BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,769
- 288,332
Dowans yataka Tanesco ibanwe
Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 1st May 2009 @ 18:51
Habari Leo
Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 1st May 2009 @ 18:51
Habari Leo
Kampuni ya kufua umeme ya Dowans Tanzania Limited imeiomba Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara ikatae maombi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) dhidi ya kuuzwa kwa mitambo yake ya kufulia umeme nchini.
Mbele ya Jaji Robert Makaramba juzi, Wakili wa Dowans Abduel Kitururu alidai kuwa maombi ya Tanesco hayana msingi wowote kwa kuwa shirika hilo limewasilisha mahakamani maombi yake kwa kutumia kifungu kisichokubalika katika kuwasilisha maombi hayo.
Katika maombi yake, Tanesco inaiomba mahakama iizuie Kampuni ya Dowans kuuza mitambo yake kwa namna yoyote hadi shauri lililowasilishwa na Kampuni ya Dowans kwenye Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa iliyoko Paris, Ufaransa, itakapotolewa uamuzi.
Kwa namna nyingine, Tanesco inaiomba mahakama iiamuru Dowans iweke mahakamani asilimia 10 ya dola 109,857,686 za Marekani kama dhamana, kutokana na gharama zitakazotumika katika kesi hiyo.
Katika hoja zake zilizowasilishwa mahakamni hapo kupinga maombi hayo, Wakili Kitururu alisema Tanesco imepeleka maombi hayo kwa kutumia kifungu 95 cha sheria ya mwenendo wa madai na Ibara ya 23 (2) ya sheria inayojulikana kama International Chamber of Commerce Rules.
Kwa mujibu wa hoja hizo, ibara hiyo haiwezi kuipa mamlaka Mahakama ya Tanzania kushughulikia maombi kama yaliyowasilishwa na Tanesco nchini, bali kipengele hicho cha sheria kinaweza kutumiwa na upande husika katika shauri kwenye mahakama ya kimataifa kutafuta amri ya zuio kabla kesi ya msingi haijamaliza kusikilizwa.
Alisema pia kuwa hata kifungu cha sheria kilichopo chini ya mwenendo wa madai nacho hakiipi mahakama kujielekeza mamlaka yake kusikiliza na kutolea uamuzi wa maombi yaliyowasilishwa mbele yake na Tanesco.
Wakili huyo alisema kuna uamuzi uliowahi kutolewa na mahakama ya rufaa nchini na nje ya nchi ambayo yanabainisha kuwa maombi yoyote yanayoletwa na mwombaji bila kutumia kifungu cha sheria kinachotakiwa, hayawezi kutiliwa maanani na mahakama na hutupiliwa mbali.
Wakili Alex Nguruma anayeitetea Tanesco, atatakiwa kuwasilisha hoja zake za majibu Mei 6 mwaka huu. Juni 23, 2006 Tanesco iliingia makubaliano ya usambazaji wa umeme wa dharura na Kampuni ya Richmond, ambayo ilielekeza majukumu yake kwa Kampuni ya Dowans Holding SA. Baadaye, Dowans Holdings ilielekeza majukumu yake kwa Kampuni dada ya Dowans Tanzania Limited.
Baada ya mapitio ya makubaliano hayo na upungufu uliojitokeza Juni 30 mwaka jana, Tanesco iliiandikia Dowans ikieleza kuwa uhamishaji huo wa majukumu ya kiutendaji haukuwa halali. Novemba 2, 2008 Dowans ilifungua kesi katika mahakama ya kimataifa ikidai dola 109,857,686 kama gharama za huduma za umeme ambazo zilikuwa hazijalipwa.
Kwa upande wake,Tanesco iliwasilisha maombi ya kutaka iongezwe muda wa kuwasilisha utetezi Novemba 11,2008, katika mahakama hiyo, lakini kabla kesi hiyo haijafikia mwisho, Dowans ilitangaza kuuza mitambo yake. Kitendo hicho kilikuwa na lengo la kuvuruga namna ukazaji wa hukumu itakayotolewa na mahakama hiyo ya kimataifa juu ya gharama za kuendesha kesi hiyo kwa upande wa Tanesco.