Riwaya: Siri

Shukran kulubule kwa kigongo hiki!
 
SIRI

Episode 14
Mtunzi. Patrick CK

asubuhi uje na mpango mzuri wa
kuwaweka watu hawa mbali
mbali.Kama ukishindwa kuwa na
mpango mzuri nitatumia hata
nguvu.Good night Nkebo”
“Good night Mr president”
Akasema Donald Nkebo akihisi joto
HAIFA - ISRAEL
Asubuhi ya saa tano siku
iliyofuata,Dick akiwa ndani ya vazi
la wagonjwa akatoka chumbani
kwake akiwa ameongozana na
muuguzi wake Salome,wakaelekea
bustanini Lengo lilikuwa aweze
kufahamiana na mgonjwa
mwenzake mwenye asili ya Afrika
ambaye ni Edger Kaka toka Tanzania.
Baada ya nusu saa tangu
wakae pale bustanini Salome
akawaona Edger na Dr Olivia
wakielekea katika bustani
akamjulisha Dick kwamba wale
ndio wanaotoka nchini
Tanzania.Dick akawatazama kwa
makini sana
“Sura ya yule mwanamke
ninahisi kama ninaifahamu,ninahisi
nimewahi kuiona mahala
Fulani.She’s so pretty” akawaza
Dick.
“Christopher yule mgonjwa
alikuwa na maradhi kama yako ya
moyo na alifanyiwa upasuaji na
kwa sasa anaendelea vizuri.Ungependa kufahamiana
naye?
“Ndiyo ningependa
kuwafahamu” akajibu Dick
Salome muuguzi maalum wa
Dick akainuka na kuwafuata akina
Edger na Dr Olivia mahala
walikokaa,akawasalimu na
kuzungumza nao.
“Naitwa Salome,ni muuguzi
hapa hospitali na kwa sasa
ninamuuguza mgonjwa toka
Zimbabwe,anaitwa Christopher
Nkosizwe.Hamtoki nchi moja lakini
wote mnatoka bara moja la
Afrika.Mngependa kusalimiana na
kufahamiana? Akauliza Salome
“Ni jambo zuri sana kufahamiana.Nafurahi kukutana na
mwafrika mwenzetu
hapa.”akasema Edger
Salome akamshika mkono Dick
aliyeonekana kama mgonjwa sana
akamsaidia kufika pale walipokuwa
wamekaa akina
Olivia.Akawatambulisha
wakasalimiana.Dick akamsalimu
kwanza Edger halafu akamshika
mkono Dr Olivia
Ninafurahi sana kukufahamu
Olivia”
“Hata mimi nafurahi sana
kukufahamu Christopher.Pole sana
na ugonjwa” akasema Dr
Olivia.Dick akaendelea kuushika
mkono wa Dr Olivia “I’m sure I’ve seen her
before.Hii si sura ngeni machoni
pangu.Gosh ! she’s so pretty.Lazima
nimfahamu kiundani mrembo
huyu” Dick akawaza akiwa bado
ameendelea kuushikilia mkono wa
Dr Olivia,Edger akamtazama Dick
kwa macho makali ndipo
alipomwachia mkono Olivia
wakaendelea na maongezi.Ulikuwa
ni mwanzo mzuri wa kuanzisha
urafiki baina yao
TANZANIA

Saa tatu za asubuhi Donald
kebo akiwa ofisini kwake na timu
ya vijana aliowapa kazi maalum ya kuwafuatilia baadhi ya wanasiasa
hasa wale ambao wameonyesha
kutangaza nia ya kuwania urais.
“Awali ya yote napenda
niwashukuru kwa kazi nzuri
mliyoifanya vijana wangu” Donald
Nkebo akafungua kikao kile
“Jana usiku baada ya kupokea
taarifa ile ya mazungumzo
yaliyofanywa kati ya Edger na mtu
wake hapa Tanzania aitwaye
Stanley,nilimtumia maongezi yale
mheshimiwa rais akayasikiliza.Kwa
ufupi mheshimiwa rais
anakupongezeni sana kwa kazi
nzuri na anataka muongeze juhudi
zaidi.Kwa kuwa kwa sasa
tumekwisha kuwa na uhakika kuwa Edger anafikiria kugombea urais
wa Tanzania,kinachofuata kwa sasa
ni kumfuatilia na kuzifahamu
nyendo zake,tujue anajipanga
vipi,timu au nani wako nyuma
yake.Tumfuatilie sana huyu Stanley
ambaye ni mtu wake wa karibu
sana na huyu ndiye atakayetupa
majibu yote kuhusiana na kile
tunachokichunguza.”Donald
akanyamaza kwa muda halafu
akasema
“Nataka nifahamu pia kwa
undani mmejipanga vipi kuhusiana
na mheshimiwa Damiani mwamba?
