1 Basi kwa habari ya mambo yale
mliyoandika, ni heri mwanamume
asimguse mwanamke.
2 Lakini kwa sababu ya zinaa kila
mwanamume na awe na mke
wake mwenyewe, na kila
mwanamke na awe na mume
wake mwenyewe.
3 Mume na ampe mkewe haki
yake, na vivyo hivyo mke na ampe
mumewe haki yake.
4 Mke hana amri juu ya mwili
wake, bali mumewe; vivyo hivyo
mume hana amri juu ya mwili
wake, bali mkewe.
5 Msinyimane isipokuwa
mmepatana kwa muda, ili mpate
faragha kwa kusali; mkajiane
tena, Shetani asije akawajaribu
kwa kutokuwa na kiasi kwenu.
6 Lakini nasema hayo, kwa kutoa
idhini yangu, si kwa amri.
7 Ila nipendalo ni kwamba watu
wote wawe kama mimi nilivyo;
walakini kila mtu ana karama
yake mwenyewe itokayo kwa
Mungu, huyu hivi, na huyu hivi.
8 Lakini nawaambia wale wasiooa
bado, na wajane, Ni heri wakae
kama mimi nilivyo.
9 Lakini ikiwa hawawezi kujizuia,
na waoe; maana ni afadhali kuoa
kuliko kuwaka tamaa.
10 Lakini wale waliokwisha
kuoana nawaagiza; wala hapo si
mimi, ila Bwana; mke asiachane
na mumewe;
11 lakini, ikiwa ameachana naye,
na akae asiolewe, au apatane na
mumewe; tena mume asimwache
mkewe.
12 Lakini watu wengine
nawaambia mimi, wala si Bwana,
ya kwamba iwapo ndugu mmoja
ana mke asiyeamini, na mke huyo
anakubali kukaa naye asimwache.
13 Na mwanamke, ambaye ana
mume asiyeamini, na mume huyo
anakubali kukaa naye, asimwache
mumewe.