RIWAYA : SALA YA SARAH
MTUNZI : ALEX KILEO
SEHEMU YA HAMSINI NA SABA.
ENDELEA..................
"kakae pale kwenye kochi uungane na wenzako" Sauti ile iliongea kwa mamlaka na kumfanya Sarah akakae na hapo akaweza kuiona vizuri sura ya yule mtu aliyemteka, alikuwa ni Strategic,
"kumbe Sarah mwenyewe ndio wewe, mbona hufanani na unyama unaoufanya?" Strategic aliuliza lakini Sarah hakujibu, strategic akatoa simu na kubonyeza namba anayoijua yeye, kisha akaiweka simu sikioni na kuisikiliza wakati ikiita,
"hoya Vin, nimefanikiwa kumteka Sarah, vipi nimmalize?" Strategic aliuliza,
"ooh, hapana, muache" Vin alitoa kauli iliyomshangaza Strategic,
"kwanini nimuache mkuu?" Strategic aliuliza kwa mshangao?
"nitakuja kukueleza, wewe muache tu, na usimdhuru" Vin aliongea,
"sawa mkuu" Strategic alijibu na kukata simu, kisha akamtupia jicho Sarah na kumuangalia kwa dakika kadhaa,
"bahati yako, tutakutana siku nyingine" Strategic aliongea na kisha akaelekea kwenye mlango na kuufungua kisha akaondoka.
Baada ya Strategic kuondoka, Sarah alivuta bastola yake na kutoka mbio mpaka nje, hakukuta mtu,
"mpuuzi huyu" Sarah aliongea kwa hasira huku akirudi ndani. Alipofika ndani aliwafungua kamba Dokta Pendo na babu yake,
"muda gani aliingia hapa?" Sarah aliuliza wakati akimaliza kumfungua kamba Dokta Pendo,
"kama nusu saa hivi iliyopita" Babu yake alijibu,
"amepajuaje hapa?" Sarah aliuliza lakini hakuna aliyejibu kwa maana hakuna aliyejua.
"hii ni hatari Sarah, yaani wamepajua mpaka hapa?" Babu yake Sarah aliuliza huku akisikitika,
"itabidi tuhame na hapa, tuhamie hotelini sasa" Sarah aliongea huku akikaa kwenye kochi,
"hakuna sababu ya kuhama, sasa tutahama hama mpaka lini?" Dokta Pendo aliuliza,
"tunahitaji kuwa sehemu salama, kwa kuwa hawa manyang'au wameshajua tunapoishi, wanaweza kuja kutushambulia" Sarah aliongea,
"kama angekua na lengo la kutuua angetumaliza mapema tu, ila mbona amekuachia?" Dokta Pendo aliuliza,
"Vin itakuwa ameanza kuelewa kitu kati yangu na yeye, ila isiwe sababu ya kujiamini kiasi cha kuwa huru muda wote, itabidi tukiwa ndani mlango yote ya geti ifungwe" Sarah aliongea kwa utulivu,
"mama nadhani ungeachana nao tu, watakumaliza hawa" Babu yake Sarah aliongea,
"hilo haliwezekani, hata nikiachana nao bado wao hawatoachana na mimi, watataka tu kuniua au kuwaua watu wote mlio upande wangu" Sarah alijibu,
"shoga pambana, maji umeshayavulia nguo" Dokta Pendo aliongea kwa ya upole,
"usimshauri mwenzako ujinga, je akifa utajisikiaje?" Babu yake Sarah aliuliza kwa ukali,
"je wakati wewe unamchongea kwa polisi ulikuwa unajisikiaje?" Dokta Pendo aliuliza huku akinyanyuka na kuanza kutembea kwa mwendo wa taratibu kuelekea chumbani na kumuacha Sarah akitabasamu,
"usimsikilize maneno yake huyo mwenzako, hana nia nzuri na wewe" Babu yake Sarah alimwambia Sarah,
"Mimi namsikiliza shoga yangu, nampenda kwa maana amenisaidia mambo mengi" Sarah aliongea kwa utani huku akielekea chumbani akicheka,
"mabaradhuli nyie, ukifa shauri yako" Babu aliongea kwa hasira huku akimtazama Sarah anavyoondoka.
**********************
Sajenti Minja alihisi kuchanganyikiwa, na kilichomchanganya Sajenti Minja ni kupotea kwa ghafla kwa Sarah huku akiwa na Dokta Pendo. Sajenti Minja akili yake ikamtuma aende uwanja wa ndege kwenda kukagua watu waliokwenda nje ya nchi ndani ya wiki hii, aliamini huenda Sarah ametoroka nchini baada ya kufanya mauaji ya familia ya Harry.
Sajenti Minja alichukua gari na kwenda moja kwa moja mpaka uwanja wa ndege, alipofika haikuwa rahisi kukubaliwa kufanya kazi yake, ilimbidi ampigie simu waziri wa wizara husika na kumueleza lengo lake, kisha waziri akapiga simu uwanja wa ndege na kuwaamuru wamuache Sajenti Minja afanye kazi yake.
"nenda kwenye chumba namba saba, uko ndipo kuna orodha yote" Mfanyakazi Mmoja alimuelekeza Sajenti Minja huku akimpatia kibali ambacho kilimtambulisha Sajenti Minja kama mtu maalum na aachwe afanye kazi yake.
Sajenti Minja alielekea moja kwa moja mpaka chumba kilichokuwa na mlango uliochorwa namba saba na kisha akabonyeza kengele iliyokuwepo hapo mlangoni, na mlango ukafunguliwa na msichana, Sajenti Minja akamsalimu na kisha akamuonesha kile kibali, akaruhusiwa kuingia ndani na kukuta watu kama watano wakiwa bize na computer, kila mtu alikuwa na computer yake.
Sajenti Minja akawasalimia, kuna waliotikia na wengine walikuwa bize kubonyeza computer zao.
"samahani jamani, mimi ni askari, nimekuja kuangalia orodha ya watu waliotoka nje ya nchi ndani ya wiki hii" Sajenti Minja aliongea kwa sauti tulivu na kufanya watu wote wamuangalie,
"ni wengi sana bro, au labda ueleze shida yako ni ipi hasa?" Kijana mmoja mtanashati alimuuliza Sajenti Minja,
"kuna mtu anatafutwa na serikali, sasa nataka kujua kama yupo ndani ya nchi au ametoroka?" Sajenti Minja aliuliza,
"una kibali cha kuruhusiwa kufanya ukaguzi ndani ya ofisi hii?" Yule kijana akamtupia swali jingine Sajenti Minja,
"anacho, waoneshe" Dada aliyemfungulia mlango Sajenti Minja alijibu huku akimtazama Sajenti Minja na kufanya Sajenti Minja awaoneshe kile kibali alichopewa,
"tupe jina lake tafadhali" Yule kijana aliongea,
"Sarah Isack" Sajenti Minja aliongea huku akiandika jina la Sarah kwenye karatasi na kisha yule kijana akaliingiza lile jina kwenye computer yake na kubonyeza sehemu iliyoandikwa "search", baada ya muda jina la Sarah likatokea kwenye computer ya yule kijana,
"bro, huyo mtu jina lake limeaonekana kwa mara ya mwisho mwaka mmoja uliopita, tena imeonesha alikuwa akiingia kama mtalii kutoka nchini uingereza" Yule kijana alimpa maelezo Sajenti Minja,
"hakuna sehemu iliyoonesha akitoka?" Sajenti Minja aliuliza,
"ipo, ila imeonesha alitokaga miaka ishirini iliyopita na amerudi mwaka uliopita" Kijana alijibu,
"na sehemu ya kutoka imeonesha ametoka kwenda wapi, na ametoka kwenda wapi na kufanya nini?" Sajenti Minja aliuliza,
"imeonesha alitoka kwenda uingereza, na alienda kwa ajili ya masomo" Kijana alijibu,
"dah, hii report yenu hapa ni ya abiria wa uwanja huu tu au ni report ya viwanja vyote?" Sajenti Minja aliuliza,
.
.
"ni ya viwanja vyote vya Tanzania" Yule kijana alijibu,
"sawa, asante kwa ushirikiano wako" Sajenti Minja aliongea huku akianza kuondoka,
"au bro kwa kukushauri, ni bora ukaangalie na vituo vya mabasi, huenda ametumia njia ya mabasi kusafiri mpaka Kenya, alafu akifika Kenya ndio achukue ndege" Kijana aliongea huku akimtazama Sajenti Minja,
"nashukuru, ngoja nikafanye hivyo" Sajenti Minja alijibu, ila kiukweli aliona hiyo njia ni ngumu sana kuitumia kwa kuwa stand ya mabasi haina utaratibu maalum wa kukata tickets na kuifadhi kumbukumbu.
Sajenti Minja alirudi mpaka sehemu alipochukulia kibali, akakirudisha na kisha akashukuru. Akatoka zake mpaka nje ya eneo la uwanja wa ndege na kisha akaingia kwenye gari lake.
Wakati akiwa anajiandaa kuwasha gari yake, simu yake iliita na kupokea,
"Minja anaongea" Sajenti Minja aliongea,
"tumeokota mwili ukiwa na majeraha ya risasi" Mtu wa upande wa pili aliongea,
"mmemtambua?" Sajenti Minja aliuliza,
"tumemtambua kupitia kitambulisho chake" Mtu wa upande wa pili alijibu,
"sawa, mpelekeni hospitali na mruhusu uchunguzi ufanyike, mimi nakuja" Sajenti Minja aliongea na kukata simu, kisha akaondoa gari.
***************
Trigger alifika hospitali na kumkuta Taita akiwa amekaa kitandani,
"Vin yupo wapi?" Taita aliuliza,
"anadai hajisikii vizuri, amerudi hotelini kupumzika" Trigger alijibu,
"na mmefanikisha kumuona Harry?" Taita aliuliza,
"tutaongea baadae, je kuna habari mpya?" Trigger aliuliza,
"mpya sina, ila cha muhimu ni kwamba nimeruhusiwa" Taita aliongea,
"kwa hiyo tunaondoka?" Trigger aliuliza,
"ndio, ebu nisaidie kusimama" Taita aliongea huku akisimama na Trigger aksmsaidia kwa kumshika mkono na kisha wakaelekea mpaka nje, wakaingia kwenye gari na kisha Trigger akawasha gari na kuondoka.
Walifika nyumbani kwa Taita na kisha Taita akafikia kukaa kwenye kochi,
"mzee, Harry ameuawa" Trigger aliongea baada ya Taita kukaa,
"ameuawa au mmemuua?" Taita aliuliza,
"Sarah ndio amemuua" Trigger alijibu,
"umejuaje kama Sarah amemuua?" Taita aliuliza,
"wakati Sarah akimuua Harry, Vin alikuwepo na yeye ndiye aliyemuona" Trigger alijibu,
"sasa kwanini Vin hakumuua Sarah?" Taita aliuliza,
"kuna kitu cha ajabu sana kimetokea, Sarah anamuaminisha Vin kuwa yeye ni dada yake, na leo ametoa damu na kumpa Vin akaipime ili ahakikisha" Trigger aliongea na kumfanya Taita ashtuke,
"na vin ameamini?" Taita aliuliza,
"itakuwa, maana alipitia hospitali na kwenda kuacha damu ya Sarah" Trigger aliongea,
"hii hatari, itabidi uende hiyo hospitali ukasimamishe huo mpango" Taita aliongea,
"kwa njia gani?" Trigger aliuliza,
"kaongee na Dokta akupe hayo majibu" Taita aliongea,
"na akikataa?" Trigger aliuliza,
"ua" Taita alijibu,
"sawa mkuu, hiyo kazi itafanyika kesho" Trigger alijibu.
***************
Siku iliyofuata Vin alipata wazo jipya, aliona ni bora amtume Strategic aende maeneo ya hospitali kuimalisha ulinzi mpaka mida ya saa kumi ambao ni muda Vin alitakiwa kufika kuchukua majibu.
Vin alifanya hivyo kwa maana alihisi huenda Sarah anaweza kufika eneo la hospital na kumteka Dokta na kumshurutisha aandike majibu ya uongo ya DNA, bado Vin hakuwa na imani na Sarah.
Strategic alifika eneo la hospital kuimarisha ulinzi, hakuwa akimjua Dokta muhusika, ila alichoenda kufanya ni kumuwinda Sarah endapo atakuja eneo hilo.
Muda ulizidi kwenda tu, ilipofika saa kumi, strategic alimshuhudia Trigger akifika eneo lile, strategic akataka kushuka ila akaamua auchune tu ndani ya gari, akatoa simu na kumpigia Vin,
"nimemuona Trigger eneo hili" Strategic aliongea,
"amekuja kufanya nini?" Vin aliuliza,
"sijui kwa kweli" Strategic alijibu,
"amekuona?" Vin aliuliza,
"hapana" Strategic alijibu,
"endelea kukaa hapo na ufuatilie amefuata nini?" Vin aliongea baada ya kuhisi huenda Trigger ameenda kwa ajili ya kuchunguza ni kipi Vin alikifuata siku iliyopita,
"sawa mkuu" Strategic alijibu.
Huko ndani Trigger alipitiliza mpaka ndani kwa Dokta na kumkuta akiwa anajiandaa kuondoka, akamsalimu,
"Dokta nimetumwa nifuate majibu ya damu" Trigger aliongea,
"na nani?" Dokta aliuliza,
"mdogo wangu alikuja jana hapa na bomba la sindano lililokuwa na damu" Trigger aliongea na kumfanya Dokta amkumbuke Vin,
"sasa kijana, hapa haturuhusiwi kumpa mtu majibu ya mwingine, ni vyema angekuja mwenyewe" Dokta aliongea huku akipekua pekua karatasi juu ya meza yake,
"kwa hiyo haiwezekani?" Trigger aliuliza,
"hiyo haiwezekani" Dokta alijibu na kisha Trigger akaondoka kwa hasira.
Baada ya Trigger kuondoka, Dokta alipekua zile karatasi mezani na kuchukua karatasi moja ambayo ilikuwa na majibu ya DNA ya Vin, akaitia kwenye bahasha ya njano.
Trigger alitoka na kusimama mlangoni, akili yake ikamtuma arudi ndani ya ofisi ya daktari. Trigger akageuka na kusukuma mlango, akaingia,
"nipe majibu niliyotumwa, vinginevyo amani itapotea" Trigger aliongea huku akiichomoa bastola yake na kumuelekezea Dokta, Dokta akapata mshtuko na kujikuta akiichomoa bahasha moja ya njano na kumpatia Trigger, Trigger akafungua na kusoma maelezo ya juu katika karatasi, alikuta kumeandikwa " DNA TEST" na chini ya hayo maneno kulikuwa na jina la Vin na Sarah.
Trigger akaitudishia ile karatasi ndani ya bahasha na kisha akamtupia jicho Dokta,
"Trigger akikuoneshea bastola uwa haishushi chini mpaka itoe risasi" Trigger aliongea huku akitabasamu na kumfanya Dokta macho yamtoke,
"unamaanisha nini?" Dokta aliuliza kwa hofu, ila Trigger hakujibu, badala yake alimfyatulia Dokta risasi mbili na kisha Dokta akaanguka chini. Trigger akafungua mlango na kutoka zake kimya kimya na bahasha mkononi utasema hajatoka kufanya tukio la kinyama........
**********ITAENDELEA************
the Legend☆