Riwaya: Jicho la sanaa - I

josephdeo

Member
Nov 23, 2015
95
196
JICHO LA SANAAA
MATAA HEIST
Based on true event

"Wakati adui anahitaji nafasi moja katika kutekeleza mipango yake ya kidhalimu, vyombo vya usalama na ulinzi vinahitaji kila nafasi, kila fursa, kila sekunde, kila dakika, kila saa, kila siku na kila wiki ili kuhakikisha wanamzuia adui huyo kutekeleza azima yake".

Ilikuwa ni Alhamisi ya tarehe 20 April 2020, katika jiji la Mwanza. Siku ilianza vizuri kwani hakukuwa na dalili yoyote ya mvua. Katika miezi hii ambayo iliitwa miezi ya masika. Mvua ni kikwazo kikubwa hasa hasa kwa wakazi wa mijini kwani huwa inakwamisha shughuli nyingi za kuingiza kipato. Kwa siku hii katika jiji hili hali hiyo haikuwepo. Kama mamlaka za hali ya hewa zilivyotoa maelekezo yake siku moja kabla ya alhamisi hii kuwa kutakuwa na jua na mawingu kiasi ndivyo ilivyokuwa.

Jua kama kawaida yake lilianza kuchomoza saa kumi na mbili na dakika arobaini kwa madaha na mwendo wa taratibu. Shughuli za kusukuma gurudumu la maendeleo ya nchi yetu zilikuwa tayari zimekwisha kuanza.

Kila kona na sekta watu walikuwa wakikimbizana na hali ya uchumi wa kati ambao taifa letu liliingia siku chache nyuma.

Asbuhi hiyo katika benki ya NMB linayopatikana katika barabara ya Kenyata huku pia ikiwa makao ya makuu ya benki hiyo kanda ya ziwa. Kulikuwa na shughuli za kila siku zikiendelea lakini siku hii kulikuwa na shughuli ya ziada, shughuli hiyo ilikuwa ni kuhamisha kiasi cha billioni nne Tanzania shilingi kuzipeleka katika tawi la NMB Igoma.

Usafirishwaji huo ulikuwa ni ushafirishaji wa kwanza kufanywa na matawi yanayopatikana jijini hapa. Msafara wa fedha mara zote ulifanywa na benki kuu ya Tanzania. Lakini ilikuwa tofauti na siku hii ambapo tawi lilipewa ruhusa kufanya usafirishaji wa fedha.

Majira ya saa mbili kamili msafara wa gari mbili aina ya Landcruser zilizokuwa na usajili wa SU35490 iliyokuwa ikiendeshwa na Joshua Samweli na SU37200 iliyokuwa ikiendeshwa na Malima Mwenda zilianza kutoka pale. Ndani ya kila gari kulikuwa na askari wawili pia kulikuwa na wafanyakazi wa NMB Kenyata road.

Msafara huo Ulianza kutoka katika benki hiyo na kushika barabara ya Kenyata na kisha kuingia katika mzunguko wa Makongoro Avenue. Walipoumaliza mzunguko ule wakachukua uelekeo wa barabara ya Nyerere. Zilipofika makutano ya mataa ambapo makutano hayo yanaziunganisha barabara za Nyerere, station na Nkuruma zilikutana na kizuizi cha taa za barabarani. Iliwabidi kusimama kama sheria za barabarani zilivyotaka. Hilo likawa kosa kubwa sana kwa gari zile kwani majambazi wakiwa na siraha za kivita SMG, LMG, AK 47 na SHOTGUN yalivamia msafara wa magari hayo yaliyokuwa yakisindikiza pesa Kutoka NMB Kenyata road kupeleka NMB IGOMA BRANCH.

******
Kabla ya tukio gari moja aina ya Corolla ilipaki kituo cha mafuta cha TOTAL kilichopo mtaa wa Kemondo huku kikitazamana na jengo la benki kuu la zamani, kisha ikafata pickup na kupaki nyuma yake. Hakuna ambaye angeweza kubashiri kama magari yale yangeleta hatari kubwa sana masaa machache mbele. Kila mmoja alifuata kilichomleta mjini na kuacha kuchukua tahadhali yoyote juu ya gari zile kwani kulikuwa na gari nyingi ambazo ziliegesha maeneo mbalimbali bila kuwa na sababu yoyote ile.

Barabara ya Station nayo pia kulikuwa na pikipiki kubwa iliyoegesha huku dereva wake akiwa kakaa mita chache kutoka kwenye pikipiki hiyo. Alikuwa kajidhatiti kiasi cha kutia shaka lakini hakuna aliyemjali kwani kila mmoja alikuwa akishughulika na kilichomleta mjini. Wakati wote dereva huyo wa pikipiki alikuwa akifanya mawasiliano huku hakiwa na hali ya mashaka lakini kwa sababu watu walikuwa bize hakuna aliyelijali hilo.

Msafara wa gari zile zilizobeba fedha ulipofika kwenye mzunguko wa Makongoro Avenue ndipo gari ile aina ya Corola ilianza kutangulia mbele na zilipopita gari za benki ndipo pickup ile nayo ilizifuata kwa nyuma. Huku dereva wa piki piki akiiwasha pikipiki yake na kuiacha ikiunguruma huku yeye akiwa juu yake.

Wale jamaa waliokuwa kwenye gari la mbele la corola walipofika kwenye makutano ya mataa na taa za barabarani zilipozuia magari yanayotokea barabara ya Nyerere kutokea kwenye mzunguko wa Makongoro Avenue. Ndipo walipoanza kuinyeshea risari gari ya mbele SU35490 hadi likakosa uelekeao na kwenda kuigonga kwa nyuma gari ya BENZ T560 DCU. Gari ya nyuma kwenye msafara SU 37200 baada ya kuona hayo ikataka kuchepuka uelekeo wa barabara ya stesheni. Hii ikawa kosa kubwa sana kwani yule aliyekuwa juu ya pikipiki aliipiga risasi nyingi sana kuliko hata ile ya kwanza hali iliyomfanya dereva kukosa uhimili wa gari na kwenda kujikita kwenye taa za barabarani.
Kila gari ilikuwa imebeba pesa kiasi cha Bilioni 2 Tanzania shilingi.

Majambazi waliokuwa kwenye pickup walishuka kwa kasi huku wakirusha risasi hewani na kusababisha wananchi kuhamaki na kushikwa na bumbuwazi wasijue kipi cha kufanya wakalisogelea na kuanza kupakua makasha ya fedha kwenye gari ya nyuma na wale wa kwenye corola nao walianza kupakua kwenye gari ya mbele na kumuacha yule wa kwenye pikipiki hakihakikisha usalama.

Wakati upakuaji unaendelea jambazi aliyekuwa akilinda usalama alionekana ana usongo sana alikuwa anazidi kupiga risasi hali iliyowafanya watu wayaache magari na kuanza kutafuta maeneo ya kujificha. Kila mmoja alikuwa akikumbushia ni kwa kiasi gani miguu yake bado ina uimara wa kuhimili mbio zisizokuwa na mshindani. Askari waongoza magari waliokuwa zamu asbuhi hiyo walibaki na mshangao kwani tukio lile lilikuwa la kushitukiza na watekelezaji walikuwa wameliratibu vyema. Hata wao pia waliwaza wanawezaje kutoka eneo hilo ambalo liligeuka kiwanja cha kivita ndani ya mda mfupi.

Katika Maaskari walikuwepo eneo la tukio, kuna mmoja aliitwa Sajenti Adam Mashimbi. Naye alikuwa kwenye mshangao sana juu ya hali ile ya ghafla katika nchi iliyojaa amani. Kwa weledi na alivyoipenda kazi yake hakuridhika kuaibishwa namna ile. Askari huyu alikimbia kwenye kituo kidogo cha polisi pale PAMBA akatoa taarifa juu ya tukio kisha akachukua SMG na kurudi tukioni akawakuta majambazi wanamalizia kushusha pesa na wanaondoka.

Afande Adam akaanza naye kuwarushia risasi majambazi huku kila mara akijikinga ndani ya mtaro wa maji machafu na kufanya nguo zake nyeupe zisitamanike kwa uchafu. Alifanikiwa kuwapotezea muda majambazi wale lakini walifanikiwa kuondoka.

Hadi majambazi wanaondoka eneo la tukio tayari yalikuwa wamemuua askari mmoja D3866 PC Mwita Jonas kutoka kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) cha jijini Mwanza na mfanyakazi wa NMB NSSF plaza Agnes Solomoni. Wote hawa walikuwa kwenye ile gari ya nyuma iliyotaka kuchepuka kuingia barabara ya stesheni. Askari wengine watatu walijeruhiwa.

Umakini, umahiri katika kurusha risasi na pia jinsi walivyoondoka eneo la tukio ndio sababu kubwa ya mashuhuda waliokuwepo eneo la tukio kuamini kuwa wale hawakuwa majambazi wa kawaida bali ni askari au watu wenye mafunzo makubwa na pia lazima walifanya majaribio kadhaa kabla ya tukio wakiwa na mipango yote A na B mpaka C ikiwa ingehitajika.

Mara baada ya kuzipata pesa majambazi wale walijigawa pale pale. Yule wa kwenye pikipiki alitoka eneo la tukio na kwenda mpaka Isamilo. Wengine waliondoka na magari yao kwa kutumia barabara ya Nyerere na kwenda kizitelekeza Kisesa mitaa ya Kanyama. Baada ya hapo walijigawa ili kuipoteza helicopter ya polisi iliyokuwa ikiwafuatilia huku wakiyateketeza magari waliyokuwa nayo kuondoa ushahidi.

Wawili kati yao walipitia njia ya Nyamongoro na kuishika Buswelu na baada ya hapo walipitia Kiseke na kuja kuishika Sabasaba na baadae kwenda Airport. Wawili wengine walipitia Nyamongoro ya chini ambapo kuna viwanja vya nanenane na kisha kuishika kishiri na baadae mahina na hapo wakaja mpaka bendera tatu na kuitafuta Bugarika na kisha Bugando wakaishia hapo.
Tukio lile lilikuwa limetekelezwa na watu walikuwa mahili sana kwani mita chache kutoka pale kulikuwa na ofisi za usalama wa taifa kanda ya Nyamagana. Pia mita chache kulikuwa na kituo cha kati cha polisi pia mita chache kulikuwa na kituo kidogo cha polisi Pamba. Achana na utitiri wa benki ambazo zote zilikuwa zikilindwa na askari wenye silaha za moto. Lakini bado wavamizi wale walifanikiwa kuondoka tena wakiwa sio peke yao bali na lundo la fedha.

*******
Wakati haya yote yanatokea aliyekuwa kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Deusi Kalumuna alikuwa njiani safarini kwenda Shinyanga na taarifa hizi zilipomfikia aligeuza gari haraka sana kurudi eneo la tukio ambapo alipofika hakuamini kama mkoa wake unaweza kuwa na majambazi wa aina hiyo. Mshango ulikuwa dhahiri katika sura yake hakuamini kuwa tukio la namna hiyo linaweza kutokea katikati ya mji tena sehemu ambayo ina kituo kikubwa cha polisi mkoa na watekelezaji wakaondoka pasipo kufahamika walipitia wapi?.

Mara moja kamada Deusi aliamuru vikosi vyote vilivyo chini ya jeshi la polisi viingie kazini ili kuwatafuta majambazi hao kwani waliamini bado wapo jijini hapo. Pia waliimarisha ulinzi njia zote ambazo zilikuwa zinatoka nje ya jiji hili kwa maji, anga na barabara. Bahati mbaya hawakuwa na pa kuanzia zaidi ya kuwa na majeruhi wasioweza kujitambua baada ya kushambuliwa kwa risasi.

INAENDELEA

Muandishi:- Joseph .D. Migini
Call/txt:- +255766604683
Josephdeo70@gmail.com

Kwa maoni na ushauri nifuate kwenye mitandao ya kijamii kama:-
Fb:- josephdeo
Insta:- falsafa70
Twitter:- falsafa70
 
Unawezakupata muendelezo wa riwaya hii kupitia group hili la WhatsApp bure kabisa...

Au tuma ujumbe kwenye namba hii ili iwe tukuunge... +255 655 500 516
 
Inapendeza kuona familia hii ya wapenzi wa riwaya inakua kila iitwapo leo nawe ujachelewa kujiunga nayo...

Gharama ni wewe pamoja na app yako ya WhatsApp tu hakuna kingine. Bofya hii link

Pic_1659680804512.jpg
 
Riwaya:- JICHO LA SANAA
MATAA HEIST
(Based on true even)
Muandishi:- Joseph .D. Migini
Call/txt:- +255655500516
Josephdeo70@gmail.com

#02

Tulipoishia…
Sehemu ya kwanza ilishia pale ambapo kesi hii imeamishwa toka kwenye mikono ya askari polisi. Mpaka kwa afisa usalama wa taifa. Ni nani aliyekabidhiwa kazi hiyo!!...wasifu wake ukoje.. endelea hapa ili kuyafahamu hayo….

Tuendelee…

Naitwa Joseph Deogratius Migini mzaliwa wa Mabatini, jijini Mwanza. Makuzi yangu yote yamekuwa katika jiji hili lililojaa miamba kila kona kiasi cha kuwa na jina la utani la jiji la miamba (the rock city). Natokea kwenye familia ya kipato cha kati ni mtoto wa pekee katika familia ya mzee Deogratius Migini.

Nilipomaliza darasa la saba mapenzi yangu ya kutaka kulitumikia jeshi la polisi ndipo yalipoanza kuingia kwenye ubongo huku yakipewa kibali ndani ya moyo wangu. Mapenzi hayo yalichochewa kwa kiasi kikubwa na kambi ya polisi iliyopo Mabatini. Mara zote tulikuwa tukishuhudia gwaride na mazoezi ya maaskari hao katika viwanja vya kambi hiyo.

Hali hiyo ilipelekea mpaka kukataa kujiunga na elimu ya kidato cha tano licha ya kupata nafasi hiyo. Badala yake nikachagua kujiunga na chuo cha mafunzo ya jeshi la polisi, Moshi.
Nilipomaliza mafunzo yangu nilipangiwa kituo cha kazi ambapo nilipangiwa kituo cha polisi Igogo, jijini Mwanza. Nilifanya kazi kwa weledi mkubwa katika idara ya upelelezi wa makosa ya jinai na hapo nilifanikisha kukamilisha kwa upelelezi wa makosa ishiri na tatu ndani ya mwaka wa kwanza kazini.

Hali hii ilinifanya kuamishwa kutoka kituo kidogo cha Igogo na kupelekwa kwenye kituo cha kati (central).
Niliipenda sana kazi yangu ya kipolisi kiasi cha kutokuelezea vyema na nikaeleweka, kulitumikia jeshi la polisi kwangu ilikuwa ni zaidi ya kutimiza ndoto zangu au kuifanya ndoto kuwa kweli.

Mwaka wa pili wa kazi yangu nao ulikuwa mzuri sana kwani juhudi na maarifa vilifanya niendelee kufanikisha kesi nyingi sana ambazo upelelezi ulikuwa unaendelea. Hali hiyo ilinifanya nikawa miongoni mwa askari ambao walichaguliwa kwenda kwenye mafunzo maalumu katika kituo cha kijeshi huko nilipata mafunzo ya kijeshi na ukakamavu.

Pia nilijifunza namna ya kusoma ramani katika uwanja wa kivita, kuboresha ulengaji wa shabaha na kuzielewa vyema silaha mbalimbali awali yalikuwa kama mafunzo ambayo nilipata katika jeshi la polisi lakini haya yalikuwa na ziada nyingi. Mateso pia yalikuwa mengi kwani kulikuwa na mazoezi makali mno ya viungo na uvumilivu.

Baada ya kumaliza mafunzo hayo yaliyochukua taklibani miezi sita na kupata ufaulu mzuri nilipata nafasi ya kuingia katika mafunzo ya kuwa afisa wa usalama wa taifa. Nilipewa nafasi katika idara hiyo ambayo iliundwa kwa sheria za bunge namba 15 ya mwaka 1996. Iliyo sainiwa na rais wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa tarehe 20 januari 1997.

Pamoja na idara hii kusajiliwa kisheria mwaka 1996, lakini ilkuwepo tangu wakati wa utawala wa kikoloni chini ya ofisi ya Gavana wa Tanganyika. Baada ya Uhuru mwaka 1961 ilihamishiwa ofisi ya Rais.
Sikufahamu ni vigezo gani mkurugenzi wa idara hiyo nyeti waliviona kwangu lakini nilipopewa taarifa hizi nilifurahi mno kwani nami nilikuwa miongoni mwa kundi kubwa la watanzania ambao wanapenda kuitumia nchi yao hasa katika namna ya kuilinda.

Sikupaswa kumwambia mtu taarifa hizi kulingana na usiri wa idara ya usalama wa taifa hivyo moja kwa moja nilijiunga na chuo cha maafisa usalama ambacho kipo nje ya jiji la Dar-es-salaam.

Mafunzo katika chuo hicho yalianza kwa kufundishwa namna ya kupambana pasipo kuwa na silaha (unarmed combat). Hapa nilifundishwa namna ya kuutumia mwili wangu katika kupambana na adui na kujilinda au kulinda nchi yangu. Mafunzo haya hayakuwa sawa na yale ambayo nilipewa nikiwa katika chuo cha jeshi la polisi au katika kituo cha kijeshi haya yalikuwa yameboreshwa sana.

Nilijifunza judo, karate, kung-fu, taikondo pia hapa nilijifunza sehemu ambazo ni dhaifu katika mwili wa binadamu ambazo mimi naweza kuzitumia ili kumzuia au kumdhibiti adui.

Nilipomaliza hatua hiyo ya mafunzo nikaingia kwenye mafunzo halisi ya ushushushu hapa nilijifunza mbinu za kukusanya taarifa za kiusalama kwa siri na kuzichambua kisha kuzifanyia kazi. Nilijifunza ushushushu wa ndani na nje ya nchi katika hilo niliweza kufunzwa na kuzifahamu vyema shughuli za adui. Yaani ujasusi (espionage), uzandiki (subversion), hujuma (sabotage) na ugaidi (terrorism). Vilevile, nilijifunza mbinu za kunasa mawasiliano (bugging), ufuatiliaji wa siri (surveillance), jinsi ya kupata watoa habari (recruitment of sources) na jinsi ya kuwamudu, ikiwa ni pamoja na jinsi ya kuwamwaga (kuachana nao) pale wanapopoteza umuhimu.

Jambo jingine ambalo kama mwanafunzi katika chuo cha usalama wa taifa tulifundishwa muda wote ni kitu kinachofahamika kama constant vigilance of an officer, yaani afisa usalama wa taifa anapaswa kuwa macho muda wote, huku akitambua kuwa uhai wa taifa lake upo mikononi mwake muda wote.

Pengine tafsiri ya kanuni hiyo ni kujitambua muda wote. Kutambua dhamana aliyonayo afisa usalama kwa taifa. Kadhalika, mafunzo yale yalihusisha pia kujenga na kuimarisha matumizi ya hisia ya sita.
Binadamu sisi wa kawaida huwa wanakuwa na hisia tano: kuona kwa kutumia macho, kusikia kwa kutumia masikio, kunusa kwa kutumia pua, ladha kwa kutumia ulimi na kuguswa (touch) kwa kutumia ngozi.

Hisia ya sita ni kitu cha zaida ya hivyo vitano. Ni vigumu kueleza katika mazingira ya kawaida ila labda kwa kifupi ni ule uwezo wa kwenda mbali zaidi ya uwezo wa kawaida wa hisia. Tunaweza kurahisha zaidi kwa kusema kuwa hisia ya sita humuwezesha jasusi kuamini au kutoamini pale inapopaswa kuamini au kutoamini, kutambua hatari hata bila ya kupewa tahadhari.

Pia nilifundishwa namna ya kutongoza, samahani hapa sisemei kutongoza wanawake japo ilikuwepo lakini nilichojifunza ni kutongoza ili niweze kupata taarifa ambazo nilizihitaji au zilizohitajika. katika muda wote wa mafunzo tulihamasishwa kuhusu uzalendo, thamani ya nchi yatu, umuhimu wa kuilinda muda wote, umuhimu wa taaluma hiyo katika ustawi na mustakabali wa taifa letu.

Siku ambayo iliokuwa kwenye matamanio yangu toka siku ya kwanza naingia katika chuo cha mafunzo ya kijeshi (Tanzania military academy), Arusha kisha chuo cha usalama wa taifa, Dar-ea-salaam. Ilikuwa imetimia leo. Nilikuwa nahitimu na kuwa afisa wa usalama wa taifa mwenye cheo cha field Officer huku kifuniko changu kikiwa ni askari polisi.

Kulikuwepo na mkurugenzi wa usalama wa taifa bwana Kelvin John, pia kulikuwepo na rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania ambaye sisi wanausalama tulimtambua kama "sponsor". Siku hii tuliapa kwa kuishika bendera ya Tanzania huku ikiwa mkabala na katiba huku tukiweka viapo vya kuitumikia nchi hii kwa uwezo wetu wote. Pia tuliapa kutotoa siri zozote za idara na nchi. Kiapo ambacho tuliapa kiliwa kizito mno kuliko hata kile ambacho niliapa wakati nahitimu na kuwa askari polisi.

Sherehe hii ilikuwa ya siri kiasi cha kutokaribisha ndugu, jamaa na marafiki kama ilivyo kwa tamaduni ya sherehe zote. Huku tukila viapo vikali ambavyo viliogopesha hata kuvisema hadharani. Mara baada ya kumalizika kwa sherehe hizo tuliruhusiwa kurudi nyumbani baada ya miaka miwili ya kutokuwa nyumbani pia kutokuwa hata na mawasaliano na nyumbani sasa nilipewa ruhusa ya kurudi nyumbani. Ilikuwa furaha kubwa kwenye nafsi yangu kurudi tena nyumbani, sehemu ambayo niliipenda nayo ilinipenda vyema….

Hiyo ni historia kwa ufupi juu ya afisa ambaye amepewa kazi ya kutuatilia kesi hiyo. Je, analo ambalo polisi walilishindwa..usiwe na shaka salia nasi kuyafahamu hayo na mengine aliyonayo…

NB: Unakaribishwa kwa maoni na ushauri. Pia vyema kama ukitusaidia kuwafikia wengine kwa kusambaza link ya group letu. Ambalo ni bure kabisa kujiunga..

 
Riwaya:- JICHO LA SANAA
MATAA HEIST
(Based on true even)
Muandishi:- Joseph .D. Migini
Call/txt:- +255655500516
Josephdeo70@gmail.com

#05

Tulipoishia…
Sehemu ya nne ilishia pale ambapo tayari tumekwisha fahamu wasifu wa afisa huyu ambaye ndie haswa anakwenda kukabidhiwa kesi hii..hivyo tuendelee kidogo kumhusu afisa huyu.

Tuendelee…

Mazingira ya nyumbani niliyakuta kama nilivyoyaacha miaka miwili na nusu nyuma. Niliamka asbuhi na mapema kisha nikaanza kufanya mazoezi ya viungo na nilipohakikisha kuwa mwili umekuwa na jasho la kutosha, nilijimwagia maji na kupata kifungua kinywa baada ya hapo nilijipumzisha huku nikiwa na mawazo ya ipi itakuwa kazi yangu ya kwanza kama afisa usalama wa taifa.

Nilikuwa na mashawasho wa kufanya kazi kwani nilipenda sana kuwajibika hasa hasa kwenye kuutafuta ukweli na kulisaidia taifa langu.

Upelelezi ni kazi ambayo ilkuwa inaniacha na furaha ya moyo na niliifanya kwa hali na moyo wangu wote. Baada ya kuchoka kufikiria niliangalia sehemu ya kwenda ili nipoteze mda na kidogo kupata mawazo tofauti na kazi hapo wazo la kwenda kwa rafiki ya Emmanuel lilipata uungwaji mkono mkubwa kwenye ubongo wangu na moyo wangu ulinisukuma kulitekeleza.

Taratibu kwa mwendo wa kichovu nilitoka nje ili nikatafute usafiri wa bodaboda. Nikiwa nje ya nyumba niliiona gari ya mzee wangu aina ya Toyota Satrlet ikiwa iko kwenye maegesho ya nyumbani.

Nilirudi ndani na kumuuliza mama.
"hivi ili toroli bado linafanya kazi?". Ulikuwa ni mzaha juu ya gari ya baba ambayo mara zote nilikuwa nikiita toroli kwa sababu ya uzee wake.

"ndio lakini sharti litiwe mafuta". Alijibu mama kejeli ambazo mimi ndio nilizitoa.

"sawa hilo wala lisikupe shida, nipe ufunguo".

Mama aliniletea ufunguo na mimi niliingia ndani ya gari na kuliwasha nikakuta mafuta yamo na gari likiwa zima kabisa. Nilimsifu baba kwa kuwa mtunzaji mzuri kwani gari hilo alilimiliki toka niko kidato cha nne. Nikiwa kwenye gari nilifungulia redio na kuweka kituo cha RADIO FREE AFRICA.

Nilikutana na habari za watangazaji wakijadili juu ya tukio la wizi ambao ulitokea wiki moja nyuma. Ambalo walilipachika kuwa wizi wa muongo kwa kuwa hakukuwahi kutokea wizi wa namna hiyo wa kuibwa kwa pesa nyingi kwa wakati mmoja.
Nilisikiliza kwa makini sana watangazaji wale wa redio namna ambavyo walikuwa wakilichambua tukio lile la wizi.

Nilipuuzia mara baada ya kusikia kuwa askari polisi wako kazini wakiendelea na upelelezi. Nililiamini sana jeshi la polisi kwa weledi wake wa kiutendaji hivyo niliamini kuwa hao majambazi ni lazima wapatikane labda wawe kuzimu na wasiwepo kabisa katika uso wa ulimwengu huu.
Kwa mwendo wa taratibu niliendelea kuendesha gari huku nikiwa makini sana kutazama jeografia ya mji huu ambao niliupoteza kwa mda wa miaka miwili na nusu.

Taratibu mpaka nikaingia kwenye nyumba za askari wa Igogo na kwenda mpaka block A alipokuwa hakiishi Emmanuel. Bahati ikawa kwangu kwani nilimkuta Emma tena na familia yake kwa ujumla, wote walinipokea kwa furaha sana. Ukaribu wangu na Emma ulikuwa umevuka viwango vya marafiki na kuingia kwenye undugu kabisa japo hatukuchangia damu wala jina la ukoo.

Stori za hapa na pale zilichukua mkondo wake na tuliongea mpaka wakati wa chakula cha mchana ambapo mke wa Emma aliandaa chakula tukala na baada ya hapo tulitoka nje mimi na Emma kwa mazungumzo yaliyotuhusu.

"na hili toroli bado zima?". Emma aliniuliza mara baada ya kuiona gari ya mzee ambayo nimekuja nayo pale kwake.

"ndio bhana hata mimi imenishangaza kuikuta bado inafanya kazi". Nilimjibu Emma.

"alafu unajua ulitoweka ghafla ulikwenda wapi? Mwanangu". Lilikuwa swali la Emma ambalo aliliuliza kimtego sana baada ya mimi kumpa mwanya wa kuliuliza kwa majibu niliyotoa juu ya gari ya mzee.

Lakini kama kanuni yangu ya kwanza inavyonieleza juu ya usiri na kutomuamini yoyote basi nilimjibu.
"nilienda kuongeza elimu kidogo kaka siunajua tunapaswa na sisi kula vizuri kama wakubwa". Lilifuata cheko kati yetu na tukiwa katikati ya cheko lile mlango uliotazamana na mlango wa Emma ulifunguliwa na alitoka binti mzuri ambaye alifanikiwa kuyashika mawazo yangu kwa mda juu ya kufikiria uzuri wake.

Alikuwa binti ambaye ana urefu wa wastani huku akitembea kwa mwendo wa paka (catwalk) kuja upande wetu. Sura ya upole uliodhihirisha ustaarabu aliokuwa nao, umbo la kiafrika ama unaweza kuita (bantu figer). Nilimtazama mpaka pale Emma aliponirudisha kwenye maongezi yetu.
"ulienda kusomea nini?".

"achana na hayo kwanza huyu ni nani?". Nilimkwepa Emma kwa swali lake japo nilihitaji sana kumjua binti yule ila zaidi sikutaka kulijibu swali la Emma.

"huyo ni kamishina msaidizi (ACP) kaka".

"kamishina msaidizi anakaa kota?!". Mshango ulinitoka ambao ulikuwa na sababu mbili moja ikiwa ni kuendeleza zile stori na pili ni mshangao halisi wa kwanini kamishina msaidizi akae sehemu ambayo wanakaa askari wa kawaida.

"uenda kaamua kukaa hapa kaka, au anamfanyia mtu uchunguzi. Mimi mwenyewe taarifa hizo nimepewa na mkuu wa kituo hichi". Emma aliingia kwenye mtego ambao niliutegesha wa kutokuuliza juu ya sehemu niliyokuwa au kile ambacho nilikuwa nasomea.

"sawa, nitampataje sasa mimi?". Nilimuuliza Emma swali ambalo liliendeleza nia yangu ya kumtoa kwenye mazungumzo ya awali.

"daaah! Hapo ndio ngumu ningesema nikuchukulie namba sema wife atazingua sana si, unamjua ma wivu yake". Emma alizidi kuingia sehemu ambayo nilimuingiza.

"kwani mkuu wa kituo hapa hana namba zake. Kama anazo taarifa zake tena nyeti kama hizo unafikiria atakosa namba zake". Nilimwambia Emma aliyeonekana kujifikiria kwa muda na kisha kuniambia.

"nitamuuliza kama anazo alafu kama atanipa nitakutumia wewe. Sawa!"

"sawa, nitashukuru kwa hilo kaka".

"usijali wewe ni ndugu yangu"
Tukiwa bado tupo pale mimi na Emma na tukiendelea na mazungumzo mengine simu yangu iliingia ujumbe mfupi niliusoma.

Ujumbe ule ulinitaka mara moja niwasili kwenye ofisi za usalama wa taifa kanda ya Nyamagana zilizokuwa mitaa ya Makoroboi. Ilinibidi kumuaga Emma na mimi kuwasha gari kurudi mjini. Ilinichukua dakika kumi kufika katika geti la kuingia kwenye ofisi hizo ambapo nilitaja namba yangu ya kazi na kuruhusiwa kuingia ndani…..

Afisa huyu mpya ameitiwa Nini kwenye ofisi za kanda. Je, ndio rasmi anakwenda kukabidhiwa kesi hiyo ya MATAA..kwa hayo na mengine mengi na kusihii kaa nasi..

NB: Unakaribishwa kwa maoni na ushauri. Pia vyema kama ukitusaidia kuwafikia wengine kwa kusambaza link ya group letu. Ambalo ni bure kabisa kujiunga..
 
Back
Top Bottom