RASIMU ya Katiba

2015ready

JF-Expert Member
Feb 15, 2011
364
250
RASIMU YA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO
WA TANZANIA
________

YALIYOMO
______
Ibara Kichwa cha Habari
UTANGULIZI

SURA YA KWANZA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SEHEMU YA KWANZA
JINA, MIPAKA, ALAMA, LUGHA NA TUNU ZA TAIFA

1. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
2. Eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
3. Alama na Sikukuu za Taifa.
4. Lugha ya Taifa na lugha za alama.
5. Tunu za Taifa.


SEHEMU YA PILI
MAMLAKA YA WANANCHI, UTII NA HIFADHI YA KATIBA

6. Mamlaka ya wananchi.
7. Watu na Serikali.
8. Ukuu na utii wa Katiba.
9. Hifadhi ya utawala wa Katiba.

SURA YA PILI

MALENGO MUHIMU, MISINGI YA MWELEKEO WA
SHUGHULI ZA SERIKALI NA SERA ZA KITAIFA
10. Malengo Makuu.
11. Utekelezaji wa Malengo ya Taifa.
12. Sera ya Mambo ya Nje.
SURA YA TATU
MAADILI NA MIIKO YA UONGOZI NA UTUMISHI WA UMMA

SEHEMU YA KWANZA
MAADILI YA UONGOZI NA UTUMISHI WA UMMA
13. Dhamana ya Uongozi wa Umma.
14. Kanuni za Uongozi wa Umma.
15. Zawadi katika Utumishi wa Umma.

(b) Mkurugenzi wa Uchaguzi

195. Uteuzi wa Mkurugenzi wa Uchaguzi.
196. Majukumu ya Mkurugenzi wa Uchaguzi.

SEHEMU YA TATU
USAJILI NA USIMAMIZI WA VYAMA VYA SIASA

(a) Vyama vya Siasa

197. Usajili wa vyama vya siasa.

(b) Msajili wa Vyama vya Siasa

198. Uteuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa.
199. Wajibu wa Msajili wa Vyama vya Siasa.

SURA YA KUMI NA TATU
TAASISI ZA UWAJIBIKAJI

SEHEMU YA KWANZA
TUME YA MAADILI YA UONGOZI NA UWAJIBIKAJI

200. Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji.
201. Uteuzi na sifa za Wajumbe.
202. Kamati Maalum ya Uteuzi.
203. Majukumu ya jumla ya Tume.
204. Muda wa kukaa madarakani kwa Mjumbe wa Tume.
205. Kuondolewa madarakani kwa Mjumbe wa Tume.
206. Uhuru wa Tume.
207. Uwezeshaji wa nyenzo na rasilimali.

SEHEMU YA PILI
TUME YA HAKI ZA BINADAMU

208. Tume ya Haki za Binadamu.
209. Kamati ya Uteuzi.
210. Kazi na majukumu ya Tume.
211. Muda wa kukaa madarakani kwa Kamishna wa Tume.
212. Kuondolewa madarakani kwa Kamishna wa Tume.
213. Uhuru wa Tume.
214. Uwezeshaji wa nyenzo na rasilimali.

SEHEMU YA TATU
MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI

215. Uteuzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
216. Sifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
217. Kazi na majukumu ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
218. Muda wa kukaa madarakani kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali.
219. Kuondolewa madarakani kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali.
220. Uwezeshaji wa nyenzo na rasilimali.

SURA YA KUMI NA NNE
MASHARTI KUHUSU FEDHA ZA JAMHURI YA MUUNGANO

(a) Mfuko Mkuu wa Hazina na Fedha za
Jamhuri ya Muungano

221. Mfuko Mkuu wa Hazina.
222. Masharti ya kutoa fedha za matumizi katika Mfuko Mkuu wa Hazina.
223. Utaratibu wa kuidhinisha matumizi ya fedha zilizomo katika Mfuko Mkuu wa
Hazina.
224. Utaratibu wa kuidhinisha matumizi ya fedha kabla ya Sheria ya Matumizi ya
Fedha za Serikali kuanza kutumika.
225. Mfuko wa matumizi ya dharura.
226. Mishahara ya baadhi ya watumishi kudhaminiwa na Mfuko Mkuu wa Hazina.

