Heshima yetu kama nchi kwa kiasi kikubwa itatokana na heshima ya Rais wetu. Ndiyo kusema Rais akijiheshimu na akaheshimiwa na sisi pia tunapata heshima. Vivyo hivyo ikitokea Rais akawa haheshimiwi nje ya mipaka yetu sisi pia tunakosa heshima kama nchi.
Akiwa makini tutaonekana makini kama nchi. Akiwa mropokaji tutaonekana waropokaji kama nchi. Akiwa mlevi tutaonekana walevi kama nchi. Akiwa mwizi tutaonekana ni majambazi kama nchi. Akiwa malaya na mzinzi tutaonekana wazinzi na malaya kama nchi.
Kwahiyo urais ni taswira ya Taifa na unabeba dhamana nzito. Ni lazima basi tumtathimini mtu yeyote anayetaka kuwa Rais wetu kwa jicho kali na macho mapana katika kila hali aliyo nayo: maneno yake, matendo yake, haiba yake, akili yake, afya yake, n.k. Ili aweze kukidhi haja ya kiti cha urais sawasawa na sawia, Rais tunayemchagua lazima asiwe mtu wa kawaida. Ni lazima awe ni mtu bora kuliko sisi wote.
Tutafanya makosa makubwa kuchagua mtu wa kawaida, anayefanana na sisi, mwenye tabia kama zetu na mwenye maono kama sisi.
Kwa kuwa Rais si mtu wa kawaida na hapaswi kuwa mtu wa kawaida, ni watu wachache sana wanaoweza kuchukua dhamana ya urais katika nchi yeyote ile duniani. Kwa sababu hii ni muhimu tuwe makini sana tunapochagua mgombea urais kwa vyama vyote ili tushindanishe watu ambao ni bora kabisa katika nchi yetu.
Tukikosea tukachagua mtu wa kawaida huyu ataendesha mambo kikawaida sana. Kwa hiyo kama wananchi walio wengi wamezoea ubabaishaji, uhuni, rushwa, wizi, n.k., tutapata Rais ambaye ni mbabaishaji, mhuni, na mpenda rushwa kama sisi na hatutasogea.
Ninajadili vigezo vya mtu anayefaa kuwa Rais wetu wa tano. Vigezo hivi nimevigawa katika makundi makubwa mawili. Kundi la kwanza linabeba sifa za kihaiba na kundi la pili ni la sifa za kikazi. Leo ninabainisha sifa za kihaiba. Kwa maoni yangu, mgombea urais anapaswa kuwa na vigezo angalau sita vinavyoangukia katika kundi la sifa za kihaiba.
Kigezo cha kwanza ni uaminifu. Ili Rais aweze kukamilisha ajenda yake, ni lazima aaminike kwa watu anaowaongoza. Bila watu kumuamini hakuna atakachofanya na watu wakakikubali. Kama watu hamwamini Rais itasababisha wabunge na vyombo vingine vya dola kuanza kumtilia shaka katika utendaji wake na hii itasababisha programu zake nyingi zikwame kwa sababu ufanisi wake unategemea kuungwa mkono na vyombo vingine vya dola likiwamo Bunge.
Tukumbuke pia kwamba Rais wa nchi ndiye msuluhi