Maisha ya upweke yakarejea tena!! Shule nzima ikazizima. Yule mtaalamu wa somo la Kiswahili na hesabu katika shule yao alikuwa ametoweka. Kila mmoja alilalamika na kuweka hisia alizozifahamu yeye. Wengi walidhani kuwa Joyce anafahamu lolote kuhusu Betty lakini hakuna alilofahamu zaidi ya kutambua kuwa marehemu mwalimu Japhari ndiye aliyemuambukiza.
MAWAZO na mtazamo wa Joyce kuwa marehemu mwalimu Japhari ndiye aliyemwambukiza Betty Ukimwi yaliingia doa baada ya kukumbuka kuwa yawezekana kabisa ni Betty aliyemwambukiza mwalimu. Aidha kwa kuambukizwa na Dulla, ama vyovyote vile. Joyce hakutaka kuendelea kuishi na kinyongo ndani yake, akaamua kumtafuta Dulla ili aweze kuzungumza naye kwa kina huku akiamini kuwa kwa kupitia majibu ya Dulla lazima ataujua ukweli tu. Alitambua fika kuwa Dulla hakuwa akitambua mahusiano yaliyowahi kutokea kati ya (Betty) na mwalimu Japhari hivyo ilikuwa kazi nyepesi tu kumvaa kwa nia ya kumshutumu kisha majibu yake yatauweka ukweli wazi. Shida kubwa ya Joy ni kuujua ukweli tu, ama ni Dulla ama mwalimu Japhari aliyemwambukiza Betty. Akiwa amefura kwa hasira kali za kukusudia ili kumtikisa Dulla na asiweze kudanganya chochote kitu. Joyce alifika nyumba ambayo alikuwa anaishi Dulla, kijana aliyekuwa akijishughulisha na shughuli unyoaji nywele (Kinyozi). Alikuta makundi makundi ya watu. Haikuwa kawaida kwa makundi yale kujijenga katika mazingira yale ya kuwakosesha uhuru wapangaji. Hata Joy hakuweza kukatiza. Kwa kutaka kujua nini kinajiri akalazimika kuuliza. Taarifa aliyopewa ililainisha zile hasira zake kisha ikamvika uoga na hofu kuu!!. Dulla alikuwa amejinyonga. Mbaya zaidi hakuacha ujumbe wowote ule. Ilifadhaisha na kushtua sana, mwili ukaota vipele vya baridi ghafla jambo hilo likamkumbusha taarifa aliyopewa siku anazinduka kutoka usingizi mzito na kuambiwa mzee Kisanga ambaye ni baba yake alikuwa amejinyonga. Joyce akajifanya hajui lolote kuhusu Dulla akatoweka bila kuaga. Huku kichwani maswali yakiongezeka badala ya kupungua. Na maisha yakaendelea huku sintofahamu ikiwa imetanda kuhusu Betty, je na yeye amejiua ama. Jambo hili Joyce hakutaka kukubaliana nalo kabisa, naye alijikuta akimlaumu sana Betty iwapo amechukua uamuzi huo. Maana ni huyo huyo Betty alimkataza katakata asifikie hatua ya kujiua kwa sababu ya matatizo. Leo hii yeye anajiua!!! Hapana. Aliongea peke yake Betty njia nzima bila kufahamu kuwa kuna watu walikuwa wakimtazama njiani kwa jinsi alivyofanania na mwendawazimu. Joyce licha ya mawazo yote yaliyomkatisha tamaa bado alijipa imani kuwa Betty atarejea tena machoni pake katika namna ya muujiza kama ambavyo alirejea baada ya kuwa ametoweka kijijini Ukala.
DAR ES SALAAM TANZANIA, 2008.
ALIZIWEKA nywele zake sawa huku akijitazama katika kioo kikubwa kilichokuwa mbele yake. Unywele ulikuwa mweusi haswaa!! Ukiongezea na mafuta aliyopakaa kiustadi zilizidi kuyavutia macho kutazama. Kisha akachukua mafuta ya kupaka midomoni akafanya hivyo kisha akaziminyaminya papi za midomo yake, vishimo kwa mbali vikaonekana katika mashavu yake, hakuwa mweupe na pia hakuwa akifanania na mkaa, lakini alikuwa na mchanganyiko wa rangi hizo mbili. Macho yake wakati akipakaa wanja yalifanya mfano wa kurembuka hivi kimahaba bila kusudio lake mrembuaji. Atafanyaje wakati amebarikiwa kuwa hivyo? Kisha akapiga hatua moja nyuma akajitazama vizuri, akafanya mfano wa tabasamu dogo. Vishimo vikachokoza tena, macho nayo yakarembuka. Alicheka kisha akajiwazia ‘Vimatiti vyenyewe vidogo halafu navaa sidiria mwee!'..hapa akacheka kicheko kikubwa kiasi. Nyama za mabegani zikavutika juu kidogo, nyonga zake zikatikisika. Ewalaa!! Ule mzigo alioubeba nyuma yake nao ukatikisika kistaarabu. Alivutia kimahaba lakini hakuwa na nia hiyo. Atafanyaje lakini?....akajitazama mara ya pili tena, kisha akachukua utuli na marasharasha akapakaza mwilini. Harufu mwanana ikatoka. Sasa alikuwa tayari. "Kidoti umependeza jamani….yaani wewe kila nguo inakukaa duh!" msichana mwenzake alimsifia. Ni nadra sana hii kutokea na ukiona hivyo kama huyo msifiaji hana unafiki basi umependeza kweli. Kidoti alikuwa amependeza. "Asante jamani.." alishukuru kwa sauti ya chini huku akipiga hatua, mkoba wake begani simu moja mkononi. Akaurudishia mlango vyema. Akaendelea kunyata. Alipokaribia mahali fulani akalazimika kulitua begi lake kisha akatoa kitambulisho chake akamwonyesha yule aliyekihitaji. Kisha akaendelea kupiga hatua zaidi akalifikia eneo tulivu kabisa mfanowe hakuna mtu ndani. Akatazama huku na kule akaketi mahali. Akafanya sala fupi kisha kwenye mkoba akaitoa kompyuta mpakato yake akaiwasha na kuendelea na kilichomfikisha hapo.
Alitumia takribani masaa mawili, kisha akaamua kutoka. Njaa ilishaanza kumuuma na alipanga kuwa atakula baada ya masaa mawili. Akakusanya vifaa vyake, akatoka. Alipofika nje akaitazama anga, akajitazama kidogo jinsi alivyovaa kisha akafumba na kufumbua macho tena. Kidoti mimi jamani, amakweli Mungu mkubwa. Kisha akatazama kushoto kwake, akakutana na picha yake chakavu kiasi. Picha iliyomkumbusha alipokuwa mwaka wa kwanza wa chuo. Picha iliyomkumbusha mbali sana. Duh! Hadi leo ipo tu! Hawa nao jamani. Alilalamika na nafsi yake. Lakini hakufanya jitihada za ziada kuibandua. Pembeni ya ile picha akaona tangazo la mwanafunzi akilalamika kuwa amepoteza kompyuta yake ndogo akaweka aina na imepotea katika mazingira gani. Akalipuuzia tangazo lile maana yalikuwa matangazo mengi sana pale yanalalamika kuhusu kuibiwa. Hatua kwa hatua akazishuka ngazi za maktaba kuu ya chuo kikuu cha Dar es salaam. Alitambua fika kuwa kila mtu alikuwa akimtazama, wasichana kwa wivu na wanaume kwa matamanio. Hakujilazimisha kuwa vile lakini! Alivaa kiheshima sana na alipendeza. Wakati anapata Chipsi mayai, alikuwa akimwangalia kwa jicho la kuibia mkaanga chipsi ambaye alikuwa akijishughulisha kukaanga sahani nne za chipsi kwa wakati mmoja, mpishi huyu alimfanya Kidoti atabasamu kila akimtazama na hivyo kufanya mlo wake kushuka taratibu kabisa. Alikuwa katika mgahawa uliofahamika kwa jina maarufu la Daruso lakini kwa wenyeji tu, wale wageni walipaita Kontena. Haya yote yalikuwa yanatokea katika chuo kikuu cha Dar esa salaam. Baada ya Kidoti kuridhika aliukwapua tena mkoba wake akaelekea bomba lilipo aweze kunawa mikono yake, wakati ananawa akakumbana tena na tangazo. Sasa alijikuta akilisoma vyema. "Nipo chini ya miguu yenu jamani, hiyo laptop haikuwa ya kwangu aliyenipa ndiyo shule yake yote ipo humo ndani, irudishe basi mimi nitakupatia pesa za kununua laptop kama hiyo ama yenye uwezo zaidi ya hiyo. Nawaombeni muwe na huruma wanafunzi wenzangu, na roho wa Mungu awatawale." Haya yalikuwa baadhi ya maneno katika tangazo lile. Kidoti akajikuta akilisoma mara mbili mbili, kisha akaichukua namba ya simu kwa ajili ya mawasiliano. Bila shaka kuna jambo alikuwa anafahamu.
Alijikuta akiumizwa sana na maelezo yale, mwaka 2008 ‘laptop' zilikuwa anasa. Na ilikuwa kwamba mmiliki lazima awe mwenye pesa zake haswa. Haikuwa tofauti sana na simu mnamo mwaka 2000. Aliyeweka tangazo kama alikuwa tayari kulipa gharama zote zile bila shaka alikuwa ana maanisha kweli kuwa shule yake yote ilikuwa ndani ya ile laptop. Kidoti akaamua kumsaidia kadri ya uwezo. Kwa lolote lile ambalo alikuwa anafahamu.
Majira ya jioni akampigia simu. Mpokeaji akaanza kuzungumza na kuuliza ni nani alikuwa anazungumza. Kidoti hakutaka mazungumzo ya kwenye simu, akamwomba wakutane. Kidoti alikuwa anaishi hosteli za ‘HALL 3' akajikongoja wakakutana katika vimbweta (sehemu zilizojengwa kwa ajili ya wanafunzi kujisomea) vilivyokuwa katika chuo cha Injinia (COET). Kidoti aliwahi kufika kabla ya mlengwa, jambo ambalo lilimkera sana kwani alitarajia kumkuta pale wazungumze kisha atoweke, hakupenda kukaa mahali bila shughuli ya msingi. Alingoja kwa dakika kadhaa akaagiza soda na kuanza kunywa taratibu, hatimaye simu yake iliita. Alipoipokea, mara akaliona kundi la wanaume wane waliovaa kisasa zaidi huku wakitembea kimagharibi wakimfuata mahali alipokuwa, hii ilikuwa kinyume na matarajio, lile tangazo lilimtanabaisha kuwa mtangazaji alikuwa mpole na mtaratibu sana. Lakini kabla hajawaza zaidi kundi lile likamfikia. Ni katika mgahawa huu ndipo alikutana na ISAYA mtoto wa AKUNAAY. Yalikuwa majira ya saa kumi na mbili jioni!!
****
Wakati Kidoti anayeaminika kuwa mrembo haswaa ana anayependeza katika kila vazi akichukua nafasi pale katika mgahawa na vijana wane watanashati na wajivuni wanaoutukuza umagharibi. Upande mwingine wa chuo kulikuwa na mabishano, wasichana wawili wapashkuna na mwingine wa tatu mshakunaku walikuwa wakinong'ona katika namna ya kung'ong'a. mmoja alisimamia msimamo kuwa Kidoti alikuwa mrembo zaidi ya yule msichana aliyekuwa mbele yao akipata juisi, wengine wawili walikataa katakata na kusema yule binti wasiyemjua jina alikuwa anamwacha Kidoti mbali sana. "Angalia mguu…Kidoti ni mrembo lakini hana mguu, tazama nyonga…..mwanamke nyonga babu wee..Kidoti mbona wa kawaida tu kwa huyu…jicho lile bibi jicho tazama anavyomwangalia yule muhudumu..haya utaona lazima huyo muhudumu atageuka yaani lazima ngoja…." Mpashkuna aliwaambia wenzake, mara kweli akageuka nabii..muhudumu akageuka kumtazama msichana asiyekuwa na jina. Wakacheka kwa sauti za juu kisha wakagonga mikono. Wapashkuna na mshakunaku wakakubaliana kuwa yule msichana wasiyemjua jina alikuwa mrembo kuliko Kidoti. "Sema ujue anachokosa huyu dada ni kitu kimoja tu….." "Kitu gani we nawe.." "Hana tabasamu…."
Wote kwa wakati wao wakamtazama, hakika hakuwa akitabasamu hata kidogo, alikuwa kama amekasirika muda wote. Mshakunaku na wapashkuna wakakubaliana tena katika hili. "Chezea chuo wewe…utakuta amepata ‘Supp' huyo….hiki nd'o chuo hakiangalii cha wewe ni mzuri wala babu yake nani..ukileta urembo tu kinakukanyaga." Mpashkuna mmoja alitoa bango. Wakasimama wakimpita dada asiyekuwa na jina. Walivyompita naye ikawa zamu yake kuwatazama. Walisimama katika mwanga hivyo aliwaona vyema. "Mh! Sasa hawa nao wamevaa suruali ili iweje dah….vimiili hawana, vimiguu vyembamba, ona yule naye amevaa kimini na makovu yote yale." Kwa mara ya kwanza tangu akanyage jiji la Dar es salaam, akafanya kicheko kidogo. Juisi nayo ilikuwa imemalizika, akanyanyuka bila kuwa na uelekeo maalumu. Akajiuliza aanzie wapi baada ya kupata hiyo juisi. Ilikuwa kama kuna nguvu inazidi kumvuta na kumtembeza huku na kule lakini hakupata kile alichokuwa anakitaka. Ni kweli alitambua kuwa anayemtafuta ni mwanafunzi katika chuo kile, lakini hakutegemea kama ni kikubwa kiasi kile. Chuo kilikuwa kikubwa haswaa na wakati mwingine alihitaji kupanda gari ili kuhama kutoka kituo kimoja hadi kingine. Alijipa moyo kuwa ikitimu saa mbili usiku akiwa hana hili wala lile basi atalazimika kufanya kama alivyofanya kabla ya kufika jijini Dar es salaam na aliamini kuwa atafanikiwa tu.
Akiwa katika barabara pweke akihangaika huku na kule mara aliona kundi la wanaume wapatao wanne, alitambua mihemko yao wakiwa kama kundi, aliamini watamsimamisha na kuanza kumuuliza maswali ya hapa na pale lengo kuu likiwa kumtongoza. Ili kuwakwepa akakunja kushoto, huku akiwa hana uhakika na njia anayoifuata akakutana na bango la matangazo, akajitia kutingwa na shughuli ya kusoma kilichoandikwa pale. Bango lile lilikuwa limezuiwa kwa kioo chepesi. Katika kupepesa huku na kule mara akajikuta kweli amevutiwa na kilichobandikwa. Zilikuwa picha kadha wa kadha. Picha moja ikamvutia sana. Msichana mmoja akiwa amevikwa kikofia cha ushindi wa mashindano nguo yake ikizungukwa na ufito ulioandikwa ‘MISS UNIVERSITY'…huyu hakumaanisha lolote kwake, bali aliyekenua meno upande wa kuume. Alifanana na yule anayemuhitaji…..au duniani wawili wawili…..akatazama kama kuna majina yao, akaambulia kapa. Akiwa katika kujiuliza mara msichana mwingine naye akalifikia bango hilo la matangazo. Msichana asiyekuwa na jina hakutaka kulaza damu. "Samahani anti…..mambo" "Poa tu niaje?" "Shwari samahani…unaweza kuwa unafahamu jina la huyu dada…." Aliuliza huku akiishika ile picha. "Sio Kidoti huyo…" "Kidoti?" "Ndiye Kidoti huyu kwani vipi?" "Hilo ndo jina lake kabisa.." "Mi first year dada hata simjui zaidi ya hapo lakini ndo anajulikana hivyo….Hall 3 ndo anapoishi, ukifika humkosi. Sema mashosti wake sasa, wanamringia kama walimzaa vile." Akajibu huku akiongezea na manung'uniko. Msichana asiye na jina akakariri hilo jina la Kidoti na pia akakariri jingo la HALL 3.
Hakutaka kulaza damu, akaendelea na shughuli yake usiku ule ule. Kweli akaipata HALL 3, na kweli akasikia kuna mtu anaitwa Kidoti lakini hakuwepo na alipouliza anarudi muda gani aliambiwa akmaulizie ‘utawala' watamjibu. Akayakumbuka maneno ya yule dada kuwa marafiki wanamringia Kidoti. "Jamani…au sio yeye….mh! kweli abadilike hivi, hapana …lakini labda." Alikata shauri kujiondokea pale kabla hayajawa mengine wakati alitahadharishwa mapema kabisa.
Wakati anaanza kutoka akasikia sauti za kufoka huko nje, akatabasamu huku akimjengea picha huyo mfokaji kama aina ya mropokaji tena mshamba. Ýaani mamtu mengine sijui yakoje tu….yanadhani kila msichana wa ku..(akatamka lugha chafu)..hovyoo kweli, yaani ningekuwepo ningewachamba hao, pumbavu zao mianaume suruali!! Aliendelea kuwaka. "Kidoti huyooo." Msicha mmoja akasema huku akiendelea na mambo yake. Msichana mgeni akasikia. Mapigo ya moyo yakaongeza mwendo wake. Sauti ikazidi kuyafikia masikio ya msichana asiyekuwa na jina. Mara macho yakawaona waliokuwa wakipayuka. Kumbe walikuwa wengi. Macho yakatembea kwa mmoja baada ya mwingine. Mwisho yakatua katika mashavu ya msichana aliyekuwa amefura kwa hasira. Shavu lile lilikuwa na kidoti cha kupendeza. Kundi lile likampita hivihivi huku akiona, akajipa ujasiri akalivaa kundi lile na kumshika mkono msichana aliyekuwa na kidoti. Wapambe wakamrukia. "Na wewe hebu tutokee hapa….shenzi zako.." akasukumwa chini akapepesuka huku na kule lakini hakuanguka. Yule mwenye kidoti akageuka, macho yao yakagongana. Waliachana umbali wa mita kadhaa. "Betiiiiiiiiiii!!!!" Kidoti akapiga kelele ya nguvu na kubwa kupita zote alizowahi kupiga hapo kabla. "Joyceeeee jamaniiiiiiii" mrembo mwingine aliyekaribia kuanguka baada ya kusukumwa akajibu kwa kupaza sauti iliyosindikizwa na mikwaruzo ya kutaka kulia….. Kimya kikatanda kila aliyekuwa na shughulia akaiacha na kuwatazama wawili wale. Wakakimbilia na kukumbatiana kwa nguvu.
Ilistaajabisha, Kidoti akawa wa kwanza kupoteza fahamu kwa mshtuko kisha msichana asiyekuwa na jina naye akaanguka chini na kupoteza fahamu, naye pia kwa mshtuko na mengine yoyote yale ambayo atayasema yeye akizinduka. Mimi kama wewe tu sijui nini kilitokea. Lakini kwa kuwa wewe haukuwepo basi tulia nitakuhadithia!!!! Lakini wale mapacha wasitoka tumbo moja. BETTY (Msichana asiye na jina) na JOYCE (Kidoti) walikuwa wamekutana tena……wote wakiwa hai…. Lakini kwa mara nyingine tena ni katika wajihi tofauti.
**BETTY alipotekea wapi kwa miaka hiyo yote?? ***JOYCE naye alipita kona zipi hadi hapo alipo…JOYCE MREMBO……. **ISAYA AKUNAAY ni nani katika riwaya hii??
USIKOSE MUENDELEZO WA SIMULIZI HII itakayokupa wakati wa kufikiria na kujifunza kitu….
Yule mwenye kidoti akageuka, macho yao yakagongana. Waliachana umbali wa mita kadhaa.
"Betiiiiiiiiiii!!!!" Kidoti akapiga kelele ya nguvu na kubwa kupita zote alizowahi kupiga hapo kabla.
"Joyceeeee jamaniiiiiiii" mrembo mwingine aliyekaribia kuanguka baada ya kusukumwa akajibu kwa kupaza sauti iliyosindikizwa na mikwaruzo ya kutaka kulia…..
Kimya kikatanda kila aliyekuwa na shughulia akaiacha na kuwatazama wawili wale. Wakakimbilia na kukumbatiana kwa nguvu.
Ilistaajabisha, Kidoti akawa wa kwanza kupoteza fahamu kwa mshtuko kisha msichana asiyekuwa na jina naye akaanguka chini na kupoteza fahamu, naye pia kwa mshtuko na mengine yoyote yale ambayo atayasema yeye akizinduka. Mimi kama wewe tu sijui nini kilitokea.
Lakini kwa kuwa wewe haukuwepo basi tulia nitakuhadithia!!!!
Lakini wale mapacha wasitoka tumbo moja.
BETTY (Msichana asiye na jina) na JOYCE (Kidoti) walikuwq wamekutana tena……wote wakiwa hai….
Lakini kwa mara nyingine tena ni katika wajihi tofauti.
Wawili hawa hawakuhitaji kukimbizwa hospitali ili waweze kurejewa na fahamu. Baada tu ya kupungiwa upepo wa haja na marafiki pamoja na kumwagiwa maji kiasi fahamu ziliwarudia. Wakaachwa watulie kidogo na kumbukumbu zao zikawakaa sawasawa.
Hapa sasa hawakuhitaji kujibu swali lolote kutoka kwa mtu yeyote yule, walihitaji kupumzika. Lakini sio katika chumba cha hapo chuoni, Joyce Keto Kidoti alichukua taksi akamuamuru dereva akawapeleka maeneo ya River Side Ubungo, huko wakachukua chumba katika hoteli ya kisasa.
Usiku huu ukawa wa aina yake!!
Ulikuwa usiku ambao kila sentensi kutoka kwa aidha Joyce ama Betty ilichangamsha ubongo na kuulazimisha kufikiri kwa uyakinifu.
Zilikuwa ni kumbukumbu za miaka sita iliyopita. Kumbukumbu za Makambako, kumbukumbu zilizotatanisha haswa. Na kisha ukazuka mtihani wa aina yake!! Mtihani ulioufanya usiku huu kuwa wa kukumbukwa tena!!!
Mazungumzo ya awali kabisa Betty alimuuliza Joyce Keto, kisa cha kuwa amekasirika vile usiku ule na inakuwa vipi anakuwa na wapambe wengi vile.
******
WANAUME wanaume wanaume aaargh!!! Alianza kulalamika Joyce. Betty akawa msikilizaji.
Joyce alielezea juu ya kushiriki kwake mashindano ya urembo chuoni na kisha kuzua kizaazaa baada ya mshindi kutajwa mwingine wakati kila mmoja akitegemea kuwa Joyce Keto ama maarufu kama Kidoti atanyakua taji hilo. Mtafaruku huo ukampa jina kubwa pale chuoni, na akapata marafiki wengi japo sitakosea nikiwaita wapambe. Ni hawa waliokuwa kama walinzi wake, wakimfuata hovyo kila mahali. Huku wakijisahau kuwa wote ni wanafunzi tu wa pale chuoni.
Joyce akamaliza kwa ufupi kisha akahamia tukio la jioni ile.
Hili alilielezea kwa ghadhabu.
Kama ambavyo hakutegemea kuwa mpotezaji wa vitu vile kuwa katika hali ya majivuno na ulimbukeni ulo'kubuhu kiasi kile, basi nd'o ambavyo hakutegemea kuwa yatazuka mambo ya ziada.
Joyce alituliza akili yake wakati wale vijana wanne wanajongea katika kimbweta alichokuwa ameketi, aliwatazama kwa jicho la kuibiaibia akawaona jinsi walivyokusudia kuvuta macho ya watu kuwatazama.
"Karibuni." Aliwakaribisha. Wakaketi wote baada ya kumpa salamu kwa kumshika mkono. Joyce alitamani kuwaomba watoke abaki na mmoja lakini aliona hilo kama haliwezekani, halafu mbaya zaidi walipofika na kumtambua ni yeye wakaongeza majisifu. Kijana aliyekuwa mbele yake kwa kudhamiria kabisa akalegeza vishikizo vya shati lake.
Ewalaa!! Mkufu wa dhahabu ukaonekana, laiti kama angekuwa msichana mwingine angeanza kuuvaa mkenge lakini Joyce Keto hakuwa msichana wa kawaida, huo aliuona ni ushamba. Akataka kusonya lakini akajikuta akiguna, akataka kuangalia kwa jicho baya lakini badala yake akajikuta akirembua jicho lake.
Joyce hakujua kuuvaa uhusika wa kukasirika, suluhu yake ni kuvimbisha mashavu kisha anatokwa machozi. Mwisho wa mchezo.
Joyce akapuuzia yote yaliyokuwa anaendelea. Akataka kuanza kujieleza jambo alilolifahamu, mara mmoja kati yao akatoa simu aina ya Nokia yenye kamera, ambayo kwa wakati ule ilikuwa katika chati. Hapa Joyce akashusha pumzi kwa nguvu bila kusema lolote.
‘Hivi wanadhani mimi wa bei rahisi hivyo!...pole yao maskini dah!' aliwaza haya huku akijitahidi asizungumze kwa hasira.
Hatimaye walianza maongezi, Joyce akaanza kujieleza lakini akakatwa kauli na mmoja wao.
"Aaah! Sorry sister, yo know hatujafahamia bado walau majina something which is not good at all." Mtumwa mmoja wa maisha ya kighaibuni akasema.
"Naitwa Joyce" akawahi kujitambulisha kwa karaha.
"Ben"
"Simon"
"George"
"Isaya" alimalizia mwanaume wa mwisho ambaye kama ni mashindano ya ujivuni alikuwa anaongoza, ni kweli alikuwa amependeza lakini ujivuni ulimfanya aonekane mpuuzi tena.
"Nafurahi kuwafahamu." Alisema kwa kujilazimisha Joyce, kisha akaendelea na alichokusudia kuwaeleza, akawaelezea kwa pamoja ni kitu gani anafahamu kuhusu kompyuta iliyopotea, alishangazwa sana na umakini wao. Hawakuwa makini kabisa kumsikiliza alichokuwa akiwaeleza, labda kidogo Isaya alikuwa anasikiliza kitu japo naye kila mara alikwenda kupokea simu bila kuomba radhi.
"Basi ni hivyo nijuavyo, kama bado haijatoka nje ya chuo basi ni mtu huyo niliyemshuhudia akitoweka nayo maktaba." Alimaliza.
Baada ya maswali mawili matatu yasiyokuwa na uzito ndipo wanaume hawa walipohamisha mada na kuibua mada iliyomkera waziwazi Joyce. Haikuwa mada mbaya, ilikuwa mada ya kuhusu mapenzi….na hapakuwa na ubaya mtu kuzungumza mapenzi, lakini walichofanya wanaume hawa ni kumtongoza kwa pamoja.
Walimfanya kama changudoa mzoefu. Mara huyu amwambie hivi mara yule aseme hiki. Kwa akili zao waliamini kuwa Joyce atazenguka na ufajari wao. Kitendo cha kutongozwa na wanaume wanne ilikuwa ni dharau iliyopitiliza kabisa. Dharau iso'kuwa stahiki yake. Ni hapa Joyce alipoamua kuwatumia ujumbe marafiki zake wa kike ambao ni mcharuko haswaa. Wakati anawatumia ujumbe walimjibu kuwa walikuwa mahali wanapata juisi, akawasihi waende alipo wakamweleza kuwa wanaenda huku wakimtumia ujumbe wa ziada kuwa wamekutana na pacha wake kwa urembo.
Walipofika wakatumia mbinu zao kumtoa Joyce katikati ya kundi lile, hapa ukazuka mtafaruku mwingine baada ya wanaume wale kudai kuwa kwa sababu rafiki zake Joy wametimia wanne na wao wapo wanne basi wagawane.
Hapa ukazuka mcharuko wa ajabu kutoka kwa rafiki zake Joy. Mcharuko ambao uliwafanya wafike hosteli huku wakitukana matusi yote wayajuayo na Joyce akiwa kimya tu.
Marafiki/wapambe hawa ni walewale wapashkuna na washakunaku waliokuwa wameketi jirani na Betty wakiujadili urembo wake huku wakiulinganisha na wa Kidoti Joyce Keto.
Ni huku walipokutana tena mapacha hawa na kubadilisha simulizi ya usiku ule!!!!
Joyce kidoti alimaliza ngwe ya kwanza ya simulizi. Betty alikuwa anatabasamu tu…
"Ila umekuwa mrembo sana Betty jamani…" alimsogelea rafiki yake na kuanza kujidekeza katika mapaja yake kama mtoto mdogo. Kisha akaanza kulia akimlalamikia kwa nini aliondoka bila kuaga.
"Yaani Betty jamani….nd'o ukaniacha pekee ukaniacha vile kweli Betty mimi mwenyewe huko….mi s'taki…..s'taki…." akazidi kudeka huku machozi mepesi yakimtoka. Betty akambembeleza huku akimfuta machozi, walikuwa wamekuwa wadada watu wazima lakini ule urafiki wao wa tangu utotoni uliwafanya waendelee kuwa watoto.
Betty aliifahamu tiba ya kumfanya Joyce atabasamu tena, baada ya kuonekana kuzidiwa na majonzi, na aliihitaji sana furaha yake ili na yeye aweze kumhadithia jambo zito.
Akasimama akimwacha Joy kitandani. Akasogea hadi katikati ya chumba. Joy alidhani anaenda uani, akajilaza kifudi fudi.
Mara…………………
"Ukutiii ukutiiiii……wa mnaziii…..wa mnaziiiiiiiiii……..mwenzetu….mwenzetu……..kagongwa ……kagongwa……na nini na nini….
Na gaaari na gaari…….."
Joyce akakurupuka kutoka kule kitandani, alikuwa na kanga iliyofunika kiguo kifupi cha kulalia, kanga ikaanguka hakujihangaisha kuiokota……akafika kwa fujo mahali alipokuwa Betty akiimba kipweke kabisa, akaunganisha mikono yao upesi kisha akendelea kwa sauti kuu yenye furaha..huku wakirukaruka.
"…Tumpeleke hosibitali asije kusema kwa mama yake….yesayesayesa yaaah…..bado kidogo….yeasayesayesa yaah!! Baaado kidogo ….yesayesayesa yaah!!"
Hakika Betty alikuwa amemkamata Joyce haswaa, waliruka ruka wakabadili kila aina ya nyimbo za utotoni na zile ambazo waliimba wakiwa wanakua. Furaha ikakipamba kile chumba.
Kisha kwa furaha wakakumbatiana huku wakilia, zile nyimbo ziliwakumbusha mbali. Enzi hizo Joyce ni mwembamba na kidoti chake kikiwa sio biashara hadimu. Betty naye akiwa ‘kimbaumbau'.
WAKATI wawili hawa wakikumbushia enzi zao kwa nyimbo za kitoto, upande mwingine wa maisha wanaume wanne ambao waliita kile kitendo cha Joyce kuondoka kinguvu na wale wasichana ambao ni rafiki zake kilikuwa ni utovu wa nidhamu. Wanaume wale waliamini hapakuwa na msichana hata mmoja ambaye ana uwezo wa kuwakatalia kimapenzi, walikuwa na kila kitu ambacho msichana wa wakati ule alikuwa anatamani kukifahamu aghalabu kama si kukipata kabisa.
"Mara ya mwisho mi kukataliwa na demu ilikuwa mwaka juzi, tena tulikuwa ikulu nd'o kitoto cha prezidaa kikanitolea nje, tena ni vile sikukaza uzi tu na alishajua kuwa nilikuwa natoka na mtoto wa waziri, hiki kishamba kutoka wapi nd'o kinisumbue. Sasa hapa naweka kando mambo yangu kwa muda. Lakini tupinge nawapa wiki mbili tu huyo Kidoti sijui nakuja kumtambulisha mbele yenu" alijiganba Isaya. Wale wanaume wengine wakapiga kelele za shangwe kumpamba Isaya.
Walizungumza mengi huku yule mtoto wa mbunge wa wilaya ya Geita (kwa sasa mkoa wa Geita) ambaye alionekana kudhamiria waziwazi kuhusiana na Joyce akiweka kiapo.
Safari zake za kwenda Marekani na uingereza mara mbili tatu akiambatana na mzee Akunaay Zingo ambaye ni baba yake mzazi na pia mbunge, zilikuwa zimempagawisha sana na kujikuta akitamani kuishi maisha ya kimagharibi katika nchi ya Tanzania.
Alijipa kiburi kuwa kwa safari zake hizo na pesa aliyokuwa nayo basi angeweza kufanya kila kitu na kila mtu akakubali.
Ni heri asingeweka kiapo kile maana alikuwa anajiingiza katika safari asiyoijua mwisho wake wala mwanzo wake!!!
Ni basi tu wanadamu hatukupewa jicho la kujua yatakayojiri wakati ujaoo…….
***
Kabla ya kulala Betty naye alisema machache kuhusu yeye.
"Joyce Kidoti." Aliita kwa utani, Joyce akacheka.
"Najua una maswali mengi ya kutaka kuniuliza, lakini baadhi nayajibu katika maelezo yangu, kwanza unajiuliza Dar nipo tangu lini na nimekuja kwa nani….Joy mpendwa mguu huu kutoka huko nitokapo ni mguu wa kuja kwako wewe." Akasita na kumtazama machoni rafiki yake.
"Nimekuja kwako wewe ukiwa ndugu yangu wa karibu sana na mwandani wa kuzifahamu siri zangu na matatizo yangu hata kama ni makubwa vipi. Nimekuja hapa nikihitaji msaada wa vitu viwili kwako, yaani vitu viwili tu! Na kama vikiongezeka nitakueleza…" Joy akamkatisha, "Betty hutakiwi kuhesabu kitu chochote kwangu Joy ni yuleyule na nitafanya kila kitu kwa ajili yako hata kama ni vitu elfu moja." Alisema kwa hisia, Betty akaipokea kwa kutikisa kichwa juu na chini. Kisha akaendelea. "Kitu cha kwanza ni hifadhi, sina hifadhi katika jiji hili na kubwa zaidi ni mara yangu ya kwanza kufika jijini hapa. Kitu kingine ambacho nahitaji unisaidie ni kunitunzia siri yangu, Joyce Ukimwi ….ukimwi hauponi hata asikudanganye mtu, mimi na afya yangu yote hii bado unaishi nami ugonjwa huo mbaya." Hapa Joyce akatikisa kichwa kwa masikitiko.
"Usiumie Joyce hiyo ilibidi itokee iuli wewe ufike hapa kisha urejee Ukala kama shujaa wangu, shujaa wa kijiji chetu. Na katika huo ushujaa ukilitaja jina langu kichwani mwako nitafarijika sana. Maana kitu ninachokiamini mimi katika vita hata wale ambao huteteketea na kupoteza uhai wao wakiligombania taifa na wao huitwa mashujaa pia. Hivyo mimi nimekufa katika harakati, ningeweza vipi kukuacha Joy uolewe…nigekuacha vipi uolewe na wale watu wazima ambao huenda wana Ukimwi wakakuambukize. Joy imekuwa heri punda afe mzigo ufike na sasa imekuwa heri Betty afe JHoyce akikomboe kisiwa cha Ukala, kisiwa kilichowameza wazazi wetu, kikawatafuna waalimu wetu kwa sababu ya kukosa huduma za kiafya. Kisiwa kilichosahaulika kabisa. Ni furaha yangu nimekukuta ukiwa hapa na utanieleza ulifikafika vipi hapo baadaye maana tupo pamoja tena…..Joy msaada huo wa kuitunza siri hiyo kwa upendo ni kwa manufaa yetu pia, najua mzigo wa kuipigania Ukala ni mkubwa sana, nilitamani tushirikiane kimasomo hadi huku lakini haikuwezekana, lakini nikaipata njia mbadala huko Lilongwe Malawi nilipokuwa naishi kwa kipindi kirefu. Nimekuja nikiwa na nia moja tu, nahitaji pesa. Pesa kwa ajili ya kijiji chetu, pesa kwa ajili ya maisha yetu. Mara ya kwanza nilivua nguo nikapata pesa, sasa ni mawili KISASI na PESA…wataumia hao walio na tamaa watambuao kuwa sisi ni vyombo vya starehe, na wataumizwa na tamaa zao, sitajiuza Joy sitamtega mwanaume kwa maksudi ili aninase lakini nasema OLE WAO wajilengeshe na kujifanya wanajua kupenda na wanayo pesa……moyo wangu umebakiza nafasi ndogo sana ya upendo, na huu ni kwa ajili yako tu Joy, sihitaji kumpenda mtu mwingine kabisa. Namaanisha ninayoyasema.
Nd'o maana nikahitaji hifadhi za aina mbili, kwanza mimi kama mimi kisha hifadhi na siri yangu hiyo nzito. Huku ukijua wazi ndugu yako sina upendo zaidi ya kwako wewe na nd'o maana ninakupa siri na mipango yangu ya sasa" alimaliza na kuweka kituo Betty kisha akamtazama tena Joyce. Joyce alikuwa ana wasiwasi mkubwa sana.
Alishangaza sana kumtazama.
****BETTY ndani ya jiji, hana urafiki wala huruma…..jilete akufyatue..
***JOYCE amebebeshwa siri hiyo…si alisema yupo tayari kwa lolote…HAPO VIPI??
***ISAYA na kiapo chake….atambeba JOYCE KIDOTI…
weeraweraaaaaaaaaaaaaaa betty...nakupenda buleeeee..wamalize wajingawajinga wasiojijali na kufilkili kila mwanamke ni chombo cha starehe......fanya yako dada kwa msaada wa ARV kutoka marekani..mbakize kakaangu tu anayetutungia hadithi....NICE STORY...
.
JOYCE alikosa cha kujibu kwa usiku ule, akatamani kumshauri Betty walale kwanza huku akifikiria nini cha kujibu lakini akajikanya kuwa huyu Betty hakufikiria mara mbilimbili wakati anaamua kufanya mapenzi na mwalimu Japhari ili aweze kupata pesa kwa ajili yake. Kumbukumbu hii ikampa ujasiri..akakifungua kinywa chake.
"Betty, nadhani unafahamu kuwa sina uwezo wa kusema hapana kwako, nadhani unajua kuwa wewe ni zaidi ya mwandani wangu, sina kipingamizi, kama ambavyo sikunyanyua kinywa changu kumshirikisha mtu yeyote juu ya mahusiano yako na mwalimu, basi hivyo hivyo sitapoteza hata sekunde moja kumshirikisha mtu yeyote juu yako. Kwa hili NAAPA!!" Alisema Joyce kwa ujasiri huku akimtazama Betty machoni moja kwa moja akimaanisha kuwa kile ambacho anakiongea anamaanisha na wala hatanii. Betty akavutiwa na jibu hilo, alitegemea elimu ya Joyce itakuwa imeanza kumbadili lakini la haikuwa hivyo. Joyce alikuwa yuleyule.
"Ehe na wewe nambie uliunga unga vipi hadi kufika huku maana sikuamini siku nilipoona jiba lako katika mtandao kuwa unajiunga na chuo hiki, hakika nilistaajabu. Sikuwa tu na mtu yeyote kule Lilongwe ambaye alikuwa anakufahamu hivyo sikuwa na wa kumweleza kuwa pacha wangu amefikia elimu ya chuo kikuu." Aliuliza kwa shauku, Betty.
"Mhhh! Kwanza nimalizie wewe ulipoteaje pale Makambako jamani watu wakaanza kusema umekufa, wee nililia sana, mara Dulla naye akajinyonga yaani nd'o nikachanganyikiwa mimi."
Hapa Betty alitabasamu kidogo kisha akajisemea mwenyewe, "Mwanaume pekee niliyemuua kimakosa ni Dulla waliosalia wote ni haki yao, watajuta kuzaliwa wanaume na tamaa zao" Baada ya kujisemea akaendelea kuzungumza tena na Joyce, akaipandisha sauti juu kidogo.
"Hofu, aibu, mawazo, na uoga wa kifo humfanya mgonjwa wa Ukimwi kujihisi anakufa kesho yake, hapa sasa hujikuta akiteswa na hivyo vitu vitatu hasahasa mawazo na uoga wa kifo. Hapa sasa mgonjwa huonekana kama aliyezidiwa tayari na anakufa muda wowote." Ni hivyo daktari aliwaeleza ndugu zangu wa kule Makambako. Kisha wakawasihi wanipeleke mbali kabisa na Makambako ambapo nitapotelewa na ‘aibu' kwa sababu hatakuwepo mtu anayenitambua, pia mawazo yatapungua kutokana na mazingira mapya.
Betty alisimulia jinsi alivyosafirishwa hadi Malawi kwa mganga wa tiba za asili. Akapewa tiba za kiasili kwa juma moja akinyweshwa madawa makali makali asiyoyajua majina yake. Madawa ambayo yalimsaidia haswa. Kisha akasafirishwa hadi Lilongwe mji mkuu wa Malawi, huku ndipo akaanza huduma za kisasa. Ushauri wa daktari ulipozingatiwa Betty akanawiri tena. Alitamani sana kusoma lakini ilimlazimu kuanza upya tena jambo ambalo hakuwa tayari kulifanya, basi akabaki kuwa msaidizi tu nyumbani kwa huyo aliyeambiwa kuwa ni ndugu yake.
Maisha yalikuwa ya wastani na familia ilikuwa na furaha tele, lakini Betty hakuridhika kabisa kuishi na kufia utumwani, hapo likamjia wazo la kutoroka. Alikutana na mwanaume kutoka Tukuyu Mbeya, katika orodha huyu ndiye wa kwanza. Akampamba Betty kwa maneno matamu. Betty akaomba kitu kimoja tu, awezeshwe kufika Tukuyu ama Mbeya mjini iwapo itawezekana.
Mnyakyusa akaingia mtegoni. Betty akatoroka nyumbani, akiwa na fikra moja tu kichwani mwake, fikra ya kufia nyumbani na si ugenini kiasi kile hata kama alikuwa akipendwa vipi, bado aliamini kuwa yeye ni marehemu wa wakati wowote. Basi kwa kitendo cha mwalimu Japhari kumpa pesa baada ya kumwambukiza Ukimwi basi alihitaji ‘ka-mchezo' kaendelee.
Ule Ukimwi aliopewa na mwalimu yeye akaamua kuufanya kitega uchumi. Betty akaamua kuuza Ukimwi kwa manufaa ya kisiwa cha Ukala.
Kutokea Tukuyu, baada ya mnyakyusa kulipia pesa nyingi ule Ukimwi ambao alipewa katika nyumba za kulala wageni mjini Mbeya. Betty akaamua kusafiri kwenda Dar.
Alifanya hivi akiamini kuwa pesa na kila wanaume punguani waliovurugwa na pesa wapo jijini Dar es salaam.
Sasa yupo Dar, yupo na Joy na amemweleza kila kitu na amekubaliwa.
Joyce akashusha pumzi baada ya Betty kusimulia.
Kwa upande wake hapaukuwa na longolongo nyingi, alifaulu kwa kiwango cha juu kidato cha nne, mkuu wa shule akaitisha mkutano wa wazazi na wanakijiji wengine, harambee ikapitishwa kwa Joyce na wanafunzi wengine wawili waliofaulu kujiunga na kidato cha tano. Pesa ikapatikana ya kutosha wakaingia shuleni bila mashaka yoyote.
Hata safari ya kwenda chuo kikuu haikuwa ngumu, serikali ilikuwa inatoa mikopo. Na bado mkuu wa shule aliendelea kuhitisha mikutano mara kwa mara hadi Joyce pekee akiwa kati ya wanafunzi watatu kutoka Makambako waliofaulu kidato cha sita na kuingia ngazi ya chuo kikuu.
Wakati Joyce anamaliza kusimulia Betty alikuwa amesinzia tayari, bila shaka hakusisimuliwa na maelezo yale ama la! Alichoka. Hivyo Betty hakupata nafasi ya kusikia juu ya Joy kugombea ‘urembo' wa chuo, jinsi wanafunzi walivyomtunuku pesa kuonyesha kuwa wanapingana na matokeo yaliyotajwa, akajitokeza mdau mwingine na kuahidi kisha kumnunulia Joyce Kidoti ‘laptop'…..
****
MACHO ya wasichana walimbwende haswa kutoka chuoni yalikuwa yakistaajabishwa na hali ya sintofahamu iliyokuwa inaendelea kati ya mwanafunzi aliyekuwa na pesa na pia majivuno huenda kuliko wanafunzi wote wa chuo hicho kikuu na msichana aliyesadikika kuwa ni mrembo aliyeshinda taji lakini akachakachuliwa na wajanja. Kwa ufupi ilikuwa ni sintofahamu kati ya watu maarufu chuoni hapo.
Walikuwa waeneo ya Mabibo Hostel, eneo maarufu kabisa kwa wapendanao ‘Block G'.
Kwa mtazamo wa macho ilionyesha kabisa kuwa msichana alikuwa akipingana na yule mvulana, mtoto wa mbunge wa Geita. Isaya Akunaay, hali ile iliwatia hasira wasichana ambao walitamani sana kuwa katika mahusiano na watu maarufu na wenye pesa zao.
Kila msichana wa kisasa angeweza kutamani kuwa na Isaya Akunaay, si tu kwa sababu alikuwa na pesa la! Alikuwa mtanashati pia, jamari wa sura ana umbo.
Vipi kuhusu Joyce? Mbona kama hana dalili za kushawishika!!! Hiyo ikawa sintofahamu kuu.
"Isaya…unanirudisha hostel ama nikapande daladala." Alihoji Joyce huku akirusha mikono huku na kule.
"Nisikilize kwanza nd'o nitakurudisha kama hunisiki…"
"Kaka, sitapanda gari yako nimeghairi, nitapanda daladala. Naomba niende tafadhali." Sauti ya Joy ilishuka chini sana, hii hutokea akiwa amekasirika sana.
Isaya alidhani Joyce alikuwa anatania, mara yule msichana akasimama wima….
"We Kidoti…Kido…." Hakumalizia kauli yake, binti akarusha mikono hewani kumaanisha kuwa hataki kusikia lolote kisha kwa mwendo wake uleule wa kilimbwende akatoweka machoni.
Isaya akabaki ameduwaa, hakika aliduwaa na ilikuwa mara yake ya kwanza.
Mara ya kwanza kudhalilishwa kama ambavyo angeweza kusema yeye iwapo angeulizwa.
Wapambe wake waliokuwa ndani ya gari la Isaya walilitazama tukio lile katika hali ya mshtuko pia, hawakutarajia kuona walichokiona. Wakapigwa na bumbuwazi na hata Isaya alipoingia ndani ya gari hakuna aliyemuuliza kitu.
Mpambe akawasha gari.
"Nipeleke room." Aliamrisha. Gari ikatoweka.
Kichwa kilimuuma Isaya.
HAIKUISHIA hapo, mara ya pili walikuwa maktaba wakijisomea, wapambe wakamtonya Isaya kuwa Kidoti alikuwa humo.
Isaya akajibebesha mkoba wake wenye laptop akaingia maktaba. Huko akamfuata tena Joyce katika namna ya kutaka kuendeleza na ombi lake la kumtaka kimapenzi.
Pasipo kutarajia baada ya kuongea maneno mengi sana kwa sauti ya kunong'ona, sasa ulikuwa wakati wa Joyce kujibu. Likatokea jingine ambalo lilimlaza Isaya hoi kitandani siku hiyo bila ugonjwa wowote kichwani.
Joyce akaandika katika kikaratasi na kukisukuma kwa Isaya Akunaay. Mtoto wa mbunge anayejihisi kuwa nay eye ni mbunge.
"DON'T MAKE NOISE IN THE LIBRARY…..haukusoma pale mlangoni??" maandishi yalisomeka hivyo. Isaya akabaki na kile kikaratasi huku akitazama kama kuna mtu yeyote ameona wakati akisukumiwa, akakikunja kunja. Akataka kusema neno lakini Joyce hakuonekana kuwa tayari kusikiliza chochote kile.
Karata hii nayo ikagonga mwamba!! Isaya akazidi kuchanganyikiwa, mapema akalala fofofo mchana, kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya chuo.
Jaribio la tatu lilikuwa shukrani alizopeleka kwa Joyce kwa kumsaidia kuipata ‘laptop' iliyokuwa imepotea maktaba. Isaya aliamini shukrani pekee ni pesa, akamtumia Joyce kiasi cha shilingi laki mbili kama shukrani.
Hapa napo mambo yakawa yaleyale na akili yake ikazidi kuduwaa. Pesa ilirudishwa bila kupungua hata noti moja.
"Amesema haukutangaza dau lolote kwa atakayefanikisha kupatikana kwa laptop nd'o maana aliamua kwa moyo wake tu!!" kauli hii ikamchanganya Isaya japo alikiri kuwa Joyce alisema ukweli kabisa. Akazipokea pesa zake kinyonge.
Kuanzia hapa hakufanya papara tena, akajifanya hana haja na Joyce tena. Lakini moyoni akikiri kuwa wale wasichana wote aliowapata zamani kwa kutumia jeuri ya pesa zake hawakuwa na ladha na hawakumkaa akilini kabisa, alifanya nao mapenzi na kuwaacha mara moja. Wengine walimlilia lakini hakujali, lakini sasa akakitambua kilio chao kilivyokuwa na maana kubwa na kikiwaachia jeraha la aina yake.
Jeraha la hisia!!
Sasa jeraha hili likaanza kumtambaa nay eye pia, akajikuta akimuhitaji sana Joyce kuliko yule mtoto wa raisi wan chi ambaye alimkataa kimapenzi.
"Kumbe pesa sio kila kitu eeeh!!" aliwaza Isaya kisha akamalizia, "Kipi sasa ni kitu zaidi ya pesa jamani." Hakuwepo wa kumjibu.
Tabia ya Isaya ikabadilika, akawa mtu wakulala tu, kila alilolifanya aliona haliendi sawa iwapo kuna msichana alimuhitaji na hakumpata.
Mara akaanza kudhoofika. Hili likawashtua rafiki zake nay eye mwenyewe pia. Alidhoofika kwa sababu ya kuwaza juu ya jeuri ya Joyce , alijiuliza nani anayempa kiburi.
Msako ukaanza ili amjue mwanaume ambaye anampa kiburi Joyce, akishampata ndipo atajua nini cha kumfanya ama uamuzi gani wa kuchukua.
*****
WAKATI huu Joyce alikuwa amehamia chumba chake mwenyewe nje na chuo, huku alikuwa akiendelea kuishi na Betty ambaye alikuwa kazini katika namna ya kipekee, kama alivyosema awali. Hataki mwanaume njaa anayetegemea mkopo wa serikalini utoke ndipo aanze mbwembwe zake chuoni, ama mwanaume shida anayetegemea wazazi wapate mishahara yao midogo wamtumie pesa za matumizi.
Betty alikuwa anahitaji wale wanaojiita watoto wa ‘misheni tauni'. Wenye pesaa zao bila kujalisha ni wapi walipozitoa. Cha msingi wasiwe na mikono ya birika, wajue kuhonga. Na kwake yeye ilikuwa lazima wahonge, hakuwa msichana wa kutongozeka kikawaida kawaida.
Alikuwa kikazi zaidi, na katika kazi yake hiyo alikuwa makini mno.
"Vipi jamaa keshaacha kukusumbua siku hizi…maana kimyaa au ndo tayari na wewe…ushadata." Betty alimchokoza Joy wakiwa kitandani.
"Aaargh asingeweza kunipata kirahisi, ameuchuna siku hizi aibu kwake…ananitishia mimi pesa ananitishia majivuno." Alijibu Joy kwa jeuri huku akiibetua midomo yake.
"Na hicho kidoti wanakomaje!!!"
Wakacheka kwa pamoja!!!
Mara simu ya Betty ikaita akaipokewa, alikuwa bwana mmoja mfanyakazi wa benki.
"Mi natoka shoga!!." Alimuaga Joyce wakati anajiandaa kwenda kwa bwana mwingine.
"Huyu ananipa laki tano leo, nakaribia kufikisha milioni nne dah safi sana. Na roho saba zipo rehani tayari pumbavu zao." Alibwabwaja huku akitangaza chuki ya waziwazi.
Akaondoka zake!!!
***ISAYA AKUNAAY ameamua kumkabili Joyce Kidoti Keto katika namna nyingine….JE KWELI YUPO MWANAUME anayempagawisha JOYCE….nini kitajiri …..
***BETTY yupo kazini na hana utani….je atatimiza azma kabla UKIMWI haujammaliza…..
JamiiForums uses cookies to help personalise content, tailor your experience and to keep you logged in if you register.
By continuing to use this site, you are consenting to our use of cookies.