Riwaya: Ukurasa wa Tisa

Kudo

JF-Expert Member
Nov 2, 2017
1,809
6,081
RIWAYA: UKURASA WA TISA
NA: BAHATI K MWAMBA
SIMU: 0758573660/0658564341

Sehemu moja maarufu ndani ya jiji la Dodoma kulikuwa na kundi kubwa la watu pembezoni mwa barabara wakiwa wamesimama kimakundimakundi. Watu hao walikuwa wamesimama kwa kuzizunguka baadhi ya meza za kuuzia magazeti zilizoko maeneo hayo maarufu kwa jina la Nyereresquare. Licha ya eneo hilo kuwa linapokea idadi kubwa ya watu kuanzia majira ya ahsubuhi hadi jua lizamapo, lakini ni aghalabu kukuta watu wengi wakiwa mbele ya mabango ya meza za wauza magazeti na vitabu zilizoko sehemu hiyo. Kwa siku za karibuni lile jambo lilianza kuzoeleka miongoni mwa watu waliokuwa wakipita au kuingia ndani ya viwanja vya Nyereresquare.

Miongoni mwa watu waliokuwa wakiwahi ahsubuhi na kuzunguka meza ya mmoja wa muuza magazeti, alikuwa ni Jane Mgale, Mama mwenye watoto wenye umri wa kuzidiana miaka miwili huku mkubwa akiwa na umri wa miaka minne na mdogo miaka miwili. Mama huyu ambae umri wake ulikuwa chini ya miaka ishirini na sita, alijikuta akiwa mtumwa wa kuamka kila jumatano na ijumaa ahsubuhi kwa lengo la kuwahi kununua moja ya jarida lililoanza kujichukulia umaarufu hapa nchini, huku likiwa na siku chache tangu kuanzishwa kwake. Jane alikuwa na sababu mbili kubwa zilizomfanya awe anawahi ahsubuhi sana kwenda kununua jarida hilo, sababu moja wapo ikiwa ni mazingira aliyokuwa akitokea kutokuwa na muuza magazeti ambae alikuwa ni wakala wa lile jarida lililokuwa likimpa safari za lazima kila jumatano na ijumaa, lakini sababu kubwa zaidi ilikuwa ni kile kilichokuwa kikipatikana kwenye ukurasa wa tisa wa jarida la Ngano Zetu lililokuwa likichapishwa na kampuni ya Mwa'se'ma Publishers.

Ukurasa wa tisa wa jarida hilo kulichapishwa simulizi za kweli kutoka kwa watu mbalimbali, kurasa nyingine zilichapishwa riwaya kutoka kwa waandishi wenye uzoefu na wale wanaochipukia. Ngano zetu lilikuwa ni jarida lilijizolea umaarufu kwa muda mfupi tangu lilipoanzishwa, watu wengi walipenda kulinunua kwa sababu ya kusoma riwaya nzuri kutoka kwa waandishi mashuhuri nchini Tanzania, lakini wengi wao walivutiwa na simulizi za kweli zilizokuwa zikichapishwa ukurasa wa tisa, zilikuwa ni simulizi zenye visa na mikasa mizito walizowahi kukutana nazo baadhi ya watu mashuhuri na wasio mashuhuri ilimaradi, walipata nafasi ya kusimulia waliyowahi kuyapitia kwenye maisha yao. Licha ya ukweli kwamba watu walisoma na kuvutiwa sana na mikasa ya ukurasa huo, lakini wakati huo kulikuwa na simulizi nzuri sana iliyokuwa ikivuta hisia za watu wengi sana hata wale ambao hawakuwa wapenzi wa usomaji, walijikuta wakivutiwa na jarida lile hasa ule ukurasa wa tisa hadi kumi na moja, walivutiwa na kisa cha mwandishi Bahati Kisarwa Mwamba ambae alipenda kuandika mikasa ya mhalifu Zuki Gadu p.a.k Miguu ya kuku, pia alipenda kuandika visa vya jasusi Honda Makubi, Zedi Wimba na Obimbo Mtei.

Kilichowavutia watu kufuatilia mkasa wa mwandishi huyo si matukio aliyokutana nayo pekee bali pia ni kuwakutanisha wahusika anaopenda kuwatumia kwenye riwaya zake kuwa sehemu ya wasimuliaji. Zuki Gadu pamoja na jasusi Honda Makubi nao walijumuika nae kwenye simulizi ile ya kweli, wasomaji hawakuishia kusoma visa na mikasa yake kwenye jambo alilokuwa akilisimulia, walisoma pia mikasa ya watu waliokuwa wakizunguka nae kwenye mkasa wake huo wa kweli uliowahi kumkuta kwenye safari ya maisha yake. Wale waliokuwa wakisoma vitabu vyake na kuwafahamu wahusika hao ambao walidhani ni watu wa kufikirika, kupitia jarida lile walipata uhakika kuwepo Zuki Gadu halisi, Honda Makubi halisi na wengineo, lakini kubwa zaidi waligundua Bahati alikuwa na urafiki na watu hao. Kwa wasomaji hao kwao si burudani tu walioipata kwa kusoma mkasa wa mwandishi wampendae, bali walipata kuufahamu ukweli wa baadhi ya maswali waliojiuliza.

Tofauti na wasomaji wengine ambao walivutiwa na matukio ya kufurahisha na kusikitisha yaliyosimuliwa na wahusika, Jane Mgale alikuwa anafuatilia jambo kwenye mkasa ule, alifuatilia maisha halisi ya Bahati Mwamba aliyoyasimulia, maisha hayo ni mahusiano. Kwa nini? Kwa sababu alikuwa akimfahamu mwanaume huyo na alimfahamu kwa sababu ndiye baba wa watoto wake wawili aliokuwa akiwalea na ndiye aliyekuwa mume wake wa ndoa. Alifuatilia kila toleo jipya kwa sababu aliamini ataendelea kufahamu mengi ambayo hakuwa akiyafahamu kuhusu mume wake, mambo ambayo mume wake hakuwahi kumwambia hata kwa bahati mbaya ijapokuwa, hata kuhusu mkasa huo kuchapishwa gazetini aliyemwambia aufuatilie ni huyohuyo mumewe, bila shaka alitaka amfahamu kupitia jarida hilo.

“Oh! Leo umechelewa kidogo na nakala ya mwisho nimemuuzia huyo dada mliyepishana.” Muuza magazeti alimwambia baada ya kufika na kukosa nakala kwenye meza zilizokuwa zikiuza jarida la Ngano Zetu.

“Mungu wangu!” Alijikuta akiponyokwa na hayo maneno huku akigeuza haraka na kwenda kumfuata mwanamke mmoja aliyepishana nae wakati akienda kwenye ubao wa magazeti.

“Samahani Dada!.” Alisema huku akimvuta bega mwanamke aliyekuwa mbele yake, mwanamama yule akageuka na kumtazama.

“Samahani kama nitakukera kwa ombi langu.” Alianza kuzungumza.

“Usijali, nakusikiliza.” Mwanamke aliyesimamishwa alimjibu.

