Chachu Ombara
JF-Expert Member
- Dec 11, 2012
- 6,042
- 10,787
Rais Dkt. John Pombe Magufuli amemsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa DART, Bi. Asteria Mlambo.
TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA - TAMISEMI
TAARIFA KWA
VYOMBO VYA HABARI
Ndugu wanahabari nimewaita hapa leo ili mnisaidie kufikisha ujumbe kwa wananchi kuhusu mradi wetu wa Mabasi yaendayo Haraka katika Jiji la Dar es Salaam (DART – BRT).
Kama mnavyofahamu Serikali ilianzisha mradi huu ili kupunguza msongamano wa magari barabarani kwa madhumuni ya kurahisisha usafiri na usafirishaji katika Jiji letu.
Kutokana na kukamilika kwa sehemu ya ujenzi wa miundombinu ya Awamu ya Kwanza ya mradi, Serikali iliamua tuwe na mtoa huduma wa mpito (Interim Service Provider) kabla ya kumpata mtoa huduma wa kudumu (Service Provider).
Mtoa huduma wa mpito alipaswa kupatikana kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma. Hata hivyo, Serikali imebaini ukiukwaji wa wazi wa sheria hiyo wakati wa kumpata mtoa huduma wa kipindi cha mpito.
Kufuatia hali hiyo nimeamua kumsimamisha kazi kuanzia leo tarehe 23 Desemba, 2015, Mtendaji Mkuu wa DART, Bi. Asteria Mlambo ili kupisha uchunguzi.
Sababu za kumsimamisha kazi ni:
i. Kushindwa kuzingatia Sheria ya Manunuzi ya Umma wakati wa kumpata mtoa huduma katika kipindi cha mpito;
ii. Kushindwa kuchukua hatua hata pale alipobaini kuwa mtoa huduma wa mpito amekiuka masharti ya mkataba wa kutoa huduma ya mpito; na
iii. Kufanya maamuzi makubwa pasipo kuishirikisha Bodi ya Ushauri ya DART.
Aidha, Serikali inatambua kuwa wapo watumishi wa DART ambao hawakumshauri vizuri Mtendaji Mkuu. Watumishi hao watachunguzwa na kuchukuliwa hatua na Kaimu Mtendaji Mkuu atakayeteuliwa.
Nimemwagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI kuendelea na taratibu za kinidhamu dhidi ya Mtendaji Mkuu aliyesimamishwa kazi.
Naitumia nafasi hii kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua kwa haraka na uangalifu ili mradi huu uweze kuanza kutoa huduma bora ya usafiri kwa wakazi wa Dar es salaam bila kuchelewa zaidi. Aidha, natoa rai kwa wananchi kuitunza na kuithamini miundombinu ya DART kwa kuwa imegharimu fedha nyingi kwa manufaa yao.
Imetolewa na:-
George B. Simbachawene,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI