Riwaya zipo sokoni

Hassan Mambosasa

JF-Expert Member
Aug 2, 2014
2,663
2,000
RIWAYA: KOSA


MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA

SIMU:+255713776843
+255762219759

WHATSAPP:+255713776843


SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU
MUUMBA WA DUNIA NA VILIVYOMO KWA KUNIPATIA
AFYA NJEMA ILIYONIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA
HII KWA MARA NYINGINEANZA SASA KUUFUATILIA MKASA HUU


SEHEMU YA KWANZA!!

Sauti ya kulalamika ilisikika ikitoka ndani ya chumba kimojawapo cha nyumba ya kifahari iliyopo katikati jiji la Tanga, ni ndani ya mtaa ambao una makazi ya watu wenye nazo katika jiji hili katika maeneo ya Raskazone. Kijana mmoja mwenye asili ya kisomali aitwae Hassan alikuwa akilalamika mbele ya pacha wake anayeitwa Hussein, machozi yenye kutiririka mithili ya chemchem ya maji ndiyo yalikuwa yamefunika mboni za macho yake hadi akawa anaona ukungu katika macho yake. Hussein alikuwa ana kazi ya kumbembeleza pacha yake huyo aliyelia akilitaja jina la msichana, kilio chake kilikuwa ni uchungu tosha kwa pacha wake aliyekuwa anambembeleza. Neno mapenzi ndiyo lilitawala kinywa cha Hassan muda wote aliokuwa analia, kupende ndiyo kulimliza kijana huyo. Muda wote mapacha hawa ambao wanapendana kwa dhati wakiwa wanabembelezana, hawakutambua kama waliacha wazi mlango wa chumba chao wanacholala zaidi ya mmoja kulia tu na mwingine akiweka mawazo yake katika kumbembeleza mwenzake.
"Hassan hebu nyamaza basi wanawake wapo wengi utapata mwingine tu" Hussein alimwambia pacha wake.
"Hussein unajua inauma sana yaani Jabir kaamua kumroga Mariam ili apendwe yeye inauma, inauma kuona mtu ninayempenda kwa dhati anachukuliwa na mtu mwingine ambaye ni rafiki wangu wa karibu" Hassan aliongea kwa masikitiko huku machozi yakimbubujika machoni mwake.
"hebu wacha fikra zako potofu, una uhakika gani kama kamloga Mariam. Kaka Mariam ndiyo kapenda pale, nakushauri tu uachane na fikra za huyo mwanamke. Tafuta anayekupenda" Hussein aliongea huku akiwa amemshika pacha wake bega.
"Mariam na urembo wake wote ule atampendaje masikini kama yule mwenye kusomeshwa na mfadhili tu halafu aniache mimi niliyekuwa nina uwezo wa kumlisha na kumvalisha" Hassan aliongea.
"kaka mapenzi si pesa wala mali ndiyo utayapata, mapenzi ni kuweza kuuteka moyo wa mtu ndiyo utayapata na moyo wa mtu hautekwi kwa pesa" Hussein aliongea.
"Hussein na wewe usinichanganye kabisa, nimekuambia namtaka Mariam na nitampata kwa gharama yoyote ile na hata ikiwezekana kuondoka na maisha ya mtu. Yaani kuogopa kwangu kumuambia kama nampenda ndiyo njia aliyoitumia Jabir kumpata yeye, nasema sikubali hata kidogo na Jabir nitamshikisha adabu kwa pesa tu. Mbele ya hela hakuna kinachoshindikana na hata mapenzi yanawezekana" Hassan aliongea kwa hasira kupingana na ushauri wa pacha wake.
"PWAA! PWAA! PWAA! PWAAA! PWAAA!" sauti ya mtu akipiga makofi ilisikika ikitokea mlangoni mwa chumba chao wanacholala. Wote kwa pamoja walishtuka kisha wakageuka upande ambao sauti hiyo imetokea, walishtuka zaidi baada ya kumuona baba yao akiwa amesimama katikati mlango akiwa anawatazama.
"sijaona mtoto wangu mwenye akili na mwenye kutoa ushauri mzuri na wenye manufaa kama wewe Hussein na sijaona mtoto asiye na akili na mwenye kudanganywa na pesa za baba yake kama wewe Hassan" Baba yao aliongea huku akitembea kusogea mahali walipo Hassan na Hussein hadi alipowafikia kisha akaendela kuongea, "pesa si chochote si lolote ndani ya dunia hii wanangu hasa kwenye mapenzi, yaani we Hassan nilidhani kukaa chuo miaka miwili utakuwa umekua kiakili kumbe bado huna akili hata za kufikiria. Kakuambia mwanamke analogwa ili kumpenda mtu ndani ya dunia hii, mwenzako kauteka moyo na usitake utende kosa kama nililotenda mimi baba yako ambalo ninalijutia hadi leo".
"kosa!, kosa gani hilo baba?" Hussein aliuliza huku uso wake ukionesha kutomuelewa baba yake, Hassan alibaki akimtazama baba yake anavyoongea.
"wanangu sikuwahi kuwasimulia kuhusu kilichowahi kunipata kipindi cha nyuma nilipokuwa kijana kama nyinyi kwasababu ya ujinga ambao hata Hassan anataka kuufanya, Hassan mwanangu pamoja na wewe Hussein tambueni tu kuwa na pesa si kupata kila kitu ndani ya dunia hii" Baba yao aliongea huku macho yake yakiwa yana dalili za kutoka machozi, hal hiyo ilisababisha hata Hussein na Hassan wamuonee huruma baba yao.
"baba tueleze" Wote waliongea kwa pamoja walipomsogelea baba yao wakiwa wamekaa pembeni yake, Hassan alikaa upande wa kulia na Hussein alikaa upande wa kushoto. Mapacha hawa walimpenda sana baba yao na kitendo cha baba yao kuonekana ana dalili za kutokwa na machozi, kwao ilikuwa ni huzuni tosha.
"nisubirini hapahapa narudi sasa hivi" Baba yao aliinuka akaelekea nje ya chumba hicho kisha akarejea akiwa ameshika shajara(diary) kubwa mkononi, aliwapatia shajara hiyo kisha akasema "someni hii nadhani itawapa fundisho na pia mtatambua kosa nililolifanya". Hassan na Hussein waliipokea shajara hiyo kwa haraka, waliifungua ukurasa wakawa wanaanza kusoma huku baba yao akiwa anatoka nje ya chumba chao.
"tukianza asubuhi hii hadi jioni tutakuwa tumemaliza yote kwani kuna maelezo marefu" Hussein aliongea.
"tulia basi tusome maneno ya nini?" Hassan aliongea kutokana na kukereka na maneno ya Hussein.

****

"Pesa unaweza ukawa nazo lakini usiwe na kitu ukopendacho ndani ya dunia hii, unaweza ukafanya chochote unachotaka bila kujali kama unakosea au unapatia. Hii ni pesa ilinifanya mimi Abdulhafidh nifanye vitu pasipo kufikiria, utajiri wa baba yangu ambaye ni raia wa Somalia ndiyo ulinipa kichwa mpaka nikajiona nina uwezo wa kufanya chochote. Mpaka sasa najuta kwa hili jambo nililolifanya bila ya kuelewa uzito wake na matokeo yake, yote haya yalianzia baada ya kufanya jambo lililonifanya nijutie nafsi yangu. Ilipita miaka kadhaa nikiwa nimelisahau jambo hilo nililolifanya na nikaamua kuwa mlevi ili kutuliza mawazo ya kumkosa yule ninayempenda ambaye amenikataa hata nilipotumia ushawishi wangu wote, nakumbuka vizuri ilikuwa ni jumapili tulivu nikiwa natoka klabu ya ya usiku ya bilicanas nikirejea nyumbani kwangu Masaki, nilikuwa nipo ndani ya gari yangu ya kifahari na pembeni yangu yupo changudoa niliyemuokota kwenye klabu hiyo kama ilivyo kawaida yangu kila mwisho wa wiki. Niliamua kununua machangudoa na kustarehe nao kwani sikutaka kuwa na mwanamke yoyote baada ya kukataliwa na Huwaida msichana mwenye asili ya kisomali kama mimi. Nilifanikiwa kufika nyumbani nikiwa salama pamoja na changudoa niiliyemchukua usiku huo kwa ajili ya kustarehe ili kutuliza mihemko ya mwili wangu kutokana na kuathirika kitendo cha kukataliwa na Huwaida tangu naanza chuo kikuu hadi muda namaliza na hadi naanza kuendesha makampuni ya marehemu baba yangu, usiku hu kabla sijaanza kustarehe na binti huyo nilianza tabia yangu kupenda kunyonya matiti ya wanawake. Kitendo cha mimi kulinyonya titi la changudoa niliyemchukua nilihisi kichwa kizito na hatimaye nikaanza kupoteza nuru katika macho yangu, hali hiyo nilijitahidi kuizuia nikajua ni dalili ya kuumwa lakini nilishindwa na hatimaye fahamu zikanitoka.
Nilikuja kugutuka baada ya kuhisi upepo mwanana ukiupiga uso wangu, nilipofumbua macho nilikumbana na anga murua lenye wingu pamoja na dalili ya kunyesha mvua. Sauti za ndege ndizo zilizo nikurupusha na nikaona hali tofauti na eneo nililolala usiku uliopita. Niljaribu kuvuta kumbukumbu ili kubaini kama nililala eneo hili lenye mchanga mwingi karibu na ufukwe wa bahari. Kumbukumhu zangu za mwisho zinaonesha sikuwa eneo hilo na nilikuwa nipo kitandani pamoja na changudoa niliyemchukua klabu ya Bilicanas. Nilibaki nimechanganyikiwa nisijue nimefikaje eneo lisilo na nyumba wakati usiku nilikuwa kitandani kwangu katika nyumba yangu, mwisho wake niliamua kuinuka na nikaanza kuzunguka maeneo ya eneo ambalo ni ngeni ili niweze kulitambua. Nilikuja kujua nipo kwenye kisiwa kidogo chenye kukaribiana na ukubwa wa nyumba yangu ya kisasa, hali ya kuchanganyikiwa ilinipata kuanzia muda huo na nikawa ninatembea kuzunguka kisiwa nyasi pamoja na miti kadhaa. Mwisho nilichoka na nikaamua kupumzika kwenye gogo nililoliona lipo katikati ya nyasi zilizopo kisiwani hapo, njaa na kiu nilianza kuhisi zikitafuna tumbo langu. Nilikuwa nahema kwa nguvu kutokana kuchoka nilipokuwa natembea kukizunguka kisiwa bila muelekeo, gogo nililokalia nilihisi likianza kusogea kwa taratibu. Nilipotazama upande wa kulia kwangu niliona nililodhani ni gogo likijikunjakunja huku likisogea mbele hadi nikawa naogopa, sikutambua kama nimekaa mgongoni mwa nyoka mkubwa ambaye hivi sasa kichwa chake kimeshaingia baharini.
"Mamaaaaa!" Nilijikuta nikitoa ukelele wa uoga kisha nikaanza kukimbia kuelekea upande wa pili wa bahari kwenye kisiwa hicho kisha nikajitupa kwenye maji, nilianza kuogelea kuelekea nisipopajua hadi nikawa nimepotea katikati ya maji na nguvu zikawa zimeniisha. Uzoefu nilionao katika kuogelea ndiyo ulinisaidia ndani ya siku hiyo, ndiyo maana hata nilipojitupa ndani ya maji sikuwa na hodu ya kufa maji na nilijua nitaweza kuogelea hadi niitafute nchi kavu. Sikuweza kutambua kutoka hapo nilipo hadi nchi kavu kuna umbali gani na pia sikutaka nikate tamaa na nife kirahisi wakati maisha bado nayapenda. Niliendelea kuogelea kwa taratibu nikiwa sina nguvu hivyohivyo hadi nilipouona mtumbwi kwa mbali ukiwa katikati ya bahari, kitendo cha kuuona mtumbwi huo kwangu ilikuwa ni tumaini jipya na nguvu mpya. Niliongeza nguvu katika kupiga mbizi hadi nikaufikia mtumbwi huo, niliupanda nikidhani nitapata mwiko wa kupigia kasia ili nisogee lakini sikuukuta zaidi ya kukuta karatasi yenye maandishi haya, 'MTUMBWI HUU NDIYO SALAMA YAKO, UKITAKA KUISHI BASI INABIDI UUPANDE NA UTULIE'. Hadi nilipomaliza kuisoma karatasi hiyo tayari nilikuwa nipo ndani ya mtumbwi huo nikiwa nimekaa tu nikihema kutokana na kuchoka, sikuweza kuongoza mtumbwi huo na ikanibidi nitulie hivyohivyo nikiwa nimejilaza ndani yake. Baada ya muda mfupi mtumbwu huo ulianza kutetemeka chini kuashiria kuna mashine, ulianza kuondoka kwa mwendo wa kasi kuelekea upande nisioujua kwa mwendo wa masaa kadhaa. Nilianza kuuona ufukwe wa bahari kwa mbali wenye mitumbwi mingi ya wavuvi ikiwa mitupu kwa muda huo wa mchana niliofika mahali hapo, mtumbwi niliopanda uliacha kusogea baada ya kukaribia ufukweni hapo kisha ukazama ndani ya maji kwa ghafla na kunifanya ninywe maji ya bahari bila kupenda hadi nilipoanza kuogelea kuelekea ufukweni. Kule ufukweni baadhi ya wavuvi waliona mtumbwi ukizama na walifika hadi kwenye maji kisha wakanitoa nje baada ya kuishiwa nguvu nilipofika kwenye maji yenye kina kifupi.
"is jy okay?(upo sawa)" Mmoja wa watu walionitoa kwenye maji aliniuliza kwa lugha ambayo nilikuwa siijui.
"is jy pyn(umeumia)?" Mwingine alishambulia kwa swali jingine ambalo nilikuwa silijui pia, nilibaki nikiwatizama kisha nikaanza kutazama mazingira ya eneo hilo nililolijua kwa umakini. Macho yangu yalitua kwenye kibao kilichopo kwenye barabara inayoingia eneo hilo, kibao hicho kiliandikwa maneno ya lugha ya kingereza niliyoyasoma 'WALVIS BAY'. Nilizidi kuchanganyikiwa zaidi na sikutambua nipo ndani ya nchi gani kwani Tanzania nilipozaliwa na kukulia hapakuwa na sehemu inayoitwa hivyo wala ufukwe wa namna.
"where am I?(nipo wapi)" Nilijikuta nikiwauliza wale watu walionitoa nje ambao kimuonekano walionekana ni wavuvi, watu hawa walitazamana kisha mmoja akaniuliza kwa tabu, "can you speak Afrikaas(unaweza kuongea kiafrikaas)?". Hapo ndipo nilipotambua nilipotambua kuwa watu hawa wanaongea lugha ya afrikaas inayoongelewa na watu wa kusini mwa Afrika, hivyo niliamua kutikisa kichwa kuonesha sikuwa na uwezo wa kuzungumza lugha hiyo.
"who are you and where are you from(we ni nani unatokea wapi?)" Yule mmoja wao aliniuliza tena huku akinitazama kwa huruma. Swali hilo nilishindwa kulijibu kutokana na kuhofia usalama wangu, neno pekee nililolitamka ni, "help me(nisaidie)" kisha nikapoteza fahamu baada ya kuhisi kichwa kimekuwa kizito.

Nilipokuja kuzinduka nilijikuta nipo kwenye kitanda kikukuu katika chumba chenye mwanga hafifu sana, dari la nyumba hiyo lilikuwa ni chakavu kuliko kawaida. Nilipoangaza pembeni yangu upande wa kulia nilikuta bakuli kubwa lenye uji likiwa lipo kwenye stuli iliyochakaa sana, nilipoangaza pembeni yangu upande wa kulia niliona mlango wa kuingilia katika hicho. Mazingira ya chumba hicho yalionesha wazi kuwa ni katika kijiji ambacho sikuweza kukitambua hadi muda huo, yalikuwa ni mazingira ambayo sikutegemea kama nitakuja kukaa walau hata kwa saa moja kutokana na maisha niliyokulia toka utotoni. Sikutegemea hata kama nitakuja kulala kwenye kitanda kichakavu ambacho kinaumiza mbavu na mgongo kama hicho, mtoto wa kitajiri niliyekulia kwenye utajiri na ninaishi kitajiri nije kulala mahali kama hapo nilipojikuta nimelala baada ya kurudiwa na fahamu. Ni ndani ya chumba ambacho nilikuwa nikiviona kwenye televisheni vikilaliwa na watu wenye hadhi ya chini ambacho kwangu nilikuwa nakiona kama choo, ewe mtoto wa kitajiri kama mimi usiombe ukalala kwenye chumba kama hicho kwani utajuta. Baada ya muda mfupi mlango wa chumba hicho uliojengwa na mabati ulifunguliwa kwa taratibu huku wakiingia watu watatu ambao wawili ni wanaume na mmoja ni mwanamke, watu hao walisogea hadi kitandani nilipolala huku wakingea lugha ya kiafrikaas. Sikuwaelewa kutokana na kutokuwa mzungumzaji wa lugha hiyo, watu hawa walizungumza kwa muda mfupi kisha wakanigeukia wote kwa pamoja wakawa wananitazama kwa tabasamu la matumaini baada ya kuniona nikiwa nimerejewa na fahamu. Kunitazama kwao huko kulisababisha niulize swali kwa lugha ya kiswahili pasipo kutambua nipo eneo lisilo na waswahili, "hapa nipo wapi?". Wote waliposikia lugha niliyozungumza walishtuka sana kisha mmoja wao akatoka nje kwa haraka sana akiwaacha wenzake ndani wakiwa wananitazama tu pasipo kuongea chochote. Baada ya dakika kadhaa ule mlango chumba nilichokuwemo ulifunguliwa tena, yule mtu aliyetoka aliingia na mwanaume mwingine ambaye baadaye nilikuja kumtambua ni mmoja kati ya wale watu waliokuwa kule ufukweni. Mtu huyu ndiye aliyekuwa ananiuliza maswali kwa lugha ya kingereza huku wenzake wakinilulza kwa lugha ya kiafrikaas, mtu huyu aliwaambia wale wenzake "ekskuuz(samahani)" huku akiwaonesha ishara ya wao kutoka nje ya chumba hicho. Wote walitoka nje ya chumba akabaki yeye pamoja na mimi, aliamua kuja kuketi kitandani nilipolala huku akinipa mkono wake.
"habari yako" Alinisalimia kwa kiswahili fasaha kabisa hadi nikamshangaa kutokana na lugha waliyokuwa na wanaongea wenzake, salamu yake hiyo nilishindwa kuijibu kutokana na mshangao niliokuwa nao muda huo.
"usishangae sana kuniona naongea kuswahili, mimi ni mtanzania niliyekimbia maisha ya Tanzania, Jonas naitwa nani mwenzangu" Aliniambia ili kuniondoa hofu niliyokuwa nayo moyoni mwangu kisha akajitambulisha jina lake.
"hapa ni wapi kwanza na nimefika vipi?" Nilijikuta nikiuliza swali badala ya kutoa utambulisho wangu kama alivyotoa wa kwake.
"hapa ni eneo la ghuba ya Walvis kijijini katika mkoa wa Erongo" Jonas alijibu swali huku akizidi kuniacha njia panda kutokana na kutoijua sehemu anayonitajia. Nilizidi kumuuliza zaidi, "Erongo?! Nchi gani?". Jonas baadaya kusikia swali langu hilo alinitazama kwa umakini kisha akasema,"Namibia". Nilijikuta nikishtuka sana baada ya kutajiwa nchi hii iliyopo Kusini mwa bara la Afrika ambayo niliwahi kufika maeneo ya Windhoek kibiashara na nilikaa katika hoteli ya nyota tano iliyopo katikati ya jiji la Windhoek.
"kwanza hujaniambia hata jina lako ndugu, pia hujaniambia ulifika pale kwenye ufukwe wa ghuba ya Walvis" Jonas alinisemesha kwa upole sana.
"naitwa Abdul" Nilijitambulisha kwa kutaja jina langu kwa ufupi kutokana na mazoea niliyokuwa katika kulitumia jina langu kwa namna hiyo kisha nikamueleza kutoka mwanzo hadi nilipojikuta kwenye kisiwa asubuhi. Maelezo yangu yalimfanya Jonas anitazame kama mtu niliyechanganyikiwa hasa nilioomuambia kwamba nililala kwenye kitanda changu cha kifahari nikaja kuamka nikajikuta nipo katika mchanga wa ufukwe wa kisiwa nisichokijua, Jonas alitikisa kichwa kwa masikitiko kisha akainuka huku akitoa bahadha ya kaki mfukoni mwake halafu akanipatia.
"hiyo bahasha imeletwa na mtoto mdogo aliyetuambia amepewa na mtu ailete, tumeitambua kuwa inakuhusu wewe kutokana picha yako kuwa juu ya bahasha. Kunywa uji huo upate nguvu mi nakuacha upumzike na uangalie kilichomo ndani ya bahasha hiyo" Jonas aliongea huku akielekea mlangoni akiniacha mimi nikiwa njia panda zaidi kutokana na mambo yaliyonikuta ndani ya maisha yangu kwa muda mfupi toka nilale na changudoa ndani ya nyumba yangu, muda mwingine nilidhani kuwa utajiri niliokuwa nao ilikuwa ni ndoto na sasa nimeamka usingizini kwenye mazingira yangu halisi ya maisha yangu ya kila siku. Nilikuwa nimechanganyikiwa kabisa na nilihisi naelekea kuwa kichaa kwa hayo yaliyonikuta ndani ya maisha yangu ndani ya muda huo, tajiri mkubwa kama mimi ambaye anamiliki kampuni kadhaa nchini Tanzania nipo kwenye nyumba mbavu za mbwa.


****

"Mmmh hivi ni kweli" Hassan alijikuta akimuuliza Hussein baada kuumaliza ukurasa wa kwanza wa shajara waliyopewa na baba yake.
"ebwanaeh utaniulizaje mimi tena, wa kuulizwa ni mshua" Hussein alimwambia Hassan huku akinyanyuka kitandani walipokuwa wamekaa halafu akasema, "muda wa msosi huu twende tukale". Wote kwa pamoja walitoka chumbani kuelekea kwenye ukumbi wa kulia chakula, walimkuta baba yao yupo mezani tayari akiwa anakula. Walijumuika naye mezani hapo huku wakimtazama sana usoni.
"hivi baba yale ni matukio ya kweli?!" Hussein aliuliza.
"kwa sasa siwezi kuwajibu mpaka mmalize kusoma yote" Baba yao aliwajibu.
"ni kisa chenye kuvutia sana" Hassan aliongea akiwa na tabasamu usoni hata kile kilio chake kilichokuwa kinamsumbua sana alikisahau kutokana na kuvutiwa na ukurasa wa kwanza wa maelezo yaliyomo ndani ya Shajara ya baba yake.
"malizeni kula kwanza ndiyo mengine yatafuata, kama kuongea basi ongeeni mkimaliza kula" Baba yao aliwaambia.


*JE NDANI YA BAHASHA YA KAKI ALIYOPEWA ABDUL KUNA NINI?

*JE KOSA HILO NI LIPI?


IPO HADI SEHEMU YA MWISHO
 

Hassan Mambosasa

JF-Expert Member
Aug 2, 2014
2,663
2,000
RIWAYA: DHAHAMA


MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA


SIMU:+255713776843
+255762219759

WHATSAPP:+255713776843


SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU
MUUMBA WA DUNIA NA VILIVYOMO KWA KUNIPATIA
AFYA NJEMA ILIYONIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA
HII KWA MARA NYINGINESEHEMU YA KWANZA!!


SURA YA KWANZA
Hali ya simanzi ilikuwa imetawala katika eneo zima la kasri la kupendeza la kifalme katika himaya ya Majichungu inayopatikana katika bahari ya hindi, himaya hii ya kijini iliingia katika huzuni baada ya mfalme wao kuwa katika harakati za mwisho za maisha yake. Mfalm huyu aitwaye Zulain mwenye miaka yapata elfu tatu alikuwa katika ugonjwa kwa muda wa miaka kumi sasa leo ndiyo dalili za kufikia mwisho wa uhai wake zilionekana dhahiri kwa majini wote wa hapo kwenye kasri hilo. Akiwa kalala kwenye kitanda chake cha thamani kwa muda wa miaka kumi kutokana na ugonjwa uliokuwa unamsumbua ambao haujulikani, kwa mara ya kwanza aliinuka kitandani ghafla akakaa kitako kisha akasimama akaelekea kwenye kiti chake cha enzi akiwaacha watumishi wake wakiwa na simanzi sana. Kuugua mfalme kwa muda mrefu kisha kuinuka ghafla ni dalili tosha ya kuwa siku za mwisho za miaka yake zimekaribia, hivyo hata watumishi wa ndani ya kasri hili walitambua kuwa siku za mwisho za uhai wa mfalme wao zimekaribia.
Hata mfalme mwenyewe alitambua kuwa ana masaa ya kuishi duniani au siku ya kuishi duniani hivyo alitaka kuongea maneno ya mwisho kabla roho yake haijaachana na mwili wake, alipokaa kwenye kiti chake jambo la kwanza kulitamka ilikuwa ni kuitiwa mawaziri wake wote pamoja na viongozi wengine waliopo chini ya utawala wake ili awaambie jambo la muhimu pamoja na kuacha kauli ya mwisho katika himaya yake. Amri ya kuitwa mawaziri na viongozi wa juu katika himaya yake ilitekelezwa mara moja na baragumu maalum likapulizwa kwa haraka sana na mpulizaji wake anayetoka katika himaya hiyo, ndani ya sekunde kadhaa chumba cha mkutano kilijaa mawaziri na viongozi wenye nyadhifa kubwa katika himaya hii ya kijini ambao walikuwa ni majini wa aina mbalimbali.
"Himaya ya Majichungu inaelekea kukumbwa na simanzi kubwa kwani kiongozi wake niliyetawala kwa muda wa miaka 2500 nakaribia kufa na dalili kuu ya kufa kwangu nadhani imeonekana kabisa dhahiri kwenu na kwa watumishi wangu, sasa basi suala la kutafutwa mrithi wa taji langu na kiti changu cha enzi nawapa nyinyi. Nahitaji mjukuu wangu Zalabain ambaye ndiye mrithi wa kiti changu cha enzi na taji langu apatikane haraka iwezekanavyo kwa namna yoyote na afutwe popote alipo aletwe huku akabidhiwe jukumu lake la ufalme kwani mwanangu Zaif ambaye ndiye baba mzazi wa Zalabain hatunaye na wote mnatambua ni jinsi alivyougua hadi akata roho katika himaya hii. Sasa basi Zaif kabla hajafa alisema duniani yupo mjukuu wangu aitwae Zalabain, sasa inabidi huyo mjukuu wangu atafutwe.kwa hali yoyote hadi apatikane ili aje kuchukua wadhifa wangu kama mrithi pekee aliyebakia. Pia nahitaji mila na desturi za himaya hii zibaki kama nilivyozikuta na zisibadilishwe kwa namna yoyote na wala asitokee kiumbe akabadilisha au akamshawishi kiumbe yoyote abadilishe. Mwisho kabisa nahitaji Sadik bin Zultash baba wa mapacha Saliim na Salmin aachiwe huru kuanzia sasa kwani uzao wake kwa faida moja umetusaidia kwa kutuletea jini mwenye nguvu kuliko wote na anayeifanya himaya yetu isidhuriwe na kiumbe wa aina yoyote, sina la ziada ni hayo tu" Mfalme Zulain alihitimisha na kikao kikamalizika mara moja karibia viongozi wote wakatawanyika wakiwa na simanzi juu ya mfalme wao. Siku iliyofuata ilikuwa ya simanzi zaidi kwa himaya nzima ya Majichungu kutokana na kifo kilichomkumba mfalme wao, himaya nzima iliomboleza kifo hicho kwa muda wa wiki saba na baada ya hapo jeshi la majini watatu ambao ni makomandoo likaundwa kwenda kumtafuta Zalabain popote alipo ili aje kurithishwa ufalme wa babu yake.

****


WIKI MOJA BAADAYE
USIKU WA MANANE
AMBONI
TANGA
Eneo la miamba yenye mapango ya kihistoria jijini Tanga jirani kabisa na mto mkubwa Tanga nzima uitwao mto Sigi kulikuwa kuna kundi la vijana kumi waliokuwa wameuzunguka mti mmoja wa mkoko ambao unasadikika kuwa mti wa ajabu kutokana na kuota eneo ambalo lipo mbali na ufukwe wa bahari. Vijana hao walikuwa wameuzunguka mkoko huo ambao ulikuwa umening'inizwa chupa ya ukubwa wa lita moja ambayo ilikuwa ikijibadili rangi kila kukicha, walikuwa wamejifunga kaniki nyeusi kiunoni na vitambaa vyekundu kichwani na kwenye mikono yao. Muda wote walikuwa wapo makini kuitazama chupa hiyo pamoja na mazingira ysnayozunguka mto Sigi pamoja na upande wa mapango ya Amboni, walikuwa wapo kimya sana na umakini wao katika kuangalia mazingira ya hapo ndiyo ulizidi kwani walikuwa wanapambana na wachawi wa kila namna ili kuilinda chupa iliyopo hapo mtini ambayo huonekana usiku kwa wenye uwezo kuiona na mchana haikuonekana kabisa.
Siku hiyo majira ya saa nane usiku vijana hao walimshuhudia Mamba mmoja mkubwa akitoka ndani ya mto Sigi na akakaka pembezoni mwa mto huo mita chache kutoka pale walipo, wote walimpuuzia mamba huyo kutokana na dawa zao wanazotumia hawezi kuwaona. Walibaki wakimtazama yule Mamba kwa jinsi alivyo mkubwa huku kuliko hata Mamba wote waliowahi kuwashudia katika mto Sigi tangu wakiwa watoto, mmoja kati ya wale vijana alishikwa na shauku ya kwenda kumtazama yule Mamba na akasogea karibu zaidi kwani dawa zao zilikuwa zinawazuia wasionwe na wanyama wakali. Alisogea akamtazama zaidi na akabaini ni mamba wa ajabu mwenye rangi tofauti na Mamba wa pale mtoni, akiwa anashangaa uajabu wa yule mamba ghafla alijikuta akipigwa mkia akatumbukia mtoni na mamba huyo naye akazama mtoni akiwaacha wale vijana waliobakia wakikimbia hadi pembezoni mwa mto wakiacha kuilinda ile chupa. Hilo lilikuwa kosa jingine kwao na hawakupata hata nafasi ya kulirekebisha kwa balaa lililotokea, kimbunga kikali kilivuma kuuzunguka ule kwa muda wa dakika kadhaa na kilipoacha ile chupa wanayoilinda ilikuwa imepasuliwa tayari. Kabla hata hawajatafakari kitu cha kufanya maji ya mto Sigi nayo yalianza kuzunguka kisha yakanyanyuka juu urefu wa mlima huku yakizunguka na yakatengeneza umbo la jitu kubwa ambalo mkono mmoja lilikuwa limemshikilia kijana yule aliyepigwa mkia na Mamba akaingia mtoni. Vijana walipoona hivyo wakajua wameingiliwa na kazi yao imeshaharibika hivyo walitaka kukimbia ili kujiepusha na hatari kwani viumbe waliowavamia sio wa kawaida, walikimbilia upande lilipo pango wakijua ni salama kwao ili wapate sehemu ya kutorokea. Walipokaribia kuingia pangoni walikutana uso kwa uso na nyoka mwenye vichwa kumi na ikawabidi wakimbilie mtoni kwa upande mwingine bila ya kutambua wanajipeleka kwenye eneo la kifo, vijana hao walijitupa mtoni kwenye maji wakiwa wanataka kuokoa maisha yao tu na wala hakukumbuka kuwa dawa waliyojipaka ya kuzuia wasidhuriwe na wanyama wakali inatoka mwilini ikiwa utaingia kwenye maji. Walipokuja kukumbuka tayari walikuwa wamezungukwa na mamba zaidi ya kumi wa mto huo, walikuwa wamejirusha sehemu yenye maskani ya Mamba bila ya kujijua na wakawa kitoweo cha Mamba.

****

Sherehe kubwa ilifanyika katika kasri la kifalme la Majichungu katika kusherekea kupatikana kwa mjukuu anayepaswa kurithi kiti na taji la ufalme wa babu yake, ilikuwa ni mara ya kwanza kwa mjukuu huyo mwenye mchanganyiko wa binadamu na jini kufika katika himaya tangu azaliwe. Sherehe ilipoisha ndipo taratibu zote za kimila na desturi za kumpatia ufalme Zalabain zikaandaliwa kama ilivyofanyika kwa wafalme waliopita. Siku iliyofuata sherehe nyingine ya kuvikwa taji la ufalme ilifanyika katika uwanja mkubwa uliopo nje ya kasri la kifalme ambayo ilihudhuriwa na wanahimaya hiyo karibia wote, kiti cha kifalme kilitolewa kikawekwa sehemu yenye jukwaa lililopambwa kwa busati lenye rangi nyeupe. Muda wa kuvikwa taji Zalabain ulipowadia Mkuu wa baraza la sheria la himaya hiyo aliingia akiwa amebeba taji la kifalme liliwekwa kwenye kasha lililopambwa na fito zenye rangi nyekundu, Zalabain akiwa nyuma ya Mkuu huyo wa baraza la sheria pembeni yake akiwa na walinzi wenye miili mikubwa pamoja na sura za ajabu. Zalabain na mkuu huyo walipanda katika jukwaa lenye kiti cha kifalme huku mamia ya wanahimaya ya Majichungu wakishangilia kwa nguvu, aliamriwa aketi kwenye kiti cha ufalme naye akatii akaketi na Mkuu wa baraza la sheria akashika kasha lenye taji la kifalme akasogea kisha akawageukia Wanahimaya ambao wapo hapo kushuhudia tukio hilo.
"Leo ni siku maalum na ya kihistoria ya kumpata kiongozi wetu aitwae Zalabain bin Zaif atakayeiongoza himaya yetu akirithi utawala wa Babu yake Zulaif, akiwa na miaka 26 tu atakuwa kiongozi mdogo kuwahi kutokea katika Himaya yetu hii hivyo naomba mumpokee" Mkuu wa baraza la sheria aliongea kisha akamgeukia Zalabain ambaye tayari ameshavaa mavazi ya kifalme akawa anatazama nae.
"Kwa mamlaka niliyokabidhiwa ninakukabidhi na kukuvisha taji hili la Kifalme litakalokufanya uwe mfalme, miongoni mwa wafalme, wa ukoo wa kifalme, waliowahi kuwa wafalme, uwe kiongozi wa kasri la kifalme. Zalabain sasa wewe ni mfalme wa himaya ya Majichungu" Mkuu wa baraza la sheria alipomaliza kusema maneno hayo aliliweka taji kichwani mwa Zalabain huku halaiki ya wanahimaya wakishangilia, kushangalia huko kulizimika ghafla mithili ya umeme unavyozimika eneo lenye giza. Wote walibaki wameduwaa baada ya taji la kifalme lililowekwa kichwani mwa Zalabain kuruka kando likaanguka kwenye busati lililotandazwa hapo jukwaani. Mkuu wa baraza la sheria aliona ni jambo la kawaida sana na aliinama akalishika ili alinyanyue lakini taji halikuinuka na lilikuwa zito sana na ikambidi alishike kwa mikono miwili na akashindwa kuliinua vilevile. Aliamua awaite wale walinzi walioingia na Zalabain walinyanyue nao wakashindwa pia kulinyanyua eneo hilo. Wanajeshi wanaoaminika wana nguvu sana nao walishindwa kulinyanyua taji hilo, Zalabain mwenyewe alibaki akiwa anashangaa kwa tukio hilo ambalo hakulielewa limetokana na nini.
Mnajimu mkuu wa Himaya hiyo aliitwa mara moja na akapewa kazi ya kulitatua tatizo hilo kwani yeye ndiye anayeaminika katika himaya hiyo, mnajimu huyo wa kijini alianza kulizunguka taji hilo la kifalme kisha akajaribu kuliinua lakini alishindwa kabisa na akaanza kubadilisha macho yake yakawa kama ya paka akamtazama Zalabain.
"Siyo uzawa wa ukoo wa mfalme huyu ndiyo maana taji limemkataa na wala siye mtoto halisi wa Zaif, taji hili linahitaji abadilishwe kiongozi kwani kizazi cha ukoo wa mfalme alibaki Mfalme Zulain tu ambaye amefariki tayari. Ufalme unatakiwa uhamishwe katika koo nyingi.." Mnajimu alishindwa kumalizia kauli yake na akajikuta amepigwa kofi zito hadi akaanguka chini, akiwa hajajua nani aliyempiga akahisi anakabwa shingoni huku akinyanyuliwa juu. Walinzi walipoona hali hiyo walitaka kusogea ili wamdhibiti kiumbe anayemkaba Mnajimu mkuu lakini walisita baadaya kiumbe mwenyewe kujitokeza hadharini, Salmin ambaye anajulikana na wanajamii hiyo kama jini mwenye nguvu kuliko wote ndiye aliyeonekana akimkaba Mnajimu huyo shingo.
"Kwanini unasema uongo ilihali wewe ni Mnajimu unayeheshimiwa na kuaminiwa katika himaya hii" Salmin alimuuliza Mnajimu huku akizidi kumkaba, Mnajimu aliomba aachiwe ili aongee na alipoachiwa ndipo akamwaga uhalisia wa jambo lenyewe.
"Wanahimaya na wakuu wote naomba mnisamehe sana kwa kusema uongo juu ya mjukuu wa mfalme, tamaa ya madaraka ndiyo imesababisha niseme uongo. Niliahidiwa kupewa nafasi ya mkuu wa baraza la sheria ikiwa tu nitafanya hila ufalme uhamishiwe katika ukoo wa waziri mkuu ili waziri mkuu awe mfalme wa Himaya hii, narudia tena viongozi wangu na wanahimaya wenzangu naomba mnisamehe kwani mimi nina nafsi na tamaa ni kitu cha kawaida kwa mwenye nafsi" Mnajimu alitoa maelezo hayo akiwa na aibu usoni kutokana na jambo alilolifanya, kuomba kwake msamaha hakukusaidia kitu kwani alikamatwa yeye na Waziri mkuu baada ya mkuu wa baraza la sheria kutoa amri hiyo. Baada ya kukamatwa kwa Waziri mkuu na Mnajimu mkuu Salmin alilitazama taji la kifalme kisha akamtazama Zalabain kwa umakini, macho yake yalianza kutoa nuru mithili ya almasi iliyomulikwa na mwanga mkali.
"Zalabain.......Zalabain mrithi wa kiti cha mfalme aliyestahiki kuvishwa taji la ufalme wa himaya hii lakini taji limemkataa kutokana na jambo moja tu ambalo mrithi wa kiti hiki hatakiwi kuwa nalo kabisa ambalo wewe unalo, udhaifu.....udhaifu wako ndiyo chanzo cha taji hili kukukataa. Ikiwa unatakiwa kuwa mrithi wa taji hil na kuna ubaya ambao umetendewa unatakiwa ulipe kisasi kwanza na si kusamehe ili upate taji hili, baba yako Zaif ameangamizwa na wanadamu akiwa na miaka 1500 na wanadamu hao ndiyo chanzo cha taji hili kukukataa na pia kuwa zito kuinuka kwa yoyote mwenye wazo la kuliweka kichwani mwako. Kisasi cha ubaya uliofanyiwa ndiyo kinahitajika ili hili taji likae kichwani mwako na hakuna mwingine atakayelivaa isipokuwa wewe, unapaswa utambue kwamba himaya hii yote inahitaji kiongozi na haiwezi kuendelea bila kiongozi na pia kiongozi ni wewe unatakiwa ulipe kisasi ili watu wako uwaongoze na si usamehe wapotee. Je upo tayari kuongoza himaya hii?" Salmin alifafanua chanzo cha kutokea jambo lililotokea kisha akamuuliza Zalabain.
"Nipo tayari kuongoza, nipo tayari kisasi cha kuuawa kwa baba yangu na nipo tayari kulipa kisasi cha ubaya uliotendwa kwangu" Zalabain aliongea huku macho yakibadilika na kuwa mekundu kabisa na yenye kung'aa, Salmin alimsogelea akamshika mkono kwa sekunde kadhaa kisha akamuachia halafu akamuambua "kazi njema". Salmin aliliokota taji la kifalme akamkabidhi Mkuu wa baraza la sheria kisha akaondoka, sherehe hizo ilivunjwa hapohapo na Zalabain akahitajika atimize kile alichoahidi mbele ya majini wote wa himaya hiyo.


****


Asubuhi ya siku iliyofuata tangu litokee tukio la kutoveshwa Zalabain taji, wafanyakazi wa kampuni ya upangishaji nyumba iitwayo Extoplus walikuwa wanasafiri kuelekea katika kijiji cha Duga Maforoni kwenda kuhudhuria sherehe ya uzinduzi wa nyumba mpya za kupangishwa za ksmpuni hiyo. Siku hiyo wafanyakazi wote waliotakiwa kwenda kwenye sherehe hiyo walijawa na hofu, karibu kila mfanyakazi alikuwa anasita kwenda anasita kwenda kwenye sherehe lakini hawakuwa na uwezo wa kukataa kwani ni idara nzima imeteuliwa kuhudhuria sherehe hiyo. Saa mbili kamili wote walikuwa kwenye basi wakielekea Duga kuhudhuria sherehe hizo, ndani ya basi kimya kilitawala kuanzia mwanzo wa safari na kilikuja kuvunjwa baada ya gari aina ya toyota coaster waliyokuwa wanaitumua kuvuka daraja la Utomfu. Mwanamke mmoja wa makamo alivunja ukimya uliopo ndani ya gari kwa kusema, " jamani mimi jana usiku nimeota ndoto ya ajabu sana".
"mmh! Hebu tueleze ni ndoto gani hiyo" Mwenzake aliyekuwa pembeni naye alidakia.
"nimeota nashuka kwenye gari natoka kazini nikakutana na mtoto wa miaka sita hizi akaniamkia kwa uchangamfu na mimi nikaitikia, yule mtoto kaniuliza unaujua mtego wa panya mimi nikamjibu ndiyo. Akaniuliza je kiumbe chochote kikiugusa unamnasa au unanasa panya tu, nikamjibu yoyote akiugusa ananaswa haijalishi kama Panya au siyo panya. Nilipomjibu akatabasamu nikamuuliza mbona umeniambia hivyo, akanijibu safari yako ya kesho Duga ni mtego wa panya ukienda utanasa ingawa wewe sio panya. Nimeshtuka usingizini hapohapo nikawa najiuliza kuhusu ndoto hiyo jamani ina maana gani" Yule mwanamke alieleza ndoto yake na alipomaliza wafanyakazi wote walikuwa wameingiwa na woga hapohapo.
"jamani hata mimi hii ndoto nimeiota" Mwanamke mwingine akadakia huku akionesha kuogopa.
"hata mimi" Mwanaume wa makamo ambaye ni mmoja wa wafanyakazi hao naye akadakia na mwishowe wote kwa pamoja wakatamka kwamba wameiota ndoto hiyo na hofu ikawa imetawala nafasi zao huku wengine wakimsihi dereva ageuze gari wasiende. Walikuwa wameshafika Amboni na sasa wapo kwenye daraja la kulia la mto Sigi hivyo dereva alikuwa yupo makini kulimaliza daraja hilo na hakuwasikiliza kabisa, baada ya kulipita daraja ndipo dereva akasema "jamani hata mimi nimeota ndoto ya namna hiyo lakini nimeipuuzia kwani si kila ndoto ni ya kweli".
"unasemaje wewe hebu simamisha nishuke nipande mabasi yanayotoka Horohoro nirudi mjini" Mwanamke yule aliyeeleza kuhusu ndoto alikuja juu.
"sawa ngoja tufike Mpirani kwenye kituo ili upate hilo gari" Dereva akimwambia yule mwanamke lakini hakutaka kumuelewa.
"simamishe gari nakuambia!" Yule mwanamke alizidi kufoka, dereva hakuwa na jinsi ilimbidi akanyage breki lakini gari ilikataa na ndiyo mwendo ulikuwa unazidi na usukani ikawa unajiongoza wenyewe.
"we mwanaharamu wewe simamisha gari nishuke sio kuongeza mwendo" Yule mwanamke alizidi kufoka baada ya kuona mwendo wa gari unazidi kuwa mkali, dereva hakumjibu yule yeye alitoka kwenye usukani akasimama kisha akawaangalia wafanyakazi wa idara nzima akiwa na hofu.
"si mimi ninayeendesha jamani gari linaenda lenyewe hili hebu oneni" Dereva aliongea huku akiwaonesha wafanyakazi wote jinsi usukani ulivyokuwa unajiongoza wenyewe, wafanyakazi wote walipoona hicho kioja walijikuta wakijaribu kutoka nje lakini walishindwa kwani milango haikufunguka na vioo vyote vilijifunga ghafla hata vile vilivyokuwa wazi vyote vilijifunga. Wafanyakazi wote walijaribu kupiga vioo ili wavunje lakini walishindwa kwani vioo vilikuwa vigumu sana, gari nayo ilizidi kuongezeka mwendo hadi ikawa kama ipo kwenye mashindano.

*Mwanzo tu ni balaa je huko mbele
 

Hassan Mambosasa

JF-Expert Member
Aug 2, 2014
2,663
2,000
pia ipo riwaya ya kijasusi iitwayo JINAMIZI kwa shs 4000 na 300 kwa episode kwa anayehitajiCHANGIA KUKUZA TAALUMA YA UANDISHI
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom