Ni Wizara ya Mifugo na Uvuvi au Uvivu?
Nizar Visram
Toleo la
371
17 Sep 2014
HATIMAYE, Mahakama imewaachia huru wavuvi raia wa China na kuamuru serikali iwarejeshee vitu vyao ikiwemo meli ya Tawaliq. Washtakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya uvuvi haramu katika Ukanda wa Uchumi wa Tanzania. (EPZ).
Hivyo, serikali imebwagwa katika kesi hiyo maarufu kama kesi ya ‘samaki wa Magufuli' iliyofunguliwa mwaka 2012 wakati Dk. John Magufuli akiwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.
Waliachiwa huru baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha mahakamani hati ya kuwaondolea mashitaka (
nolle prosequi) .
Hii ni mara ya pili kwa wavuvi hao wa kigeni kuachiwa. Mara ya kwanza waliachiwa na Mahakama ya Rufaa Machi 28 mwaka huu, lakini walikamatwa tena na kushtakiwa upya kwa mashtaka hayo hayo yaliyofutwa.
Sasa mahakama imewaachia huru na kuamuru warejeshewe vitu vyao vilivyokuwa vinashikiliwa. Hapo ndipo pagumu, kwani meli ya Tawaliq ilizama baharini wakati kesi ikiwa bado inaendelea.
Hii ni baada ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kushindwa kuitunza tangu ilipokamatwa Machi 8, 2009 ikiwa na tani 293 za samaki aina ya Jodari iliyowavua katika bahari ya Tanzania (EPZ) bila kibali.
Meli hiyo ilizama baada ya wajanja wachache kukata vyuma vyake na kuviuza. Walibeba vifaa vya shaba na kwenda kuviuza mitaani.
Halikadhalika, samaki waliokutwa ndani ya meli hiyo wanaokadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi bilioni mbili wote waligawiwa katika taasisi mbalimbali kwa uamuzi wa Waziri Magufuli. Hapo awali alitaka kuwauza, lakini baada ya kukosa wanunuzi, alidai kuwa "serikali haiwezi kufanya biashara."
Kabla ya kuwagawa samaki hao, walikuwa wamehifadhiwa katika bohari ya barafu mali ya kampuni binafsi. Yaani serikali ililipa fedha nyingi kuwahifadhi na kisha ikawagawa bure.
Bahati mbaya wananchi hawaambiwi ni sababu zipi zilifanya mashtaka kufutwa. Ni kwa sababu hakukuwa na ushahidi wa kutosha? Kama ni hivyo kwanini basi tuingie hasara zote hizo bila ya kuhakikisha kuwa kuna ushahidi wa kutosha?
Kwanini mara ya kwanza watuhumiwa hao waachiwe huru na mahakama halafu wakamatwe tena kwa mashtaka hayohayo? Labda wataalamu watatusaidia.
Kwa upande wa mashtaka kuwasilisha ombi la ‘nolle prosequi' ni kitu ambacho kinatia wasiwasi. Kuna wanaolaumu ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG). Pia kuna wanaoelekeza lawama kwa Magufuli.
Chama kimoja cha siasa kimemtaka Rais Kikwete amfukuze kazi Magufuli kwa kuisababishia hasara Serikali. Wanasema mazingira ya kesi yalikuwa hayaonyeshi kuwa watuhumiwa hao wanaweza kushinda na kuibwaga Serikali.
Wanasema ni vizuri Kikwete pia aangalie kwa umakini ofisi ya mwanasheria mkuu pamoja na wanasheria wa serikali kutokana na "kushindwa kwa kesi mara kwa mara."
"Kuna uwezekano baadhi ya vijana wake wanachukua rushwa ili kukwamisha baadhi ya kesi kwa kuandaa maelezo yasiyojitosheleza," kimesema chama hicho.
Sijaona maoni ya vyama vingine au hata asasi za kiraia. Labda wanaona ni afadhali kuzungumzia bunge la katiba tu, mambo mengine si muhimu. Bila shaka mengi yanaweza yakasemwa kuhusu jinsi kesi hii ilivyoendeshwa hata serikali ikaangukia pua. Nchi imeingia hasara ya mabilioni, na itashangaza iwapo tutanyamaza kimya kana kwamba hakuna tatizo.
Ila wakati tunazungumzia kesi hii, ni vizuri pia tukaangalia kwa mapana suala zima la uvuvi haramu na jinsi unavyoathiri nchi yetu pamoja na jirani zetu. Kwani hili ni suala nyeti sana, ni changamoto inayotukabili sote.
Hii kesi ya "samaki wa Magufuli" ni mfano mmoja tu unaotuonyesha jinsi maliasili yetu ya baharini inavyoporwa. Tumekuwa tukizungumzia gesi, mafuta na madini wakati bahari yetu pia ni chanzo kikubwa cha maliasili ambayo inaporwa kwa wingi.
Wataalamu wanakisia kuwa uvuaji haramu unalinyima taifa letu asilimia 80 ya mapato ambayo yangepatikana kutoka sekta ya uvuvi. Pia wanakisia kuwa inawakosesha mapato wavuvi wadogo wapatao 40,000 ambao wanashindwa kupata samaki wa kutosha kutokana na uvuvi haramu.
Kwa ujumla watu milioni nne katika nchi hii wanategemea sekta ya uvuvi ili kuendesha maisha yao kutokana na bahari na mito. Huu ni umuhimu wa sekta ya uvuvi.
Mwambao wa Tanzania bara una urefu wa kilometa 750 wakati Unguja na Pemba zina mwambao wa kilometa 675. Haya ni maeneo yenye samaki wengi wa kila aina pamoja na vivutio vingine.
Bahati mbaya serikali imeshindwa kudhibiti uharibifu wa chanzo hiki cha utajiri. Kuna wanaovua samaki wadogo sana, wengine hutumia mabomu au kemikali. Wengine hutumia nyavu zenye tundu ndogo na wengine hutumia hata gesi.
Matokeo yake ni uteketezaji wa mazalia ya samaki kama matumbawe, mapango na mikoko pamoja na uchafuzi wa maji ya bahari.
Katika bahari zetu ndipo uvuvi haramu unaendeshwa kwa kiasi kikubwa, tena ni wizi wa kimataifa unaofanywa na meli za kigeni zinazoingia katika ukanda wa kiuchumi. Ni ukanda wa maili 200 ambao kwa mujibu wa sheria ya kimataifa ni bahari inayodhibitiwa na Tanzania.
Bahati mbaya udhibiti huu ni dhaifu mno na ndipo inakisiwa tunapoteza zaidi ya dola milioni 220 kila mwaka kutokana na uvuvi wa magendo unaoendeshwa na meli za kigeni. Udhaifu huu si wa Tanzania tu bali ni pamoja na nchi za jirani, kwani bahari si sawa na ardhi. Hatuwezi kuweka alama za mipaka, kisha samaki hawatambui mipaka. Leo wako Tanzania kesho wanahamia Msumbiji. Meli pia inaweza kuhama kwa urahisi kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine.
Matokeo yake ni kuwa bara la Afrika linapata hasara kubwa. Kwa mfano ripoti ya mwaka 2005 ilisema Angola ilikuwa inapoteza dola milioni 49 kila mwaka. Wakati huohuo Somalia ilikuwa inapoteza dola milioni 94. Guinea, Liberia na Sierra Leone zilipoteza dola milioni 140 na Msumbiji dola milioni 38.
Hivyo, uvuvi haramu ni tatizo linaloikumba si Tanzania tu bali nchi zote zilizo mashariki mwa Afrika na hata Afrika nzima.
Ripoti kadha zimeeleza kuwa tatizo hili linazidi kuongezeka kutokana na kutoaminika kwa maofisa wahusika ambao wanahongwa. Kwa mfano mara nyingi wavuvi wadogo hukamatwa kwa kutumia nyavu ndogo. Viwanda vya nyavu viko ndani ya nchi lakini havichukuliwi hatua zozote. Na hata kama nyavu zinatoka nje, wanaoziingiza hawaulizwi, na ilhali kuna maofisa wa forodha wenye wajibu wa kudhibiti uingizaji wa nyavu hizo.
Halafu kuna viwanda ambavyo vinamimina maji yenye sumu za kemikali katika mito, maziwa na bahari. Matokeo yake ni kuchafua maji na kuua samaki pamoja na mimea ya majini. Hawa nao hawachukuliwi hatua za kisheria ipasavyo.
Tatizo la uvuvi haramu kwa hivyo linachangiwa na uzembe wa watawala wetu. Matokeo yake mamia ya meli za kigeni zinaingia katika bahari za Afrika na zinavua kila aina ya samaki bila ya leseni. Ripoti moja iliyofadhiliwa na Uingereza inasema kwa njia hii Afrika kwa ujumla inapoteza dola bilioni moja kila mwaka.
Kisheria ilitakiwa tutunze samaki wetu wasiibiwe na wavuvi kutoka nje. Kama ilivyo dhahabu na gesi yetu, na samaki wetu pia ilitakiwa tuwe tunasafirisha nje na fedha kuingia nchini mwetu. Hii haifanyiki. Ndipo serikali inakosa kodi na ushuru kutokana na uvuvi na usafirishaji haramu wa samaki.
Sheria ya kimataifa inatupa haki ya kudhibiti utajiri huu. Ndio maana mwaka 1982 ilipitishwa sheria ya bahari inayosema kuwa maili 200 kutoka ufukwe ni eneo letu na maliasili yote iliyo chini ya bahari hiyo ni mali yetu.
Hivyo, tuna wajibu na haki ya kuhakikisha kuwa meli za kigeni haziingi katika eneo hili kiholela na kuchukua maliasili hii bila ya kibali chetu. Ukiachia lile tatizo la maofisa wetu wasio na uadilifu, kuna tatizo lingine kubwa la kutokuwa na nyenzo na weledi ili kufuatilia jambo hili.
Mpaka sasa Namibia na Afrika Kusini zimefaulu kwa kiasi fulani, nasi ni vizuri kushirikiana nao. Ni kwa sababu si rahisi kwa nchi moja moja kudhibiti uvuvi haramu. Tunahitaji kushirikiana katika kupeana Habari na utaalamu. Meli hizi huwa zinahamahama kutoka eneo moja kwenda eneo jingine.
Tatizo hili la uvuvi haramu limekuwa likizungumzwa muda mrefu. Mwaka 2008 nchi wanachama wa jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika (SADC) zilitangaza kuwa zitashirikiana ili kutokomeza uvuvi haramu katika nchi hizo zinazopakana na bahari ya Hindi.
Mawaziri wanaohusika na uvuvi kutoka nchi za Tanzania na SADC wakakutana nchini Namibia na wakajadili suala la uvuvi haramu katika bahari ya Hindi. Magufuli akawaambia wenzake kuwa Tanzania inapoteza utajiri wa baharini kutokana na uvuvi haramu.
Akasema meli nyingi za kigeni zinaingia katika ukanda wa uchumi na kuvua bila leseni. Matokeo yake Tanzania ilikuwa inapoteza dola milioni 220 kila mwaka, akasema Magufuli.
Akaongeza kuwa takwimu ilionyesha kuwa kulikuweko na meli si chini ya 171 zilizosajiliwa mnamo 2004. Lakini hakuna hata moja kati ya hizo ambayo ilikuwa ikiripoti idadi ya samaki waliowavua kama wanavyotakiwa kisheria, na serikali haikuwa na uwezo wa kufuatilia. Ili kufuatilia meli hizi serikali ilihitaji boti ziendazo kasi pamoja na ndege.
Maana yake ni kuwa meli nyingi zinakwepa usajili na kuendelea kuvua bila ya lesenin. Na sasa tunaona meli moja iliyokamatwa na kufikishwa mahakamani inafutiwa mashtaka. Mwandishi mmoja aliilaumu wizara ya maendeleo ya mifugo na "uvivu".
Labda aliteleza na kuandika uvivu badala ya uvuvi. Lakini msomaji mmoja alisema "kosa" hilo linakubalika kwani kuna uvivu uliokithiri katika wizara hiyo na serikali kwa ujumla.
Source:
Raia Mwema - Ni Wizara ya Mifugo na Uvuvi au Uvivu?