(b) Deni la Taifa na Mikopo ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano

227. Deni la Taifa.
228. Mamlaka ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano kukopa.
229. Mamlaka ya Serikali za Nchi Washirika kukopa.
230. Masharti ya kutoza kodi.

(c) Vyanzo vya Mapato ya Serikali ya Jamhuri ya
Muungano na Ununuzi wa Umma

231. Vyanzo vya mapato vya Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
232. Ununuzi wa umma.

(d) Benki Kuu ya Jamhuri ya Muungano

233. Benki Kuu ya Jamhuri ya Muungano.
234. Benki za Serikali za Nchi Washirika.

SURA YA KUMI NA TANO
ULINZI NA USALAMA WA JAMHURI YA MUUNGANO

(a) Ulinzi na Usalama wa Taifa

235. Usalama wa Taifa.
236. Vyombo vya Ulinzi na Usalama wa Taifa.
237. Kuanzishwa kwa Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa.
238. Majukumu ya Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa.

(b) Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania

239. Kuanzishwa kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.
240. Uteuzi wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi.
241. Madaraka ya Amiri Jeshi Mkuu.
242. Tume ya Utumishi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.(c) Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Muungano

243. Kuanzishwa kwa Jeshi la Polisi.
244. Misingi ya utendaji wa Jeshi la Polisi.
245. Uteuzi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi.
246. Majukumu na uhuru wa Mkuu wa Jeshi la Polisi.
247. Tume ya Utumishi wa Jeshi la Polisi.

(d) Idara ya Usalama ya Jamhuri ya Muungano

248. Kuanzishwa kwa Idara ya Usalama wa Taifa.
249. Uteuzi wa Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa.
250. Usalama katika Nchi Washirika.

SURA YA KUMI NA SITA
MENGINEYO

251. Utaratibu wa kujiuzulu katika utumishi wa umma.
252. Masharti kuhusu kukabidhi madaraka.
253. Baadhi ya watumishi wa umma kutoshika nafasi za kisiasa.
254. Ufafanuzi.
255. Jina la Katiba na kuanza kutumika.
256. Kufutwa kwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977
Sura ya 2.

SURA YA KUMI NA SABA
MASHARTI YATOKANAYO NA MASHARTI YA MPITO

SEHEMU YA KWANZA
MASHARTI YATOKANAYO

257. Matumizi ya baadhi ya masharti ya Katiba.

SEHEMU YA PILI
MASHARTI YA KIKATIBA NA SHERIA ZA NCHI

258. Kuendelea kutumika masharti ya Katiba.
259. Kuendelea kutumika sheria za nchi.

SEHEMU YA TATU
UTUMISHI WA UMMA
(a) Serikali ya Jamhuri ya Muungano

260. Kuendelea kuwepo kwa Rais madarakani.
261. Kuendelea kuwepo kwa Makamu wa Rais madarakani.
262. Kuendelea kwa Waziri Mkuu, Mawaziri na Naibu Mawaziri.

(b) Watumishi wa Umma

263. Kuendelea kwa utumishi wa umma.


SEHEMU YA NNE
BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO

264. Kuendelea kwa Ubunge na Uongozi wa Bunge.
265. Kuvunjwa kwa Bunge.

SEHEMU YA TANO
MAHAKAMA YA JAMHURI YA MUUNGANO

266. Kuendelea kwa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu.
267. Kuendelea kwa mashauri yaliyopo mahakamani.

SEHEMU YA SITA
MASHARTI YA MPITO

268. Muda wa Mpito.
269. Utekelezaji wa masharti ya Katiba Mpya.
270. Kamati ya kusimamia Muda wa Mpito.
271. Kufutwa kwa Masharti Yatokanayo na Masharti ya Mpito.
UTANGULIZI

KWA KUWA, sisi wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua rasmi
na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayoheshimu na kuzingatia misingi ya utu,
uhuru, haki, usawa, udugu, amani, umoja na mshikamano katika nyanja zote za maisha yetu;

NA KWA KUWA, tunaamini kuwa misingi hiyo inaweza tu kutekelezwa katika jamii
yenye mfumo wa demokrasia na utawala bora ambayo Serikali yake inasimamiwa na Bunge
lenye Wabunge waliochaguliwa na wanaowakilisha wananchi, na Mahakama huru
zinazotekeleza wajibu wa kutoa haki bila woga wala upendeleo wowote, na kuhakikisha
kuwa haki za binadamu zinalindwa na kudumishwa na kwamba wajibu wa kila mtu
unatekelezwa kwa uaminifu;

NA KWA KUWA, tunatambua umuhimu wa kutunza mali ya Mamlaka za Nchi na ya
pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu, ubadhirifu na kuhimiza matumizi bora na
endelevu ya rasilimali na maliasili zetu pamoja na kulinda na kuhifadhi mazingira yetu kwa
mustakabali wa maisha ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo;

NA KWA KUWA, tunatambua umuhimu na faida za kujenga, kukuza na kuendeleza
amani, umoja, urafiki na ushirikiano miongoni mwa Watanzania, mataifa mbalimbali ya
Afrika na dunia kwa ujumla;

NA KWA KUWA, azma ya kujenga Umoja wa Bara la Afrika inadhihirishwa na
Muungano wa iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar;

NA KWA KUENDELEZA DHAMIRA YETU HIYO, ni muhimu:
(a) kulinda, kuimarisha na kuudumisha Muungano wa nchi za Jamhuri ya Tanganyika
na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar;
(b) kujenga Taifa huru na linalojitegemea;
(c) kuimarisha na kuendeleza utawala wa sheria;
(d) kukuza na kuendeleza maadili, uwajibikaji na uwazi;
(e) kujenga umoja na mshikamano utakaowezesha kutimiza malengo ya kisiasa,
kiuchumi, kijamii, kimazingira na kulinda urithi kwa ujumla;
(f) kujenga na kuendeleza ukuu wa mamlaka ya watu;
(g) kujenga na kuendeleza utii wa mamlaka ya Katiba; na
(h) kuimarisha na kudumisha uzalendo kwa Taifa miongoni mwa Watanzania;

NA KWA KUZINGATIA, urithi tulioachiwa na Waasisi wa Taifa letu wa kujenga nchi
yenye umoja wa watu wake ambao hawabaguani kwa misingi ya ukabila, dini, rangi, jinsi au
ubaguzi wa aina nyingine yoyote;

NA KWA KUZINGATIA, uzoefu wa zaidi ya Miaka Hamsini ya Uhuru wa Tanganyika,
Miaka Hamsini ya Mapinduzi ya Zanzibar na Miaka Hamsini ya Muungano wa Jamhuri ya
Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, na umuhimu wa ushiriki mpana na bayana wa
wananchi katika utungaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

HIVYO BASI, KATIBA HII YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
ILIYOPENDEKEZWA NA BUNGE MAALUM LA KATIBA imetungwa na SISI
WANANCHI WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA kupitia KURA YA
MAONI kwa madhumuni ya kujenga jamii kama hiyo, na kuhakikisha kuwa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania inaongozwa na Serikali yenye kufuata misingi ya demokrasia na
utawala wa sheria, kujitegemea na isiyofungamana na dini.

SURA YA KWANZA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SEHEMU YA KWANZA
JINA, MIPAKA, ALAMA, LUGHA NA TUNU ZA TAIFA

1.-(1) Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi na Shirikisho
lenye mamlaka kamili ambalo limetokana na Muungano wa nchi mbili
za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ambazo
kabla ya Hati ya Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964, zilikuwa
nchi huru.
(2) Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Shirikisho la
kidemokrasia linalofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa, usawa wa
binadamu, kujitegemea, utawala wa sheria, kuheshimu haki za
binadamu na lisilofungamana na dini.
(3) Hati ya Makubaliano ya Muungano iliyorejewa katika ibara
ndogo ya (1), ndio msingi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na Katiba hii, kwa kadri itakavyorekebishwa, itakuwa ni mwendelezo
wa Makubaliano hayo.

2. Eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni eneo lote la
Tanganyika likijumuisha sehemu yake ya bahari na eneo lote la
Zanzibar likijumuisha sehemu yake ya bahari.

3.-(1) Alama za Taifa zitakuwa ni:
(a) Bendera ya Taifa;
(b) Wimbo wa Taifa; na
(c) Nembo ya Taifa,
kama zitakavyoainishwa katika sheria za nchi.
(2) Sikukuu za Kitaifa zitakuwa ni:
(a) Siku ya Uhuru wa Tanganyika, itakayoadhimishwa tarehe 9
Disemba;
(b) Siku ya Mapinduzi ya Zanzibar, itakayoadhimishwa tarehe
12 Januari;
(c) Siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar,
itakayoadhimishwa tarehe 26 Aprili; na
(d) Sikukuu nyingine zitakazoainishwa na sheria za nchi.
(3) Kila Sikukuu ya Kitaifa itakuwa ni siku ya mapumziko.

4.-(1) Lugha ya Taifa ya Jamhuri ya Muungano ni Kiswahili na
itatumika katika mawasiliano rasmi ya kitaifa na kiserikali.
(2) Bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (1), lugha ya
Kiingereza au lugha nyingine yoyote inaweza kutumika kuwa lugha
rasmi ya mawasiliano ya kiserikali pale itakapohitajika.
(3) Serikali itaweka mazingira yatakayowezesha kuwepo kwa
mawasiliano mbadala zikiwemo lugha za alama, maandishi
yaliyokuzwa na nukta nundu kwenye sehemu muhimu za umma na
katika vyombo vya habari vinavyotangaza habari zake kitaifa kwa ajili
ya watu wenye mahitaji maalum.

Tunu za Taifa. 5. Jamhuri ya Muungano itaenzi na kuzingatia Tunu za Taifa
zifuatazo:
(a) utu;
(b) uzalendo;
(c) uadilifu;
(d) umoja;
(e) uwazi;
(f) uwajibikaji; na
(g) lugha ya Taifa.

SEHEMU YA PILI
MAMLAKA YA WANANCHI, UTII NA HIFADHI YA KATIBA
Mamlaka ya
wananchi.
6. Jamhuri ya Muungano ni nchi inayofuata misingi ya
demokrasia inayozingatia haki ya kijamii, na kwa hiyo:
(a) wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata
madaraka na mamlaka yake kutoka kwa wananchi ambao
kwa umoja na ujumla wao wanaimiliki na kuipatia Katiba
hii uhalali;
(b) lengo kuu la Serikali litakuwa ni maendeleo na ustawi wa
wananchi;
(c) Serikali itawajibika kwa wananchi; na
(d) wananchi watashiriki katika shughuli za Serikali kwa
mujibu wa masharti ya Katiba hii.

Watu na
Serikali.
7.-(1) Muundo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo
vyake, katika uendeshaji na utekelezaji wa shughuli zake, utazingatia
azma ya kukuza umoja wa kitaifa na kudumisha heshima ya Taifa.
(2) Kwa madhumuni ya masharti ya ibara ndogo (1), mamlaka
ya nchi na vyombo vyake vinawajibika kuelekeza sera, sheria na
shughuli zake zote kwa lengo la kuhakikisha kwamba:
(a) utu, heshima na haki nyingine za binadamu zinalindwa,
zinathaminiwa, zinahifadhiwa na kudumishwa kwa
kuzingatia mila na desturi za Watanzania na mikataba
mbalimbali iliyoridhiwa na Jamhuri ya Muungano;
(b) sheria za nchi zinasimamiwa na kutekelezwa;
(c) shughuli zinazofanywa zinatekelezwa kwa njia ambazo
zitahakikisha kwamba utajiri wa Taifa unaendelezwa,
unahifadhiwa na kutumiwa kwa manufaa ya wananchi
wote kwa jumla na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu
mwingine;
(d) ardhi ikiwa rasilimali kuu na msingi wa Taifa inalindwa,
inatunzwa na kutumiwa na wananchi wa Tanzania kwa
manufaa, maslahi na ustawi wa kizazi cha sasa na vizazi
vijavyo;
(e) maendeleo ya uchumi wa Taifa yanapangwa na kukuzwa
kwa ulinganifu na kwa pamoja na kwa namna ambayo
inawanufaisha wananchi wote;
(f) kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi anafanya kazi, na
kazi maana yake ni shughuli yoyote ya halali inayompatia
mtu kipato chake;

(g) kunakuwepo fursa na haki zilizo sawa kwa wananchi wote,
wanawake na wanaume, bila ya kujali rangi, kabila,
nasaba, itikadi, dini au hali ya mtu;
(h) aina zote za dhuluma, vitisho, ubaguzi, unyanyasaji,
rushwa, uonevu au upendeleo zinaondolewa nchini;
(i) utajiri wa rasilimali na maliasili za Taifa unaelekezwa
katika kuleta maendeleo, kuondoa umaskini, ujinga na
maradhi; na
(j) nchi inaongozwa kwa kufuata misingi ya demokrasia,
utawala wa sheria na kujitegemea.

Ukuu na utii
wa Katiba.
8.-(1) Katiba hii ni sheria kuu katika Jamhuri ya Muungano kwa
kuzingatia masharti ya Katiba hii.
(2) Kwa madhumuni ya ibara ndogo ya (1), endapo masharti ya
sheria yoyote yatatofautiana na masharti ya Katiba hii, masharti ya
sheria hiyo yatakuwa batili na yatatenguka kwa kiwango kile
kinachotofautiana na masharti ya Katiba hii.
(3) Mtu yeyote, chombo, taasisi, jumuiya na wakala wowote wa
mamlaka ya nchi na mamlaka binafsi zinao wajibu wa kuzingatia
masharti ya Katiba hii na sheria za nchi na kuzitii.
(4) Sheria yoyote, mila, desturi au uamuzi wowote wa chombo
cha dola, ofisa wa Serikali au mtu binafsi ni sharti ufuate na kuendana
na masharti yaliyomo kwenye Katiba hii na kwamba sheria, mila,
desturi au uamuzi wowote ambao hautawiana au kwenda sambamba na
masharti ya Katiba hii utakuwa batili.
(5) Serikali itaweka utaratibu wa kuwawezesha wananchi
kuifahamu, kuilinda na kuitii Katiba.

Hifadhi ya
Utawala wa
Katiba.
9.-(1) Mtu au kikundi cha watu hakitachukua au kushikilia
mamlaka ya nchi isipokuwa kwa mujibu wa Katiba hii.
(2) Kitendo chochote kinachokiuka masharti ya ibara ndogo ya
(1) ni batili na ni kitendo cha uhaini kama itakavyoelezwa katika sheria
za nchi.

SURA YA PILI

MALENGO MUHIMU, MISINGI YA MWELEKEO WA
SHUGHULI ZA SERIKALI NA SERA ZA KITAIFA

Malengo
Makuu.
10.-(1) Lengo Kuu la Katiba hii ni kulinda, kuimarisha na
kudumisha haki, udugu, amani, umoja na utengamano wa wananchi wa
Jamhuri ya Muungano kwa kuzingatia ustawi wa wananchi na kujenga
Taifa huru lenye demokrasia, utawala bora, maendeleo endelevu na
kujitegemea.
(2) Bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (1), lengo hilo
kuu litaendelezwa na kuimarishwa katika nyanja zote kuu,
ikijumuisha nyanja za kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na
kimazingira.
(3) Katika kutekeleza malengo ya Taifa ya:
(a) kisiasa, Serikali itachukua hatua zinazofaa ili -
(i) kuhakikisha kuwa inazuia, inapinga na kuondoa
dhuluma, vitisho, ubaguzi, unyanyasaji, rushwa,
uonevu na upendeleo miongoni mwa wananchi kwa
misingi ya itikadi, asili ya mtu, sehemu anayotoka,
nasaba, kabila, jinsi, dini au imani yake;
(ii) kuhakikisha uwepo wa amani na kujenga utamaduni
wa kuenzi, kuheshimu na kudumisha amani, umoja na
utengamano, ushirikiano na uvumilivu wa kisiasa kwa
madhumuni ya kukuza maendeleo ya kijamii na
kiuchumi;
(iii) kuhakikisha uwepo wa ulinzi, usalama na ustawi wa
watu na mali zao, na kuepuka kufanya jambo lolote
litakalohatarisha au kwenda kinyume na lengo hilo;
(b) kijamii, Serikali inachukua hatua zinazofaa ili -
(i) kuhakikisha kwamba heshima ya binadamu
inahifadhiwa na kudumishwa kwa kufuata mila,
desturi na Kanuni za Tangazo la Dunia kuhusu Haki
za Binadamu na mikataba mingine ya kimataifa
iliyoridhiwa na Tanzania;
(ii) kuhakikisha kwamba Serikali na vyombo vyake vyote
vya umma vinatoa nafasi na fursa zilizo sawa kwa raia
wote, bila ya kujali itikadi, jinsi, rangi, kabila, dini,
nasaba, hali ya mtu au mahali alipo;
(iii) kujenga utamaduni wa kuwepo ushirikiano,
maelewano na maridhiano, uvumilivu na kuheshimu
mila, desturi na imani ya dini ya kila mtu;
(iv) kuhakikisha kuwa msaada na hifadhi ya jamii
inatolewa kwa watu wasiojiweza, wazee, wagonjwa,
watoto na watu wenye ulemavu;
(v) kuwezesha upatikanaji na utoaji wa huduma ya
msaada wa kisheria kwa wananchi wasiokuwa na
uwezo wa kumudu gharama za uwakili;
(vi) kuweka utaratibu unaofaa kwa ajili ya kufanikisha
utekelezaji wa haki ya mtu kujipatia elimu na kuwa
huru kupata fursa sawa ya kutafuta elimu katika fani
anayoipenda hadi kufikia upeo wowote kulingana na
stahili na uwezo wake;
(c) kiuchumi, Serikali inachukua hatua zinazofaa ili -
(i) kuwaletea wananchi maisha bora kwa kuondoa
umaskini;
(ii) kuhakikisha kwamba shughuli za Serikali
zinatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha kuwa
utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na
--------- kwa manufaa ya wananchi wote kwa
jumla na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine;
(iii) kuweka mazingira bora kwa ajili ya kuanzisha na
kuendeleza vyombo vya uwakilishi wa wakulima,
wafugaji na wavuvi;
(iv) kuweka mazingira bora ya kufanya biashara na
kukuza fursa za uwekezaji;
(v) kuweka mazingira bora kwa ajili ya kukuza kilimo,
ufugaji na uvuvi kwa kuhakikisha kuwa wakulima,
wafugaji na wavuvi wanakuwa na ardhi na nyenzo
kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao;
(vi) kuweka mazingira bora ya uzalishaji wa mazao kwa
wakulima, wafugaji na wavuvi, utafutaji na
uendelezaji wa masoko ya mazao yao;
(vii) kuweka utaratibu mzuri wa upangaji na usimamiaji
wa mizania ya bei za mazao na pembejeo;
(viii) kuimarisha na kuendeleza uwekezaji wa ndani,
upatikanaji wa pembejeo za kilimo, maeneo ya
ufugaji na vifaa vya uvuvi;
(ix) kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa fursa na
nafasi za wazi kwa watu wote na kuanzisha shughuli
za kiuchumi na kukuza mazingira yaliyo bora kwa
ajili ya kuhamasisha sekta binafsi katika uchumi;
(x) kuhakikisha kuwa kila mtu mwenye uwezo wa
kufanya kazi anapata fursa ya kufanya kazi, kwa
maana ya kufanya shughuli yoyote halali
inayompatia kipato;
(xi) kuhamasisha uwekezaji wa pamoja baina ya raia na
wasio raia katika miundombinu ya uchumi, uvunaji
wa rasilimali na maliasili za Taifa;
(xii) kuweka utaratibu wa usimamizi wa kiuchumi na
uandaaji wa mipango, kuwezesha malengo ya muda
mfupi, muda wa kati na muda mrefu kutekelezwa;
(xiii) kuwezesha na kuendeleza matumizi ya sayansi na
teknolojia na kukuza ubunifu katika shughuli za
kiuchumi na maendeleo ya Taifa kwa jumla;
(d) kiutamaduni, Serikali itachukua hatua zinazofaa ili -
(i) kulinda na kuhifadhi urithi wa asili, malikale na
sehemu zenye umuhimu wa kihistoria au kidini ili
kuepuka uharibifu, udhalilishaji, wizi au utoroshaji
nje ya nchi;
(ii) kulinda, kuhifadhi na kuendeleza tamaduni za watu
wa jamii mbalimbali ambazo zinaendeleza na kukuza
utu na hadhi yao kwa namna ambayo haikinzani na
Malengo Muhimu, Misingi ya Mwelekeo wa
Shughuli za Serikali na Sera za Kitaifa;
(iii) kutambua, kulinda na kuendeleza lugha ya Kiswahili;
na
(e) kimazingira, Serikali itachukua hatua zinazofaa ili -
(i) kuhakikisha kuwa ni haki na wajibu wa kila mtu
kulinda na kudumisha mazingira kwa faida ya kizazi
cha sasa na vizazi vijavyo;
(ii) kuhakikisha kuwa taasisi za umma na asasi za kiraia
zinawajibika kusimamia utekelezaji na uzingatiaji wa
matakwa ya kisheria katika kulinda na kuhifadhi
mazingira;

(iii) kuhakikisha kuwa wananchi wa Tanzania ndiyo
wenye haki ya kumiliki rasilimali za kijenetiki za
Tanzania kwa manufaa ya Taifa.

Utekelezaji
wa Malengo
ya Taifa.
11.-(1) Malengo ya Taifa yaliyoainishwa ndani ya Katiba hii
yatakuwa ni mwongozo kwa Serikali na mamlaka nyingine na kwa
kila mwananchi katika matumizi au kutafsiri masharti ya Katiba hii
au sheria nyingine yoyote na katika utekelezaji wa uamuzi wa kisera
kwa madhumuni ya kujenga jamii iliyo bora, huru na makini.
(2) Serikali itatoa taarifa Bungeni si chini ya mara moja
katika kila mwaka, kuhusu hatua zilizochukuliwa na mamlaka ya
nchi ili kuhakikisha utekelezaji wa malengo ya Taifa yaliyoainishwa
katika Katiba hii.

Sera ya
Mambo
ya Nje.
12.-(1) Sera ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Muungano
inalenga na kuzingatia maslahi ya Taifa na mamlaka kamili ya nchi
na kwamba sera hiyo inatekelezwa kwa uwazi ili -
(a) kukuza ujirani mwema, ushirikiano wa kikanda na wa
kimataifa;
(b) kukuza maendeleo na ushirikiano wa kiuchumi wenye tija
kwa Taifa na raia wake;
(c) kuunga mkono na kuendeleza jitihada za kuimarisha
Umoja wa Afrika, sera ya kutofungamana na upande
wowote na ushirikiano na nchi zinazostawi duniani;
(d) kuheshimu sheria za kimataifa;
(e) kuzingatia mikataba ya kimataifa na ya kikanda yenye
maslahi kwa Jamhuri ya Muungano na kutatua migogoro
ya kimataifa kwa njia ya majadiliano, usuluhishi,
maridhiano au mahakama;
(f) kukuza uzingatiaji wa haki za binadamu na uhuru wa
watu;
(g) kupambana na makosa ya kimataifa ya jinai; na
(h) kuheshimu uhuru wa mataifa mengine.
(2) Bunge litatunga sheria, pamoja na mambo mengine,
itakayoelekeza na kusimamia utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje.

SURA YA TATU
MAADILI NA MIIKO YA UONGOZI NA UTUMISHI WA UMMA

SEHEMU YA KWANZA
MAADILI YA UONGOZI NA WATUMISHI WA UMMA

Dhamana ya
Uongozi wa
Umma.
13.-(1) Madaraka anayopewa kiongozi wa umma:
(a) ni dhamana na atatumia madaraka hayo na kutekeleza
wajibu wake kwa:
(i) kuzingatia masharti ya Katiba hii;
(ii) kuheshimu wananchi;
(iii) kukuza hadhi ya Taifa na kulinda heshima ya ofisi
anayoitumikia; na
(iv) kukuza imani na heshima ya ofisi kwa wananchi;
(b) yanatoa wajibu kwa kiongozi kuwatumikia wananchi.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom