Role and significance of tribal norms in good governance and china`s evil plan for Africa

zacha

JF-Expert Member
Feb 28, 2009
1,064
2,000
ROLE AND SIGNIFICANCE OF TRIBAL NORMS IN GOOD GOVERNANCE AND CHINA`S EVIL PLAN FOR AFRICA.

NA Cde a.s. Ulanga

Napenda kutoa maoni yangu kuhusu haya mambo mawili ambayo nimeyasoma katika Group, ulilolianzisha.


Mjadala wa “Significance of Tribal Norms in Good Governance” unaonyesha kuwa kuna ombwe kuhusu “norms” ambazo mimi naziita “Mila, Desturi, na Kanuni. Na “good governance” huzungumzwa panapokuwa na ombwe katika “uongozi”. Na hii hutokea wakati Taifa linapofuata dhana ya “Utawala” na kuacha dhana ya “Uongozi”.


Napenda kujikumbusha kwamba mambo yanayohusu “tribal norms and good governance” ndiyo yaliyokuwa katika fikra za Baba wa Taifa Mwl. J.K.Nyerere mara baada ya Uhuru wa Tanganyika tarehe 9/12/1961. Fikra hizo ndizo zilizomfanya ajiuzulu Uwaziri Mkuu tarehe 22/1/1962.

Maandishi na Mapokeo yanatuambia kuwa alijiuzulu ili apate nafasi ya kujifunza vitendo katika jamii, Mila, Desturi na Kanuni. Utaratibu wa kujifunza vitendo katika jamii kwa ajili ya kupata mawazo mapya, umeelezwa na Mao-Tse-Tung kwa kusema, “Mawazo sahihi hutoka katika vitendo vya kijamii, na katika vitendo vya kijamii tuu, huwa na aina tatu ya vitendo vya kijamii, mapambano ya kitabaka, mapambano ya uzalishaji mali na majaribio ya kisayansi. (Mao-tse Tung: Four Essays on Philosophy; Peking Foreign Languages Pres: 1966 uk 136-tafsiri ni yangu).


Maelezo haya yanaweka msingi wa kiyakinifu wa kujifunza mifumo ya jamii kwa Mwanafikra mwenye fikra za aina fulani kutambua ni mfumo gani wa jamii upo katika jamii, katika kipindi husika, na hapo ni pamoja na “norms and governance” ambazo zipo katika matabaka yaliyopo.


Baba wa Taifa alitaka kujifunza upya vitendo katika jamii kwa sababu Uhuru uliondoa Ukoloni kwa maana ya bendera, lakini vitendo katika jamii vilikuwa bado vya kikoloni na kwamba Machifu wa makabila mbalimbali ndiyo waliokuwa wahimili wa “norms” zao, ambazo zisingeweza kujumuishwa wakati ule ili ziwe “norms” za Taifa ambalo alidhamiria kuliasisi.


Mapokeo yanatueleza kuwa alijifunza mambo mengi, ikiwemo siasa, uchumi, maendeleo ya jamii, mila na desturi, uongozi pamoja na utawala. Baada ya kutafakari mambo aliyojifunza akayaweka mahali pamoja katika ile Insha mashuhuri iitwayo “Ujamaa – The Basis of African Socialism”.


Kwa kusoma na kutafakari Insha ile utaona kuwa Baba wa Taifa alijifunza vitendo katika jamii kiyakinifu na aliona kuwa Ujamaa utajibu hoja ya kuwa na mfumo wa jamii ambao utahusisha siasa, uchumi, maendeleo ya jamii, mila na desturi, uongozi na utawala. Mfumo ambao utaondoa baadhi ya “tribal norms”ambazo zilikuwa za kibaguzi, uonevu kwa wanawake na vitu vingine ambavyo havingestahimiliwa katika Taifa jipya.


Baada ya kutoa Isha ile, Baba wa Taifa alianza kuueneza ujamaa, kuanzia katika Chama chake cha TANU, katika nchi ya Tanganyika, Taifa la Tanganyika na baadaye Taifa la Tanzania, na wakati wote wa uhai wake.


Ndiyo maana katika Tanzania yapo maelezo mengi kuhusu Ujamaa na Ujamaa na kujitegemea. Lakini mimi nitaeleza machahe sana yanayohusu hoja yangu.