“Naomba uniuzie hilo jarida uliloshika mkononi.” Alisema huku akitoa noti ya elfu tano na kuipunga hewani.

“Mh! Lakini si yapo kwenye meza za hawa wauzaji?” Yule mwanamke alimwambia huku akionekana kushangazwa na ombi lile.

“Yaani meza zote hazina nakala na bahati mbaya ni kwamba,hapa mjini jarida hilo linauzwa hapa tu.” Alimwambia huku bado akiwa ameshika pesa mkononi mwake.

“Hapana mdogo wangu, siuzi. Siwezi kukosa simulizi ya ukurasa wa tisa.” Yule mwanamke alimwambia kwa kumaanisha.

“Tafadhali sana, naomba uniuzie kwa pesa yote hii.” Alimwambia huku akiwa anamwonesha ile elfu tano iliyokuwa mkononi mwake.

“Hapana! Yaani ulivyo na shida na uhondo huo na mimi nina shida mara nyingi zaidi yako.” Mwanamama alimkatalia.

Jane alivuta mkoba wake na kuufungua, akiingiza mkono na kutoka na noti ya elfu kumi na kuipunga hewani.

“Nalinunua kwa hii pesa.” Alisema huku akimuonesha ile elfu kumi.

Wahenga walisema, pesa maua, pesa sabuni ya roho, mwanamke yule aliishia kujiumauma huku akinyoosha mkono na kuipokea ile pesa na kuliacha jarida la Ngano Zetu likiwa mali halali ya Bi. Jane Mgale.

“Ahsante sana, ubarikiwe kwa msaada huu ulionipa. Kuipata nakala hii kwangu ni zaidi ya pesa niliyokupa.” Jane aliongea wakati akiagana na yule mwanamke, akageuza na kukamata barabara kuelekea stendi ya daladala ili kurejea nyumbani kwake maeneo ya Msalato.
 
Alifika nyumbani ikiwa ni majira ya saa nne na nusu ahsubuhi, aliingia ndani na kuutupa mkoba kwenye kiti kisha akaelekea chumbani kwake na kupunguza nguo alizokuwa amevaa, akajitanda khanga na kurejea sebuleni, akaufungua mkoba wake na kulitoa jarida la Ngano Zetu, alitaka kulisoma kabla hajafanya kazi nyingine yoyote pale ndani kwake pia, alitaka kusoma kabla wanae hawajarejea kutoka kwa bibi yao ambae aliwachukua ahsubuhi na kwenda nao nyumbani kwake.

Hakuhangaika na kurasa nyingine moja kwa moja alienda kuufungua ukurasa wa tisa na kukutana na sehemu ya tano ya simulizi aliyokuwa akiihitaji na wakati huu alikutana na jina la mtu aliyekuwa akiendelea kusimulia yaliyomkuta, mtu huyo alikuwa ni rafki wa karibu sana na mwandishi Bahati Mwamba, alikuwa ni rafiki yake wa karibu kutoka kanda ya Ziwa na mshereheshaji maarufu ndani na nje ya jiji la Mwanza.

Alisoma hivi…

MC. PAUL KUSEKWA

Ilikuwa ni kawaida yangu kuchangamsha ubongo wangu kwa chupa mbili au tatu za bia kabla ya kuanza kusherehesha, huwa ninajihisi kuwa huru zaidi kama ubongo wangu ukiwa na kiasi fulani cha kilevi, huwa nakuwa mchangamfu na mwenye maneno mengi yanayowaacha wageni waalikwa kwenye tabasamu muda wote. Watu wengi walipenda kuniita Mc Kicheko, waliniita hivyo kwa sababu ilikuwa ni kawaida yangu kucheka na kutabasamu kila wakati maiki ikiwa karibu na mdomo wangu, kiukweli naipenda kazi yangu.

Ilikuwa ni kawaida kwangu kusafiri kilomita nyingi mbali na nyumbani kwa ajili ya kusherehesha kwenye shughuli mbalimbali, iwe sherehe ama mikutano iliyohitaji uwepo wa huduma yangu. Nakumbuka siku ile nilikuwa Shinyanga mjini nikiendelea na majukumu yangu, simu yangu iliyokuwa mfukoni ilikuwa ikitetema mara kwa mara kuashiria kuna mtu alikuwa akinipigia, mwanzo niliona kama ni usumbufu kutoka kwa mtu aliyekuwa akinipigia na sikumpokelea, niliona hivyo kwa sababu kiungwana mtu unapopiga simu na haikupokelewa na unaempigia, ni vema ukatuma ujumbe mfupi kama ni muhimu au kuacha kupiga kabisa kwa sababu huwezi jua sababu iliyofanya simu yako isipokelewe.

Lakini kupiga simu kila mara inakuwa usumbufu na hilo ndilo nililohisi kwa wakati huo, nikaona kero na nikapanga kumporomoshea maneno mazito mtu huyo wakati ambao ningelimtafuta na kumpata. Licha ya kukereka kwangu lakini mpigaji aliendelea kupiga na wakati huu yale mawazo ya kukereka yakanitoka, nikaanza kuhisi mpigaji alikuwa na jambo kubwa alihitaji kunitaarifu na hapo nikamkumbuka mke wangu, Mama D, mama wa watoto wangu watatu wa kiume na mlezi wa mwanangu mmoja wa kike. Nilimuwaza yeye kwa sababu ni mtu pekee anaeweza kunipigia simu muda wowote hata kama ni saa tisa za usiku, lakini hufanya hivyo endapo akijua sina kazi.

“Kutakuwa na tatizo gani?” Nilijiuliza huku nikitazama mishale ya saa yangu iliyokuwa imeupamba mkono wangu wa kushoto, mishale ilisoma ni saa sita na nusu usiku.

“Mh”Niliguna huku nikimeza mate na kuwatizama watu waliokuwa ndani ya ukumbi, baadhi walikuwa wamekaa na wengine walikuwa wanacheza kuwalekea maharusi kwa ajili ya kutoa zawadi kwao, sherehe zilikuwa mwishoni kabisa na wale watu wangeliisha basi ratiba ilionesha ni wakati wa kupata maakuli na kisha kuhitimisha rasmi sherehe zile za wapendanao wawili waliokuwa wamefunga ndoa siku moja iliyopita.

Mpigaji wa simu aliendelea kupiga bila kukoma na kwa harakaharaka nilihisi ulikuwa ni muito wa zaidi ya mara ishirini, nilijikuta nikitamani kuipokea simu hiyo lakini nilijionya kufanya vile ili nisije kukutana na ujumbe ambao utaniondoa kwenye hali yangu ya kawaida na, nikajikuta naharibu shughuli ya watu. Simu aliendelea kuita na nikashindwa kuvumilia, nikaangaza pembeni alipokuwa DokaJoka wa sherehe ambae mara nyingi huwa naambatana nae, nikamuona kijana wangu mmoja ambae huwa namfundisha kazi ya ushereheshaji, nikampa ishara ya kumuita, akachukua maiki ya ziada na kunifuata.

Aliponifikia, nikazima maiki yangu na kumwelekeza jambo kisha bila kusubiri majibu yake, nikageuka na kuelekea upande wa maliwatoni ambako niliamini nitakuwa salama kupokea simu usiku huo. Nilitembea huku nikifanya jitihada za kuitoa simu mfukoni na kabla sijausukuma mlango, tayari simu ilikuwa imejaa kwenye kiganja cha mkono wangu wa kushoto na wakati huohuo ilikuwa ikiita kwa mara nyingine, nikasimama kutizama jina la mpigaji, nikajikuta nakunja sura yangu kwa udadisi kidogo, nikaacha simu iite hadi ilipokata huku lengo langu kubwa likiwa ni kutizama aliyekuwa akinipigia mfululizo, nilifanya vile ili nimjue aliyekuwa akinipigia mfululizo na si yule aliyenipigia wakati ule nilipokuwa nikitoa simu mfukoni. Nilifungua sehemu ya kumbukumbu za simu ambazo hazikupokelewa, kulikuwa na jumla ya miito ishirini na saba na mpigaji alikuwa mmoja na ni yule yule ambae sikumpokelea simu yake.

“Huyu jamaa anashida gani usiku huu? Mbona hana kawaida ya kunipigia simu nyakati kama hizi?” Nilijiuliza huku nijiandaa kuruhusu kitufe cha kupiga namba ile iliyokuwa ikinipigia, kabla sijabonyeza, simu yangu ikaita na mpigaji alikuwa ni yule yule, nikapokea huku nikiwa nimeganda hatua moja mbele ya mlango wa kuingilia malawitoni. Niliganda vile kwa sababu nilikumbuka kesi ya yule mtu aliyekuwa amenipigia, kesi ambayo ni ngumu kueleweka kwa akili ya kawaida tuliyonayo wanadamu, hata mimi iliniwia ugumu kukubaliana na kile ambacho aliwahi kunambia yule bwana, hata siku hiyo nilipokumbuka, bado nilikuwa simuamini.

“Bwana Shemeji! “ Alianza kuniita kwa namna alivyozoea kuniita, ni mara chache sana huwa analitaja jina langu. Kwangu pia ilikuwa ni kawaida kumuita vivyo hivyo na hiyo ni kwa sababu, niliwahi kuishi na mwanamke ambae alikuwa anatoka ukanda mmoja na yule bwana na ndiye mama wa mtoto wangu wa kwanza.

“Samahani kwa kukupigia mara nyingi kiasi ambacho hata mimi naona ni kero, lakini sina namna, imenilazimu kufanya hivyo wakati huu kwa sababu sina mtu wa karibu ambae naweza kumsumbua kwa wakati huu zaidi yako.” Alisema kisha akakaa kimya, bila shaka alitaka kusikia upande wangu nitasema nini kabla ya kuendelea kuongea kilichomfanya anipigie usiku ule.

“Usitake kunambia lile jambo ulilonambia siku ile ndilo lililokufanya unipigie tena.” Hatimae nilisema huku nikiwa nimekereka kiasi fulani, kiukweli sikuwa nimependa namna yule bwana alivyokuwa ametumia muda mwingi kuipiga simu yangu, sikuona kama alistahili kufanya vile, lakini sikuwa na namna ya kumfokea au kukataa kumsikiliza, mimi na yeye tuliheshimiana sana na mbali ya kuheshimiana, pia alikuwa ni swahiba wangu wa ukweli kabisa na ndiyo maana hata yeye alinichagua mimi na si mtu mwingine.

“Najua nimekukwaza Mr Paul, lakini kuna jambo la muhimu sana lililonifanya nikupigie mara zote hizo, nashukuru umepokea na unanisikiliza lakini naomba unisikilize kwa umakini sana.” Alisema na kunyamaza kidogo, nami sikutaka kuingiza neno lolote, nilimuacha aseme.

“Lile tukio limejirudia tena.” Alimalizia kauli yake. Nikashusha pumzi kwa nguvu kisha nikaipata sauti yangu na kumuuliza.

“Una maanisha mtu aliyekwishafariki amekupigia simu tena?”

“Wala siyo utani, amepiga simu na sauti ni yake kabisa.” Alisema huku akisikika kuhema harakaharaka, bila shaka alikuwa kwenye mhaho mkubwa.

“Una hakika umeisikia sauti ya marehemu Robhi? Au huwa unaota?” Nilimuuliza kwa sauti ya utulivu kidogo huku nikiwa bado nipo katikati ya kuamini na kutokuamini alichokuwa akinambia.

“Wakati huu siyo mke wangu Robhi, ni rafiki yake Asulia.” Alinijibu.

“Huyo Asu nae amefariki? Yaani nae ni marehemu?” Nilimuuliza huku kicheko kikianza kuchukua nafasi kwenye uso wangu, niliona ni jambo la kusimuliwa ambalo halina ukweli wowote.

“Alikufa siku tatu baada ya kifo cha mke wangu..” Alinijibu, lakini nilimkatisha kabla hajaendelea kusema alichokuwa anataka kuendelea kukisema kuhusu Asu.

“Sikia Bahati,” Nilisema huku nikiinua mkono wangu wa kushoto na kutizama saa yangu, muda wa kuahirisha sherehe ulikuwa umewadia na sikuwa na uhakika kama msaidizi wangu angelizingatia muda huo, lakini nisingeweza kukatisha mazungumzo.

“Najua hali unayopitia kwa kuondokewa na mkeo katika mazingira ya kutatanisha, lakini inabidi ukubaliane na hali halisi ya kuwa mkeo hatunae tena. Punguza mawazo juu yake na kama unashindwa kuhimili hali hiyo, naomba nikusaidie kupata mtalaamu wa afya ya akili ambae ataweza kukusaidia kukuweka sawa, nipo tayari kugharamia matibabu hayo. Tafadhali, nakuomba uniruhusu nisimamie hilo jambo.” Niliamua kumshauri kwa kuwa nilihisi kilichokuwa kikimsumbua ni msongo wa mawazo baada ya kifo cha mke wake kilichokuwa kimetokea mwaka mmoja uliopita.

“Bwana Shemeji unaniamini.?” Bahati aliniuliza.

“Nakuamini kwa asilimia zote lakini kwa hili inabidi tusaidiane ili hali unayopitia sasa, uweze kuimudu na kurudi kwenye hali yako ya kawaida.” Nilimjibu swali lake na kumsihi akubaliane na wazo langu.
 
Basi nimeamini huniamini na unahisi nipo kwenye ugonjwa wa akili kama unavyodhani, lakini nataka nikwambie kitu kimoja; hali ya mke wangu kuniacha Duniani nilishaimudu na nilikuwa naendelea na maisha yangu nikimlea mwanangu. Ninachokwambia ni ukweli kabisa wala sina haja ya kukudanganya wala kutafuta huruma kwako, lakini kwa kuwa unahisi ninaumwa basi hakuna namna, endelea kuhisi hivyohivyo lakini tambua mwenzio napitia wakati mgumu sana kwa sasa na nakuomba kitu kimoja..” Bahati alisema huku akimalizia kwa kukisema kitu alichokuwa amedhamiria kunambia, alipokwisha kusema hakutaka kunipa muda wa kumjibu akichoniomba, akaongeza ombi lingine..

“Naomba mwanangu aje kuishi hapo kwako kwa muda fulani kisha nitakuja kumchukua.” Alinambia lakini ilikuwa ngumu kidogo kumkubalia kwa sababu mwanae alikuwa shule na wakati huo shule zilikuwa zinaendelea na vipindi, kuja kwangu ilimaanisha mtoto angelisimama shule kwa muda ambao haukufahamika, lakini hofu kubwa ilikuwa ni sababu niliyoihisi kuhusu kilichokuwa nyuma ya lengo la mtoto kuletwa kwangu.

“Lakini huyo mtoto si anasoma shule na hawajafunga?” Nilimuuliza.

“Najua hawajafunga na anatakiwa kuwa shule, lakini naomba umpokee na kama ukishindwa kunikubalia nitampigia mkeo Mama D, naamini atanikubalia.” Alisema huku nikijua ni kwa nini aliamua kulitaja jina la Mama D kwenye ule mjadala wetu, alitambua isingelikuwa rahisi kumkatalia kwa kuwa kama lingefika kwa Mama D na ikaonekana nilitaka kukwamisha suala hilo, nyumba ingelikosa amani kwa saa kadhaa na hili lilichangiwa na ukweli kwamba, mke wangu kwa muda mrefu alikuwa akiomba kuishi na mtoto wa Bahati kwa kuwa aliamini alipaswa kufanya hivyo ili kumpunguzia majukumu shemeji yake, siku zote alisihi kumpa mapenzi ya mama mtoto huyo ambae wakati huo alikuwa akikosa kitu hicho muhimu maishani mwake.

“Lakini itabidi tufanye mpango aendelee kusoma kwenye shule za huku Mwanza, nipe siku mbili nitafute shule nzuri itakayokuwa na mazingira mazuri kwake.” Nilimjibu kwa kukubali ombi lake na nikampa wazo la kutaka mwanae asomee nyumbani kwangu kwa kipindi hicho chote nitakachoishi nae.

“Sawa, ila naomba unipe namba za akaunti yako ya benki ili niweze kukuwekea kiasi kadhaa kitakachohudumia ada yake.” Alinambia.

“Hapana, acha nigharimikie mimi mwenyewe. Itu ni mwanangu pia, ondoa wasiwasi.” Nilimwambia huku nikicheka ili kumfanya ajisikie sahihi kumleta mwanae nyumbani kwangu, lakini kiukweli moyoni mwangu nilikuwa na wasiwasi sana na uamuzi wake, nilikubaliana nae lakini nilikuwa sina imani na usalama wake, niliamini alikuwa akipanga kitu kibaya dhidi yake lakini sikuwa na namna ya kufanya, aliishi Dar es laam na mimi niliishi Mwanza, wazazi wake nao waliishi Musoma hivyo kwa namna yoyote ile, nilichokuwa nikihisi anataka kukifanya kulingana na mwenendo wake kwa siku za karibuni, sikuwa na uwezo wa kukizuia na kiasi fulani niliona ni busara endapo ni kweli alikuwa akikusudia kufanya kitu nilichokuwa nakihisi.

“Itabidi nikuongezee hata kama unataka kubeba jukumu hilo peke yako.” Alinambia kisha akaniaga na kukata simu, nilipohakikisha simu haipo hewani, nilishusha pumzi nyingi huku nikifumba macho na kupitisha sala fupi kumuombea, nilihuzunishwa na mazito aliyokuwa akipitia, kufiwa na mtu wako wa karibu ni pigo ambalo wengi hawataki kulisikia, lakini likikuta inahitaji moyo wa ziada kuweza kulikabili na kuliishi.

Kwa kuyajua hayo ndiyo maana nilihisi aliyokuwa akipitia yalimpa msongo wa mawazo hadi kufikia hatua ya kuhisi mke wake anampigia simu kila mara usiku, jambo ambalo akili ya kawaida ni ngumu kukubaliana nalo na si mke wake tu, aliibua na simu ya rafiki wa mke wake. Kwangu mimi niliona ni ndoto za alinacha na hata nilipojilazimisha kukubaliana na alichombia, bado nafsi yangu iligoma kukubaliana nae na kitu pekee nilichokihofia kwake ni usalama wa maisha yake, niliamini kama ataendelea kuwa katika hali hiyo ingelikuwa rahisi kwake kujidhuru, nikapanga kuwasiliana na wazazi wake ili wanisaidie kumsihi akubaliane na ushauri wangu wa kumwekea mwalimu wa afya ya akili hasa msongo wa mawazo.

Baada ya kumaliza kuwasiliana nae nikarejea ukumbini na bahati nzuri nikamkuta msaidizi wangu akiwa hatua za mwisho kuahirisha sherehe ile, nikampokea na kuhitimisha shangwe za wanandoa na ndugu na jamaa waliokuwa wamejumuika pamoja usiku huo. Baada ya sherehe nililazimika kumalizia baadhi ya mambo ikiwemo kuhakikisha muziki umefungwa na kuagana na wanasherehe walionialika kusherehesha.

Baada ya hayo yote nilirejea kwenye hoteli niliyokuwa nimefikia kwa siku zote nilizokuwa Shinyanga, nilalala huku nikiwa na wazo la kuamka na kuanza safari ya kurejea jijini Mwanza kuiona familia yangu, huku nikipanga kushauriana na mke wangu kuhusu hali aliyokuwa akipitia rafiki wa familia yetu, lakini kati ya yote ambayo ningelimshirikisha, suala la mtoto wa Bahati kujumuika nasi lingekuwa ni jambo jema zaidi kwake kuliko mambo mengine yote. Lakini ni kwa kuwa misemo ya wahenga huwa ni ngumu kuizingatia hadi likukute jambo, kiukweli ni kwa kuwa sikujua yajayo na laiti kama ningelijua, ningejitahidi kwa kadri ya uwezo wangu kuepuka. Maisha ya binaadamu ni fumbo lisilo mfanowe, nikalala nikiwa na malengo yangu ya kimaisha kama kawaida huku jambo kubwa likiwa ni kuomba afya njema ili niyafanikishe yote niliyojipangia.
____________

Jane alifunika ukurasa wa tisa wa jarida lililokuwa mkononi mwake, aliinua uso wake na kuitazama picha kubwa iliyokuwa ukutani, ilikuwa ni picha ya mume wake, mume ambae simulizi ya mapito yake ilikuwa inaendelea kwenye jarida la Ngano Zetu. Jambo kubwa liliomfanya ainue kichwa na kuitazama picha iliyokuwa ukutani, ni baada ya kusoma ukurasa wa tisa na kugundua aliyekuwa akimtazama ukutani, alikuwa na mtoto mwingine ambae alikuwa ni mkubwa kuliko watoto wake wawili aliokuwa nao wakati huo.

