SEHEMU YA THELATHINI NA MOJA
Isaya akapata nafasi ya kuzungumza na yule mpelelezi na kumueleza juu tukio la marehemu Beka kumteka nyara pia mchumba wake na kisha kumbaka. Isaya aliamini kuwa ni Betty pekee awezaye kumwokoa mzee Akunaay na kuuthibitishia umma kuwa mzee huyu hana hatia.
Inspekta Mushi alivutiwa sana na maelezo ya Isaya, maana alikuwa akihitaji sana mtu yeyote ambaye yupo hai aweze kuelezea tukio lolote lililotokea ndani ya nyumba ya mzee Akunaay. Hili lilikuwa tatizo kubwa sana. Kesi isingeweza kwenda hivihivi bila kupatikana mtu mmoja wa kuzungumzia hali ya ndani ya nyumba na nje kabla ya mauaji ya kutisha.
Maana askari aliyetegemewa kuelezea chochote alikuwa amepararaizi na hakuweza kuzungumza hadi siku hiyo, kuna madhara makubwa yalikuwa yamejitokeza katika uti wake wa mgongo na kuithiri akili yake.
Huyu alikuwa ni Inspekta Ndayanse.
Vijana watatu waliotegemewa waliuwawa mapema eneo la tukio. Msichana aliyekutwa hoi na kupigwa risasi na maaskari baada ya juhudi za kumsalimisha Assistant super retendant Seba ambaye alikuwa ameng'atwa meno na binti yule kushindikana, sasa alikuwa amefariki.
Beka naye alikuwa amefariki!!
Assistant super retendant, fahamu zikiwa hazijamrudia.
Sasa linaibuka jina la Betty!!
Ni hapa ndipo ilipofufuka ile kesi ya binti kutekwa, jitihada za polisi zikagongwa mwamba kumpata. Sasa amepatikana na inasemekana alikuwa ametekwa na marehemu Beka!!
Betty akahitajika kwa namna yoyote kituo cha polisi. Aweze kuthibitisha kutekwa na kisha kubakwa, na huenda atakuwa na maneno ya kuongezea juu ya kutekwa kwake. Na maneno hayo yangeweza kuwa mwanga mkali wa kesi hiyo ya aina yake iliyohusisha watu wengi na wenye vyeo vyao serikalini.
MOROGORO MJINI
WAKATI ULIOPO
ILIKUWA ni kawaida ya Fonga kutoka nje kwa ajili ya kununua chakula na mahitaji mengine wakati Joyce alikuwa mtu wa kukaa ndani tu katika nyumba ya kulala wageni ambayo walikuwa wamepanga kwa malipo ya juma moja.
Hata siku hii ya aina yake ambayo Fonga alikuwa ameagizwa vitumbua na maandazi ilifanana na siku nyingine zote zilizopita.
Joyce ambaye alikuwa ameridhia hatimaye Fonga kuwa mpenzi wake bila kipingamizi japo waliahidiana kuwa watakapopata uhuru waende kupima afya zao, alikuwa amejibweteka kitandani huku kanga mpya aliyonunuliwa na Fonga ikiwa haijamstiri vizuri mwili wake. Fonga aliifikisha alichoagizwa huku akimtengea Joyce vitumbua na soda ya kopo ambayo ilikuwa chaguo la Joyce.
Joyce hakuwa na haraka ya kula, aliendelea kujivinjari kitandani kwa dakika kadhaa kisha akainuka na kuisafisha mikono yake kabla hajaanza kusosoa alicholetewa.
Alipokua akinyanyua kitumbua cha pili kutoka katika gazeti ambalo lilitumika kufunga vitumbua vile alivutiwa na alichokiona. Aliona jina linalofanana na la rafiki yake kipenzi, Betty. Kwanza hakutilia maanani kuisoma habari ile ndefu inayoambatana na jina la Betty. Lakini mara umakini ukaongezeka baada ya kuona jina jingine, Isaya mara akaona Beka na kisha Akunaay.
Hapa kitumbua hakikulika, akamwita Fonga na kumwonyesha juu ya ile habari. Fonga naye akavutika kuisoma.
Ilimuhusu Betty ambaye alingojewa kwa hamu kumwezesha mzee Akunaay kubaki huru kwa ushahidi wake thabiti kuwa alibakwa na mzee Beka ambaye ni marehemu tayari.
Baada ya kuisoma wote wawili wakabaki kimya!!
Joyce akiwa kimya akistaajabu kuwa kumbe Betty yu hai! Lakini akizizima baada ya kusikia kuwa rafiki yake huyo alibakwa na Beka, kama Beka alimbaka bila shaka hakutumia kinga, na Betty ni muathirika hivyo aliondoka na virusi kiuhakika. Na baada ya hapo akamwingilia Joyce kimwili, japo alitumia kinga. Joyce aliingiwa na baridi kali!!! Baridi ya uoga.
Uoga wa kujitambua kuwa yu marehemu mtarajiwa.
Fonga yeye alikuwa kimya akisubiri kauli ya Joyce ambaye ndiye alikuwa na uchungu wa dhati juu ya rafiki yake huyu.
DAR ES SALAAM
SIKU MBILI NYUMA
JOYCE na Fonga walikuwa katika nyumba ya kulala wageni yenye hadhi ya chini kabisa mathalani ‘mbavu za mbwa!'. Fonga akiwa na uzoefu wa simulizi kadha wa kadha alizopata akiwa gerezani kutoka kwa wafungwa wa kesi za ujambazi na unyang'anyi alijifunza namna ya kukwepa mkono wa dola ama adui kwa kujihifadhi mahali ambapo hatarajii unaweza kujihifadhi.
Joyce akawa mtiifu akafuata kila alichoelekeza Fonga. Ni katika nyumba hii ya kulala wageni yenye hadhi duni, Joyce na Fonga walifungua begi ambalo kila dakika lilikuwa mgongoni mwa Joyce baada ya kulitwaa katika nyumba ya Akunaay ambayo ilisemekana Betty alikuwa ametekwa.
Pesa hizo alizitoa Beka kwa hiari yake baada ya mambo kumuwia magumu. Hizo zilikuwa pesa kwa ajili ya malipo ya vijana wake baada ya kumaliza zoezi zima la kufanikisha kumteka Betty na hatimaye Joyce kuingia mikononi mwake kama mpenzi wake. Fonga ambaye alikuwa amerejea katika hali yake ya kawaida alizihesabu pesa zile na kufikia makadirio ya shilingi milioni kumi na nane
Pesa nyingi sana kwa wakati huo. Fonga akatabasamu na kujaribu kumshirikisha Joyce juu ya pesa zile lakini uso aliokutana nao haukuonyesha kujali kuhusu pesa hata kidogo.
Joyce aliamini kwa kuzifurahia pesa zile ni kufurahia moja kwa moja aidha kifo ama kupotea kwa rafiki yake kipenzi, Betty. Joyce hakutaka kuonyesha unafiki wowote mbele ya Fonga bdala yake alimwambia moja kwa moja kuwa hana furaha bila Joyce.
Tabasamu la Fonga likayeyuka na kisha akajawa na mashaka na fadhaa. Akamtazama Joyce usoni, hapa akapata neno la kusema.
"Joyce mpenzi wangu, umekuwa shuhuda tangu mwanzo tumejaribu tukiwa bega kwa bega kumtafuta Betty, usidhani ninafurahia kumkosa lakini tazama hali ilivyokuwa Joy, kama asingekuwa Husna huenda tungekuwa tumekufa na asingepatikana wa kutambua nini kimemsibu Betty. Sikia Joy hapa kitu cha msingi ni kuangalia namna nyingine ya kumtafuta Betty lakini kwa wakati huu hatutakiwi katika mji huu Betty. Nawajua polisi vizuri, nadhani nilikusimulia mkasa ulionikumba hadi nikafungwa jela. Sasa tujiweke mbali huku tukiangalia hatua kwa hatua ya tukio hili kabla hatujaamua tena kuingia kumtafuta Betty. Kitu kimoja ambacho unatakiwa kujua ni kwamba kwa sasa hivi tukijitokeza hadharani ujue kabisa tuna kesi ya kujibu. Kesi ya kumteka nyara mheshimiwa mbunge na mauaji yote yaliyotokea mbele ya macho yetu nasi tutahusishwa. Sasa jiulize hivi tukiwekwa rumandfe tutakuwa na uwezo gani tena wa kumtafuta Betty?" Fonga alimaliza kutoa maelezo hayo, akanyanyua uso na kumtazama Joy, sasa alikuwa amebadilika na maneno yale yalikuwa yamemuingia haswa.
Wakabadili mada!! Mwisho wakafikia makubaliano.
Asubuhi iliyofuata wakadamka alfajiri na kukwea mabasi yaendayo Morogoro. Joyce na Fonga wakawa wakimbizi katika nchi yao wenyewe.
WAKATI ULIOPO
Wakiwa na siku mbili mjini Morogoro maeneo ya Kihonda ambapo walikuwa wamejihifadhi kwa mara nyingine katika nyumba ya kulala wageni ndipo linatokea tukio la Joyce kukutana na habari kuhusiana na Betty.
Sasa yu kimya na Fonga anangoja kauli yake!!
Joyce anatumia dakika kadhaa kufikiria, hapa unamrudia mlolongo wa matukio yote. Hasahasa tukio la kujitoa muhanga kwa ajili ya rafiki yake kipenzi na kumfichia siri nzito juu ya gonjwa lake hatari. Kisha akakumbuka pia alikuwa na mtihani wa kumzuia Betty asije kumwambukiza Isaya Ukimwi, na hapohapo alikuwa na jambo zito kabisa mkononi mwake, elimu. Alihitaji kuitetea elimu yake ipasavyo.
Sasa alikuwa anakaribia kupoteza kila kitu alichokuwa anajaribu kukitetea.
1. Penzi la Isaya; hili alijipa asilimia miamoja kuwa hana uwezekano wowote wa kulipata, na hakuwa na haja na penzi la mwanaume ambaye baba yake anajishirikisha na vitendo viovu. Joyce alikumbuka yule bwana aliyewateka na kumfyatua risasi Mark alidai kuwa aliagizwa na mzee Akunaay kufanya yale yote ambayo alikuwa anayafanya. Joyce akakiri kuwa Isaya hakuwa riziki yake.
2. Masomo; licha ya kwamba alikuwa anayo ruhusa kutoka chuoni na angeweza kurejea na kupokelewa, lakini angeweza vipi kusoma bila kuwa na amani moyoni, angeweza vipi kusoma wakati Fonga amemwambia kuwa na wao watakuwa na kesi kubwa ya kujibu iwapo tu watatiwa mikononi mwa polisi. Hili nalo likazua utata.
3. Kudumisha urafiki wake na Betty, hili nalo akaliona likielekea ukingoni. Maana ilionekana dhahiri kuwa Betty yupo tayari kusimama upande wa kumkomboa baba mkwe wake yaani mzee Akunaay ambaye gazeti lile lilitaja kuwa kauli ya Betty pekee nd'o ambayo itamuweka huru moja kwa moja huku kesi ikibaki kwa marehemu mzee Beka. Joyce yeye alikuwa kinyume na Betty japo hawakuwa wameonana na kuzungumza, lakini Joyce hakuwa upande wa Akunaay, masikio yake hayakumdanganya hata kidogo. Hata Fonga alikuwa shahidi wa kulitambua jina la Akunaay japo hakuwa ametambua kama ndiye baba yake Isaya. Joyce akauona kwa mara ya kwanza upinzani wa waziwazi dhidi ya rafiki yake iwapo tu ataendelea na utetezi wake kwa mzee Akunaay.
Hapa ndipo Joyce akakiri kuwa wahenga hawakuwa wanafiki waliposema mshika mbili moja humponyoka lakini huenda hii ingeweza kuwa heri kwake. Yeye alitakiwa kusimamia katika msemo wa ‘mtaka yote kwa pupa hukosa yote'.
Naam! Joyce alikuwa anaelekea kukosa kila kitu alichojipangia yeye.
Hapa pia akakiri kuwa ‘mipango si matumizi'. Alichopanga yeye kimeshindikana kutimia.
Anafanya nini sasa? Alijiuliza na aliamini kuwa hata Fonga ambaye alikuwa kimya alikuwa akingojea kauli yake!!!
Ghafla Joyce akazungumza.
"Fonga, nadhani nirejee Dar es salaam. Ujue huyo Akunaay akiwa huru na kisha agundue kuwa tunatambua siri yake atatusumbua sana, nadhani unajua kuwa ni waziri hivyo atatufanya lolote atakalo. Fonga sitaki huu uwe mwisho wa elimu yangu sitaki kabisa maisha yangu ya uyatima yaishie hapa. Lazima nifanye kitu hapa." Alizungumza kwa hisia kali Joyce.
Fonga akamtazama Joyce kisha akamjibu, "Usemalo Joyce ilimradi unaona lipo sahihi, nalibariki. Lakini nakusihi kuwa makini sana na kauli zako huko uendapo. Usijiumeume, kama ni kusema sema kweli. Neno moja nakusihi, kabla hujaenda huko lazima uundwe uongo mtakatifu! Uongo mtakatifu.." alisita Fonga kisha akamtazama usoni Joyce, kisha akaendelea "neno kuwa ‘tulimteka Beka' liondoke kichwani mwako, neno ‘tulienda na Beka Chamanzi' liondoke kabisa maana litakufunga…"
"Sasa naenda kusemaje kule jamani!!"
"Tupa shutuma zote kwa marehemu, kiri jambo moja mbele ya hadhara kuwa marehemu aliwahi kuwa mpenzi wako, lakini mlitengana. Baada ya rafiki yako kutoweka ukaamua kumwona kwa msaada wowote iwapo itabidi. Ni hapo ndiupo ulipotambua kuwa kuna jambo anajua kuhusu tukio hilo. Baada ya kukubali kurudisha mahusiano akahitaji kufanya mapenzi na wewe na hapo ndipo mlipotekwa na watu msiowajua. Sasa hapo unaweza kuendelea na simulizi ya Chamanzi, wakati wa kuzungumza jifanye hujui lolote kuhusu mimi. Wala humtambui Mark, lakini kikubwa mtambue yule mwanaume aliyedai ametumwa na Akunaay kumuua mzee Beka na kisha kuwaua ninyi wote. Ulifikia hapo elezea ukombozi kutoka kwa Husna ambaye haufahamu anahusika vipi katika huu utata. Hapo utakuwa umeunda uongo mtakatifu kabisa na utakuweka mahali salama. Cha msingi kumbuka kucheza na maneno, usiwe muoga na usiwe muongeaji sana." Fonga alimaliza kutoa nasaha zake. Akamkatia Joyce fungu kubwa kwa ajili ya safari hiyo.
Siku iliyofuata akaondoka kurejea jijini Dar es salaam kukutana na mtihani mkubwa katika maisha yake!!
Mtihani wa kupingana na Betty kwa mara ya kwanza katika maisha yake!!
****
WAKATI Joyce akimezeshwa uongo mtakatifu na kamanda Fonga. Jijini Dar es salaam, Isaya alimpa Betty kila alichokuwa anataka ilimradi tu amtetee mzee wake na aweze kuachiwa huru.
Akaunti ya Betty ilikuwa ina shilingi milioni kumi kwa ajili tu ya neno lake moja kuthibitisha kuwa alitekwa na Beka na kisha kubakwa na katika kubakwa Beka alimtaja Akunaay kuwa atamuua baada yake. Kauli zake hizi zingemweka pabaya marehemu Beka na kujikuta lawama na aibu vikimfuata kaburini.
Maswali makuu japo hayakuwa yamepata utatuzi, Inspekta Ndayanse ambaye amepararaizi alifuata nini Chamanzi, Assistant Super retendant naye alifuata nini kule. Mkewe alisema kuwa alipigiwa simu na Ben, Ben sasa ni marehemu. Huu ukawa utata, akaongezea kuwa kabla ya hapo alipigiwa simu na mke wa Ndayanse. Mke wa Ndayanse alipoulizwa akadai ni wivu ulimtuma kuhisi Ndayanse anaenda kwa mwanamke mwingine. Huyu hakuwa na msaada mkubwa!!
Nani wa kuunganisha matukio haya sasa. Lipatikane jibu sahihi.
Akunaay alichokuwa anajaribu kukikwepa ni kuingia katika mlolongo huu wenye utata. Sasa alitakiwa Betty athibityishe kuwa wakati Beka anambaka alimweleza mipango yake kuhusu kumuua Akunaay na kisha ile nafasi ya uwaziri apewe yeye baada ya kifo cha waziri huyo.
Sasa Betty amepokea pesa na anatakiwa kusema uongo mwingine mtakatifu pia!!!
Joyce amemezeshwa uongo wa kujilinda na Betty naye amemezeshwa uongo wa kumlinda Akunaay.
**JOYCE VS BETTY……ni hili tunaweza wote kulisema wakati huu….
**Kipi kitashinda…ni uongo wa Joyce ama wa Betty…..
mcubic mareche slim5 Sangomwile mugaru mbalu byb sac mangimeza Joharia ulimbaga Jullie Z Igunga Mojarammuuza ubuyuKhantwe