Maybach 255
Member
- Jan 25, 2020
- 18
- 31
WAHUSIKA, SEHEMU, MAJINA NA MATUKIO YALIYO KWENYE RIWAYA HII NI KAZI YA SANAA NA SIO HALISI. UFANANI WA AINA YOYOTE NA MAMBO HALISI NI NASIBU.
____________
1
____________
1
Kwenye Jumamosi tulivu; mawingu meusi ya masika yalitanda, mvua ilitishia kunyesha...na matope kwenye njia nyororo iliyopita kati ya kati shamba kubwa la katani yalikuwa yamekauka. Watoto wawili walipita wakisimama kwa dakika kadhaa, kubishana na kisha kuendelea na safari yao iliyokuwa inaonekana kutishiwa na mvua, ambayo walionekana kuto kujali.
"Mel," Maya, mwenye umri wa miaka mitano hivi alimuita yule mtoto aliyekuwa mbele yake, akitembea kwa kasi kidogo.
"We Mel!" Maya aliita kwa sauti ya juu kuliko ya kwanza. Ila yule mtoto alijifanya kutosikia.
"Kaka Mel wee," Maya alijaribu kwa mara nyingine. Mara hii yule mtoto wa mbele yake alisimama na kumgeukia.
"Nini sasa? " Melvin aliuliza. Kwa hasira. " Unashindwa kuwahi? Yaan nyie wasichana mko waviv..."
"Af Mel! Nitamwambia mama, tukirudi nyumban...ashasema, hiyo mbaya."
"Sa huwezi kuwahi..tu kuniita ita...na kushitaki shitaki"
"Ila Mel," kalisimama ka Maya na kupiga tumakofi twake, kama wamama walioko kwenye mabishano. " Kwani sukari si nimekukuta unailamba? Mama ashasema hamna kulamba sukari...we..."
"Haya! Haya, umeshinda..wahisha tumiguu twako," Alisema Melvin akimtazama mdogo wake kama kituko.
"Afu Mel! Ni miguu sio tumig..."
Melvin na Maya, waliendelea kubishana kwa dakika kadhaa, na Maya alipoelekea kushindwa alilia kumlazimu Melvin anyamaze. Ilikuwa kawaida yao kama ilivyokuwa kwa watoto wengine kwenye kijiji cha Chiro. Vutoto vywa kike vuliwaiga mama zao kimatendo na kitabia...baadhi kama, Maya, vuliwaiga hadi kimatamshi.
Mawingu yalizidi kutanda, nao walikuwa kwenye mzozano mwingine.
"...nilikusema? Eeh Eh, jibu kwanza...we ulipo dokoa nyama, nlikusema?" Aliuliza Melvin kimajigambo.
Melvin alimzidi mdogo wake miaka miwili tu, na walifanana katika namna tofauti, kikubwa ni kuwa walipenda kuingia kwenye mizozano na kuona yupi alishinda. Maya alionesha kushindwa hivyo alibaki kimya na kuanza kuondoa tumagugu kwenye ka gauni kake ka zambarau.
Melvin alijihisi vibaya, alidhan labda amezidi mipaka kwa kumsumbua mdogo wake kiasi kile...hivyo alijaribu kubadili mada;
"Wahi basi, sikusumbui tena...mvua itatukuta njiani, barua ya shangazi iloe...aanze kukasirika," alisema Melvin.
Maya aliacha kuondoa magugu kwenye gauni lake, na kumpa mkono Melvin amshike, walikuwa wamekuwa marafiki tena. Ila kulikuwa na kitu hakiko sawa, kulikuweko wanaume wawili waliofanana waliolekea kwao kwa haraka. Walikuwa mapacha. Waliwatazama kwa hali ya kutisha, na kuendana na walivyokuwa wamevaa na walivyowaangalia, Melvin alijua moja kwa moja kuwa hawakuwa wanakijiji wa Chiro na hawakuwa na nia njema.
"Shkamoo," Maya alisalimia, ila hawakuitikia.
"Unawajua..au tu unasalimia salimia?" Alinon'gona Melvin.
"Ila Mel..." Maya alianza, ila hakumaliza sentensi yake. Japo bado alikuwa mdogo, miaka mitano, alihisi kuna kitu hakikuwa sawa. Wale watu waliangaliana na kutabasamu kisha kuongeza kasi wakielekea Mel na Maya walikokuwa.
"Mel..tukimbie," Maya alinong'ona kwa Melvin na bila mahojiano, walianza kukimbia kuelekea waliko toka. Ila walikuwa watoto, na waliowakimbiza walikuwa watu wazima, hivyo hapo hapo...kabla hata ya kupiga hatua ya maana, walidakwa.
Melvin, akiwa mwepesi, alimuuma pua yule pacha aliyekuwa amemshikiria, na kumponyoka. Alienda akipiga mayoe ya kila aina, kama akili yake ya utotoni ilivyomtuma.
"Mel! Mel! Mel! " alisikika Maya akilia kwa mbali, na baada ya muda sauti iliishiria kabisa. Hawakuwa wakimkimbiza, aligundua; na wao walikuwa wakikimbia na Maya. Hivyo aliongeza juhudi na baada ya muda alikuwa nyumbani.
Mama yake, aliyekuwa akianika nguo, alijua papo hapo kuna kitu hakikuwa sawa, hivyo alimkimbilia.
"Poa, Poa baba 'angu, nambie kulikoni? Maya? Maya yuko wapi?" Alimuuliza Melvin ambaye alikuwa akitafuta pumzi.
"Poa, Poa,"
"Watu...pacha...piga...beba Maya...mi...mi...kaja kuita...mi..ponyoka" alijitetea Melvin.
Hakuhitaji kuambiwa mara mbili,
"Baba Mel, Baba Mel!" Mama Melvin aliita huku machozi yakimtoka.
Siku tatu nzima, Maya alitafutwa nyumba baada ya nyumba, ila hakuweza kupatikana, hai au hata mwili, matangazo yalifanywa kwenye redio, mapolisi na wapelelezi waliitwa, ila hapakuweko namafanikio. Maya, akiwa mdogo, miaka mitano, aliibwa, na hakuweza kupatikana.
Tatizo liliokuwa limeukabiri mkoa wa Arusha, tatizo lililokuwakuwa likisika kwenye redio, lilikuwa limekifikia kijiji cha Chiro, na Maya akiwa muathirika wa kwanza.
ITAENDELEA