“Kwa nini hukuwahi kunambia kama una mtoto mkubwa kuliko watoto wangu? Kwa nini ulinificha?” Alijiuliza huku akiwa bado ameikodolea picha ya mume wake ukutani, alitamani kuuliza kwa sauti ili ajibiwe lakini aligundua haingewezekana picha kumjibu, alitamani anyanyue simu yake na kumpigia mumewe na kumuuliza kuhusu hilo jambo, lakini alijionya kwa kuwa hakutaka kuzua mgogoro na mume wake na hakutaka kuikosa simulizi ile ambayo aliamini ilikuwa na mengi ambayo alihitaji kuyafahamu, alihofia endapo angezua mgogoro pengine mume wake angelisitisha uchapishwaji wa simulizi hiyo na yeye angelikosa mengi ambayo alihitaji kuyafahamu. Alishusha macho yake na kuutazama ukurasa wa kumi ambao ulikuwa unamhusu mtu aliyekuwa anamtazama kwenye picha ukutani, akaanza kusoma.
 
angelikosa mengi ambayo alihitaji kuyafahamu. Alishusha macho yake na kuutazama ukurasa wa kumi ambao ulikuwa unamhusu mtu aliyekuwa anamtazama kwenye picha ukutani, akaanza kusoma.

----Bahati Mwamba---

Kwangu mimi lilikuwa ni jambo la kushangaza na kuogofya, simu mbili kutoka kwa watu ninaofahamu mahali walipo kuita kila ilipofika majira ya saa sita usiku. Watu hao tayari walishatangulia mbele ya haki, uwepo wao Duniani ulibaki jina tu na historia kwamba na wao walipata kuishi.

Baada ya kuwa napokea simu usiku kutoka kwenye namba ya marehemu mke wangu, niliamua kuwa naizima kila nilipokuwa nikienda kulala, lakini ajabu iliyonikuta siku namba ya rafiki wa mke wangu iliponipigia, ni pale simu ilipojiwasha yenyewe na kuanza kuita kwa fujo na nilipotizama mpigaji, ilikuwa ni namba ambayo mmiliki wake nilikuwa najua alikwishafariki siku chache baada ya kifo cha mke wangu, Mama Itu. Nilitetemeka na jasho likaanza kunitoka licha ya kwamba nilikuwa nimewasha kipoozajoto.

“Ni nini hiki!?” Nilijiuliza huku mkono wangu wa kushoto ukifanya jitihada za kugusa masikio yangu ili kuhakikisha kama sikuwa naota, nilifumba macho na kuyafumbua mara kadhaa ili kuhakikisha nilikuwa timamu na si ndoto zilizokuwa zikinisumbua. Nilikuwa kwenye utimamu wangu wala si ndoto, haraka nilitupa shuka na kuweka miguu yangu chini kisha nikapiga hatua za haraka kuelekea kwenye kiwasha taa, nikawasha taa na kuangaza kila kona ya chumba changu ili kuhakikisha kama nilikuwa peke yangu. Chumbani nilikuwa peke yangu na hakukuwa na mtu mwingine wala dalili ya uwepo wa mtu mwingine.

“Au na mimi ndo nakaribia kufa?” Nilijiuliza huku nikirejea simulizi za watu ya kwamba, kuna wakati mtu aliyekwishatangulia kufariki huwa anaweza kupendekeza mtu wa kwenda nae na mara nyingi huwa ni kwa wale wapendanao. Wakati nikiwaza hayo, masikio yangu yalikuwa yakisikia kelele za muito wa simu yangu iliyokuwa kando ya mto niliokuwa nimeegesha kichwa muda mfupi uliopita.

“Hapana, inawezekana ni mambo ya ajabu yananiandama.” Nilijisemea huku nikifyatua komeo la mlango wa chumbani kwangu, nilitoka sebuleni na moja kwa moja nikanyoosha kwenye chumba alichokuwa amelala mwanangu mwenye umri wa miaka sita, alikuwa ni mtoto wa kiume na tangu kufariki kwa mama yake, aliogopa kulala chumbani kwangu kwa sababu kulikuwa na picha za mama yake ukutani na mara nyingi alilalamika kuziota picha zile.

Tukatengana vyumba na hakuwa akitaka tujumuike pamoja kwa sababu alikuwa akihisi uwepo wa mama yake kila akiniona hasa nyakati za usiku, kiufupi ndani ya nyumba tuliishi na kivuli cha mama mwenye nyumba, si mimi wala yeye ambae hakuwa akisumbuliwa na hisia za aina hiyo, lakini mimi ikawa ni zaidi ya hisia na ikageuka kweli baada ya simu yangu kuanza kupigwa na namba iliyokuwa sawasawa na ya mke wangu na nilipoipokea, mtu aliyezungumza sauti yake ilifanana kwa kila kitu na sauti ya mke wangu.

Nilifika kwenye mlango wa chumba cha Itu, nikausukuma mlango na kuingia ndani taratibu sana, Itu alikuwa amelala chali huku shuka likiwa mbali na mwili wake, mwanangu alikuwa ni mlalavi. Niliinua mkono wangu na kumgusa mara kadhaa hadi alipoamka.

“Kumekucha?” Aliniuliza huku akipiga miayo mfululizo na kujinyoosha mara kadhaa.

“Hapana, bado usiku mbichi kabisa.” Nilimjibu huku nikimsaidia kuinuka na kushuka chini.

“Baba, siku hizi mimi sikojoi kitandani, mbona unaniamsha?” Aliniuliza kwa sauti ya kulalamika huku akionekana kukereka na kile nilichokuwa nimemfanyia.

“Nifuate mwanangu.” Nilimwambia huku nikipiga hatua kuelekea mlangoni, alinifuata huku akipiga miayo mfululizo.

Tulipofika sebuleni nilimuomba asimame.

“Unasikia sauti ya kitu gani?” Nilimuuliza huku nikimtazama usoni kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha namuona akiwa kwenye utimamu wake.

“Mh!” Aliguna huku akiinua macho yake na kunitazama, sikujua alichokuwa akiniwazia wakati huo lakini alionekana kuwa kwenye kwaziko fulani lakini alishindwa kusema kwa sababu aliyekuwa mbele yake ni baba yake mzazi.

“Hiyo si ni simu yako inaita!” Alinijibu huku miayo miwili mfululizo ikimtoka.

“Good! Hebu rejea chumbani kwako na ulale.” Nilimwambia huku nikiweka tabasamu la uongo usoni mwangu.

“Labda tulale wote, tayari usingizi umekata na sitaweza kulala peke yangu usiku huu.” Alinambia huku akijibweteka kwenye sofa lililokuwa kando yake.

“Utalala chumbani kwangu au mimi nikufuate chumbani kwako?” Nilimuuliza.

“Chumbani kwako silali, naomba tulale chumbani kwangu.” Alinijibu huku akifumba macho kwa uchovu, nilijua bado usingizi ulikuwa unayatesa macho yake na si kweli kama alikuwa hana usingizi.

“Lala hapo kwenye sofa, nitakuchukua muda mfupi tu.” Nilimwambia huku nikielekea chumbani kwangu ambako bado simu yangu ilisikika ikiita, na ilipokata, iliita tena.

Nilipoingia chumbani simu yangu ilianza kuita kwa mara nyingine, mara hii nikajivika ujasiri na kuichukua baada ya kuhakikisha simu ilikuwa ikisikika kwa masikio ya kawaida na ndiyo sababu nilienda kumuamsha Itu anipe uhakika.

Namba iliyonipigia ilikuwa ni ile ile namba ya Asulia, rafiki kipenzi wa marehemu mke wangu. Nikaipokea na taratibu nikaiweka sikioni huku mkono wangu ukitetemeka kwa hofu, pumzi zangu zilitoka bila mpangilio, hakika niliogopa sana siku ile na ilikuwa ni moja ya siku ngumu sana maishani mwangu.

“Hey shemeji usiogope bwana..” Sauti ya Asu ilisikika na kufuatiwa na kicheko cha kawaida kabisa ambacho mara zote nilikisikia kutoka kwa shemeji yangu Asulia. Haraka niliitoa simu sikioni mwangu na kutazama kama ni kweli nilikuwa sahihi kuifananisha ile namba, naam, ilikuwa ni namba ile ile na hakukuwa na tofauti. Nikairejesha sikioni na bila kusema kitu nikaendelea kusikiliza.

“Naomba usiingie kwenye mnyororo uliotufunga, wakija, wape wanachotaka.” Sauti ilisikika kwa utulivu kisha simu ikakatwa, nikabaki nikiwa nimeganda mithili ya mtu aliyeponyokwa na kijambo mbele ya jopo la wana kikao cha upangaji mahali.
Kiukweli nilishindwa cha kufanya usiku ule, moyo uliingiwa na ubaridi wa ajabu, akili yangu iliyokuwa imevamiwa na uoga ilishindwa kuchanganua kilichokuwa kikiendelea kwa siku za karibuni. Nilichanganyikiwa zaidi na maonyo ya watu wawili tofauti na wote wakiwa ni marehemu, sauti ya mke wangu ilinionya nisitoe wanachotaka, lakini sauti ya rafiki wa mke wangu inanisihi nitoe wanachotaka. Maswali mawili yakabaki kichwani mwangu na hakukuwa na wa kuyajibu; Wanataka nini? Kina nani hao? Yote yalikuwa ni maswali ambayo hakukuwa na kuwayajibu, lakini swali ambalo halikuwa na jibu kabisa ni kuhusu waliokuwa wakinipigia simu, ni kina nani? Ni kweli kuna watu wakifa huwa wanageuka kuwa mizimu? Yalikuwa ni maswali ambayo hakukuwa na kuyajibu asilani labda hao waliokufa siku wakififuka.

Unaweza kuhisi lilikuwa ni jambo la kufikirika, lakini lilikuwa ni jambo la ukweli na lilinokuta siku hiyo na jambo la kuchanganya zaidi ni kwamba, simu yenye kadi aliyokuwa akiitumia mke wangu ilikuwa pale ndani na mimi ndiye niliyeohifadhi kwenye begi la vitu vya muhimu vya mke wangu, lakini namba za kadi hiyo ya simu zilikuwa zinanipigia na sauti ikiwa ni ile ile ya mwenye kadi hiyo ambae alikuwa ni mke wangu. Wakati nikiwa napambana na kutatua kitendawili cha upande wa mke wangu, kitendawili cha rafiki yake nacho kinajitokeza, hakika kwangu ulikuwa ni mtihani mgumu kujibika na sikuona mtu anaeweza kunisaidia kuujibu na ni hata nilipowaza kuwashirikisha watu wengine, niliamini wataishia kuniona naelekea kuchanganyikiwa na mawazo yangu yalikuwa sahihi, rafiki yangu wa karibu ambae nilihisi anaweza kunielewa, nilipomwambia alikuwa wa kwanza kuniruka huku akinishauri kunikutanisha na mwalimu wa afya ya akili.

“Hili jambo lazima nilijue likoje, haiwezi kuwa bahati mbaya, kuna kitu kitakuwa kinaendelea.” Niliwaza huku nikipiga hatua kuelekea sebuleni ambapo nilijumuika na mwanangu kwenye sofa, alilala, mimi nilikaa pembeni yake nikimtizama.

“Siwezi kuanzisha harakati zozote nikiwa na huyu kiumbe karibu yangu, lazima nimweke mbali na hii nyumba.” Niliwaza huku nikipitisha mkono kichwani kwake na kuzigusa nywele zake bila kummbugudhi, niliendelea kuwaza mengi yaliyokuwa yakiendelea kwa siku za hivi karibuni hadi nilipopata wazo la kumtafuta rafiki yangu, Paul Kusekwa.

Lengo la kumpigia simu usiku huo si kumwambia kuhusu mazingaombwe yaliyokuwa yakiendesha akili yangu, nilijua hata nikimwambia itakuwa si rahisi kunielewa kwa sababu siku chache nyuma nilipomshirikisha, aliishia kuniomba nimruhusu anitafutie mtaalamu wa masuala ya saikolojia, aliamini nahangaishwa na msongo wa mawazo na alihofia hali hiyo ikiendelea naweza kuugua hata uchizi au kufanya mambo ambayo kwangu nitaona ni sawa. Sikutaka kumlaumu sana kwa sababu hata mimi kama ningeliambiwa na mtu mwingine habari kama zile, hakika ingenichukua muda mrefu sana kuamini. Ilikuwa ni sawa na mtu kukusimulia ndoto ambayo kwa kiasi kikubwa huwa hakuna uhalisia, lakini kiukweli yote niliyomwambia yalikuwa ni kweli na hakukuwa na uongo wala ndoto katika hilo, lakini nani angeniamini?

Lilibaki ni swali ambalo hakukuwa na wa kunijibu na hata nilipofikiria kuwashirikisha wazazi wangu, niliona ni kuwapa mzigo ambao ungeishia kuhangaisha nafsi zao, sikutaka kuendelea kuwapa maradhi ya moyo, niliacha waishi kwa amani na kila nilipowasiliana nao sikuwambia yaliyokuwa yakinisibu. Kitu ambacho siku zote nilikiamini ni kujipa muda, mara zote ambazo huwa napitia nyakati tatanishi huwa ni mara chache sana kuomba msaada kwa mtu, niliamini ni ngumu mtu mwingine kubeba uzito wa jambo lako kama ambavyo utakuwa umelibeba, mtu pekee ambae ningeliweza kumshirikisha kwa wakati huo hakuwepo na hatokuja kuwepo, mtu huyo ni mke wangu mama Itu.

Niliwasiliana na Paul kisha nikamuomba mwanangu akaishi nyumbani kwake kwa muda ambao sikuwa nimemwambia na sikumwambia kwa sababu, hata mimi sikuwa najua itanichukua muda gani kukabiliana na mambo yaliyokuwa yakiendelea dhidi yangu, mambo ambayo niliona ni kama ushirikina ulikuwa ukihusika, lakini sikuwa nimeweka mawazo yangu sana kuwaza ushirikina, niliondoa mawazo yangu upande huo baada ya kujihakikishia sauti zilizokuwa zikitoka kwenye simu, zilikuwa ni sauti zinazoweza kusikiwa na mtu mwingine tofauti na mimi, hivyo nililiweka jambo lile kwenye mzani mwingine ambao niliamini unahitaji majibu yangu ili kujua uzito wa jambo hilo.

Maongezi yangu na Paul yalichukua zaidi ya dakika kumi na tano, yalichukua muda wote huo kwa sababu ilitokea kutofautiana kidogo, kabla sijamwambia sababu ya kumpigia simu tayari yeye alikuwa ameshaanza kunishauri kuhusu kunitafutia tabibu wa afya ya akili, hakuwa tayari kuacha niendelee kuweweseka na ndoto ambazo aliamini ndizo zinazonichanganya. Baada ya ubishani wa hapa na pale, nilimwambia lengo langu na kisha nikamwambia jambo lingine ambalo sikuwa na uhakika kama atalizingatia, sikuamini kwa sababu wakati nazungumza nae niligundua alikuwa ameshachangamka kwa kunywa kilevi, lakini kwa kuwa lengo langu lilikuwa ni kumuomba hifadhi ya mwanangu, nami sikuzingatia sana hilo jambo lingine ambalo nilimwambia, kikubwa tulikubaliana mwanangu aende kuishi nyumbani kwake na sikuwa na wasiwasi kwa sababu nilimfahamu vema mke wake, Mama D. Mama D alikuwa ni miongoni mwa wanawake wenye roho za kipekee sana, mchangafu, mcha Mungu na kikubwa zaidi alikuwa ni mwanamke anaejali sana watu wanaokuwa karibu na familia yake, hata baada ya kifo cha mke wangu, alikuwa mtu wa kwanza kuomba kuishi na mwanangu kwa sababu aliamini majukumu yangu yalihitaji msaidizi ambae atakuwa karibu na mwanangu, lakini kubwa zaidi alihofia kama nitaoa mapema, mwanamke wangu mpya angeliweza kuwa si mwema sana kwa mwanangu. Mama D alikuwa ni mwanamke mwenye roho yake hapa Duniani.

Baada ya kuwasiliana na Paul na kuelewana, niliitupa simu pembeni na kukaa huku mawazo yakichukua nafasi kichwani mwangu, niliwaza mengi kuhusu simu zilizokuwa zikipigwa nyakati za usiku na kisha kuongea na watu waliokwisha kufa; kuna wakati mawazo yalinipeleka kwenye hofu na kunawakati nilijipa moyo. Usingizi ulipaa na sikutamani kulala, zaidi niliendelea kukaa kwenye sofa huku nikiwa nimechukua shuka chumbani na kumfunika mwanangu Itu, ambae alikuwa amelowea kwenye usingizi mzito na mara chache alijigeuza huku akitoa sauti za raha ya usingizi wake.
 
Mawazo mengi yalipita lakini wazo moja lilikuwa likijirudia kichwani mwangu, utata wa kifo cha Mama Itu. Licha ya kumuachia Mungu, lakini sikuwahi kuamini mazingira ya kifo cha mke wangu, kulikuwa na utata mwingi ambao kila nilipoufikuria niliona kuna jambo ambalo lilikuwa haliko sawa, jambo hilo lilinifanya niombe usaidizi wa tabibu niliyemuamini kuchunguza mwili wa mke wangu, lakini bahati mbaya nilipuuza kwenda kuchukua majibu ya uchunguzi nilioomba, nilipuuzia baada ya kuhisi naweza kununua ugomvi ambao sijui mwanzo wala mwisho wake, nilijionya hivyo baada ya kifo kingine cha utata cha mtu wa karibu na mke wangu, tena alifariki saa chache baada ya kutoka nyumbani kwangu ambako tuliweka msiba wa mama Itu, na kabla ya kuondoka alinifuata na kuniaga kwamba anaenda kuoga na kubadili mavazi, lakini alinambia kuna jambo alihitaji kuongea na mimi akirejea na hakurejea hadi nilipopata taarifa za kifo chake. Mwili wake ulikutwa ndani kwake huku taarifa zikitoka kwamba, alikutwa kajinyonga na hakuacha taarifa yoyote.

“Kwa nini vifo vyao vilifuatana? Asulia alitaka kunambia kitu gani?” Nilijiuliza lakini hakukuwa na wa kunipa jibu na maswali hayo sikuwahi kujiuliza huko nyuma, nilijionya kwa sababu sikutaka kumuacha Itu akiwa hana wazazi kwa sababu niliamini kama kulikuwa na jambo nyuma ya vifo vyao, basi ni vema nikaishi bila kulifahamu ili niwe salama, nikajionya kwa msemo maarufu kwenye nyanja za kijasusi, msemo ambao mara nyingi niliusikia kutoka kwa rafiki yangu Honda Makubi ambae alikuwa ni jasusi na mpelelezi wa kuaminika sana hapa nchini, mara zote alipenda kunambia, GET OFF X.

Alipenda kunambia hivyo kila nilipokuwa nikimfuata anipe visa vichache ambavyo alikutana navyo kwenye harakati zake, lakini mwishoni aliishia kunionya kwa kauli hiyo akimaanisha, nikae mbali na matatizo yasiyo ya lazima hasa kwenye baadhi ya mikasa ambayo aliona bado ina mnyororo ambao haukuonekana mwisho wake. Niliishi na kauli hiyo, hata wakati nilipohisi kuna utata kwenye mazingira ya kifo cha mke wangu, niliamua kukaa mbali ili kumlinda mwanangu lakini japo nilikaa mbali, lakini tatizo lilianza kunifuata; simu za kila usiku ziliibua hisia mbaya kichwani mwangu na sikuwa na namna zaidi ya kupata ufumbuzi ili niishi kwa amani. Lakini ni kwa kuwa sikuwahi kujua yajayo ni mazito kuliko yaliyopita, na laiti ningelijua, hakika ningekaa mbali zaidi na balaa lililokuwa likinizonga. Hakika sikujua!

******
Mapambazuko yalinikuta nikiwa bado nimekaa kwenye sofa, sikuwa na hata lepe la usisingizi wala sikujisikia kulala, usingizi ulinipaa. Kwa kuwa ilikuwa ni siku ya shule kwa wanafunzi, niliamka na kuelekea jikoni huko nilitayarisha chai na maji ya uvuguvugu kisha nikarejea na kumwamsha Itu, aliamka na kunisalimia lakini hakuacha kuniuliza swali.