1. Uthibitisho kuwa Baba wa Taifa ndiye aliyeasisi fikra za Ujamaa. Hayo yapo aliposema, “Nilikuwa wa kwanza kutumia neno Ujamaa kueleza maisha tunayotaka kuishi katika nchi yetu…! Alimalizia maelezo haya kwa kusema, “…Hivi ndivyo tunavyotaka kuishi kama Taifa. Tunataka Taifa lote tuishi kama familia moja” (Uhuru na Umoja uk. 137-tafsiri ni yangu).
Hapa pamoja na uthibitisho mimi naona kuwa ameonyesha tofauti kati ya Nchi na Taifa, jambo lenye umuhimu wa pekee.


2. Ujamaa ni Imani, kwani hauna budi kujengwa na watu wanaoamini kanuni zake (norms) (Azimio la Arusha na Siasa ya TANU juu ya Ujamaa na Kutjitegemea uk. 8)

3. Maelezo kuwa ujamaa unaeleza mawazo yetu kwani unapinga ubepari na unapinga utaratibu wa kujenga Taifa katika misingi ya uhasama baina ya mtu na mtu. (Ujamaa uk.12). Napenda kukubaliana na (Crankford Pratt aliposema, “Ni kwamba Itikadi ya ujamaa wa Tanzania ina asili halisi ya Kiafrika. Siyo utekeelzaji wa fikra za Kiafrika zilizotokana na fikra zilizoigwa kutoka Ulaya. (Crankford Pratt- The Critical Phase in Tanzania 1945-1968- Nyerere and the Emergency of Socialist Strategy-uk. 6 –tafsiri ni yangu). Kwa hiyo siyo sahihi kuendelea kuuita “Ujamaa” kuwa ni “ Usoshalisti”. Hilo ndilo lililoleta woga na hofu kwa baadhi ya Mataifa ya Magharibi, kwani wao wanajua kuwa “Usoshalisti” ni hatua ya kwanza kueleekea kwenye ukomunisti. Na wao wakati ule walikuwa wanapiga vita ukoministi.


Ijapokuwa Baba wa Taifa alianza kuelezea ujamaa kwa kutumia neno usoshalisti, yeye alitumia utaratibu wa kueleza kitu kigeni kwa kutumia kile kinachofahamika. Lakini nawashangaa wanasiasa na wasomi ambao huendelea kuuita ujamaa kuwa ni “usoshalisti”.

4. Baba wa Taifa alieleza kuwa, “Sababu kubwa ya kuwa na ujamaa ni maisha bora ya watu na msingi wake mkubwa ni watu kuukubali usawa wa binadamu” (Ujamaa uk. 75,76). Lakini Baba wa Taifa aliendelea kusema kuhusu msingi wa kukubali usawa wa binadamu kuwa, “Mtu asiyekubali msingi huo anaweza akakubali mawazo mengi yaliyotolewa na wapenda ujamaa, lakini yeye si mfuasi wa ujamaa” (Ujamaa uk. 75,76). Hii ndiyo changamoto iliyopo.


5. Maelezo ya msingi kuhusu ujamaa yamo katika kile kitabu kidogo kinachoitwa “Azimio la Arusha na Siasa ya TANU juu ya Ujamaa na Kujitegemea”.


6. Urasimishaji wa Ujamaa – Ujamaa umerasimishwa kuwa mfumo wa maisha ya Taifa la Tanzania kwa kuwekwa katika Ibara 3(1) ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na katika Ibara ya 9. Dola imepewa utaratibu wa kutekeleza mfumo wa Ujamaa na Kujitegemea.


7. Mapokeo ya Baba wa Taifa kuhusu Maisha ya Ujamaa- Utaona kuwa aina ya maisha aliyotaka tuishi ni ya kudumisha Uhuru na Umoja, kuwa na usawa, udugu, Demokrasia, haki, wajibu, upendo, wema, ukweli, utii, kuthamini kazi, na kwamba kuhusu mambo ya kiuchumi, lugha iwe yetu, chetu, vyetu n.k.

Hapa nimetaja baadhi ya mambo ambayo alitaka yawekwe katika “norms” za Taifa ndani ya ujamaa na yawe kwa wananchi wote.


Aidha Baba wa Taifa alitaka Taifa lipige vita uonevu, wizi, rushwa, ufisadi, ubaguzi, uzururaji, ubabaishaji na “norms” zote zisizoendana na mfumo wa maisha ya ujamaa.


Ukiacha mambo ya siasa na uchumi, hizo nilizotaja hapa juu alitaka zijenge msingi wa “norms” za Taifa kwa kutumia dhana ya “Uongozi-Leadership”.