Akauliza Donald
Paul ambaye ndiye kiongozi
wa timu ile akajibu “Donald,tayari tumekwisha
jipanga vya kutosha kuhusiana na
Mr Mwamba.Tumeanza zoezi la
kumfuatilia na muda si mefu
tutakuwa na taarifa kamili juu
yake.Tukishapata taarifa kamili
ndipo tutakapopanga vizuri
mpango wetu wa kumuondoa
kabisa katika ulingo wa
siasa.Umaarufu alionao kwa sasa
usiwatie shaka.Mimi na timu yangu
tuna imani kubwa kwamba pindi
tutakapoanza kazi yetu utakuwa
ndio mwisho wake.Hatasikika tena
katika ulingo huu wa siasa”
Donald akatabasamu na
kusema
“Vizuri sana Paul.Ninachowaomba ni kuongeza
juhudi na kasi zaidi ili tuweze
kuendana na muda na kasi ya
wapinzani wetu.Nataka tumalize
haraka kwa hawa watu wawili
ndipo tugeukie na vyama pinzani”
“Usijali Mr Donald.Tunafanya
kazi vizuri na hata hivi sasa vijana
wetu wako kazini wakimfuatilia Mr
Mwamba toka aamkapo asubuhi
hadi aendapo kulala.Naomba
umuhakikishie rais kuwa kamwe
hatutamwangusha” akasema Paul
na Donald akatabasamu
Baada ya kumaliza
mazungumzo na akina Paul Donald
Nkebo akampigia simu rais Dr
Evans kama alivyokuwa amemuahidi usiku uliopita
walipozungumza
“Mr Donald,habari za toka
jana? Akasema Dr Evans baada ya
kupokea simu
“Habari nzuri kabisa
mheshimiwa rais”
“Sawa Donald,nipe habari.Jana
ulisema utakuja na mpango mzuri
sana wa namna ya kufanya ili
kumweka Edger mbali na
Olivia”akasema Dr Evans
“Mheshimiwa rais ,nimetoka
kujadiliana na vijana muda si mrefu
na tumeafikiana kuwa Olivia
asiondolewe karibu na Edger.Kuna
kila dalili Edger anampenda Olivia
na hataweza kumueleza kuhusu nia yake ya kuwania urais kwani Olivia
hataki Edger aendelee na mambo
ya siasa.Edger hayuko tayari
kuachana na siasa hivyo basi
ataendelea kuwasiliana kwa siri na
rafikiye Stanely na hivyo kutupa
sisi nafasi nzuri ya kujua kila
anachofanya.Iwapo tutamuondoa
Olivia kwa haraka kama
unavyotaka inaweza ikasababisha
Edger naye akaomba kurudishwa
nyumbani ili aendelee kuhudumiwa
na Olivia.Ushauri wangu tumuache
Olivia awe karibu na Edger ili
tuendelee kupata taarifa zake
wakirudi Tanzania tutafanya kila
tuwezalo kuwaweka mbali mbali
kama ardhi na mbingu” akasema Donald
Dr Evans Mwaluba akatulia
kidogo akatafakari yale
aliyoambiwa na Donald halafu
akajibu.
“Nimekuelewa Mr
Donald.Endeleeni na mipango yenu
lakini sitaki ukaribu huo wa Olivia
na Edger udumu muda mrefu”
“Usijali mheshimiwa rais tuko
makini sana katikahilo
suala”akajibu Donald.
“Sawa Donald nataak unipe
taarifa za mara kwa mara kila
mnachokifanya.Vipi kuhusu
Damian Mwamba? Mmeanza
kumfanyia kazi? Akauliza Dr Evans
“Tayari kazi imeanza mheshimiwa rais na vijana
wameahidi kwamba
hawatakuangusha.Nitakupa taarifa
kila pale watakaponipatia”
akasema Donald Nkenbo na
kuagana na rais
HAIFA - ISRAEL
“Nimefurahi sana kukutana na
kufahamiana na waafrika
wenzangu hapa Israel.Nilipoletwa
hapa sikujua kama nitakutana na
wenzangu kutoka Afrika.Japo
hatujatoka nchi moja lakini
tunatoka bara moja la Afrika hivyo
sisi ni ndugu.Naomba tuishi kama ndugu kewa muda ambao tutakuwa
wote hapa hospitali” Akasema Dick
baada ya kukutana na Olivia na
Edger bustanini.
“Hata sisi tumefurahi sana
kukufahamu.Ni faraja kubwa
unapokuwa sehemu kama hii
halafu ukakutana na mtu wa rangi
yako hata kama hamtoki nchi
moja.Unasema unatoka Zimbabwe?
Dr Olivia akauliza.
“Ndiyo.Natokea Harare
Zimbabwe.Ninafanya kazi katika
benki kuu ya Zimbabwe.Nimeanza
kuumwa toka mwanzoni mwa
mwaka huu.Nimetibiwa katika
hospitali kuu pale Harare lakini
bado hali yangu haikuwa nzuri na ndipo nikaletwa hapa kwa kwa
matibabu zaidi”
“Pole sana.Mimi naitwa Dr
Olivia Themba ni daktari wa
maradhi ya moyo toka
Tanzania.Huyu hapa ni mgonjwa
wangu anaitwa Edger ni mbunge
katika bunge la jamhuri ya
muungano wa Tanzania.Ninafanya
kazi katika hospitali kuu ya moyo
Tanzania ambayo ni kimbilio la
wagonjwa wengi katika nchi za
afrika mashariki na kati lakini bado
kuna nyakati tunalazimika
kuwaleta wagonjwa wetu katika
hospitali kubwa kama hizi nje ya
nchi kwa ajili ya matibabu
zaidi.Nitafurahi sana kama siku moja utatembelea hospitali yangu”
Dr Olivia akasema na kumfanya
Dick atabasamu.Edger bado
alikuwa akimuangalia Dick kwa
macho makali ya wizi.Ni dhahiri
hakupendezwa na uwepo wa Dick
mahala pale.
“Nimeshawahi kufika Dar es
salaam mara moja.Nilikuja
kuhudhuria semina ya masuala ya
uchumi na fedha kwa nchi za
mashariki na kusini mwa
afrika.Nilipapenda sana Dar es
salaam,nitakuja tena kutembea
safari hii nitafurahi zaidi kwani
nitakuwa na wenyeji wangu” Dick
akasema huku kila mmoja akiamini
kuwa Dick si mtanzania kwa namna alivyokuwa anazungumza.
“Karibu tena
Tanzania.Utakapokuja tena Dar es
salaam utakuwa na wenyeji”
akasema Dr Olivia
“Dr Olivia nitakuja Dar es
salaam.Ninashukuru sana
kuwafahamu.Kwa kuwa tuko
hospitali moja ninatumai tutazidi
kuonana na kuzungumza mambo
mengi zaidi”Akasema Dick huku
akijiweka katika mkao wa
kuondoka.Hakutaka kukaa sana
mahala pale kwa sababu
alikwishagundua kuwa Edger
hakupendezwa na uwepo wake
mahala pale.
“Hata sisi tumefurahi sana kukutana nawe
Christopher.Tutazidi kuonana” Dr
Olivia akashikana mkono na Dick
wakaagana.
“Kwa ugonjwa kama huu wa
Christopher ,ungeweza kutibika
kabisa pale hospitalini kwetu Dar
es salaam.Kuna ulazima wa
kuitangaza zaidi hospitali yetu nje
ya mipaka ya Tanzania” Dr Olivia
akasema mara baada ya Dick
kuondoka.
“Unaonekana kuvutiwa sana
na Christopher” akasema Edger
“Christopher??..Yes.Nimevutiw
a naye ,japokuwa ni mgonjwa lakini
bado ni mtu mcheshi sana.Ni mtu
ambaye huchoki kumsikiliza akiongea.Nitamshawishi siku moja
atembelee Tanzania na afike katika
hospitali yetu atibiwe ili kuokoa
fedha nyingi alizotumia kwa
matibau huku Israel.Au we
unasemaje Edger?akauliza Dr
OLivia
Edger hakujibu
kitu.Alionyesha dhahiri kukerwa na
kitendo cha Dick kuonana na Olivia.
“Edger mbona uko kimya
hivyo?”Dr Olivia akauliza.
“Nahisi uchovu
mwingi.Tafadhali nirudishe ndani”
Edger akasema na kumfanya Dr
Olivia kushangaa.Bila ubishi Dr
Olivia akamrudisha Edger
chumbani kwake. “Olivia nadhani unaweza
kwenda hotelini kwako kupumzika
,nahisi uchovu nahitaji kupumzika”
Edger akasema baada ya kufika
chumbani kwake.
Dr Olivia akamuangalia Edger
usoni akagundua kuna kitu
kinamsumbua.Hakutaka
kumbughudhi,akachukua mkoba
wake akamuaga na kutoka.Siku hii
alikuwa peke yake.Judy alibaki
hotelini akipumzika.Akiwa
amesimama akisubiri lifti ili ashuke
chini huku bado anatafakari ni kwa
nini Edger abadilike ghafla vile
mara akastuliwa na sauti ya
muuguzi ambaye mara moja
akamtambua kuwa ni yule muuguzi wa Dick
“Samahani Dr
Olivia.Nimetumwa na Christopher
kuwa anahitaji kukuona chumbani
kwake kama hutajali”
Dr Olivia akatabasamu na
kusema
“Sintajali.Nipeleke kwake”
Muuguzi yule akamchukua
Olivia na kumpeleka katika chumba
cha Dick.
“Christopher,nilikuwa
naondoka kurudi hotelini kwangu
nikakutanana na muuguzi
akaniambia unanihitaji” Dr Olivia
akasema baada ya kuingia
chumbani kwa Dick
“Ndiyo Dr Olivia,” Dick akajibu huku akimuonyesha ishara Olivia
aketi kitini.
“Dr Olivia shida yangu ni
ndogo tu.Wakati tukiwa kule
bustanini,mgonjwa wako Edger
kama sijakosea jina lake,alionekana
kama vile hakufurahia uwepo
wangu pale.Muonekano wake,kauli
zake vyote vilidhihirisha kuwa
hakupenda mimi kuungana nanyi.
Sikuwa na lengo baya lengo langu
lilikuwa ni kukutana na waafrika
wenzangu sehemu kama hii
ambayo ni nadra kumuona mtu
mweusi.Nimekuita hapa kusema
samahani kama niliwakera na
ninapenda kuahidi kuwa haitatokea
tena.Samahani sana Dr Olivia” Dick akasema
Dr Olivia akamtazama Dick
kwa makini usoni halafu
akatabasamu
“Ouh Christopher, nakuomba
usikwazike na Edger hata
kidogo.Edger naye ni mgonjwa
kama wewe kwa hiyo naomba
usimjali.Unachotakiwa kufahamu ni
kwamba sisi sote ni waafrika na
kwa vile tumekutana huku ugenini
bila kujali tumetoka katika nchi
tofauti tayari tunakuwa ni ndugu”
Dr Olivia akajibu huku
akitabasamu.
“Nashukuru sana Dr Olivia kwa
kunielewa.Nafurahi kukutana
nawe.Ningefurahi sana kama ningepata wasaa mzuri wa kukaa
,kuongea nawe zaidi.”
“Usijali Christopher,nitatafuta
wasaa ,tutakaa na tutaongea na
kufahamiana zaidi.” Dr Olivia
akasema akampa mkono Dick
akamuga na kuondoka.

*********************
Baada ya Dr Olivia kuondoka
Edger akakaa kitandani akiwa na
mawazo mengi
“Huyu Christopher ametokea
kumvutia Olivia ghafla.Sina shaka
na hilo kwa sababu
nimemshuhudia mwenyewe mara
tu alipomuoan Christopher Olivia alibadilika kihisia.Yes ! Christopher
ni kijana anayevutia kwa kila ktu
lakini kwa nini atokee kwa wakati
huu? Anazidi kuniwekea wakati
mgumu zaidi wa kumpata
Olivia.Kwa sasa kuna vitu viwili
vinavyonichanganya akili,moja ni
jinsi gani nitakavyoweza kuweka
wazi azma yangu ya kugombea
urais wa Tanzania.Pili ni jinsi gani
nitaweza kuyaondoa mawazo ya
Olivia toka kwa Christopher.Hivi ni
vitu viwili ambavyo ni lazima
nishughulike navyo kwa sasa ili
kuweka mazingira mazuri ya kuwa
na Olivia.Lakini kati ya haya yote
kubwa ni hili la kugombea Urais wa
Tanzania.Ngoja nimpigie simu Stanley ili nifahamu amefika wapi
katika uchunguzi wake kabla
sijachukua hatua ya pili.”
Edger akachukua kompyuta
yake na kupiga simu Tanzania kwa
rafikiye Stanley.
“Hallow Stanley.Habari za toka
jana? Edger akauliza.
“Habari nzuri Edger
.Unaendeleaje leo?”
“Ninaendelea vizuri
sana,nashukuru Mungu” Edger
akajibu
“Nafurahi kusikia hivyo Edger
.”
“Nipe ripoti ya
uchunguzi.Umepata nini? Edger
akasema “Edger nimejaribu kufanya
uchunguzi wa kina japokuwa ni wa
haraka haraka lakini nimefanikiwa
kupata picha halisi ya hali ya
kisiasa ilivyo ndani ya
chama.Kwanza kabisa rais Evans
Mwaluba anawania muhula wa pili
wa uongozi kupitia chama
chake.Kama unavyoelewa Dr Evans
ni rais wa nchi na kwa maana hiyo
ana uungwaji mkono mkubwa sana
ndani na nje ya chama.Hiyo haina
shaka kuwa ni lazima chama
kitampitisha ili agombee kwa
awamu ya pili.Ukiacha Dr Evans
ambaye na anataka kugombea kwa
awamu nyingine ya pili,mwingine
ambaye ameonyesha nia ya kuwania nafasi ya kugombea urais
ndani ya chama ni mbunge mwenye
nguvu Mr Damiani
Mwamba.Nadhani unamfahamu
vyema.Mwamba kama lilivyo jina
lake amekuwa ni mmoja kati ya
wanachama wenye nguvu kubwa
ndani ya chama na kwa siku za hivi
karibuni nguvu yake imeonekana
kuongezeka hivyo kutishia vigogo
wenzake ambao nao wana dhamira
kama yake ya kuwania tiketi ya
kugombea urais kupitia chama
tawala.Hivi nikwambiavyo tayari
kampeni za chini kwa chini
zimekwisha anza ili kutafuta
uungwaji mkono katika zoezi la
kura za maoni na katika vikao vya juu vya uteuzi ndani ya chama.Kwa
hivi sasa kunaonekana kuwa na
makundi ndani ya chama.Lipo
kundi linalomshabikia rais wa sasa
na lingine linamshabikia Mr
Mwamba.Kwa hiyo kuna mchuano
mkali wa chini kwa chini kati ya
vigogo hawa wakubwa na
ukumbuke kuwa vigogo hawa wote
waliwahi kuwa maswahiba
wakubwa lakini kwa sasa
wamekuwa mahasimu
wakubwa.Kwa ufupi hiyo ndiyo hali
hali ilivyo ndani ya chama Edger”
Stanley akasema na kumfanya
Edger ashushe pumzi
“Nimekuelewa Stanley.Kwa
muda mrefu nilikwisha hisi Damian Mwamba lazima atagombea urais
nilitegemea mnyukano mkubwa
kati yake na Dr Evans.Wawili hawa
wamekigawa chama katika sehemu
mbili.Watu hawa wawili wote wana
nguvu na ushawishi ndani ya
chama.Sipati picha mtikisiko
utakaokuwepo ndani ya chama
katika uteuzi.” Edger akasema
“Kweli kabisa Edger kuna kila
dalili za mpasuko ndani ya
chama.Vigogo hawa wamekigawa
chama kati kati” akasema Stanley
“Nakubaliana nawe
Stanley.Kwa hiyo unanishauri kitu
gani ?
Satnley akakaa kimya kidogo halafu
akasema “Edger sipendi kukuficha
rafiki yangu lakini ni ukweli
usiopingika kuwa utapata wakati
mgumu sana katika dhamira yako
hii.Ninasema utapata wakati
mgumu kuteuliwa ndani ya chama
kwa sababu ya vigogo hawa wawili
kuwana nguvu kubwa zaidi lakini
wewe nguvu yako iko nje ya
chama.Katiba yetu bado
haijaruhusu mgombea binafsi
ningekushauri ugombee kama
mgombea binafsi kwani ndani ya
chama hutaambulia chochote na
ukumbuke pia kwamba unao
maadui ndani ya hicho hicho chama
ambao wamediriki hata kupanga
mikakati ya kukuua.Si kwamba nakukatisha tamaa Edger ,nimeona
niwe wazi kwako ili kwa pamoja
tutafute njia muafaka ya kufanya ili
lengo lako liweze kutima.” Stanley
akasema
“Nakuelewa vizuri sana
Stanley na ninafurahi kwa kunipa
ukweli halisi.Nilipofikiria suala la
urais nilijua ugumu uliopo.Lakini
pamoja na ugumu uliopo bado
siwezi kukata tamaa hata
kidogo.Nitapambana kwa kila jinsi
nitakavyoweza,hata kama
nikishindwa safari hii basi
nitajaribu tena wakati mwingine”
“Nafurahi kusikia hivyo
Edger.Lakini pamoja na hayo yote
bado nina ushauri” Stanley akasema
“Ushauri gani Stanley”
“Kwa kuwa ndani ya chama
hauna mizizi mikubwa na
uwezekano wa kuteuliwa ni mdogo
kwa nini usigombee kwa kupitia
chama cha upinzani?akauliza
Stanley
Kimya kifupi kikapita halafu
Edger akauliza
“Una maana nianzishe chama
cha siasa?
“Hapana Edger si kuanzisha
chama kipya cha siasa.Kuanzisha
chama kipya cha siasa kuna
mlolongo mrefu na kipindi hiki
kilichobaki ni kifupi sana kabla ya
kufika uchaguzi mkuu.Kwa kuhofia kushindwa katika uchaguzi vigogo
wanaweza wakafanya kila
wawezalo ili mradi chama
utakachokianzisha kisishiriki
katika uchaguzi
mkuu.Ninachoshauri ni kwamba ni
kwa nini usitafute chama chochote
cha siasa chenye usajili wa kudumu
na chenye wanachama hata kama si
wengi lakini chenye sera na
mwelekeo mzuri,ujiunge
nacho?Nina imani kwa kiasi
kikubwa kuwa hata kama chama
kina wanachama mia moja lakini
wakisikia kuwa umejiunga nacho
kwa lengo la kugombea urais basi
ni siku moja tu chama kitakuwa na
mamilioni ya wanachama.Edger usiache kuitumia nafasi hii ya
kukubalika kwako katika jamii
kuingia ikulu.Ni wakati wako sasa
wa kuhakikisha unaingia
ikulu”akashauri Stanley.Ilimchukua
Edger muda akitafakari na kusema
“Stanley nakuelewa
unachokisema lakini kukiacha
chama nilichokitumikia kwa miaka
zaidi ya ishirini !! ni kazi ngumu
kidogo” Edger akasema huku
akikuna kichwa.
“Nimekuwa mwanachama
mtiifu kwa miaka hii yote na hata
siku moja sijawahi kufikiri au kuota
kukihama chama changu.Pamoja na
misuko suko yote,mapungufu yote
ndani ya chama lakini bado nimeendelea kusimama imara na
kukitetea chama kwa nguvu zangu
zote.Leo hii nikisimama katika
jukwaa na kuwaambia wananchi
kuwa nimekihama chama kwa
sababu moja tu eti nataka niwe rais
wao ,wataniona kama msaliti
mkubwa na mtu nisiye na
msimamo na mwenye uchu wa
madaraka.”akasema Edger na
Stanley akatoa kicheko
“Edger usiwe mwoga namna
hiyo.Wananchi wa Tanzania ni
waelewa sana na wanahitaji mtu
kama wewe uwaongoze na
kuwavusha katika kipindi hiki
kigumu.Wanaelewa fika kuwa kwa
mtu kama wewe katika mazingira ya kawaida ni vigumu kupewa
nafasi ndani ya chama kugombea
urais.Hivyo watakaposikia kuwa
una lengo la dhati la kuwatumikia
hata kama utajiunga na chama cha
upinzani idadi kubwa ya
Watanzania watakupigia kura”
Stanley akaendelea kumshawishi
Edger .
“Edger nakubali kwamba kwa
sasa mimi ni maarufu sana na ninao
mtaji mkubwa wa wafuasi lakini
wazo lako la kuhama chama
linanipa ukakasi kwani wengi
wananiamini kwa kuwa niko katika
chama hiki nitakapohama nitajenga
picha ambayo si nzuri mbele ya
jamii na nitaonekana ni mtu mwenye uchu wa
madaraka.Nafikiria kwa nini
nisiendelee kujenga mizizi kwanza
ndani ya chama na kutafuta
uungwaji mkono badala ya
kukihama chama? Wasi wasi wangu
ni kwamba ninaweza kuhama
chama lakini nisifikie malengo
yangu.Ipo mifano mingi tu ya
wanasiasa ambao walikuwa na
nguvu kubwa ndani ya chama lakini
mara tu walipotoka ndani ya chama
wakafifia na kufa kabisa
kisiasa.Sitaki hilo linikute
Stanley”akasema Edger
“Edger usiwe na hofu ndugu
yangu.Kilichowatokea hao
wanasiasa hakiwezi kukutokea wewe hivyo ondoa hofu kaka huu
ni wakati wako umefika na kuna
kila dalili kwamba umeushika
ufunguo wa lile jumba jeupe”
akasema Stanley
“Stanley nakufahamu hukubali
kushindwa.Kama nikifanya
maamuzi hayo ya kuhama chama
na kujiunga na upinzani itanilazimu
kuwaeleza wafuasi wangu na
umma wa watanzania juu ya
kilichonitokea na kwa nini nimefika
uamuzi huu mgumu wa kukihama
chama na kujiunga na chama cha
upinzani.Nadhani wakisikia hivyo
ninaweza nikaeleweka ndani na nje
ya chama”akasema Edger
“Kwa upande Fulani ninakubaliana na wewe kuhusu
jambo hilo” akasema Stanley
“Sawa Stanley,hata hivyo
itatubidi tupate muda mzuri zaidi
wa wa kulijadili suala
hili.Ninachoomba ufanye kwa sasa
hebu jaribu kuvipitia vyama vyote
vya siasa vyenye usajili wa kudumu
ambavyo unaona vinaweza kufaa
kwa mimi kuhamia huko halafu
utanipa taarifa.”akasema Edger
“Sawa Edger nitafanya
hivyo.Nitafanya utafiti wangu na
nitakujulisha.Hujanipa taarifa
kuhusu Dr Olivia,anaendeleje?
Stanley akauliza swali la kichokozi
“Stanley najua umeuliza
makusudi kabisa lakini narudia tena kukiri kwamba nimetokea
kumpenda sana Dr Olivia na
ningefurahi kama ningefanikiwa
kuwa naye katika maisha yangu
kwa sababu ni mmoja kati ya
wanawake adimu kupatikana
katika dunia hii ya sasa.Lakini kwa
sasa kumeibuka changamoto
ambayo natakiwa kukabiliana
nayo.Kuna kila dalili Olivia
amevutiwa sana na kijana moja
ambaye tumekutana naye leo hapa
hospitalini anaitwa
Christopher.Kijana huyu ni
mgonjwa na amekuja hapa
kutibiwa maradhi ya moyo
anatokea Zimbabwe.Alipotuona
tumekaa bustanini akaja kutusalimu,tukaongea machache na
Olivia alishindwa kuzificha hisia
zake kwa jinsi alivyokuwa
amevutiwa na kijana yule.Hii nayo
ni changamoto mpya ambayo
ninatazama jinsi ya kukabiliana
nayo. Stanley masuala haya
yananiumiza kichwa ,niache
nipumzike tutaongea vizuri
baadae”akasema Edger
“Sawa Edger lakini jitahidi
mambo haya yasikuumize kichwa
kabisa.Bado mimi ushauri wangu ni
ule ule stay far away from
her”akasema Stanley
“Stanley ,sidhani kama hilo
litawezekana kwa jinsi
alivyoniingia moyoni.Tutaongea baadae vizuri Nahitaji kupumzika
kwa sasa”akasema Edger na kukata
simu
“Haya mambo ya kisiasa
yananiumiza sana kichwa
changu.Stanley anaweza kuwa
sahihi kwamba siwezi kupata nafasi
ndani ya chama changu hivyo
itanilazimu nihamie katika chama
cha upinzani kama nikitaka
kuwania urais.Huu ni mtihani
mkubwa kwangu.Sikuwahi
kufikiria kuhama chama
changu,pamoja na misuko suko
yote niliyoipata lakini nimeendelea
kuwa mtiifu kwa chama lakini
kitendo changu cha kuhama chama
kitanigharimu sana na kama nisipokuwa makini kinaweza
kuniondoa kabisa katika ulingo wa
siasa.Natakiwa umakini mkubwa
sana katika hili suala vinginevyo
nitapotea kabisa katika ulingo wa
siasa” akaendelea kuwaza Edger.
 

Similar Discussions

Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…