“Ni kwa nini uliniacha nilale hapa?” Aliuliza huku akijinyoosha na kupiga miayo. Nilitabasamu na bila kumjibu swali lake nikamtaka aelekee bafuni kukoga, alienda na ndani ya muda mfupi alirejea, nilimwacha akajiandae kisha alipomaliza alikuja kujumuika nami mezani. Baada ya kumaliza kupata kiamsha kinywa, nilimsindikiza barabarani ambapo alipitiwa na gari la shule. Nilipohakikisha mwanangu amekwenda shule, nilirejea nyumbani na moja kwa moja nilielekea chumbani na kitu cha kwanza nilichokifanya ni kufungua sanduku la chuma nililokuwa nimehifadhi baadhi ya vitu vya muhimu vya marehemu mke wangu.

Baada ya kulifungua macho yangu moja kwa moja yaliangukia ilipokuwa simu yake, niliichukua na kuiwasha na muda mfupi baadae laini zake zikawa hewani, jumbe kadhaa ziliingia ila nyingi zilikuwa kutoka kwa makampuni ya kuendesha bahati na sibu, lakini ujumbe mmoja ulikuwa umetoka kwenye namba ya rafiki yake Asu. Mwanzo nilihisi ni michezo ile ile inaendelea kutoka kwa watu au mtu anaetumia namba ya Asu, lakini nilipochunguza tarehe ulipotumwa ujumbe ule, nikagundua ilikuwa ni ileile siku aliyokuwa amefariki mke wangu na ilikuwa saa mbili kabla ya kifo chake kilichotokana na ajali ya gari, ina maana ujumbe ule siku ile uliingia lakini haukusomwa na ndiyo maana nilifanikiwa kuona licha ya ukweli kwamba, ilikuwa imepita miezi kumi na tatu tangu ajali hiyo ya kutatanisha itokee. Lakini hata kabla sijajiuliza sana kuhusu ujumbe ule, nikawaza kuhusu kadi ya simu ya mke wangu kuwa inaendelea kutumika hadi wakati huo kwa sababu, tangu siku aliyofariki simu yake haikuwashwa na yeyote na kawaida ya makampuni ya kadi za simu huwa wanafunga laini zisizokuwa hewani kwa kipindi cha kuanzia miezi saba, hivyo sikutarajia kukutana na kadi inayofanya kazi na kupokea jumbe mpya.

“Ina maana ni kweli hii kadi ya mke wangu inakuwaga hewani? Nani anaeitumia na kwa nini zote mbili zinafanya kazi?” Nilijiuliza huku nikiendelea kukagua ile simu kwenye boksi la kuhifadhi jumbe fupi, nilishangazwa na hilo jambo kwa sababu kwa kawaida endapo utaamua kurejesha matumizi ya kadi ambayo haipo hewani, hata kama mtu atataka kutumia ile kadi ya zamani haitawezekana kutumika, kiukweli ilinishangaza sana kwa sababu namba ya ile kadi iliyokuwa kwenye simu ya mke wangu, ndiyo hiyohiyo iliyokuwa ikinipigia usiku na sauti ya marehemu ilisikika ikizungumza.

“Ina wezekanaje?” Nilijiuliza bila kupata majibu na kwa kuwa hakukuwa na wa kunipa majibu, nikapanga kuyatafuta kwa kuuliza baadhi ya watu ambao niliamini wangenipa majibu sahihi, hata kama nisingeliridhika basi ingenilazimu kuingia mtandaoni na kuyatafuta mwenyewe.

Nilirejesha mawazo yangu kwenye ule ujumbe uliokuwa umeingia kwenye simu ya mke wangu na hakuwa ameusoma, ulisomeka hivi…
‘HUKO KUNA MKASI, PLEASE USIENDE MY DEAR.’

Nilirudia kuusoma zaidi ya mara mbili na sikupata maana zaidi ya onyo, ilioneka alimuonya mke wangu asiende mahali fulani ambako kwa mujibu wa ujumbe, kulikuwa na MKASI. Tafakari yangu ikabaki hapo kwenye neno MKASI, ni nini kitu hicho? Ni wapi kuliko na huo MKASI? Na kwa nini alimuonya?

“Kwani hawa watu walikuwa na jambo gani walilokuwa wakilifanya?” Nilijiuliza huku nikiendelea kuperuzi jumbe walizokuwa wakitumiana, nyingi zilikuwa za kawaida, michambo ya hapa na pale lakini kuna baadhi ya jumbe hazikuwa za kawaida, zilikuwa ni jumbe zenye maana fulani hivi ambayo sikuilewa. Mfano, kulikuwa na ujumbe uliosomeka hivi; ‘PALE PALE KWENYE TT065, NA UKIINGIA NI KICHWA CHA MZEE WANGU, 2>4-2-8-4.’ Huo ulikuwa ni ujumbe wa mke wangu kwenda kwa Asulia na Asu nae alijibu.. ‘HAKUKUWA NA DALILI ZA MACHO YA TAI?’ Mke wangu akajibu, ‘MWEWE HAJIWINDI' Baada ya ujumbe huo hakukuwa na ujumbe mwingine uliokuwa na mafumbo magumu ambayo yalinishinda kuyaelewa na hapo likaja swali lingine kichwani kwangu.

“Mama Itu na Asulia ni kina nani?” Nilijiuliza vile kwa sababu nilihisi jumbe zile zilikuwa na ujasusi ndani yake, watu wa kawaida wasingeliweza kuwasiliana kwa namna ile, lakini hisia hizo zilikosa nguvu kichwani kwangu kwa sababu nilimfahamu vema mke wangu, sikuwahi kudhani wala kuona dalili za kuwa ni kipepeo mweusi, lakini hapo tena nikaukumbuka msemo wa rafiki yangu Honda, ambae mara nyingi alipenda kunifundisha nisimuamini kila mtu hata kama ni baba yangu mzazi na mara zote usemi huo aliusema kwa lugha ya kigeni, Trust no one.

“Yawezekana sikuwa nikimfahamu mwanamke wangu.” Nilijiambia huku nikiizima ile simu na kuirejesha kwenye sanduku, nikalifunga sanduku lenyewe baada ya vitu vingine kukosa jambo lenye msaada, nikalirejesha nilipolitoa na kubaki nikiwa nimesimama katikati ya chumba huku nikiwaza kuhusu zile jumbe, baada ya mawazo kidogo, nikakumbuka kitu na bila kujiuliza mara nyingi, nikapiga hatua na kulifikia kabati la nguo, nikalifungua na kwenye vyumba vya juu nilichukuwa kitabu changu cha kumbukumbu, nikachukua na kalamu na kuandika baadhi ya vitu muhimu nilivyoviwaza ahsubuhi ile kisha, nikairejesha na kulifunga kabati.

“Ngoja nianze na kifo chenyewe.” Nilijisemea huku nikichukua ufunguo wa gari langu na kutoka nje ya chumba, nilipanga kuelekea zilipokuwa ofisi alizokuwa akifanya kazi Mama Itu, huko nilitaka kwenda kufuatilia malipo yaliyotakiwa kulipwa kwa familia yangu baada ya kifo cha mfanyakazi wao, lakini si kufuatilia tu, bali nilikuwa na jambo langu kichwani.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom