RIWAYA : MKONO WA CHUMA.
MTUNZI : ALEX KILEO.
SEHEMU YA SABA.
______________
ENDELEA........
______________
Tom alisimama kwa muda huku akijiuliza maswali mengi, mpenzi wake anashirikiana na yule Dada kichaa au kuna nini kinaendelea?
Tom aliendelea kusimama huku akitafakari, na wazo la mwisho aliloliona linafaa ni kurudi alipotoka, hakuwa na imani na mpenzi wake tena. Tom akageuza na kuanza kurudi kwenye kituo cha basi, ila hata kabla hajapiga hatua tano, alisikia sauti kutoka nyuma ikimuita, wala hajaumiza kichwa kuijua sauti hiyo ni ya nani? Ilikuwa ni sauti ya mpenzi wake, Tom akasimama na kugeuka,
"vipi mbona unaelekea uko wakati nyumbani ni huku?" Mpenzi wake Tom aliuliza huku akishangaa,
"nilikuwa narudi kule juu kuchukua vocha" Tom aliongea huku akitabasamu,
"jamani!!!! Mbona hata pale jirani na kwangu kuna maduka tu" Mpenzi wake Tom aliuliza kwa kudeka,
"OK, basi turudi. Kwema lakini?" Tom aliuliza huku akigeuza njia,
"kwema, nilichelewa kuja kukupokea kwa maana nilikutana na Dada mmoja alikuwa akiulizia nyumba ya kulala wageni mtaa huu, ikabidi nikamuoneshe" Mpenzi wa Tom aliongea huku akichukua begi kutoka kwenye mikono ya Tom.
"huku kuna guest kumbe? umempeleka guest gani sasa?" Tom aliuliza huku lengo lake likiwa ni kupafahamu alipofikia yule Dada kichaa,
"we twende tu nitakuonesha, kwa maana tunapita hapo hapo, ndio njia ya kuelekea kwangu" Mpenzi wake Tom alijibu,
"tunapita hapo hapo??? Kwani hakuna njia nyingine?" Tom aliuliza kwa mshangao kwa maana hakutaka kupita ile njia kwa kuhofia kuwa akipita ile njia, huenda yule Dada kichaa anaweza kumuona,
"hee!!! Mwenzangu mbona hivyo!? Kwani hii njia ina nini mpaka uhamaki hivyo? Au una mwanamke mwingine huku?" Mpenzi wa Tom aliuliza kwa hasira huku chembe za wivu zikiuteka moyo wake,
"sijamaanisha hivyo, ujue nimechoka sana, sasa nilitaka kujua kama kuna njia rahisi zaidi ya hiyo ili niwahi kufika nikapumzike" Tom alijitetea kwa njia hiyo ili kumpoza mpenzi wake huyo,
"twende, njia ni hii hii moja, usijifanye hujui mazingira ya huku" Mpenzi wake Tom aliongea huku akiwa ametangulia mbele.
"sawa twende, mimi sitii neno tena" Tom aliongea huku akimfuata kwa nyuma,
Ukimya ukawazingira, njia nzima hakuna aliyemuongelesha mwenzake. Walitembea katika hali hiyo mpaka walipofika kwenye usawa wa duka moja dogo, mpenzi wake Tom akasimama,
"duka Hilo hapo, si ulikuwa unataka vocha?" Mpenzi wake Tom aliongea huku akimtazama Tom,
"twende bwana, nitarudi baadae kununua, nimechoka sana" Tom aliongea huku akimpita mpenzi wake, hakutaka kusimama,
"khaaa, yaani wewe mwanaume kigeugeu, nilikukuta unarudi barabarani kutafuta vocha, nikakuzuia, sasa tumefika dukani hutaki tena vocha!!" Mpenzi wake Tom aliongea huku akitikisa kichwa,
"na wewe ukishaanzaga kuongea uwa humalizi, nambie umeniandalia chakula gani?" Tom alijaribu kubadili maongezi,
"Wewe twende tu, utachokikuta ndicho utachokula" Mpenzi wake alijibu huku akiwa anasonga mbele,
"alafu, mbona hukunionesha Ile guest uliyosema ipo njia hii?" Tom aliuliza,
"ile pale mbele, Ile yenye rangi ya zambarau" Mpenzi wake alijibu huku akionesha kwa kidole,
"aaha, kuna wateja kweli huku? Maana huku ni uswahilini sana" Tom aliongea,
"wapo wateja wengi tu, wazinifu wenzako ndio wanapapenda huku" Mpenzi wake alijibu,
"basi yaishe, naona hauko sawa" Tom aliamua kutotaka kuuliza maswali kutokana na majibu aliyokuwa akipewa,
"na bora yaishe, maana maswali yako ya kijingajinga, sijui utakuwa lini wewe Thomas?" Mpenzi wake aliongea kwa hasira huku akimtazama Tom aliyekuwa akitabasamu tu.
Ukimya ulitawala mpaka walipofika kwenye chumba ambacho anakaa mpenzi wake, wakaingia na Tom akafikia kitandani na kujilaza,
"nisaidie kuvua viatu basi" Tom aliongea huku akiwa anamuangalia mpenzi wake,
"lazy, yaani hubadiliki tu, kuanzia tabia mpaka matendo" Mpenzi wake aliongea kwa kulalamika,
"basi kama hutaki kunivua viatu, nibandikie maji ya kuoga" Tom aliongea huku akianza kuvua viatu,
"isiwe shida, nabandika tu, jiko lenyewe la gesi, yaani ni chap na kwa haraka" Mpenzi wake aliongea na kuingia jikoni, kisha akachukua sufuria na kuinjika kwenye mtungi wa gesi, kisha akaweka maji ya kutosha.
Muda wote Tom alikuwa akitabasamu tu, alipenda sana namna mpenzi wake anavyoongea, na ndio maana alipenda kumchokoza kila muda ili mradi amsikie tu akiongea.
*********
Ndani ya nyumba ya wageni, Dada kichaa alipoingia tu, kitu cha kwanza alienda mariwatoni, akajiswafi mwili, kisha akarudi na kujifunga shuka. Akakaa kitandani na kuchukua mkoba wake, kisha akatoa laptop ndogo sana, akaiwasha na kupachika moderm pembeni, akaanza kubofya na kisha akapata kitu anachokitaka, ilikuwa ni ramani ya wizara ya katiba na sheria, kisha akasoma pia baadhi ya vipengele kwenye sheria za kimataifa, baada ya hapo akachomoa moderm na kuzima laptop.
Akainuka kwenye kitanda na kutoa kaptula kwenye pochi na kuvaa, akaenda mpaka sehemu ya mapokezi,
"samahani Dada, hapa chakula kinapatikana wapi?" Dada kichaa alimuuliza Dada wa mapokezi,
"chakula gani unachohitaji?" Dada wa mapokezi aliuliza,
"nadhani chipsi inatosha" Dada kichaa alijibu,
"nipe hela, nitamuagiza mtu aniletee, alafu nitakuletea ndani" Dada wa mapokezi aliongea,
"sawa, nitashukuru" Dada kichaa alijibu na kutoa pesa kisha akampatia yule Dada wa mapokezi.
Baada ya hapo, Dada kichaa akarudi ndani kwake na kukaa kitandani, akawa anaandaa mipango yake ya siku inayofuata.
**********
Siku iliyofuata, asubuhi ya saa moja, Dada kichaa alitoka kwenye Ile nyumba ya wageni huku akiwa amevaa baibui yake nyeusi na hijabu pia, na begani alitundika pochi yake.
Alitoka kwa mwendo wa kawaida mpaka kwenye kituo cha daladala na kuingia kwenye daladala moja.
Daladala haikukaa sana kituoni, ikaondoka. Daladala ilivipita vituo viwili, kituo cha Tatu yule Dada akatelemka na kushika njia iliyokuwa inaelekea kwenye jengo refu la ghorofa tano lilikuwa na maandishi makubwa yalioandikwa kwa uzuri kabisa "WIZARA YA SHERIA NA KATIBA".
Dada kichaa akapiga hatua kadhaa mpaka kwenye mlango wa lile jengo na kuingia mpaka eneo la mapokezi na kumkuta mwanaume mmoja aliyekuwa amekaa.
"habari kaka, samahani unaweza kunielekeza ilipo ofisi ya waziri?" Dada kichaa aliuliza,
"ulikuwa na mihadi nae?" Kijana aliuliza,
"hapana, ila nina shida muhimu sana, naomba unisaidie tu" Dada kichaa aliongea kwa upole,
"hapo sina msaada, ungekuwa na mihadi nae ningekusaidia, ila huna mihadi nae, cha kukusaidia ni kukupa barua pepe ya hapa, alafu urudi nyumbani ukaandike maombi ya kuonana na mheshimiwa, alafu kama utakubaliwa, utapangiwa siku ya kuja tena hapa" Kijana aliongea huku akimtazama yule Dada kichaa,
"kaka nisaidie kwa maana nimetoka mbali sana, alafu sina pesa ya kukaa muda mrefu mjini, naomba unisaidie tu ndugu yangu" Dada kichaa aliongea kwa kulalamika,
"Dada nielewe, hii ofisi ina utaratibu wake, fuata maelezo niliyokupa" Kijana aliongea, ila safari hii aliongea kwa hasira baada ya kuona yule Mwanamke anamsumbua,
"kaka hunionei huruma hata ulemavu nilionao?" Dada kichaa aliuliza huku akiutazama mkono wake uliokatika,
"Dada naomba ukae pembeni, kuna watu wengine wanataka kusikilizwa pia" Kaka yule aliongea baada ya kuona watu kadhaa wakiwa wamepanga foleni nyuma ya yule Dada.
Dada kichaa akageuka nyuma na kuona watu kadhaa wakiwa nyuma yake, akasogea pembeni na kuwaacha wasikilizwe, waliposikilizwa wote, Dada kichaa akarudi tena pale kwenye sehemu ya mapokezi,
"kaka hivi nyumbani huna mama? Mbona hunijali mimi mwanamke kama alivyo mama yako?" Dada kichaa aliuliza kwa upole,
"Dada acha usumbufu, kwanza waziri hayupo, yupo ziarani mkoani" Kaka yule alijibu kwa ukali,
"yupo tu, sema unanijibu hivyo kwa kuwa unaona nakusumbua, unataka tu niondoke" Dada kichaa aliongea huku akitabasamu,
"Ni kweli hayupo, yupo mkoani kwa ziara" Dada mwingine aliyekuwepo mapokezi alimsaidia kuongea yule kaka,
"basi mimi nitasubiri hapa mpaka muda wa kufunga ofisi utapofika" Dada kichaa aliongea na kwenda kukaa kwenye makochi yaliyokuwepo eneo hilo.
Alikaa hapo kwa muda wa nusu saa, kabla yule kijana wa mapokezi hajapokea simu na kuanza kuongea huku akimtazama yule Dada, maongezi hayakuwa marefu sana, kisha yule kijana akakata simu na kumtupia jicho yule Dada,
"nenda ghorofa ya Tatu, ofisi namba 31" Kijana wa mapokezi alimwambia yule Dada kichaa, yule Dada akainuka taratibu na kuelekea kwenye ngazi.
"nani amemuita juu?" Dada aliyepo mapokezi alimuuliza yule kijana,
"naibu waziri, alikuwa anatuona kupitia camera jinsi tunavyobishana nae hapa, amenitaka nimruhusu akaonane nae" Kijana wa mapokezi alijibu.
Dada kichaa alipanda mpaka ghorofa husika, akaelekea kwenye mlango namba 31, ulikuwa na maandishi yaliyosomeka "NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA" , Dada kichaa akatabasamu na kugonga hodi, akaruhusiwa kuingia, alipofungua mlango macho yake yakagongana na mwanamke aliyekuwa amekaa kwenye kiti na mbele yake juu ya meza kulikuwa na kibao kinachomtambulisha kuwa huyo ndiye naibu waziri, hakuwa mtu mzima, ila alikuwa ni mama wa miaka 35-40.
"karibu" Naibu waziri aliongea huku akimuonesha kiti cha kukalia yule Dada kichaa,
"asante" Dada kichaa aliongea na kukaa,
"muda mrefu nimekuona ukiwa mapokezi, una shida gani?" Naibu waziri aliuliza,
"nina shida ya kisheria, nahitaji msaada wenu nyinyi kama serikali" Dada kichaa aliongea na kumtazama naibu waziri,
"shida ipi sasa, ongea maneno yote, usiongee nusunusu" Naibu waziri aliongea huku akiendelea kuandika makaratasi yake yaliyokuwa mezani,
"nina mikataba yangu hapa, ambayo ina makubaliano tuliyofanya na makamo wa rais, ila sasa serikali imenigeuka, haitaki kufuata mkataba unachotaka" Dada kichaa aliongea na kuweka mfuko wake mezani, kipindi hicho naibu waziri alishtuka, akaacha kuandika na kumtupia macho yule Mwanamke,
"ebu nione hiyo mikataba" Naibu waziri aliongea huku akimtazama yule Dada kichaa, Dada kichaa akatoa Ile mikataba kutoka kwenye mfuko na kumpatia naibu waziri, naibu waziri akavaa miwani na kuanza kusoma zile karatasi, alisoma kwa muda kidogo, kisha akamtupia jicho yule Dada,
"sasa mbona ukisema ufuate sheria, wewe ndiye utaingia kwenye matatizo, kwa maana mtu uliyefanya nae mkataba tayari alishakufa na pia alikuwa akitakiwa akamatwe kutokana na mauaji ya rais wa kipindi kile" Naibu waziri aliongea,
"hicho sicho kilichonileta hapa, nadhani umesoma mikataba vizuri, hiyo ndio iliyonileta hapa" Dada kichaa aliongea na kutabasamu,
"sawa ondoka, siwezi kukusaidia" Naibu waziri aliongea kwa hasira,
"kwa hiyo unataka kuniambia kuwa rais amekuweka eneo ambalo hustahili? Kwa maana unashindwaje kunisaidia wakati hayo masuala yanahusu wizara yako?" Dada kichaa aliuliza,
"Binti toka nje, ulikuja kuomba msaada na wala sio kunifundisha kazi" Naibu waziri aliongea kwa jazba,
"sasa nakuomba kitu kimoja, andika barua inayoonesha umekubaliana na hii mikataba na pia utie sahihi chini ya barua" Dada kichaa aliongea na kumtazama naibu waziri,
"hivi una kichaa wewe? Ngoja nikuitie security" Naibu waziri aliongea na kupiga simu kuwaita walinzi wa jengo lile, kisha akashusha simu chini, Dada kichaa alikuwa akimuangalia tu huku akitabasamu,
"kabla security hawajafika, roho yako itakuwa imeshafika mbele ya haki'" Dada kichaa aliongea na kucheka, naibu waziri wala hakushtuka, alijua yule Dada hawezi kuwa na silaha kwa maana mpaka ufike ndani ya jengo lile, ujue umekaguliwa ipaswavyo, na kweli alikuwa sahihi, ila kitu ambacho hakukijua ni kuwa yule Dada kila kitu kwake ni silaha.
Wakati naibu waziri akiwa anamtazama yule Dada, alimuona akivuta karatasi moja kutoka mezani na kuishika, pasipo kutegemea, Dada kichaa aliirusha Ile karatasi kwa ufundi na ikachana kidogo koromeo la naibu waziri, naibu waziri akainuka kwa mshtuko na kujishika shingo, alihisi damu zikimvuja, akaanza kupiga kelele za kuomba msaada, Dada kichaa akainuka kwa kasi akiwa na kalamu mkononi, akapiga hatua za haraka za kwenda mlangoni, alipofika mlangoni akageuka kwa kasi na kuirusha Ile kalamu kumuelekea naibu waziri, Ile kalamu ikapenya moja kwa moja kwenye shingo ya naibu waziri, sauti ikakata, damu ikawa inaruka kama kuku aliyechinjwa, kisha Naibu Waziri akapiga magoti na kuanguka kifudifudi, ulikuwa mwisho wa uhai wa naibu waziri, kisha yule Dada kichaa akachovya damu na kidole na kuandika sakafuni, "KAMA HUJUI KAZI YAKO, HAMNA HAJA YA KUENDELEA KUWEPO HAPA" , kisha akainuka, akachukua karatasi zake za mikataba na kuziweka kwenye pochi, akaanza kupiga hatua kuelekea nje, ila hata kabla hajaufikia mlango, mlango ulifunguliwa kwa fujo na kundi la Askari likaingia, wote walikuwa na silaha mkononi. Askari walipoingia tu, wakatupia macho kwenye mwili wa naibu waziri, kisha wote wakamuangalia yule Dada kichaa,
"ametaka mwenyewe" Dada kichaa aliongea huku akitabasamu na pia mkono wake aliunyoosha juu, ishara ya kujisalimisha....
**********ITAENDELEA**********
the Legend☆