Ndiyo maana alianza kuueleza “Ujamaa” katika Chama cha TANU ambacho kilitumia dhana ya Uongozi katika kuikomboa nchi. Na katika kuasisi na kujenga Taifa, Baba wa Taifa alitaka TANU kiwe Chama cha Uongozi wa shughuli za jamii ikiwa pamoja na “norms”. Ndiyo maana muundo wake ulianzia kwenye “shina.”


Mambo mengi aliyoyaongoza Baba wa Taifa katika TANU na baadaye CCM yalilenga kuwa na “norms” za kitaifa za kuchochea ujenzi wa ujamaa na kujitegemea ili kuwaletea wananchi maendeleo. Nitaeleza machache:-

1. Kuingiza fikra za ujamaa katika katiba ya TANU 1962.
2. Kuuondoa Uchifu katika mfumo wa utawala wa nchi na wananchi.
3. Kupiga marufuku vyama vya kikabila
4. Kuhamasisha matumizi ya Kiswahili
5. Kuanzisha Chuo cha Uongozi – Kivukoni
6. Kuanzisha Jeshi la kujenga Taifa
7. Kupitisha Azimio rasmi la Ujamaa na kuliweka katika kitabu kiitwacho “Azimio la Arusha na Siasa ya TANU juu ya Ujamaa na Kujitegemea”. Kwa kifupi “Azimio la Arusha”. Kujitegemea, kuliunganishwa na ujamaa baada ya mambo yaliyolipata Taifa kati ya mwaka 1964-1966.
Baba wa Taifa aliieleza nafasi ya Azimio la Arusha, katika hotuba aliyoitoa Dodoma tarehe 5/2/1987 aliposema, “Azimio la Arusha ndilo linaloeleza Itikadi ya Chama chetu.


Ndiyo kauli kuu ya lengo letu na misingi yetu, ndilo msingi wa maamuzi yote ya Sera za Chama na Serikali”


Baada ya Azimio la Arusha iliwekwa mikakati ya ujenzi wa Ujamaa na kujitegemea kwa kutumia Dola, na kutunga sera za kutekeleza mikakati hiyo. Baadhi ya sera zinazohusika na hoja yangu ni-Ujamaa vijijini-Elimu ya kujitegemea – Waraka wa Rais Namba 1 wa 1969 na Ushirika.


Kwa maoni yangu sera hizo zililenga kulifanya Taifa liwe familia moja. Ndiyo maana Taifa zima tulikuwa tunaitana “Ndugu”.


8. Kuandika kitabu cha “Ujamaa”.
9. Kuunganisha vyama vya TANU na ASP kuwa CCM. Katika “Azimio la Mkutano Mkuu wa Taifa wa Pamoja wa TANU na ASP uliofanyika tarehe 21/1/1977 tunasoma “Chama tunachokiunda tunataka kishike barabara hatamu za uongozi wa shughuli zote za umma kwa maslahi ya wafanyakazi na wakulima wa Taifa letu…” “Chama tunachokiunda tunataka kiwe chombo madhubutu katika Muundo wake na hasa katika fikra zake…”


10. Kujenga msingi wa uchumi wa kijamaa kwa kuunganisha kilimo na viwanda ili Taifa lijitegemee.

11. Kutamka rasmi kuwa Taifa la Tanzania halifungamani na siasa ya upande wowote katika vita baridi kati ya mataifa ya magharibi na mashariki.

12. Kurasimisha ujamaa na kujitegemea katika katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kama tunavyosoma katika Ibara 3(1) na utekelezaji wake katika Ibara 9-(a-k). Jambo hili lilifanya ujamaa na kujitegemea kuwa mfumo rasmi wa maisha katika Tanzania

13. Kutoa Mwongozo wa CCM 1981.
Pamoja na kutoa ufafanuzi kuhusu fikra na mfumo wa ujamaa na kujitegemea, Mwongozo ulionya juu ya kuwepo kwa vishawisi vya ubepari kwa kusema katika Ibara ya 36, “Aidha kuna matatizo ya kijamii kama vile kuongezeka kwa rushwa, hujuma za kiuchumi, wizi, ujambazi, ubadilifu wa mali ya umma, mambo ambayo yanatupunguzia nguvu zetu za kiuchumi na kudhoofisha dhamira ya kujenga ujamaa. Ibara ya 52 ilitoa maelezo zaidi kuwa, “Leo ubepari una vishawishi zaidi nchini kuliko ilivyokuwa kabla ya Azimio la Arusha. Kwa sababu pamoja na kwamba sasa tuna sekta kubwa ya Umma, lakini kutokana na udhaifu wa kupambana nao, ubepari umefaulu kujipanua na kujipenyeza hata ndani ya sekta yenyewe ya Umma. Na ndiyo maana ubepari sasa unathubutu kujitokeza hadharani kukashifu Ujamaa, kubabaisha baadhi ya viongozi na kutaka tubadilishe siasa yetu”.


14. Kutoa sera ya Ushirika wa Uzalishaji mali Vijijini. (1985) Ushirika kuwa nguzo ya kujenga Ujamaa na Kujitegemea.

15. Kutoa Programu ya Chama cha Mapinduzi 1987-2002-Ilieleza utekelezaji wa Ujamaa na kujitegemea katika kipindi cha Mpito kuelekekea kwenye ujamaa na kujitegemea.

Nilikuwa Mkufunzi wa mada,”Utekelezaji wa Azimio la Arusha katika kipindi cha Mpito kutoka uchumi ulio nyuma na wa kikoloni- Mamboleo kuelekea Ujamaa na Kujitegemea”


16. Kutoa Mwelekeo wa Sera za CCM katika Miaka ya Tisini. Mwelekeo ule ulibadilisha mkakati wa dhana na nadharia ya kuwatumia wananchi wenyewe katika ujenzi wa Ujamaa. Ibara ya 5 ilisema, “Siasa ya msingi ya CCM itaendelea kuwa ujamaa na kujitegemea kwa kuzingatia kwamba ndiyo iliyotuundia mazingira ya Amani, utulivu na umoja wa Taifa letu, na ndiyo siasa inayolingana na matarajio ya wananchi walio wengi”
Aidha Ibara ya 6 inasema, “Lengo la ujamaa na kujitegemea katika Miaka ya Tisini litakuwa kuhakikisha kwamba wananchi wenyewe wanamiliki na kuendesha uchumi wa nchi yetu”.


17. Mwelekeo wa Sera za CCM katika Miaka 2000 hadi 2010- Mwelekeo ulibaini kuwa ujinga, umaskini na maradhi ni matokeo ya uchumi ulio nyuma (Backward Economy) na tegemezi. Kwa hiyo ulielekeza kuwa kazi iwe ni kujenga msingi wa uchumi wa kisiasa wa Taifa linalojitegemea (Modenaizeni ya uchumi) na kwamba kazi hiyo iende sambamba na kuwawezesha wananchi kiuchumi.


Baada ya maelezo haya marefu ya mikakati ya kujenga Ujamaa ili kuwe na “norms” za kitaifa na vile vile kujitegemea ili tusiwe tegemezi kwa mataifa wala ya magharibi wala ya mashariki na tusishirikiane wala ubepari wala ukomunisti. Linalofuata ni kujiuliza nini kilitokea mpaka kufikia baadhi yetu kukumbuka “tribal norms” na kuogopa” China’s Evil Plan for Africa?”

Kwa maoni yangu, jibu lipo katika Ibara ya 52 ya mwongozo wa CCM 1981, ambayo sehemu yake nimeinukuu hapo awali.

Aidha tafakari yangu inanifanya nikumbuke nadharia ya Taasisi inayosema kuwa taasisi ni mambo makubwa matatu kwa pamoja. Lengo, Wadau na Mazingira yanayoizunguka taasisi. Katika hoja hii nalichukulia Taifa kuwa ni taasisi.


Taifa huwa na lengo, huwa na wadau ambao ni wananchi na viongozi, mazingira ambayo ni mataifa mengine au nchi zinazolizunguka Taifa na mataifa mengine duniani, na taasisi na mashirika ya kimataifa. Mataifa na taasisi za kimataifa zinaweza kuwababaisha baadhi ya viongozi na wananchi ili kupiga vita na kutaka kubadilisha lengo la taifa.

Katika Tanzania tujiulize, kwa nini tunashabikia ukabila, uchifu na kubishana juu ya matumizi ya Kiswahili. Kutotilia mkazo dhana ya uongozi, hasa katika vyama vya siasa. Watu wanapewa majukumu ya uongozi bila kuandaliwa. Uongozi hujengwa juu ya misingi ya Imani na Imani inapatikana kwa kutumia dhana ya uongozi kwa mafundisho, maelezo, majadiliano ya hoja, ushawishi na makubaliano.


