KITABU: PIGO LA MWISHO (1)
MTUNZI / MWANDISHI: INNOCENT A. NDAYANSE (ZAGALLO)
CHAPA YA 2015
DAR ES SALAAM
SIMU: 0653 593 546 / 0755 040 520
***** ***** ***** ***** *****
SURA YA KWANZA
KAMBA Kiroboto alishusha pumzi ndefu mara tu alipokuwa nje ya Gereza la Keko jijini Dar es Salaam. Akaangaza macho huku na kule kama mgeni aliyeletwa hapo huku kafumbwa macho. Akageuka na kulitazama lango kuu la gereza, kisha akageuka tena na kuyatupa macho mbele ambako aliwaona watu wakipita na hamsini zao.
Kama aliyezinduliwa usingizini, alianza kuvuta hatua ndefu akiliacha eneo hilo. Akatembea kikakamavu, akijihisi kama ambaye bado hajawa huru na kwamba labda muda mfupi ujao atapigiwa filimbi ya kuashiria kuwa ametoroka. Baada ya hatua kama mia mbili hivi, akasikia honi nyuma yake.
Alipogeuka, akaliona gari dogo, jeupe likimsogelea. Akakunja uso na kulitazama kwa makini huku na yeye akipunguza mwendo. Lilipokuwa usawa wake, likasimama kisha vioo vikashushwa. Kamba naye akasimama na kuinama kidogo ili amwone huyo anayeliendesha gari hilo.
Nyuma ya usukani kulikuwa na mwanamume aliyevaa suti nyeusi, maridadi huku uso wake ukiwa umenawiri na akitabasamu. Macho yake ya kujiamini, macho yaliyowaka ukwasi sanjari na ndevu changa zilizochongwa kiufundi na kinyozi aijuaye kazi yake, ilikuwa ni taswira tosha iliyomweka mtu huyo katika kundi la wenyenazo.
“Twen’zetu mshkaji wangu,” mtu huyo alimwambia Kamba huku akimfungulia mlango.
Kamba alishangaa na kusita. Huyu mtu ni nani? alijiuliza. Hata hivyo, hakuwa na hisia za kujiwa na mtu huyu kwa dhamira mbaya. Hakuwa na kumbukumbu ya kufanya kosa lolote dhidi ya mtu mweusi au mweupe kiasi cha miaka saba iliyopita. Na kosa lililomfanya asote humu Keko hadi siku hii halikumhusu mtu mweusi, hivyo akaamua kuingia garini akiamini kuwa hiyo ni lifti ya msamaria mwema.
Gari likaondoka huku muziki laini ukisikika sanjari na kiyoyozi kilichoongeza starehe ndani ya gari hilo la kifahari.
“Pole sana msh’kaji wangu,” mtu yule aliuvunja ukimya. “Maisha ni mzunguko. Mtu hupita kwenye milima na mabonde hadi siku ya mwisho wa uhai wake hapa duniani. Yote ni maisha na mwanamume umezaliwa ili upite kwenye mfumo huo wa maisha. La kushukuru Mungu ni kuwa umetoka ukiwa salama salimini. Unaona, unatembea, unanusa, unasikia, mikono mizima, ilimradi uko fiti na tayari kupambana tena na maisha ya huku uraiani.”
“Ni kweli,” Kamba aliitika bila ya kuwa hapo kimawazo. Akili yake ilikuwa nyumbani kwake akimkumbuka mkewe na mwanaye, Safi.
Hata hivyo, mara kwa mara mawazo hayo yalikatishwa na sura mpya ya Jiji la Dar es Salaam lenye majengo makubwa yaliyooteshwa kando ya barabara na hivyo kumfanya ajikute akiyakodolea macho na kujiona kuwa yuko katika Tanzania nyingine na Dar es Salaam nyingine. Kwa maana nyingine alichukulia kuwa miaka aliyosota gerezani ni karne nzima.
Waliiacha Keko, wakaipita Kariakoo eneo la Karume, wakaikanyaga Kigogo, Magomeni hadi wakaja kuibukia Mkwajuni Kinondoni. Pale, mtu huyo akakanyaga breki na kumuuliza Kamba, “Njia gani?”
“Niko huko uswahilini, Moscow,” Kamba alijibu huku akifungua mlango.
“Naweza kukupeleka,” mtu huyo alisema, akionesha kumtaka Kamba asiteremke.
Kamba akatulia. Hata hivyo, akashangazwa na ujenzi wa barabara hiyo; hakukuwa na eneo la kuweza kuchepuka na kuingia eneo la Moscow. Mtu huyu alilazimika kuendesha gari hadi Kinondoni ‘A’ kisha akageuza na kuanza kurudi Mkwajuni.
“Nikatie hapa Studio au Mkwajuni,” alimuuliza wakati wakipita eneo la Studio.
“Hata hapa panafaa,” Kamba alijibu huku akiwa hafurahishwi na msaada huu unaozidi kutolewa. Hakuwa radhi kumfunulia kila kitu huyu mtu. Hivyo, baada ya kupita mitaa kadhaa akamwamuru asimame.
Ulikuwa ni mtaa wa pili kutoka ule alioishi Kamba. Hakutaka kumfikisha mlangoni. Utampelekaje mtu hadi mlangoni kwako ilhali humjui? Lifti tu ndiyo kiwe kigezo cha kumkaribisha hadi chumbani? Siwezi kuwa bwege kiasi hicho, alijisemea kimoyomoyo huku akijiandaa kuteremka.
“Kwangu hapafikiki kwa gari,” alimhadaa mtu huyo. “Kama unavyoiona Moscow imekaa shaghalabaghala, hapa kuna mtaa, hapa uchochoro. Kwangu ni ndani, ndani sana msh’kaji wangu.”
“Ok, hakuna tabu,” mtu huyo alisema huku akiingiza mkono ndani ya mfuko wa shati na kuchomoa noti ya shilingi 10,000 na kumpatia Kamba.
“Dah! Poa wangu, umeniwezesha, ” Kamba alishukuru huku akiachia tabasamu kubwa.
“Us’jali,” aliambiwa. “Eeh…” mtu huyo alisema na kusita.
Kamba akamgeukia. Wakatazamana, kimya kikitawala katika vinywa vyao kwa nukta chache. Kisha mtu huyo akafunguka, “Unaweza kuwa na chance kesho tuonane na kuongea kwa kirefu?”
Kamba akafikiri haraka na kusema, “Inawezekana au isiwezekane, kwa sababu hata home sijatia tim mwanangu. Naweza kuwa na jibu sahihi nitakapofika home.”
“Yeah, ni kweli. Ok, us’konde. Fika kwanza home na kama mambo yatakuwa shwari basi fanya juu, chini kesho tuonane.”
Kamba alikunja uso na kuuliza, “Kwani kuna ishu gani hasa?”
“Mojawapo ni kufahamiana,” mtu huyo alijibu. “Lakini pia kuna mengine ya kawaida ya kuzungumza kama wanaume.”
“Kwa hiyo tutawasiliana vipi?”
Mtu huyo alitwaa kijikaratasi na kalamu katika dashibodi, akaandika tarakimu kadhaa za mitandao mitatu ya simu kisha akampatia Kamba, akisema, “Hizo nd’o namba zangu. Nitafute kwenye mtandao wowote utanikuta hewani.”
“Poa,” Kamba aliitika huku akikipachika kijikaratasi hicho mfukoni.
*****
Saa tano asubuhi, mama Safi alikuwa bafuni akioga. Hiyo ilikuwa ni baada ya kumaliza kufanya usafi wa nyumba na kufua. Wakati akiendelea na hicho kilichompeleka bafuni humo, mara akasikia mlango ukigongwa.
Akashtuka na kutulia kidogo. Baada ya ukimya kurejea, akahisi labda masikio yake hayakuwa sahihi, akachota tena maji na kujimwagia. Lakini tena akasikia mlango ukigongwa. Sasa akayaamini masikio yake na akahisi huenda ni rafiki yake, mama Sikudhani wa nyumba ya tatu ndiye aliyegonga mlango.
Mlango ukagongwa kwa mara ya tatu.
“Nakuja, niko bafuni,” alisema kwa sauti ya juu, akidhamiria huyo mgongaji asikie, mgongaji ambaye bado akili yake ilimtuma aamini kuwa ni mama Sikudhani.
Ukimya ukarejea tena. mama Safi akaendelea kuoga lakini sasa akiongeza kasi ili amalize mapema. Hatimaye alimaliza. Akajifuta maji harakaharaka na kutoka. Moja kwa moja hadi mlango mkubwa.
Akiwa ndani ya vazi moja tu la kanga bila nguo nyingine huko ndani, na akiamini kuwa huyo mgongaji wa mlango ni mama Sikudhani, alikizungusha kitasa na kuuvuta mlango.
Hakuwa mama Sikudhani!
*****
Siku ya mwisho kwa Kamba na mkewe, mama Safi kuonana gerezani, Kamba hakumwambia bayana kuwa alibakiza siku chache kuachiwa huru. Wala hakumwambia kuwa lini atakuwa huru. Na alifanya hivyo ili amshtukize.
Akitambua fika kuwa ametumikia kifungo kwa muda mrefu, alijenga hisia kuwa mkewe hataweza kuvumilia kwa kipindi chote hicho. Akiwa ni binadamu, kama binadamu wengine wenye afya njema, wanaoweza kupatwa na hisia na msisimko wa mapenzi, kwa vyovyote vile naye angejikuta akiingia majaribuni na hatimaye kutafuta njia ya kuyatuliza mashetani yatakayokuwa yakimsumbua.
Atatongoza au atatongozwa. Hapo atampata mwanamume, na huenda hatimaye mwanamume huyo akapewa mamlaka ya kuitawala nyumba hiyo hadi kitandani. Hisia hizo zilimtawala Kamba, zikiambatana na kilo lukuki za wivu!
Wivu!
Ndiyo, alikumbwa na wivu kwa kuwa alijua jinsi mkewe, mama Safi anavyojua kulea, malezi ya hadharani na faraghani. Je, kwa hii miaka saba ambayo hawakuwa pamoja, huyo mwanamume atakayebahatika kupewa malezi ya faraghani hatachanganyikiwa kiasi cha kuhamia hapo moja kwa moja?
Ni fikra hizo zilizomfanya asite kumtamkia moja kwa moja mkewe kuwa ni lini ataachana rasmi na maisha ya gereza hilo la Keko. Zaidi, alimwambia, “Vumilia tu mama Safi. Nitatoka na nitarudi tuishi kama zamani na mwan’etu, Safi.”
Ni asubuhi hii ndiyo alikuwa amerudi. Alirudi bila ya kutoa taarifa yoyote kabla. Hapo mlangoni walitazamana kwa sekunde kadhaa. Kamba akaugundua mshtuko na mshangao uliompata mama Safi, mshangao na mshtuko uliompeleka Kamba mbali kimawazo kiasi cha kuibua ule wivu wa mapenzi.
Kwa nini ameshtuka? Kwa nini anashangaa? Kuna mwanamume ndani? Kuna…kuna... Maswali mengi yalimjia kichwani na akajisikia kunyong’onyea.
“Mbona hunikaribishi?” hatimaye alijikakamua kumuuliza. “Au sina nafasi tena ndani ya nyumba hii?”
*****KAMBA KIROBOTO KAREJEA NYUMBANI BAADA YA KUPEWA LIFTI NA MTU ASIYEMJUA. HISIA ZA WIVU KUHUSU MKEWE ZINAMWINGIA. NI KIPI KITAFUATA? TUMEANZIA HAPA. TUKUTANE TENA JUMAPILI IJAYO. KWA ATAKAYEHITAJI RIWAYA NZIMA AJE INBOX*****
https://www.facebook.com/photo.php?...C1bO7nXAzyjZggfKGhShwHfnsQLr2hdrSxYDaWrdN4wm2