CCM tuwape haki yao stahiki, tuwaambie asanteni, tuwapigie makofi ya pongezi na kuwasifu kwa walivyotuongoza kuelekea huko tupatakapo.

  Tuwaambie ukweli kuwa tunawarudisha tena waendelee kutuongoza katika safari hii ndefu, ngumu na yenye maashaka makubwa ya kuelekea kwenye maendeleo, safari ambayo tumeianza tangu Desemba mwaka 1961, tulipopata uhuru wetu kutoka kwa wakoloni.

  Wale waliotupa ahadi nyingi nzuri lakini wakashindwa kuzitekeleza, tuwaambie watupishe hatuna haja nao, hatutaki kufanywa wajinga au kutumikishwa kama watumwa na kupewa tusischokitaka kwa wakati tusioutaka.

  Tuwaambie hadharani kuwa tunataka kuwachagua viongozi ambao tutawatuma na wakaenda haraka, tutawaita na wakaja kwa kukimbia sio kwa kutembea kwa nyodo na maringo kama walivyokuwa wakitufanyia wabunge na madiwani wa CCM.

  Watu ambao walifikia hatua za kutudharau, wakisahau kuwa ni kura zetu ndizo zilizowafikisha hapo walipo, wakafikia hatua za kuuza viwanja vya kuchezea watoto wetu na vile vya kupumzikia, lakini hawakuwajibishwa hata tulipowashitakia kwa marais wetu wakati huo.

  Hapana! Tumewachoka na muda umefika wa sasa wa sisi kusimama na kuwakatalia maombi yao hadharani, tuwaambie kuwa hatutawachagua kwa sababu hawakutenda tulichowatuma acha tuwachague wale ambao tutawatuma na wakatutekelezea.

  Wale ambao watatuletea kile tukitakacho kwa wakati tuutakao, tofauti na wao ambao walikaidi na kujichukulia maamuzi kila baada ya kupita uchaguzi mkuu.

  Ninaamini na ndio ukweli wenyewe kuwa maendeleo ya kweli tuyatakayo, yataletwa na viongozi kutoka vyama vya upinzani, ambao watakuwa tayari kutumikia sisi badala ya kuwatumikia viongozi wa juu na swahiba zao.

  Ni kutokana na hilo ninawaomba Watanzania kila mmoja kwa nafasi yake popote alipo, aelewe kuwa jukumu la kuikomboa Tanzania ya kesho linapaswa kuanza leo hivyo kila mmoja wetu analo jukumu na wajibu wa kufanya maamuzi haya ya kuwachagua watu watakaotutumikia.

  Kila mmoja anapaswa kukumbuka na kumkumbusha mtu wake wa karibu umuhimu wa kuwasikiliza wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi ili tuweze kujua ni nani kati yao tunaopaswa kuwachagua ili tuwatume tupatakapo.

  Kisha tunapaswa kukumbushana na kuhimizana kuwa sote tunaowajibu wa kujitokeza na kuwachagua viongozi waadilifu siku hiyo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, ili tuwapate watu tuwatakao.

  Wale ambao watatuongoza kuelekea katika safari yetu hiyo ndefu ya kuelekea kwenye maendeleo ya kweli tuyatakayo ambayo, bila shaka yoyote tutaikamilisha iwapo Oktoba 31 tutafanya uamuzi wenye busara wa kuwapiga chini wasanii na badala yake tuwachague wale ambao tunawataka.

  Watu tutakaowaamini, ambao kuwachagua kwao hatutaangalia ubora au uchanga wa vyama vyao bali uwezo wao na jinsi wanavyotusikiliza tunapowatuma ambao watatuongoza badala ya kututawala, ili mwisho wa wote tufike katika safari yetu ya maendeleo.
   
 2. Henge

  Henge JF-Expert Member

  #2
  Oct 6, 2010
  Joined: May 14, 2009
  Messages: 6,767
  Likes Received: 78
  Trophy Points: 145
  Thanks mkuu!
   
 3. e

  ejogo JF-Expert Member

  #3
  Oct 6, 2010
  Joined: Dec 19, 2009
  Messages: 994
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 35
  yep!
   
 4. kibhopile

  kibhopile JF-Expert Member

  #4
  Oct 6, 2010
  Joined: Aug 5, 2010
  Messages: 1,309
  Likes Received: 128
  Trophy Points: 160
  good job.
   
 5. W

  We know next JF-Expert Member

  #5
  Oct 6, 2010
  Joined: Sep 9, 2010
  Messages: 664
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 35
  Hakika tunakaribia kufika Mkuu!
   
 6. omarilyas

  omarilyas JF-Expert Member

  #6
  Oct 6, 2010
  Joined: Jan 24, 2007
  Messages: 2,127
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 0
   
 7. The Dreamer

  The Dreamer JF-Expert Member

  #7
  Oct 6, 2010
  Joined: Feb 2, 2009
  Messages: 1,280
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Swadakta
   
Loading...