Hali hiyo hujaenga uelewa wa pamoja wa mambo ya msingi yanayohusu uongozi ambao hutokana na Imani ya Chama cha siasa na taifa na hivyo kujenga utaifa na uzalendo. Kwa mfano, uelewa wa sera ya Ujamaa Vijijini ni kuwafanya wananchi waishi mahali pamoja ili iwe rahisi kuwaptaia huduma muhimu za miundo mbinu, maji, shule, umeme, huduma za afya, mawasiliano n.k ili maisha ya vijijini yalingane na maisha ya mijini hivyo kuwafanya wananchi wasikimbilie mijini na kuwa “Lumpen ploritariat”.


Sera ya Elimu ya Kujitegemea ililenga kuzalisha mafundi mchundo hata sanifu wa kutumika katika viwanda na hivyo kuendeleza sera ya kujitegemea.


National Vocational Training Division (NVTD) ilianzishwa ili kuwapima (Trade Test) wanafunzi waliomaliza miaka miwili ya “Post Primary Education”. Shule za Sekondari za mafunzo maalumu kama vile ufundi, biashara, kilimo zilianzishwa kwa ajili ya kuwapata mafundi sanifu baada ya kufanyiwa mitihani ya kidato cha nne. Waliopasi vizuri ndiyo walioendelea na elimu ya form v na vi, wakiwa na ujuzi waliokuwa nao tangu shule za msingi!


Mambo ya kueleza ni mengi, lakini kwa maoni yangu jambo jingine ni ukosefu wa uelewa wa pamoja wa dhana ya nchi na Taifa. Nchi ni dhana inayotokana na ardhi amabyo huwekewa mipaka kwa ajili ya utawala wa nchi yenyewe na wananchi, kwa kutumia dhana ya taifa. Taifa hutokana na wananchi katika jamii ya kitabaka. Na ili taifa litambulike huwa na lengo litokanalo na Imani. Imani hutokana na fikra baada ya kujifunza jamii ya nchi husika na kuwa na uelewa wa pamoja kwa kutumia dhana ya uongozi kama nilivyoeleza hapo awali.


Mambo haya yapo katika kujifunza uyakinifu katika historia (Historical Materialism). Na ni mambo hayo yaliyokuwemo katika ukombozi wa nchi zetu Tanganyika na Zanzibar, Uasisi wa mataifa ya Tanganyika na Zanzibar na uasisi wa Taifa la Tanzania. Dhana iliyotumika ni uongozi ambayo Baba wa Taifa aliupanua na kuiingiza katika “Ujamaa” na baadaye “Ujamaa na Kujitegemea”.


Kama nilivyosema hapo awali alianzisha “National Norms” na kwamba taifa la Tanzania katika kujitegemea lijikinge na kuingiliwa na wala mataifa ya magharibi wala mashariki.


Mambo yaliyotokea hivi karibuni katika taifa letu la kuingiliwa na mataifa ya magharibi na mifumo yao wanayoiita ya kimataifa yalifanya taifa letu liwe kama Shamba la Bibi. Kutokana na utajiri wa Ardhi ya nchi yetu mataifa ya mashariki hasa China yalijiona kama wamechelewa kuvuna utajiri wa ardhi ya nchi zetu na wakatafuta mkakati wa kuingia na ndipo tukaona fikra za “China’s Evil Plan of Africa”.Sasa tufanye nini na kwa nini? Hayo ni maswali ambayo nayaelekeza kwa Makada wenzangu tuliobaki, Wafanyao utafiti kuhusu mambo ya msingi ya CCM, na wasomi wenye kuelewa historia ya taifa hili na kulitakia mema katika maendeleo yake kisiasa, kiuchumi, na kijamii.Kwa maoni yangu, mahali pazuri na kuanzia ni kutafakari yale mambo machache niliyoyaeleza hapo juu aliyoyaongoza Baba wa Taifa katika TANU na baadaye CCM aliyotaka yawe msingi wa “Norms” za taifa, kama nilivyoeleza kutoka 1-17, hapo juu.Katika tafakari hiyo naomba tuongezwe na maandishi na Hotuba za Baba wa taifa, TANU na CCM na baadhi yake ni:-

1. Kitabu cha TANU na Raia

2. Kitabu cha Tujisahihishe

3. Ile Insha mashuhuri inayoitwa “Ujamaa the Basis of African socialism”

4. Kitabu “Azimio la Arusha na Siasa ya TANU juu ya Ujamaa na Kujitegemea”

5. Kitabu cha “Ujamaa”

6. Mwongozo wa TANU 1971

7. Katiba ya CCM 1977, hasa “Azimio la Mkutano Mkuu wa Taifa wa Pamoja wa TANU na ASP” uliofanyika tarehe 21/1/2977

8. Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, hasa sura ya Tisa

9. Mwongozo wa CCM 1981

10. Hotuba ya Baba wa Taifa aliyoitoa tarehe

5,February 1987, inayoitwa “Kujitawala ni kujitegemea”

11. Hotuba ya Baba wa Taifa aliyoitoa Oktoba 22, 1987.

12. Programu ya CCM 1987-2002

13. Hotuba ya Baba wa Taifa aliyoitoa kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa Taifa wa Agosti 16, 1990, inayoitwa “Wosia wa Mwalimu Nyerere kwa CCM.

14. Mwelekeo wa Sera za CCM katika Miaka ya Tisini

15. Mwelekeo wa Sera za CCM katika Miaka ya 2000 hadi 2010

16. Hotuba ya Baba wa Taifa inayoitwa “Peace, Unity and People-Centred Development in Africa”, iliyopo katika kitabu kinachoitwa “Africa Today and Tomorrow” hasa uk 23.

Lakini wakati tunaposoma na kutafakari maandishi haya, tuwe tunaangalia na kutafakari maneno yaliyomo katika Nembo ya Taifa la Tanzania, “Uhuru na Umoja”. Maneno haya kwa maoni yangu, Uhuru unatutaka tukumbuke mapambano ya kukomboa nchi zetu, Tanganyika na Zanzibar. Mpambano yaliyotufanya tujitambue kuwa sisi katika umoja wetu wa kitabaka la wakulima na wafanyakazi ni wanyonge, kama tunavyokumbushwa katika Kitabu cha Azimio la Arusha uk. 9.

Neno “Umoja” linatutaka tukumbuke Uasisi wa Mataifa ya Tanganyika na Zanzibar na hatimaye Taifa la Tanzania. Tunatakiwa tukumbuke kuwa Taifa lazima liwe na lengo, likitaka liwe endelevu. Na lengo la Taifa la Tanzania ni kujenga, “Ujamaa na Kujitegemea”.


Comrade, mambo ya kutafakari ni mengi, lakini kwa hoja hii ya “Tribal Norms and China’s Evil Plan For Africa”, maandishi haya yatasaidia katika kujenga uelewa wa pamoja kuhusu jambo hili.


Lakini naweza kuulizwa kwa nini kutafakari na kufanya utafiti kuhusu mambo haya yote? Hoja yangu ni “Ownership and Sustainability” ya mambo anayoyafanya Rais Magufuli. Yeye anaendeleza fikra na ndoto za Baba wa Taifa. Lakini anaonekana kama vile yuko peke yake, ana wafuasi wachache sana kama alivyokuwa Baba wa Taifa. Hii inadhihirishwa na woga wa kweli walio nao baadhi ya watu, kuwa huenda baada ya kamliza muda wake tunaweza kurudi nyuma.


Hapo ndipo hoja ya “Ownership and Sustanability” Inapokuwa na umuhimu.
Ijapokuwa katika CCM huwa kuna Ilani ya uchaguzi, lakini Ilani hiyo haionyeshi “Owneship” kwani haionyeshi uunganisho wa Imani, na sera za msingi za Chama hicho, kwa viongozi wanaosimamia utekelezaji wa Ilani hiyo.

Ndiyo maana napendekeza kuwa kwa kutumia dhana ya uongozi ambayo Baba wa Taifa aliweka ndani ya “Ujamaa” na kwa kutumia kanuni ya wakati wa mahali tunaweza kuziendeleza “National Norms” alizoanzisha Baba wa Taifa. Aidha kwa kuendeleza “Kujitegemea” tunaweza kuondoa woga wa “ China’s Evil Plan for Africa”, na haya yanawezekana tuu kwa kutumia “Ujamaa na Kujitegemea” kwa pamoja. Na siyo “Kujitegemea” peke yake kama inavyopendekezwa katika Katiba Mpya. Kwa kufanya haya ndipo tunapoweza kujenga “ownership and sustainability”.


Camrade, naona kuwa nimejieleza sana na huenda hiyo ikawa mada yangu ya mwisho, kwani sasa nakumbuka mafundisho ya “kujifunza kusahaulika bila kusahau niliyojifunza”, hasa fikra za Baba wa Taifa kwani mimi ni muumini na mfuasi wa fikra zake.
 

The weekend

JF-Expert Member
May 3, 2020
250
500
Mwalimu alikua na maono ya mbali, but ujamaa ni lazima uchanganye na ubepari kdogo
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom