Robert Mugabe na Chimurenga,Afrika Kusini na xenophobia

May 3, 2019
53
150
ROBERT MUGABE NA CHIMURENGA,AFRIKA YA KUSINI NA XENOPHOBIA.

Leo 10:20am,07/09/2019.

Pumzika kwa Amani komredi Robert Mugabe rafiki wa Tanzania na mwenzi katika harakati.

Komredi Robert Mugabe mwanamapinduzi wa kuigwa katika bara la Afrika na mzalendo wa kweli wa Afrika.

Komredi Robert Mugabe,Shujaa uliyepambana na Mawaziri Wakuu wote wa Uingereza,Pumzika kwa amani,hakika umetuachia kitabu chenye kurasa nyingi za kujifunza ujasiri na uthubutu wako.

Komredi Robert Mugabe msomi kweli kweli uliyewapita wazungu kwa shahada saba za umahiri hata kupewa tuzo na Malkia,ulipinga ubeberu wa mataifa makubwa ya magharibi dhidi ya ustaarabu wa Kiafrika na wa watu wa Zimbabwe ambapo ilipelekea Malkia wa Uingereza kukupokonya tuzo ya "knighthood" lakini haukujali na daima uliendelea kuwapinga wazungu na kuwatetea waafrika wazawa wa Zimbabwe.

Mwalimu Robert Mugabe sera zako za Elimu, Afya na Ustawi wa Jamii zilipigiwa mfano hata na mataifa makubwa wa Magharibi.

Ulikuwa ukifanya kazi ofisini kwa saa 16. na ahadi kuu ya ukombozi wa Zimbabwe iliyowekwa na ZANU kwa watu wa Zimbabwe uliitimiza kwa kuirudisha ardhi ya Zimbabwe kwa Wananchi wa Zimbabwe ili Wazimbabwe wapate matunda ya Uhuru kupitia kugawiwa ardhi.

Utekelezaji wa ilani ya chama cha Zanu ikawa chanzo cha mgogoro mkubwa na ugomvi wako na mawaziri wakuu waliofuatia wa Uingereza baada ya Magreth Thatcher.

Daima tutaikumbuka sera yako ya ' indigenisation of the economy' ikiwa na maana ya kunyang'anya ardhi kwa nguvu kuwapa wazawa na kununua ugomvi wa Wananchi na wakubwa. Kukawa na vitisho vya wenye mashamba - Wazungu kumpeleka Mugabe mahakamani.

Mugabe akawajibu;

" I, Robert Mugabe, cannot be dragged to court by a settler".

Ahsante Robert Mugabe,hakika umewaonyesha wazungu namna mwafrika anayejitambua anavyokuwa,ulikuwa kiongozi mahiri uliyetetea waafrika na kuacha kuwafuata Mabeberu namna wanavyotaka,japo hivi sasa tunaaminishwa kuwa asiyefuata watakayo mabeberu ni dikteta,hili ni somo kwetu waafrika kuwa kabla ya kukubaliana na wanavyosema mabeberu ni muhimu kujifanyia utafiti wa kina na kujidhihirishia wenyewe,je wana jema lolote kwetu awa mabeberu!?

-Kumbukizi za harakati kumuondoa Ian Smith nchini Zimbabwe.

Katika mkutano wa Wakuu wa nchi uliofanyika London,Uingereza mwaka 1966,Mwalimu Julius Nyerere aliomba hatua zichukuliwe kwa mtawala wa Zimbabwe ikiitwa Rhodesia enzi hizo kwa ubaguzi mkubwa dhidi ya wazawa wa Zimbabwe.

Waziri Mkuu wa Uingereza alikataa na kupendekeza yafanyike majadiliano na maridhiano kabla ya kumuondoa Ian Smith nchini Zimbabwe.

Ndipo Viongozi wa nchini za Afrika wakaitisha mkutano wao uliopewa jina "Nibmar" (No independence before Majority African rule" hakuna Uhuru kabla ya Afrika yote kuwa huru.

-Robert Mugabe Mwanamapinduzi mwenye kufikiri.

Mwaka 1979 Uingereza ilifikia makubaliano ya kuicha huru Zimbabwe na kutengenezwa kwa katiba mpya ya Jamhuri ya Zimbabwe na mwezi wa pili mwaka 1980 uchaguzi wa kwanza wa serikali mpya ulifanyika.

Uchaguzi ulimalizika kwa ushindi mkubwa sana kwa Robert Mugabe ingawa kulikua na malalamiko kutoka kwa baadhi ya watu,lakini kwa sentensi moja tunasema Zanu ilipata ushindi wa kutosha.

Ushindi wa Mugabe ulimaanisha Wazungu wengi(Masetla) waanze kufunga mizigo yao tayari kwa kuondoka Rhodesia, Hii ilileta furaha kubwa kwa Wazimbabwe ambao kwa furaha walikesha wakicheza mitaani.

Hotuba za mwanzo za Rais Robert Mugabe zikaweka mambo sawa, Rais Mugabe aliahidi serikali yenye ushirikiano,na kuondoa mawazo ya wengi ya namna yoyote ya kutaifisha mali binafsi, lengo lake lilikuwa ni kufikia maridhiano na makubaliano na masetla waliokuwa na ardhi kubwa ya mashamba yenye rutuba.

-Afrika ya kusini na Xenophobia.

Ghasia dhidi ya wahamiaji kutoka mataifa ya Afrika nchini Afrika ya kusini sasa limeota mizizi na kushamiri katika tabaka la Wazulu nchini Afrika Kusini,Shukrani kwa maafisa wa usalama na serikali ya Afrika kusini kulaani vitendo hivyo.

Kundi la vijana ambao hawana ajira linatumia kigezo cha ajira kuwapiga wahamiaji wa kiafrika kutoka nje ya Afrika kusini wanaoishi katika mji kama Durban Afrika kusini jambo lililochangia viongozi kutoka vyama vitatu vikuu kushutumu mashambulio dhidi ya raia wa kigeni.

Mamia ya watu wamekuwa wakionekana wakikimbia na kupora mali za watu katika maeneo mengi yenye shughuli za kibiashara wakichoma moto maduka yanayoaminiwa kumilikiwa na wahamiaji kutoka mataifa ya Afrika.

Ghasia,vurugu na uporaji zilienea katika maeneo ya Jeppestown, katika wilaya ya kati yenye shughuli za biashara,zikasambaa hadi kwenye maeneo mengine kama vile Denver, Malvern, Turffontein, Tembisa na maeneo mengine ya vitongoji vya jiji la Johansburg.

Awali tulidhani ni vurugu na uhuni tu wa vijana lakini kadri siku zilivyokwenda tuliona kikundi kikubwa cha watu kinachoelekea katikati mwa jiji na wanasomba kila wanachokiona njiani.

Ni siku za huzuni kwa bara la Afrika wakati watu wanapoamua kutumia kigezo cha ajira,kuua na kuendeleza ukiukaji wa sheria au uhalifu .

Kinachoendelea Afrika ya kusini sasa ni zaidi ya utumwa wa mtu nweupe dhidi ya mweusi,maana ni mwafrika anaumuua mwafrika mwenzie kisa ajira na ikiwa asilimia themanini ya maliasili ya bara la Afrika bado haijatumika kutengeneza ajira.

-Afrika ni moja.

Rais Mugabe tulimpiga tafu wakati wa kugombea uhuru wa taifa la Zimbabwe na yeye alitupiga tafu sana kwenye utawala wa awamu ya pili ulipoingia madarakani huku nchi ikiwa hoi kifedha mwaka 1985.

Undugu kufaana wakati wa dhiki, siyo kama Wasouth Afrika wanachoma waafrika wenzao moto,lakini Afrika iliwatunza,Rais Mandela alipewa passport ya hadhi maalum na Mwalimu Julius Nyerere na kufanywa raia wa muda wa Tanzania.

Tusihangaike na mitizamo ya watu,wakati Makaburu wakimwona Nelson Mandela ni Mhaini Wananchi wa Afrika kusini walimwona ni Mkombozi. Wakati Martin Luther King Jr akionekana ni mchochezi nchini Marekani, Wamarekani weusi walimwona ni mkombozi wao, wakati Robert Mugabe akirudisha ardhi kwa wazawa,Wazungu mabeberu walimuona ni Dikteta, lakini wazawa walimwona Mkombozi.

Kiongozi yeyote mahiri anayetetea waafrika na kuacha kufuata Mabeberu wanavyotaka tutaaminishwa kuwa ni dikteta kwa hiyo kabla ya kukubaliana na wanavyosema mabeberu ni muhimu kujifanyia utafiti wa kina na kujidhihirishia wenyewe kama mibeberu inatutakia mema.

Ahsante Mwenyezi Mungu kwa ajili ya maisha ya Robert Gabriel Mugabe,Pumzika kwa amani mwamba wa Afrika.

Nikiishia hapa,Mimi ni,
Msemakweli Chakubanga,
Morogoro.
0755078854.
 

BURUTA

JF-Expert Member
Apr 27, 2015
313
500
Ilikuwaje tena miaka 37 baadaye Wazimbabwe walijitokeza kuikomboa tena nchi yao?
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom