Peter Dafi
JF-Expert Member
- Apr 1, 2012
- 389
- 272
Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi {CCM} na Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt Jakaya Mrisho Kikwete jana Aprili 23, 2016 ametembelea Chuo Kikuu cha Kilimo na Misitu cha jimbo la Fujian (Fujian Agriculture and Forest University-FAFU) kilichopo katika mji mkuu wake Fu Zhou.
Mwenyekiti alikaribishwa chuoni hapo kuonyeshwa hatua ambazo jimbo hilo imepiga katika kuendeleza kilimo cha kisasa, teknolojia ya kuzalisha mbegu na teknolojia ya kupambana na magonjwa na wadudu waharibio mazao. Akiwa chuoni hapo, alikutana pia na wanafunzi wa kitanzania wanaosomea shahada za uzamivu kwa ufadhili wa serikali ya China.
Katika mazungumzo yake na Mkuu wa Chuo hicho Profesa Lan Siren, Mhe Kikwete amependekeza kuanzishwa kwa mahusiano na ushirikiano baina ya Chuo Cha Kilimo SUA na Chuo hiko. Pia amependekeza wanafunzi na wakufunzi wa chuoni hapo kuja Tanzania kufanya mafunzo ya vitendo na tafiti zao.
Kufuatia pendekezo hilo, Rais wa Chuo hicho ameelezea utayari wa Chuo hicho kushirikiana na SUA. Aidha, ameelezea kulipokea ombi la Mwenyekiti la kuongeza nafasi za masomo kwa vijana wa Tanzania na kuahidi kulifanyia kazi ombi hilo.
Chuo Kikuu cha FUFA kina takribani wanafunzi elfu arobaini (40,000) ambapo wanafunzi kutoka Afrika ni takribani 120 kati yao watatu tu (3) wanatoka nchini Tanzania.
Mhe Kikwete yuko nchini China kwa ziara ya kichama iliyotokana na mualiko rasmi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China na Katibu Mkuu wa Chama Cha Kikomunisti cha China Mhe Xi Jinping.